Pinda: "Nilisomeshwa kwa kuuza pumba"
Dodoma. Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoboa siri yake kuwa alisomeshwa kwa kuuza mahindi na pumba, na kwamba anajisikia raha kuitwa mtoto wa mkulima kutokana na sababu mbalimbali za kihistoria na uhalisia.
Pinda anayetajwa kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 alisema kuwa jina; ‘Mtoto wa Mkulima’, linampa faraja kutokana na ukweli kwamba wazazi wake walikuwa wakulima wa kawaida wa jembe la mkono, jambo ambalo naye alishiriki na hata sasa anaendelea na kilimo.
Chanzo: Mwananchi.
Maoni huru kwa Mheshimiwa Pinda
Sawli kwako Mheshimiwa Mizengo Pinda: Je, ukiwa rais wa nchi hii utajenga jamii jumuishi ambayo kila raia atakuwa huru kutembea popote na kufanya shughuli yoyote halali? Je, ndugu zetu albino watalindwaje ili kuhakikishiwa uhuru na haki yao ya kuishi? Na hawa wanafunzi wenye ulemavu, hasa wasioona na viziwi ambao wamekosa haki ya shule kutokana na kukosa walimu wenye taaluma ya elimu maalum nao watapatiwa walimu pamoja na vifaa saidizi?
Nakukumbusha Mheshimiwa Mizengo Pinda, kuwa chozi ulilolimwaga pale bungeni kwa machungu ya kuuawa albino liliweka alama ya kudumu moyoni mwangu kuwa wewe ni binadamu mwenye ubinadamu. Nina ombi kwako: Ikitokea umepata kuwa rais wa nchi hii, fanya mambo yaliyoonekana kuwa ni ndoto za mchana kwa watu wenye ulemavu. Hii ni pamoja na sera mfu zilizojaa maofisini kwenye halmashauri zetu nchini. Mtu mwenye ulemavu akienda kwa rejea ya zile nyaraka na sera za wenye ulemavu huambuliwa kuambiwa "wewe ndiye unajifanya unajua sheria sana?"
Kila lakheri Mheshimiwa Pinda kwenye kinyang'anyiro cha urais 2015!