Sunday, September 27, 2015

Haki na Ustawi wa watu wenye ulemavu baada ya uchaguzi mkuu Tanzania, 2015



 
Siku zote binadamu ili kupata mahitaji yake lazima adai haki ya mambo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Haki ya Mtanzania yeyote ndiyo haki ya mtu mwenye ulemavu. Ulinzi wa Mtanzania ni haki ya mtu mwenye ulemavu, haki ya mafanikio ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya Mtanzania yeyote ni ya mtu mwenye ulemavu pia! Naam, habari njema yoyote inayohubiriwa kwenye majukwaa ya siasa kwa Watanzania ni ya mtu mwenye ulemavu pia.

Nimejaribu kujiuliza mambo kadhaa kutokana na historia ya Tanzania kwa mapito ya watu wenye ulemavu.


1. Habari ya kuwaondoa watu wenye ulemavu Dar miaka ile kwa kisingizio cha kusafisha jiji haitaendelea?


2. Habari ya kuondoa biashara za watu wenye ulemavu kando ya barabara imeshakwisha?


3. Tabia ya kutuma sungusungu wahusike kuwatafuta albino wakitekwa imesitishwa?


4. Habari ya wanafunzi kadhaa wenye ulemavu kwenye mikoa ambayo haina shule maalum kwao imekwisha?


5. Mauaji ya wenzetu albino hayataendelea tena?


Kama maswali yote haya yatakuwa na majibu hasi, basi uchaguzi mkuu kwa watu wenye ulemavu utakuwa si wa furaha wala wenye ustawi kwao.

Tunapokuwa tunaongea habari za watu wenye ulemavu kwenye siasa tusidhani kuwa wao hawana vionjo vya moyo na hisia. You feel, they feel!


Hakika, ustawi wa Watanzania kwenye nyanja yoyote ya maisha ndio ustawi wa watu wenye ulemavu pia!

Ninatamani kuiona Tanzania yenye kuleta usawa kwa binadamu kwa nyanja zote za maisha na kwa ngazi zote kuanzia kaya, mtaa, kijiji, wilaya, mkoa na, taifa kwa ujumla wote. Nimesema haya kwa kuwa nimeshuhudia huduma hafifu kwa watu wenye ulemavu, hasa za kijamii. Tuijenge nchi yetu iwe mahali pa kutengeneza na kusambaza usawa kwa mataifa mengine.  






Fikiri Kijumuishi ~ Tenda Kijumuishi ~ Jenga Taifa Jumuishi!

Thursday, May 21, 2015

Kwa tukio hili kwa walemavu serikali ijitazame upya




Walemavu wanaofanya biashara katika soko la Karume Mchikichini wamelazimika kulala katika makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya masaa sita wakilalamikia kuvunjiwa meza zao za biashara na halmashauri ya manispaa za Ilala, hali iliyosabaisha baadhi ya barabara kushindwa kupitika kutokana na kuwepo kwa msongamano mkubwa wa magari.

ITV imeshuhudia walemavu hao wakiwa wamekaa katikati ya makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru bila woga, huku wakifukuza watu ovyo kwamba hawahusiki katika kuwasidia, ambapo katika mahojino na baadhi yao wamesema wamesikitishwa na kitendo cha serikali ya wilaya ya Ilala kuwavujia meza zao na kusababisha upotevu wa baadhi ya mali zao na kuongeza kuwa iwapo serikali haitaingilia kati sakata lao watalala hapo barabarani.

Licha ya barabara mbalimbali kushindwa kupitika kutokana na sakata hilo ambalo limevuta hisia za watu wengi, baadhi ya madereva wamelalamikia kusimama katika msongamano kwa masaa mengi
Huku wakidai kuwa kuendelea kwa sakata hilo inasababisha shughuli mbalimbali muhimu ikiwemo shughuli za maendeleo kusimama.

Kutokana na hasira za kuvunjiwa meza zao majira ya usiku bila taarifa, baadhi ya viongozi waliofika katika eneo hilo ili kuzungumza nao walijikuta katika wakati mgumu huku askari wa polisi wakitumia hekima ya kutowatawanya watu hao kwani kwa kufanya hivyo wengi wao wangeumia.


