Tuesday, October 1, 2013

Sitasahau Kauli ya GWANTWA MWALYAJE, Albino Mwimbaji Wa Nyimbo za Injili




Ni katika kipindi maarufu cha ITV cha 'HAWAVUMI LAKINI WAPO'. 
Pamoja na nyimbo zilizochambuliwa kwa kina na mchambuzi aliyebobea RAJABU ZOMBOKO, pia mahojiano na mwanamuziki anayechipukia katika nyimbo za injili GWANTWA MWALYAJE (mwenye ulemavu wa ngozi-albino) alielezea changamoto za kukataliwa na kudharauliwa na jamii pindi anapoomba kuimba kwenye matamasha mbalimbali.

Kauli yake yenye uzito wa aina yake ilikuja baada ya kuanza kuelezea namna alivyoweza kufika studio za ITV. Alimshukuru Dr. Reginald Mengi ambaye ni mmiliki wa makampuni ya IPP kwa kuwajali watu wenye ulemavu. Mwimbaji huyu anaimba nyimbo ambazo nyingi ni kwa ajili ya kutokomeza mauaji ya albino Tanzania na duniani kote. Kauli yake ni hii, nanukuu: "Siku nimefika hapa katika studio za ITV na kuanza kuhojiana na mtangazaji NILISAHAU ULEMAVU wangu". 

Neno KUSAHAU ULEMAVU maana yake ni nini? Kulitokea kitu gani katika akili na ufahamu wake mpaka ajisahau ulemavu wake? Je, baada ya kipindi kuisha ameendelea kusahau ulemavu wake? Maswali haya na mengine mengi yalipita ghafla kwenye ufahamu wangu na kisha kuanza kuelimisha nafsi yangu. Pamoja na majibu mazuri uliyonayo juu ya maswali haya, nyongeza yake ni hii hapa.

Kwanza tujue kabisa na bayana kuwa ulemavu una athari kubwa kwa maisha ya binadamu kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kama hatua za dhati na za mapema hazitachukuliwa ili kupunguza hizi athari dhidi ya huyu mtu mwenye ulemavu.

Maana ya 'KUSAHAU ULEMAVU'
Hii ni hali ambayo mtu mwenye ulemavu anapokuwa kwenye mazingira yanayoashiria kumwacha huru kutokana na ulemavu wake. Mazingira haya yanaweza kuwa ni binadamu wanao mzunguka, miundombinu iliyoboreshwa, hali yenye kutia matumaini ya maisha ya kufanikiwa, kukutana na huduma ambayo hapo awali hakuwa na uwezo wa kuipata, nk.

Bwana GWANTWA MWALYAJE yeye lengo lake ni kufanikiwa kiuchumi pamoja na kutetea hatima ya ualbino wake na wa wenzake juu ya mauaji na masumbufu wayapatayo kila siku kwenye maisha yao. Anadai kuwa huwa anakataliwa kuimba kwenye matamasha mbalimbali ambako angeweza kuuza kanda zake za muziki.

Sababu za KUSAHAU ULEMAVU wake:
Mosi, mapokezi aliyopata ITV. Hapa utagundua kuwa, kwenye jamii zetu si mara nyingi watu wanaweza kuwachangamkia watu ambao ni albino na walemavu wengine wote. Kwa hiyo kwa kupokelewa vizuri na kuchangamkiwa kulimfanya asahau utofauti wake ambao huwa anauona kila siku kwenye jamii.

Pili, kutangaza biashara yake. Kama anavyosema kuwa mara nyingi huwa hapati mahali pa kutangazia uimbaji na kipaji chake cha kuimba. Hivyo kwa kufika kwenye studio za ITV kulionyesha nyota mpya ya maisha ya kufanikiwa kiuchumi kwa kutangaza biashara yake ya uimbaji.

Tatu, kutoa hisia zake juu ya mateso wanayopata albino. Pamoja na kutangaza uimbaji wake, pia alipata nafasi ya kutoa hisia zake kwa watazamaji wa ITV walioenea kote ulimwenguni kuwa wao (albino) hawapendezwi na wala hawaoni haki ikifanyika kwa kutendewa hayo matukio kwenye jamii wanamoishi. Katika wimbo wake mmoja aliouita kwa jina la "dili", ameonyesha wazi kuwa albino wamekuwa kitega uchumi cha binadamu wenzao kwa kukatwa viungo. Anasema huko nchini Malawi majangili hao hutamba kabisa kuwa soko zuri la viungo vya albino ni Tanzania.

Tuingie kwenye sehemu ya mwisho ya swali kama ni kweli ameendelea kusahau ulemavu wake. Jibu la haraka ni hapana na litabaki kuwa hivyo. Mazingira yanatofautiana, binadamu vilevile tuko tofauti. Utakavyoweza ku 'socialize' na mtu huyu si sawa kabisa na mtu yule, ufahamu na mitazamo ya mtu X si sawa na ya mtu Y. Pia ijulikane kuwa kujikomboa mtu mmoja kati ya kundi kubwa huo uhuru ni batili, kwa hivyo ndugu GWANTWA MWALYAJE pamoja na watu wengine wenye ulemavu Tanzania na kwingineko duniani, watambue kuwa kukaa ikulu kwa ulinzi na maisha yenye uhakika kwa mtu mmoja mwenye ulemavu haimaanishi umemaliza kazi. Tena kwa mazingira hayo mazuri ndipo mahali pa kufanya 'advocacy' ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Mwisho, napenda kuwajulisha binadamu wenzangu kuwa "people experience differently in life styles". Vionjo vya maisha vya binadamu mmoja hutofautiana na vya mwenzake. Wakati huyu anaona maisha mazuri na ya kifahari, mwingine anataabika hata kiasi cha kulaani siku aliyozaliwa. Hivyo basi, maneno wayaongeayo watu wenye ulemavu katika maisha yao ndio ukweli wote upo hapo. Anapopatikana mwakilishi wa kundi fulani la wenye ulemavu huyo hubeba 'experiences' za maisha ya waliobakia.


FIKIRI KIJUMUISHI ~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI


No comments: