Thursday, December 11, 2014

Mara nyingine ulemavu ni njia ya kufikia mafanikio


Ni ukweli usiopingika, mtu mwenye ulemavu anapitia changamoto nyingi sana! Inafika mahali mtu mwenye ulemavu anatabiriwa mabaya tu kila wakati. Namkumbuka profesa wangu mmoja mwenye ulemavu, aliniambia kitu cha ajabu sana. Alisema: "Heshima ya mtu mwenye ulemavu inajengwa na mtu mwenyewe mwenye ulemavu". Alitoa historia yake kuhusu shule. Sekondari ya kwanza aliyopangiwa kufundisha walimkataa walimu na wanafunzi wote. Alipopewa dakika 5 za kuonyesha uwezo wake alizitumia kikamilifu, kisha akaaga kuondoka kwa vile hakuwa na nafasi ya kufundisha shule ile kwa sababu za kukataliwa. Alipofika ofisi ya mkuu wa shule tu ili aage kurudi wizarani waliompangia shule, wanafunzi wakatuma mwakilishi ili kuomba msamaha na kumtaka aendelee kuwafundisha. Mwalimu yule alikubali kubaki na kuendelea kufundisha.

Mwaka mwingine mwalimu huyu aliomba kwenda kusoma Masters Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam. Alipofika chuoni wanachuo wenzake wakaulizana: Naye huyu amekuja kusoma? Profesa huyu anasema baada ya wiki mbili walitambua kuwa kweli alikwenda kusoma.

Hayo maneno na kejeli za hapa na pale juu ya ulemavu wake ndiyo yaliyompelekea kuongeza bidii ili kuwahakikishia kwa vitendo kuwa "Ulemavu Si Kukosa Uwezo" (Disability isn't inability). Bila shaka huyu mwalimu asingekuwa profesa kama asingepitia hizi changamoto. Asingekuwa mtu mwenye kujua mengi kuhusu ulemavu kama yeye mwenyewe asingekuwa kwenye hali ya ulemavu halisi.

Sometimes, disability is a golden chance for the hidden opportunities; because through disability state the prudent person finds gains!

Wednesday, December 10, 2014

Nilimfundisha asidharau watu wenye ulemavu


Kati ya vitu vigumu sana kwa watu wenye ulemavu ni kudharauliwa kwenye jamii zao. Hata wewe waweza kumbuka vitendo hivyo kwa ukaribu.

Naikumbuka siku ile! Nikiwa stationery moja hapa mkoani Morogoro, kwa nje kidogo kuna sofa ya kukaa wateja. Mara akaja kijana mmoja aliyekuwa na mtindio, akakaa kwenye sofa hilo. Katika hilo sofa alikuwa amekaa mama mtu mzima, tena ni mfanyakazi, zaidi ya yote ni mwalimu. Ghafla nikaona yule mama amesimama pembeni mwa sofa huku anajisemea polepole huku akisonya. Nikamwangalia kwa dakika kama tano hivi, nikaona amekosa amani kwa vile lile sofa amekalia kijana mwenye ulemavu.

Nikamsogelea kidogo yule mama, nikamwuliza: Unamfahamu huyu kijana? Akasema hapana! Nikamwambia: Huyu kijana ana mama yake na baba yake. Nikaongeza kwa kumtaarifu kuwa: Ulemavu unaweza kumpata mtu yeyote na wakati wowote wa maisha ya mwanadamu.

Nilichogundua ni kwamba kuna baadhi ya watu hudhani ulemavu wameandikiwa jamii fulani tu ya watu. Pia kwa kukosa uzoefu wa kuchangamana na jamii ya watu wenye ulemavu kunawapelekea wao kuwa na mitazamo ya kibaguzi. Siku inapotokea wamepata watoto wenye ulemavu hawa watu ndio huwaficha ndani watoto wao, au wanawaua mapema kabla hawajawa wakubwa.

Hata kama hawataki kuwaona watu wenye ulemavu, lakini wajue ubinadamu wa binadamu wote unafanana, na kuwa na haki sawa za kimaisha. Pia, binadamu ni mtu yeyote aliyezaliwa na binadamu, na anayo haki ya asili kwa kuwa amezaliwa binadamu bila kujali umbile lake.

Fikiri kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi!

Monday, December 8, 2014

Kona za Elimu Maalum/Corners of Special Education


Elimu Maalum ni maalum kwa watu maalum. Hii elimu inahusisha watu wa aina mbili; wakwanza ni yule mhitaji wa elimu hii maalum; na wa pili ni mtu ambaye amejitoa kwa moyo wake wote na kwa nguvu zake zote ili kutoa huduma ya elimu maalum kwa wahitaji wa elimu maalum.

Rose Yona, zao la chuo kikuu cha SEKOMU (Sebastian Kolowa Memorial University); amejikita zaidi katika kusaidia kutafsiri maneno kwa lugha ya alama kwa watu viziwi.

Anajenga jamii jumuishi!

Angalia hii video kwa makini.

Special Education is special for special people. This education involves two kinds of people; the first person being the one who is in need of special education; and the second one is that person who is devoted to intervene the one with special needs and who is exactly needs special education.

Rose Yona, the product of SEKOMU; is devoted to help deaf people to by translating normal words into sign language.

She is creating an inclusive society!

Check this video carefully.


Fikiri Kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi!

Saturday, December 6, 2014

Watu Wenye Ulemavu Sasa wapata mkombozi


Kuanzishwa kwa Baraza la watu wenye ulemavu Tanzania ndiyo mwanzo wa huduma bora kwa watu wenye ulemavu nchini. Chini ya uongozi wa mwenyekiti wake, profesa Edward Bagandanshwa, mambo yatatengemaa.
Katika picha (hapo juu), profesa Bagandanshwa alikuwa akitoa hotuba kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani tarehe 3 Disemba 2014, mkoani Iringa.

Tujenge jamii jumuishi kwa ustawi Watanzania wote!

Friday, December 5, 2014

Tumsaidie mtoto MASHAKA AMIN aende shule kusoma




MASHAKA AMINI HOSSEN ni mtoto mwenye ulemavu. Taarifa zake ni hizi hapa:

Aina ya ulemavu: Kiziwi (Deaf) na Ububu (Dump)
Umri: Miaka 9
Mahali alipo: Mtaa wa Mangedere
                      kijiji cha Kichangani, Turiani
                      mkoa wa Morogoro, Tanzania.

Wazazi wa MASHAKA AMINI ni wakulima wa kipato cha chini, hawamudu kumhudumia mtoto wao kwenda shule ya viziwi. Hitaji kuu la mtoto ni kutafutiwa shule ya watoto viziwi na kusomeshwa.

Mawasiliano:

Baba mzazi- +255714679645

Mwalimu Philemon Sokime: +255655410031/+255766750941/sokime2012@gmail.com

Mzazi wa mtoto MASHAKA AMINI anawaomba wasamaria wema waweze kumsaidia kitaalam na kifedha ili mwanae aweze kusoma shule za viziwi ndani ya Tanzania. Tatizo linalomkabili huyu mtoto MASHAKA AMINI ni kukosa shule iliyo jirani na huku wilaya ya Mvomero. Wilaya hii haina shule hata moja kwa ajili ya wanafunzi viziwi. Mtoto aliwahi pelekwa shule ya msingi Kichangani mwaka 2012 lakini walimu walishindwa kumfundisha kwa kuwa hawana utaalam wa elimu maalum.
Wadau wote wa elimu yatupas tufikirie namna ya kutatua tatizo hili kwa mtoto MASHAKA AMINI ili aweze kuelimika na baadae kuondoa utegemezi usio wa lazima.


Mwl Philemon Sokime akiwa na mtoto 
MASHAKA AMINIkatika mitaa ya 
soko kuu la Kichangani, Turiani



AMINI akiwa na jirani yake mitaa ya sokoni



Mwl Philemon Sokime yuko na MASHAKA AMINI




MASHAKA AMINI akifurahia madhari yake!

MASHAKA AMINI akiigiza kuuza vyombo!



















MASHAKA AMINI akifurahia gari la kuchezea
watoto alilomnunulia mwalimu Philemon Sokime


Wednesday, December 3, 2014

Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani Disemba 3, 2014


Maudhui: Maendeleo Endelevu: Ahadi ya Kiteknolojia

Siku ya Kimataifa ya Watu wenye ulemavu duniani mwaka huu inaangazia majukumu ya teknolojia katika:

-Kupunguza hatari ya majanga kwa watu wenye ulemavu
-Kujenga mazingira wezeshi ya kazi kwa watu wenye ulemavu
-Ulemavu na ujumuishi wa malengo ya maendeleo endelevu

Kwa maudhui haya ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani; teknolojia ndiyo uti wa mgongo kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kupunguza utegemezi usio wa lazima kwa watu wenye ulemavu kwenye mazingira yao ya maisha ya kila siku.

Fikiri Kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi

Tuesday, November 11, 2014

Hatari kwa watu wapatao ulemavu ukubwani


Watu wengi hudhani kuwa ulemavu ni laana, mikosi au balaa. Watu wengine huenda mbali zaidi kwa kuwabagua watu wenye ulemavu kwa ulemavu wao. Hebu tuweke bayana madhara wayapatao watu wenye dhana hizi potofu mara wao wenyewe wakutwapo na ulemavu.

Moja, watu hawa maisha yao huwa ni mafupi sana kwa kuwa huwa na msongo wa mawazo wakijiona kuwa wamebeba uzito wa dunia. Huishia kuwa na msongo wa mawazo.

Pili, watu hawa hushuka sana umaarufu wao.  Watu hawa huanza kujitenga na wenzao kwa kujinyanyapaa wao wenyewe.

Tatu, ni watu wa lawama sana. Hupenda kulalamika na kunung'unika mno baada ya kukosa uwezo wa kufanya vitendo fulanifulani ambavyo awali alipendelea kuvifanya.

Nne, watu hawa hujishusha thamani, hawaoni umuhimu tena wa kuishi.

Ushauri!

Ni vema tukawa na msimamo chanya juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Hii itatusaidia kipindi ambacho tunakutwa na ulemavu; kwa kuwa ulemavu si wa mtu mmoja; ulemavu unaweza kumpata mtu yeyote, wakati wote na mahali popote. Hata hivyo ulemavu hauepukiki kwa namna yoyote kwenye jamii zetu. Ukimwona mtu mzee lazima atalalamika kuhusu macho kutokuona vema, masikio kukosa ufanisi wake, kumbukumbu kupungua, nk.

Cha zaidi sana, ni kwamba, ulemavu ni fikira za mtu binafsi. Tumeshuhudia watu wengi tunaowaita wanaulemavu wakiwa wasomi wa juu, wenye uchumi mzuri, wana familia za kutamaniwa na wengi, nk.