Majira ya saa kumi jioni huku msongamano wa magari ikiendelea kutesa watu, baadhi ya watu walionekana kutembelea kwa mguu katika baadhi ya barabara kwa kukosa usafiri huku mkuu wa wilaya ya Ilala Reymond Mushi akikubali kuwepo kwa maelezo ya maaandishi kuwa wafanyabiashara hao watarudi katika maeneo yao huku uchunguzi ukianza mara moja ili kubaini madhara ya vunjavunja hiyo pamoja na suala la fidia.

Tujiulize kidogo!

Kwa miaka mingi watu wenye ulemavu wamebandikwa (labeled) majina ya kuwa ni ombaomba, ilifika mahali miaka ya 1990's katika jiji la Dar Es salaam watu wenye ulemavu walikusanywa na kurudishwa katika mikoa waliyotoka wakidaiwa kuharibu jiji hilo. Siku zote tunaimba taifa jumuishi kumbe si mtazamo wa kitaifa hasa.
Je, serikali inataka watu wenye ulemavu waendelee kuwa maskini?
Je, kuna fikira za kijumuishi hapo?
Je, serikali inataka kuwaondoa tena watu wenye ulemavu Dar?
Je, hawajui kuwa hata watu wenye ulemavu wana haki ya maisha bora?

Tufikiri kijumuishi ~~~ Tutende Kijumuishi ~~~ Tujenge taifa jumuishi

Chanzo: ITV Tanzania

Tuesday, April 28, 2015

Mheshimiwa January Makamba ana uzoefu wa kuhudumia na kuwajali watu wenye mahitaji maalum



 

 Simulizi ya Mheshimiwa January Makamba

Kazi yangu kumhudumia Mark miaka 17 iliyopita na ninayojifunza katika maisha ya kila siku. 

Niliandika kumbukumbu hii mwaka jana mwezi Novemba nikiwa safarini kwenda Magu. Nilimkumbuka rafiki yangu wa zamani aliyekuwa na matatizo ya akili, rafiki ambaye sitamsahau. Mwaka 1998, mwaka mmoja baada ya kufika nchini Marekani kwa masomo yangu ya Chuo Kikuu, nilitafuta na kupata kazi ya muda katika majira ya joto katika jiji la Boston kuhudumia wagonjwa wa akili katika nyumba ambazo wagonjwa hao huwekwa kwa uangalizi maalumu. Kazi ya namna hii ilikuwa kazi ya kawaida kwa wanafunzi na wahamiaji kama mimi katika kujikimu kwa kipato - ilikuwa rahisi kupata, masaa ya kufanya kazi uliweza kuyapanga kwa namna nyingi, malipo yalikuwa ya kuridhisha, na uliweza kuendelea na masomo chuoni huku ukifanya kazi. 

Boss wangu alikuwa mtu mwenye kuelewa wafanyakazi wake na hali zao kwa ukaribu, Mmarekani mwenye asili ya Ugiriki kwa jina la Nick. Alianza kunipanga kazi kwa wagonjwa ambao hawakuwa katika hali mbaya, ambao wakati mwingi walikuwa sawa na ambao walikuwa katika mwelekeo wa kurudi katika maisha ya kawaida bila kusimamiwa na watu wengine. Kazi yangu ikawa kuwapeleka kwa madaktari miadi yao ya kupelekwa inavyofika kuendana na ratiba, kuhakikisha wanameza dawa kwa wakati, kuwapeleka katika mafunzo ya kazi ili kujiandaa kurudi katika maisha ya kawaida na wakati mwingine kuwapeleka kwenye kazi zao halisi - baadhi walikuwa waosha vyombo katika migahawa maarufu ya MacDonald's, walinzi kwenye maduka makubwa ya bidhaa, n.k; ikimaanisha kwamba kazi yangu wakati mwingine ilikuwa kuwatazama wao wakifanya kazi zao. Mara nyingi hakukuwa na tukio la ajabu isipokuwa mara chache ambapo unakuta mmoja wao anakasirika ghafla na kufanya fujo kiasi ambapo ilinibidi kuingilia kati na labda kutatua au kumrudisha katika nyumba ambapo tulikuwa tukiwahudumia.

