Thursday, February 18, 2016

NAFASI YA WATU WENYE ULEMAVU KWENYE JAMII

Ninapenda sana kuzungumza habari za ulemavu na watu wenye ulemavu. Hii si kwa sababu zinapendeza na kufurahisha mioyo ya wengi, bali ni habari ambazo zinahitajika sana kwa wakati uliopo kwa ukombozi wa fikra, nafsi na mitazamo ya watu kwenye jamii zetu. Huwezi kupata vionjo kamili vya moyo na hisia juu ya athari za ulemavu hadi uguswe na ulemavu; kwa maana ya kwamba wewe mwenyewe uwe na ulemavu na/au uwe na mwanafamilia mwenye ulemavu.

Nimesoma vitabu vingi, majarida mengi na magazeti pia. Nimeona jinsi jamii zetu zinavyojitahidi kuchambua habari ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Jambo moja kuu katika maandiko yote hayo waandishi huishia kuwajengea watu hisia za huruma bila kutaja wazi wazi na kwa ujasiri uthabiti wa watu wenye ulemavu kwenye jamii zao. 

Ulemavu unaweza kumpata mtu yeyote kwenye maisha wakati wowote na mahali popote.

Biblia imemtaja mjukuu wa mfalme Sauli, yaani mtoto wa Yonathani kuwa alikuwa mlemavu.

2Samweli 4:4
"Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu.....Na jina lake aliitwa Mefiboshethi."

Makazi ya watu wenye ulemavu

1. Makazi katika ardhi
Mazingira mengi ya watu wenye ulemavu wanaishi kwenye mazingira mabaya na magumu, mazingira yasiyosadifu maisha ya maendeleo.
Mfano, mjukuu wa mfalme Sauli aliwekwa katika eneo lililoitwa Lo-Debari.
Lo-Debari- ni eneo lisilo na malisho, eneo lenye ugumu wa kuishi. Kwa mantiki hii watu wengi wenye ulemavu wanaishi Lo-Debari zao katika nchi zao.

2. Fahamu zetu zinawaweka mahali gani watu wenye ulemavu?
Hata wewe ni shahidi, watu wenye ulemavu wamefikiriwa kuwa ni watu wasio na faida kwenye jamii zetu. Adolf Hitler wa Ujerumani kwa kupitia dhana hii aliwaita watu wenye ulemavu kuwa ni USELESS EATERS (walaji wa rasilimali za jamii wasio na faida (see Eugenic Movement: The War Against the Weak).

3. Mamlaka za watu wenye ulemavu ziko wapi?
Kwa utamaduni wa binadamu Tanzania na dunia nzima kwa ujumla zinaonyesha kuwa watu wenye ulemavu wanatawaliwa na kila mtu. Hii ndiyo dhana ya watu wengi. Utamkuta mtu mwenye ulemavu msomi, ana pesa, ana ufahamu wa mambo mengi ambayo yangekuwa msaada kwa wengi. Kinyume chake utakuta kila mtu asiye mlemavu anahisi yeye ndiye mtawala wa mtu mwenye ulemavu. Ushahidi ni pale utakapoona mtu mwenye ulemavu akisemwa na kusimangwa na kila mtu, na hata pengine huwa na kuzushiwa na kusingiziwa tu.
4. Tujifunze kwa mfalme Daudi

"1  Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani?
2  Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye.
3  Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu.
4  Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.
5  Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.
6  Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako!
7  Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima.
8  Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?" 

MANENO MAGUMU HAYA
2Samweli 9:8 
 "Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?" 

Siku zote ukitaka kujua mtu alikuwa na mazingira magumu kabla ya kusaidiwa fuatilia "SHUKRANI ZAKE". Huwa ni za kipekee sana. Soma 2Sameli 9:8 ujionee.

NIONAVYO
Watu wenye ulemavu wamepitia, naam, wanaendelea kupitia kwenye mazingira magumu. Shida za watu wenye ulemavu zinafanana kote duniani zikiwa kwenye vipengele vya Miundo mbinu, Mtazamo wa jamii na mawasiliano. Tujitahidi kujenga jamii jumuishi ili tuishi kwenye taifa ambalo halimtengi mtu kwa namna yoyote ile. Nikumbushe pia kuwa leo mtu ambaye ndiye kikwazo kwa mtu mwenye ulemavu ndiye pia anaweza akawa kwenye orodha ya watakaopata ulemavu muda mfupi ujao. Jumuisha ili ujumuishwe.

