Wednesday, January 8, 2014

MARY PETRO: MLEMAVU WA VIUNGO NA UGUMU WA MAISHA YAKE




Kwa muda mrefu kumekuwepo na taarifa za ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu; tumesikia walemavu wa ngozi (Albino) kwa namna walivyofanyiwa na wanavyoendelea kufanyiwa ukatili kisa eti Imani za kishirikina. Pamoja na yote uliyosikia lakini hebu fuatilia kisa hiki, ambapo mlemavu asiyejiweza kabisa anavamiwa, anabakwa, anapewa Mimba, mwisho wa siku anajifungua, lakini baada miaka kadhaa mwanaye aliyemzaa akiwa mzima naye ghafla anakuwa mlemavu.
Tangu nchi yetu ipate Uhuru waka 1961 Serikali kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii imekuwa inatoa huduma kwa watu wenye ulemavu bila kuwa na sera timilifu.
Mary Petro, akiwa amepumzika
Kuwapo kwa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ni matokeo ya miaka mingi ya majadiliano baina ya Serikali na wadau. Pamoja na kutokuwapo kwa sera, Tanzania imekuwa inajihusisha na mipango mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa inayohusu masuala ya ulemavu.
Kimataifa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu hususan mikataba ya Haki kwa watu wenye Ulemavu (1975), Haki za Mtoto (1989) na Haki na Fursa sawa kwa Watu wenye Ulemavu (1993).
Barani Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi waasisi wa Mpango wa utekelezaji wa muongo wa Watu wenye Ulemavu na mwanachama wa Taasisi ya Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu (African Rehabilitation Institute – ARI).
Hapa nchini serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kampeni za chanjo ya kuzuia ulemavu utotoni (kwa mfano polio), kutunga sheria zinazolinda maslahi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, kuwapo kwa swali kuhusu ulemavu katika sensa ya Taifa ya watu na makazi (2002) na ile ya mwaka jana (2012)  na mandalizi ya kuridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki na Fursa Sawa kwa Watu wenye Ulemavu.
Sera inatoa mwongozo na inaweka vigezo vya utoaji huduma. Sera imejengwa kwa kuzingatia utamaduni wetu na inalenga katika kuleta maendeleo, haki na heshima kwa Watanzania wenye ulemavu.
Changamoto iliyopo ni kutafsiri kwa vitendo matumaini yaliyomo kwenye Sera hiyo na kilichopo tu ni kwamba kundi hili limekuwa likikumbukwa pale tu linapotokea janga au unyanyasaji fulani na baada ya hapo hakuna tena atakayejali na kulitilia maanani,kwani kukosa kwao huduma mbalimbali za jamii, kunawafanya walemavu waathirike kisaikolojia na wengi wao kukata tamaa ya maisha.
Pamoja na jitihada hizo za serikali lakini bado kuna ukweli usiopingika kwamba kuna baadhi ya walemavu ambao serikali haijawafikia mahali walipo, lakini kibaya zaidi hata jamii yenyewe inayowazunguka haijaona umuhimu wa kuwatolea taarifa mahali husika.
Miongoni mwa watu wenye ulemavu ambaye anaonekana wazi kwamba yuko katika hali ngumu huku serikali ikiwa haijui taarifa zake lakini kibaya zaidi jamii nayo ikionekana kumtenga na kutomjali ni Mwanamke Mary Petro (51) mkazi wa kitongoji cha Sima kijiji na kata ya Bupandwa wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Mary Petro: Ulemavu wake ni miguu na mikono
Mlemavu huyo ambaye hana uwezo wa kutembea,huku akiwa ni mtu mwenye kubebwa na watu wawili wakati wowote anapotaka kufanya jambo lolote ikiwa ni pamoja na kwenda kujisaidia haja kubwa ama ndogo,kula chakula mwenyewe kwa kutumia mikono yake miwili hilo ni jambo ambalo halijawahi kumtokea tangu azaliwe miaka 51 iliyopita.