Kazi hii ilihitaji kupewa mafunzo ya namna ya kuhudumia watu na uelewa wa hali ya juu wa historia ya mgonjwa ikiwa ni pamoja na kujua maneno gani ukitumia kwa mgonjwa fulani yangeweza kumtuliza kama hali yake kiakili ingebadilika ghafla. Kazi pia ilihitaji uwe na leseni ya udereva, na mimi nilikuwa ndio nimepata leseni lakini nilikuwa sijawahi kuendesha gari mjini mbali na wakati niko mafunzoni, kwa hiyo sikujua njia kwenda huku na kule. Siku moja boss wangu Nick akaacha ujumbe wa maandishi kwamba niwapeleke wagonjwa kwa daktari sehemu moja inayoitwa Lynn, hapo Boston. Kwenye karatasi aliandika pia anuani ya sehemu anakopatikana daktari, akaniachia na funguo za gari. Mmoja ya wagonjwa ambaye alikuwa katika kundi la ninaopaswa kuwapeleka kwa daktari akasema anapajua Lynn, alipo daktari ni wapi na angenielekeza njiani hadi tufike. Baada ya dakika kama kumi za kuendesha gari tukielekea Lynn, akawa amesahau! Tukapotea na kuzunguka mjini, hatukula siku nzima, tukakosa kumuona daktari, wakakosa kumeza dawa kwa wakati. Wakapoteza subira na walikuwa karibu kuanza kugombana na mimi. 

Nick alipigiwa simu na daktari masaa mawili baada ya muda wa miadi kupita kwamba mimi na kundi la wagonjwa tulikuwa hatujafika kwake. Akapata mshangao, asijue la kufanya. Sikuwa na simu, gari lilikuwa na simu (outbound-only) lakini sikuwa nafahamu namna ya kuitumia. Nilichofanya ikabidi niendeshe hadi kwa Polisi wanaosimamia Barabara Kuu (Highway Police) ambao walituongoza hadi nyumbani. Nilijua siku ile ningefukuzwa kazi bali Nick alinielewa, hakunifukuza lakini ikabidi kulipia kosa lile kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi. 

Baada ya hapo Nick akanihamishia kwenye nyumba nyingine ambayo ilikuwa na mgonjwa mmoja tu - Mark. Mark alikuwa na umri wa miaka 37 lakini alikuwa na mwili kama wa mtoto wa miaka 10. Mark alikuwa na akili nyingi (super-genius) mwenye uwezo mkubwa wa kuweka kumbukumbu, uwezo katika hisabati na utaalamu wa kompyuta. Sijawahi kukutana na mtu aliyejaliwa vipaji katika hayo kama Mark. Lakini Mark alikuwa na magonjwa mengi ya mishipa ya fahamu, magonjwa ya kupenda jambo kupita kiasi (Obsessive Compulsive Disorder), ulevi wa madawa ya kulevya, pombe na mengine mengi. Alikuwa ametumia madawa mengi, mengi sana katika kutibiwa ambayo yalikuwa na athari hasi pia katika mwili wake. Mark alikuwa na ratiba ya kipekee kabisa - na kabla ya kupangiwa kazi ya kumhudumia ulipatiwa mafunzo kwa wiki mbili. Mark alikuwa mpole lakini angeweza kudhuru pia. Alikuwa pia mwongo mwerevu na angeweza kupima kiwango cha uvumilivu cha mtu yeyote hadi uvumilivu wa mtu huyo ufikie kikomo kwa kukuchezea akili. 

Hakuna aliyetaka kupangwa amhudumie Mark, angekuchosha kimwili na kiakili - macho yako yalitakiwa yawe naye wakati wote hata akiwa chooni kwa sababu kuna nyakati alikuwa akijiumiza mwenyewe makusudi. Akipangiwa mfanyakazi mpya, Mark alikuwa anazunguka nyumba nzima kwa haraka haraka na kukuagiza hiki na kile kwa masaa matatu bila kupumzika ili tu akuchoshe halafu anakuuliza, "Hujioni mjinga kunifuata muda wote?" Tabia yake mbaya zaidi ilikuwa kukimbia toka nyumbani na kwenda kwenye duka lolote karibu la vinywaji kisha anachukua chupa ya bia au wiski (bila kulipa) na kuinywa yote kwa mkupuo kisha anazimia. Kwa hiyo kumhudumia Mark ilibidi milango yote ufunge na funguo uzitunze, lakini Mark alikuwa na tabia ya kuwachomolea funguo wale waliokuwa wanamhudumia. 