FIKIRI KIJUMUISHI~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI

Saturday, February 6, 2016

WALIMU WA ELIMU MAALUM NA WANAFUNZI WA ELIMU MAALUM WAKUTANE SHULENI





Mwanafunzi mwenye mahitaji maalum anamhitaji mwalimu mwenye taaluma ya elimu maalum; pia mwalimu wa elimu maalum anamhitaji mwanafunzi mwenye mahitaji maalum. Ni mtegemeano wa aina yake.


Tanzania, kama nchi zingine duniani, ina wanafunzi wenye mahitaji maalum. Pia ni bahati iliyoje kuwa na vyuo vyenye kutoa elimu maalum kwa walimu ili kukidhi mahitaji maalum ya wanafunzi hao wenye mahitaji maalum.

Hata hivyo kuna kila dalili ya kushuka kwa huduma za elimu maalum nchini Tanzania. Walimu wengi wanaomaliza kozi za vyuo vya elimu maalum wamekuwa wakipangiwa shule za kawaida (normal schools) zenye watoto wasio na mahitaji maalum.

Kwa upande mwingine wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini wameendelea kuwepo mitaani bila kwenda shule kwa kigezo kuwa hakuna walimu wa kuwafundisha hawa watoto.

Elimu jumuishi bila mipango inaumiza wachache.


HOJA

Walimu wenye fani ya elimu maalum wapelekwe kwenye shule maalum za watoto wenye mahitaji maalum; sambamba ni hilo, pia kuanzishwe shule maalum kwa watoto hao kwenye maeneo yasiyo na shule hizo. Zipo wilaya nyingi zisizo na shule maalum, mfano halisi ni wilaya ya Mvomero, haina shule za viziwi na wasioona.


Sunday, January 24, 2016

Ukishindwa Kuwajengea furaha, basi angalau usiwe sehemu ya Maumivu yao

Katika maisha kwenye jamii zetu jukumu letu kuu ni kusaidiana. Tunapaswa kuwa wajenzi wa furaha kwa watu wenye ulemavu, na kwa watu wote ambao wanaonekana kwa namna moja ama nyingine wamekandamizwa na mifumo ya jamii zetu. Hii ni kwasababu tayari asili (nature) imeshaharibu furaha yao ya asili.

Kama tumeshindwa kuijenga furaha yao, tumeshindwa kuwasaidia kwa hili au kwa lile; basi angalau tujitahidi tusiwaumize, na wala tusiwe sehemu ya watu wajengao maumivu kwenye maisha yao.

 

Tuishi kijumuishi... Tutende kijumuishi.... Tujenge taifa jumuishi

Tuweke Mkazo wa Kuwajengea Uwezo Kijamii Watu Wenye Ulemavu

Nimeona utofauti mkubwa wa mtu aliyepata ulemavu wa kuzaliwa na ule wa ukubwani kwenye maisha. Dhana ya ulemavu inaogopwa kuliko hata ulemavu wenyewe. Watu hawataki kusikia habari za ulemavu kwenye masikio yao. Nimeshuhudia watu wenye ulemavu wakihojiwa na media, wengi wetu ambao tumezaliwa na ulemavu tunaonyesha kuwa tumeendelea kuishi kwa sababu tu ya ubishi wetu juu ya kukataliwa kwetu, tunapuuza kukataliwa kwetu. Wenye machungu na magumu zaidi ni hawa wenzetu wanaoendelea kupata ulemavu ukubwani. Hawa wanajua jinsi walivyouogopa ulemavu, wakajitenga mbali na watu wenye ulemavu, wakaenda mbali zaidi kwa kudhani watu wenye ulemavu ni jamii ya pembezoni ukilinganisha na jamii ya watu wasio na ulemavu. Hii ni sababu tosha kuwa kundi hili la pili lipatapo ulemavu huyaona maisha magumu kana kwamba wameibeba dunia nzima kwa uzito.

Hakika, makundi yote haya yenye ulemavu (congenital and Acquired Disabilities) kwa pamoja yanahitaji huduma fulani ya Kisaikolojia ili kuwapumzisha mizigo ya fikra zao za muda mrefu. Ingekuwa vema tukawa na vituo vya kisaikolojia kwenye media zetu; mathalan magazeti, TV na redio ziweke programu kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya ulemavu. Hii itasaidia kuweka ufahamu wa jumla juu ya ulemavu, kuwaweka sawa kisaikolojia wanaoathiriwa na ulemavu na, pia kuweka akiba ya maarifa na kisaikolojia kwa wote ambao wanaweza kupata ulemavu ukubwani.

