Sunday, October 13, 2013

Dr. Wilbroad Slaa na Taifa Jumuishi; Elimu Ikiwa Ndiyo Kiini Cha Uhai wa Watu na Taifa Lao



Ilikuwa ni tarehe 09/10/2013 wakati wa kipindi cha AFRICA NOW. Pamoja na mambo mengine waliyojadili, Dr. Wilbroad Slaa aliulizwa swali na mtangazaji kuwa ni kipaumbele gani katika nchi ya Tanzania angekizingatia kama angekuwa ndiye rais wa nchi.

Majibu ya Dr. Slaa yalikuwa; kipaumbele cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu, cha tatu ni elimu (sijakosea kuandika, ndivyo alivyorudiarudia). Majibu haya ya mheshimiwa Dr. Slaa , yenye kujirudiarudia kama shairi lenye kuimbika yalinifanya nikae kando kidogo, niache kumfikiria yeye (Dr. Slaa) bali nichunguze sababu iliyompelekea kusema neno “elimu” kwa kurudiarudia.

Katika uchunguzi wangu, niliangalia kipengele kimoja tu kuhusu elimu, nacho ni “Nguvu ya Elimu kwa Maisha Binadamu”.

Plato (429-347 KK),mwanafalsafa wa zamani wa Kigiriki  katika kitabu chake kiitwacho ‘Republic’, alivitaja vitu vitatu vinavyoweza kuleta uhai na kuimarisha taifa lolote. Vitu hivyo ni ‘mfumo mzuri wa elimu’, ‘ulinzi imara’, na ‘uongozi imara’. Nikaendelea kidogo kuangalia mwanafalsafa huyu alisema nini kuhusu elimu. Nikakutana na maneno haya:

The object of education is to turn the eye which the soul already possesses to the light. The whole function of education is not to put knowledge into the soul, but to bring out the best things that are latent in the soul, and to do so by directing it to the right objects. The problem (task) of education, then, is to give it the right surrounding”.

Hebu tuyatafsiri haya maneno ya Plato kwa tafsiri isiyo rasmi kwa lugha rahisi ya Kiswahili:

“Lengo la elimu ni kurudisha macho ambayo tayari nafsi inayamiliki (macho) kuelekea kwenye mwangaza. Kazi nzima ya elimu si kuweka maarifa kwenye nafsi, bali kwa kuibua vitu vilivyo bora na ambavyo ni vigeni kwa nafsi, na hufanya hivyo kwa kuielekeza (nafsi) kwenye vitu sahihi. Jukumu la elimu sasa linakuwa ni kuipa hiyo nafsi mazingira sahihi”.

Pia, Bloom (1956); Krathwohl, na wenzake (1964); na Harow (1972); walipendekeza mtaala ambao unamuelimisha binadamu katika Nyanja zote za kujifunza ambazo ni “Nyanja ya Utambuzi” ambayo hujihusisha na Ufahamu,  “Nyanja ya Vionjo vya moyo na hisia” ambayo hujihusisha maono na kuweza kuchambua jambo na kulifurahia au kulichukia. “Nyanja ya misuli” yenyewe hujihusisha na kuwezesha viungo vya mwili kujifuza kwa vitendo kama vile kucheza mpira, kukimbiza vijiti, nk. Jumla ya Nyanja hizi huunda elimu kamili kwa maisha ya binadamu.

Ukichunguza kwa makini utaona kuwa lengo kuu la elimu kwa taifa lolote lile ni kupitisha utamaduni wa wanajamii kupitia mfumo rasmi wa elimu, na kwa upande mwingine upo utamaduni ambao hupitishwa kwenye mfumo usio rasmi wa elimu; watu wanajifunza kwa kuiga kwa wengine, ndicho kisomo chenye manufaa kama alivyokitambulisha baba wa taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Nyerere.

Kwa hivyo, elimu ndiyo huadabisha au huelekeza jamii ifuate mfumo fulani wa maisha ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hapa ndipo tunakuja kuona kuwa elimu ni muhimu kwa jamii, na kwamba, ni lazima kila mwanajamii aipate ili aweze kwenda sawa na mfumo wa utamaduni tuliouchagua kwenda nao.

Pia tukumbuke kuwa, kama elimu ndiyo hujenga utamaduni, na kwamba, utamaduni ndio jumla ya mambo yote yanayomwezesha mwanadamu kuishi, basi elimu ndiyo maisha yenyewe. Hapa ndipo tunakutana na mstari maarufu wa biblia katika kitabu cha mithali.
Mithali 4:13; imeandikwa hivi:

“Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako”.

Tumekwishaona umuhimu wa elimu kwa jamii, na tumeweza kufikia mahali pa kusema elimu ndiyo maisha yenyewe, elimu ndiyo uhai. Inatuwezesha kuyashinda mazingira yetu ili tuendelee kuwa hai. Hii ina maana kuwa binadamu siku zote ana vita na mazingira yake, na hii vita ni ya maisha yote ya mwanadamu. Vita hii huisha tu pale maisha ya mwanadamu yanapokoma. Hivyo kipindi hiki chote cha mpambano kati ya mwanadamu na mazingira yake, silaha kuu ya mwanadamu huwa ni elimu.

Hebu sasa tuchunguze elimu yetu hapa nchini Tanzania, tuone ni kweli ni uhai kwa kila mtu.
Jamii yetu ya Kitanzania ina watu wenye uwezo (abilities) mbalimbali; wapo watu wasio na ulemavu na wenye ulemavu wa aina mbalimbali. Shule za watu wenye ulemavu ni chache ukilinganisha na idadi yao pamoja na mtawanyiko wao hapa nchini. Ni nadra sana kukuta shule zenye kutosheleza aina zote za ulemavu  kwa mahitaji yao katika wilaya moja. Mathalan, huwezi ukakuta shule ya viziwi, ya wasioona, ya wenye mtindio wa ubongo, na ya wenye ugumu wa kuongea (speech impairment) katika wilaya moja hapa nchini. Wenye mahitaji maalum wapo kila mahali kama watu wengine; na wanahitaji huduma zote kama wanajamii wengine.

Kama tulivyoweza kuthibitisha kuwa elimu ndiyo uhai, hapa tunaweza kuona kuwa; wapo wenzetu kwenye jamii wanaonyimwa huu uhai, tunaweka mbali na kuuficha huu uhai ili wasiufikie. Tunawanyima hii silaha ya kuwawezesha kupambana na mazingira. Kwa tafsiri isiyo rasmi, ni kwamba wapo watu ambao tumeona waendelee kuishi kwa kuupata huu uhai, na wengine ambao tunahisi ni ‘unfit to the society’ kuupata huu uhai wanatakiwa wafe. Hapa pia  tunaweza kufananisha ukosefu wa shule na huduma za kielimu kwa watu wenye mahitaji maalum na mpango wa “Eugenic Movement-the War Against the Weak” ambao ulianzishwa na mwanasayansi wa Uingereza Sir Francis Galton (1822-1911), ambapo vita kuu ilikuwa ni kuondoa kabisa kizazi cha watu wenye ulemavu, wenye IQ ndogo na walio maskini kwenye uso wa dunia.

Hitimisho
Kwa ujumla sasa nimetambua ni kwa nini Dr. Wilbroad Slaa alisema kipaumbele chake cha kwanza, cha pili, cha tatu na kuendelea kingekuwa ni elimu kama angekuwa ndiye rais wan chi hii. Nahisi anafahamu kuwa elimu ndiyo uhai wa binadamu, uhai wa familia, na ni uhai kwa taifa zima. Tunahitaji elimu imfikie kila mtu hapa nchini na kwingineko duniani. Sote tunautafuta na tunauhitaji huu uhai. Elimu, Elimu, Elimu, …, Uhai, Uhai, Uhai, …


“Elimu Kwa Uhai Wa Mtu Mmoja Mmoja Na Kwa Taifa Zima”