Mark alifanya kitendo hiki cha kukimbia, kuchukua pombe madukani na kunywa mara tatu wakati mimi nikiwa namhudumia. Wakati mmoja kwa sababu alikuwa na umbo dogo sana alijificha kwenye mashine ya kufulia nguo. Nilimtafuta nyumba nzima lakini sikufanikiwa kumpata, nilipofungua mlango kuangalia nje akapata upenyo akatoka nje na kujificha nyuma ya nyumba kwenye maua marefu, sikumuona na niliporudi ndani akaondoka. Baadaye nilimkuta katika duka la jirani na alikuwa ameshakunywa nusu lita ya dawa ya kuosha mdomo - Listerine. Kumbe Listerine ina kilevi ndani yake. 

Mark alikuwa na haki zake ambazo tulipaswa kuziheshimu. Alikuwa na haki ya kwenda nje ya nyumba lakini chini ya uangalizi wangu, kununua vitu lakini sana sana kuvua samaki. Alikuwa ana mapenzi ya kupitiliza na uvuvi wa samaki. Alikuwa na haki ya kutumia kompyuta kwa lisaa limoja kwa siku - na mimi nikiwa nyuma yake nilipaswa kutazama kila anachofanya. Ikiwa ni moja ya matatizo yake kiakili Mark alitaka kuwa mbele ya kompyuta yake saa kumi na mbili kamili jioni, sio kasoro, wala na dakika 5, 6, hapana. Kumi na mbili juu ya alama. Kikubwa alichokipenda katika kompyuta ni kupiga soga - chatting, wakati huo AOL chat ilikuwa maarufu. Nilipaswa kutazama hizi chats zake na kujua anafanya nini, ilikuwa ni sehemu ya kazi yangu, lakini kiukweli sikuweza kwa sababu Mark angeweza kuwa na chats katika kurasa mbalimbali kama 12, zote kazifungua na anapitia moja baada ya nyingine kwa kasi kama ya upepo, zote 12 kwa wakati mmoja.

Siku moja, Mark, kirafiki akaniambia anajua siri yangu: kwamba natumia leseni feki ya udereva. Haikuwa kweli. Akasema anataka kunionyesha tofauti kati leseni feki na leseni orijino. Kwa hiyo nikatoa pochi yangu mfukoni pamoja na leseni na kadi zangu za benki. Haikupita dakika moja baada ya kuziangalia kadi zangu akawa ameshakariri taarifa zangu za kadi ya benki - tarakimu zote 16, tarehe ya mwisho kutumika, n.k.

Siku iliyofuata saa tatu asubuhi kengele ya mlango ikagongwa, haikuwa kawaida. Nikaenda mlangoni na kukutana na kina dada wawili ambao walionekana wanafanya biashara ya kujiuza wakiwa mlangoni na kuniuliza kama pale ni anuani sahihi ya Mr. Makamba. Mark alikuwa ametumia kadi yangu ya benki kuagiza kina dada wanaojiuza kupitia mtandao wa intaneti. Nilipowaonyesha mshangao na kuwaambia kwamba sijui lolote, Mark akaniomba tuongee pembeni kidogo. Alikubali kwamba alifanya kitendo kile na kuniambia, "Usiwe na wasiwasi, wewe ni mwanaume, chukua mmoja ambaye unamtaka nami nitachukua mwingine". Sikujua nicheke au nimchape kibao. Nikawaambia wale kina dada waondoke, nao wakaondoka. Baadaye Nick alinirudishia fedha ambazo Mark alitumia kuagiza huduma hiyo toka katika akaunti yangu.

Mark hakuwahi kukaa na mfanyakazi mmoja zaidi ya wiki tatu, kwa sababu aliwachosha na watu kuamua kuacha kazi na pia kwa sababu kila wakati alitaka mfanyakazi mpya. Alikuwa anakusoma haraka na kama ulikuwa mpenzi wa mpira kwenye TV, yeye angeomba umpeleke kuvua samaki wakati mpira unaanza. Kwa kuwa ingekukera angesema kitu gani umpe ili akuache utazame mpira. Wakati wa baridi japo bwawa liikuwa limeganda barafu bado alitaka umpeleke kuvua samaki, niliambiwa kwamba kama angeona hupendi kabisa baridi angeomba umpeleke kuvua hadi mara tatu kwa siku - na ili akuache labda umkubalie kufanya kitu ambacho hatakiwi kufanya. 

