Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imetoa Rasimu ya Pili ya Katiba ikiwa na mambo sita mpya,
huku ikiendelea kupendekeza Muungano wa Serikali tatu na kurejea kwa nchi ya
Tanganyika.
Rasimu hiyo
ya Pili ambayo imetolewa miezi saba baada ya Rasimu ya Kwanza, ilikabidhiwa
jana kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika hafla
iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Akizungumza kabla ya
kukabidhi rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema ina Ibara 271, tofauti na ile ya
kwanza iliyokuwa na Ibara 240.
Alisema
ripoti ya rasimu hiyo pia ina maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, sera,
sheria na utekelezaji maoni ya Mabaraza ya Katiba, takwimu za ukusanyaji wa
maoni ya wananchi, makala za utafiti kuhusu mabadiliko ya Katiba na
viambatanisho vya ripoti ya mabadiliko ya Katiba.
Mambo mapya
Maeneo
yaliyofanyiwa marekebisho baada ya mchakato wa Mabaraza ya Katiba yaliyokutana
kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu ni kuongezwa kwa vipengele kuhusu
haki za binadamu.
Miongoni
mwao ni haki ya kutoa na kupata habari. Pia imetaja haki za makundi maalumu
yakiwamo ya watoto, vijana, wazee, walemavu na wanawake.
Kuhusu
uraia, Jaji Warioba alisema imependekezwa uraia wa Tanzania kuwa mmoja tu na
kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na wa kujiandikisha wa nchi moja. Alisema
imependekeza pia kutoa fursa kwa uraia wa nchi mbili.
Jambo
jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo
vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji
kuthibitishwa na Bunge.
Aidha,
alisema rasimu hiyo imependekeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwe
taasisi inayojitegemea badala ya kuwa sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
kama ilivyokuwa katika Rasimu ya Kwanza.
“Rasimu
inapendekeza kuwepo na Jeshi moja la polisi na Idara moja ya Usalama kwa taifa
zima, siyo kama tulivyokuwa imependekezwa katika rasimu ya kwanza kwamba kila
upande unaweza kuanzisha jeshi lake la polisi,” alisema.
Muundo wa Muungano
Alisema
katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar, Tume imebaini kuwa muundo wa Muungano
wa Serikali mbili umeifanya Serikali ya Muungano kushughulikia zaidi mambo ya
Tanzania bara, hasa maendeleo na uchumi.
Kwa mujibu
wa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977, Serikali ya Muungano ina mamlaka ya
kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo na muungano kwa upande wa bara... “Kwa
msingi huo, Serikali ya Muungano inashughulikia sana kilimo, elimu, afya, maji,
nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii na mengine ya Tanzania
bara yasiyo ya Muungano.”
Alisema
kutokana na hali hiyo, Tume haikuwa na njia nyingine kwa sababu Serikali ya
Muungano haina madaraka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo na uchumi kwa
upande wa Zanzibar na kwamba hata utafutaji wa rasilimali zaidi ni kwa ajili ya
Tanzania bara kuliko Zanzibar.
Alisema
Zanzibar inafanya mipango yake ya maendeleo, kwamba ili ipate rasilimali, kama
mikopo na misaada, ni lazima ipitie Serikali ya Muungano jambo ambalo
utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi.
“Njia pekee
ambayo ingeiwezesha Zanzibar kufaidi shughuli za Serikali ya Muungano wa
maendeleo ya Zanzibar ni mambo yote kuwa chini ya Muungano kwa maana ya kuwa na
Serikali moja, lakini hilo likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa,” alisema.
Alisema tume
hiyo imefanya uchambuzi wa mambo 22 ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia
hadhi ya uhuru wa Zanzibar na kubaini kuwa siyo yote yanayotekelezeka. Mengi
yamebadilishwa bila kubadili Katiba au kwa makubaliano ya pande mbili.
Aliyataja
mambo hayo kuwa ni kodi, bandari, viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga,
utafiti, posta na simu, uraia, takwimu, mafuta na gesi na Mahakama ya Rufaa.
“Kama Katiba
ya Zanzibar ikibaki kutakuwa na nchi mbili; zikiwa nchi mbili haitawezekana
nchi moja iwe na hadhi na uhuru na nchi nyingine isiwe na hadhi na uhuru, kwa
tathmini yetu, tunaona ukarabati huu ni mgumu. Serikali tatu ndiyo suluhisho,”
alisema.
Source: Gazeti la Mwananchi.