Fikiri Kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi

Tuesday, January 19, 2016

Thursday, November 5, 2015

Tuna majukumu gani juu ya jamii ya watu wenye ulemavu?

Katika maisha kwenye jamii zetu jukumu letu kuu ni kusaidiana. Tunapaswa kuwa wajenzi wa furaha kwa watu wenye ulemavu, na kwa watu wote ambao wanaonekana kwa namna moja ama nyingine wamekandamizwa na mifumo ya jamii zetu. Hii ni kwasababu tayari asili (nature) imeshaharibu furaha yao ya asili.

Kama tumeshindwa kuijenga furaha yao, tumeshindwa kuwasaidia kwa hili au kwa lile; basi angalau tujitahidi tusiwaumize, na wala tusiwe sehemu ya watu wajengao maumivu kwenye maisha yao.

 

Tuishi kijumuishi... Tutende kijumuishi.... Tujenge taifa jumuishi

Saturday, October 17, 2015

Ulemavu kama alama ya Baraka na Maagano na Mungu

https://lh4.ggpht.com/Qu-lslyhv1zyNL6ZwuzuPwEKo2_j2MQRkXHwGhhKC6UaeM3D5Ujop3DdkoKdUzlzJvM=w300 

Akili zetu binadamu zina ukomo wa uelewa wa maarifa, na siku zote tukishindwa kutafsiri dhana huwa tunakimbilia kuihusisha na nguvu ya Kimungu (Divine Power).

Ulemavu ni miongoni mwa dhana ngumu sana kueleweka kwa watu wa jinsi zote, rika zote, taaluma zote na hata mataifa yote duniani. Imedhaniwa kuwa ni laana kwa. mtu kuwa na ulemavu.

Tunayo mifano mingi ya watu wenye ulemavu ambao wamekuwa baraka kwa watu na kwa Mungu kwa jinsi walivyoweza kutoa michango ya maendeleo kwa jamii zao.

Angalia hawa binadamu wenye ulemavu kwa uwezo wao

Nabii Musa
Ulemavu: Ugumu wa kuongea (Speech Impairment)-Kutoka 4:10-11

Biblia inamtaja Musa kuwa alipendwa na Mungu kupita manabii wote waliowahi kuishi duniani
1. Ndiye aliyepewa jukumu la kuwakomboa wana wa Israel kutoka Misri (Kutoka 3:1-10).
2. Ndiye aliyepokea amri kumi kutoka kwa Mungu pale mlima wa Sinai zilizoandikwa kwenye kibao ambazo kwa sasa ziko ndani ya Biblia Takatifu na hutumiwa na madhehebu ya Kikristo hadi leo hii (Kutoka 20:1-26).
3. Kwa upendo Mungu alijionyesha sura yake kwa Musa. Ilikuwa ni kawaida kuwa kila aliyeona uso wa Mungu hakuishi, bali Musa aliishi (Kutoka 33:18-23).

Yakobo wa Biblia
Alipata ulemavu kwa kutenguliwa na Mungu sehemu ya uvungu wa paja lake (Mwanzo 32:24-30)

Frankline Delano Roosevelt

 Kenneth Branagh as Franklin Delano Roosevelt in the Movie "Warm Springs"
Ulemavu: Viungo (miguu)

Alikuwa rais wa Marekani kuanzia 1933-1945. Ndiye aliyekuja na slogan ya 'the New Deal' yenye sera bora kwa Waamerika. Ndiye aliyeiwekea sera nzuri za Amerika kama malipo ya uzeeni na malipo ya ulemavu, ndiye aliyetoa ajira kwa Waamerika wote waliokuwa na uwezo wa kufanya kazi.

Lisha akili yako leo
Ulemavu hauondoi asili ya binadamu, haumtengi na upendo wa Mungu, haumwondolei haki zake; kikubwa zaidi ni kwamba binadamu ndiye mhusika mkuu wa ulemavu na anaweza kuupata kabla ya kuzaliwa au baada ya kuzaliwa. Tujitahidi sana kuwa na mtazamo chanya juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu, ndipo tutakapofanikiwa sana katika taifa letu.

Fikiri Kijumuishi, Tenda Kijumuishi, Jenga Taifa Jumuishi