Nilikaa naye miezi miwili, Mark sasa hakuwa tena "mgonjwa" tu ninayemhudumia bali rafiki. Tulielewana vizuri. Wakati nahamishwa kutoka kuwa mhudumu wake, ilikuwa majonzi kiasi fulani, niliona upande wa pili wa Mark, Mark aliye na hisia na nafsi ya kuumia kwa hisia kama binadamu wengine, kwa mara ya kwanza. Alinikumbatia akaniambia: "Nitakukumbuka siku zote kwa kitu kimoja, hukuwahi kunipiga wala kuniumiza". Mpaka wakati ananiambia maneno haya sikuwa najua kama alitarajia katika muda niliomhudumia siku moja ningempiga. 

Nimeandika jina lake katika mtando wa Google leo kuangalia taarifa zake (Kwa sababu za faragha sitataja jina lake la pili) lakini sikupata taarifa yoyote kumhusu. Nimekutana na watu wengi maishani lakini Mark alikuwa mtu wa kipekee.

Lengo la kuandika hili ni kwamba maisha yana mafunzo mengi - baadhi ya mafunzo haya huja kutoka sehemu au watu tusiowatarajia. Nimejifunza uvumilivu katika kumhudumia Mark. Nimejifunza pia kushukuru Mungu kwa kuwa na afya njema jambo ambalo mara nyingi tunasahau. Nimejifunza kutohukumu na kuwa na chuki dhidi ya wengine. Lakini pia nimefunza magonjwa ya akili yapo na wagonjwa wa akili nao wana hisia na ubinadamu kama sote tulivyo licha ya magonjwa yao. Nimejifunza pia jamii isiyo na mfumo na utamaduni kuhudumia watu wake wenye mapungufu bado haijastaarabika. Hatuongelei sana kuhusu magonjwa ya akili Tanzania. Tunawatelekeza haraka wagonjwa wetu wa akili na kusema ni kwa sababu tu ya: uchawi, dawa za kulevya au laana. Ni muda wa kubadilika.


Tufikiri Kijumuishi ~~ Tutende Kijumuishi ~~ Tujenge Taifa Jumuishi

Sunday, April 19, 2015

Mhe. Edward Lowassa atetea albino



Waziri Mkuu mstaafu, EDWARD LOWASSA amewataka watu wenye Albinism kuongeza msukumo ili majina ya watu sita waliohukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuua na kukata viungo vya albino yapelekwe kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi.

LOWASSA pia amempongeza Rais KIKWETE kwa hatua alizochukuwa katika kupambana na vitendo vya mauaji ya Albino.

Ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam baada ya matembezi yaliyoandaliwa na vijana wa Temeke yaliyokuwa na lengo la kupinga mauaji ya watu wenye Albinism .

Tufikiri Kijumuishi ~~ Tutende Kijumuishi ~~ Tujenge Taifa Jumuishi



Chanzo: ITV Tanzania



Monday, April 6, 2015

Kanisa Katoliki na wanafunzi albino Shule ya Kabanga

KANISA KATORIKI KASULU WALIPOTEMBELEA KITUO CHA WALEMAVU KABANGA



Paroko,mwenyekiti wa kigango cha Murubona na Kumsenga pamoja na waumini
 wengine wa Kanisa Katoriki Kasulu mjini,ahsantemi sana kwa kutembelea shule/kituo 
chetu cha Kabanga na kutoa msaada wenu wa hali na mali na kubwa zaidi mchango wa 
Tsh.1,700,000/=(Cash.Tsh.1,590,000/= pamoja na ahadi ambazo hutimiza jumla ya 
kiasi tajwa hapo juu) kwa ajili ya mwanafunzi wetu Gilbert. Mbarikiwe sana ndugu zetu.
"MOYO USIO NA SHUKRANI HUKAUSHA MEMA YOTE"
Umati wa waumini wa Kanisa Katoriki Jimbo la Kasulu mjini walioambatana
 na Paroko lakini pia viongozi mbalimbali wa kanisa hilo kuja kuwajulia hali
na kuwafariji walemavu wa ngozi(ALBINO) na kuwaletea zawadi kemkem
siku moja kabla ya Pasaka (kwa kweli wamevunja rekodi haijawahi kutokea)
kutembelewa na umati mkubwa kama huu. TUMEFARIJIKA SANA

Baadhi ya wanafunzi na wakazi wengine waishio katika kituo
 cha walemavu Kabanga wakifurahia zawadi walizoletewa
na waumini wa Kanisa Katoriki-Kasulu.(4.4.2015)


Tufikiri Kijumuishi ~~ Tutende Kijumuishi~~ Tujenge Taifa Jumuishi


Saturday, March 28, 2015

Disability is sometimes an opportunity

 



Most people  in most cases  consider disability as the grand total of human disasters!
 I have played a bad game to many people.  Do you know it? Can you guess?  It was just the sweet game to consider the  advantages and disadvantages of being disabled person!  It was the stage of struggling to see ability  against disability.

 Look! Within the World of chaos someone can  create meaningful contexts.  There are some vacancies that their solely qualification  is the lame organ of human body.  For instance, to represent people with disabilities  in the parliament of the United Republic of Tanzania, the  major criteria is for an individual to  have disability.

 To be an MP is a decent job, it is admired by  the majority.

 Calculate advantages over disadvantages for someone  having a lame organ.

 Think inclusively, Act inclusively, create an  inclusive nation!

Je, Tanzania imeshindwa kuwalinda albino?


Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa hapo limeamua kumteua mtaalamu wa kuchunguza maovu wanayotendewa watu wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakizidi kushambuliwa Afrika Mashariki. 

Baraza hilo la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 47 lilipitisha azimio kwa kauli moja la kuundwa wadhifa wa mtaalamu wa kuchunguza maovu dhidi ya Albino ambaye atahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

Baraza hilo limeeelezea wasiwasi mkubwa kutokana na mashambulizi na mauaji ya kikatili dhidi ya Albino wakiwemo wanawake, watoto, walemavu na wazee.

Azimio hilo liliwasilishwa na Algeria kwa niaba ya kundi la mataifa ya bara la Afrika baada ya Mkuu wa Kamisheni ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein mapema mwezi huu kulaani vikali mashambulizi dhidi ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi ambayo alisema yameongezeka katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki.

Watu 15 wauawa ndani ya nusu mwaka

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kiasi cha watu 15 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa nchini Tanzania, Malawi na Burundi na albino wengine wametekwa nyara, kujeruhiwa kwa kakatwa viungo vya mwili na wengine wamelazimika kuyatoroka makaazi yao kuepuka ukatili huo.

Mashambulizi dhidi ya Albino huwa mara nyingi yanachochewa na imani za kishirikina kutokana na dhana potofu kuwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi husaidia waganga na wachawi kufanya matambiko yanayoleta utajiri na ufanisi.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Albino hasa nchini Tanzania katika kipindi cha hivi karibuni huenda kukahususishwa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo baadhi ya wanasiasa wanatafuta nguvu za kishirikina kujipatia ushindi katika uchaguzi huo.

Tanzania yapiga marufuku uganga

Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku shughuli za kiganga nchini humo mwezi Januari kama sehemu ya hatua inazozichukua kukomesha ukatili dhidi ya Albino.

Kati ya watu 1,400 nchini humo ni Albino ikilinganishwa na takwimu zilizoko katika nchi za magharibi ambapo kati ya watu 20,000 mmoja ndiye Albino. Azimio hilo lililopitishwa hapo jana pia limeelezea wasiwasi wake kuwa katika baadhi ya sehemu duniani watu wenye ulemavu wa ngozi wanakabiliwa na unyanyapaa katika jamii na wanazuiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo na kukabiliwa na vitendo vya ukiukaji wa haki zao za binadamu.

Umoja wa Mataifa umesema juhudi zaidi zinahitajika ili kuweza kushughulikia changamoto wanazokabiliana nazo Albino na mtaalamu huyo atakayeteuliwa na Rais wa baraza hilo la umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu atakuwa na jukumu la kuripoti visa vya ukatili dhidi ya albino, kusaidia katika kufutilia mbali dhana potofu, unyanyapaa na mila zilizopitwa na wakati kuwahusu Albino.

Chanzo: DW