Sunday, August 18, 2013

Mtazamo wa Biblia Juu ya Watu Wenye Ulemavu

Biblia inasemaje juu ya ulemavu na watu wenye   ulemavu?

Biblia ni kitabu cha maandiko matakatifu ya Mungu. Ni muunganiko wa vitabu vidogovidogo vingi vikipelekea jumla yake kuwa 66, agano jipya likiwa na vitabu 27, na agano la kale likiwa na vitabu 39. Biblia ni kitabu cha pekee ambacho kimeathiri mtazamo wa dunia nzima kuhusu masuala ya kalenda, mfano mtu akitaka kurejea tukio la kihistoria lazima aonyeshe kama ni BK (baada ya Kristo) au KK (kabla ya Kristo).
Katika mada hii tutaangalia na kuchunguza maandiko matakatifu, hususan Biblia, inasemaje juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu.

Upofu (Visual Impairment)
Kwa mujibu wa Biblia Takatifu, upofu si dhambi wala laana; ni mpango wa Mungu kuonyesha utofauti katika uumbaji wake. Katika huo ulemavu wa macho ndipo na utukufu pamoja na nguvu za Mungu zinajidhihirisha (Yohana 9:1-3).

Nabii Musa ahojiana na Mungu kuhusu ulemavu wake
Kutoka 4:10-17, nabii Musa anatumwa na Mungu tayari kwa ajili ya kazi ya kuwatoa wana wa Israel kule utumwani Misri. Musa alikuwa na ugumu wa kuongea (Speech Impairment), na wakati anajitetea juu ya ulemavu wake na ugumu atakaoupata kwa kazi aliyotumwa Mungu alisema maneno haya
“Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kipofu? Si mimi Bwana?”

Yesu azungumzia kundi la watu wenye mahitaji maalum
Katika kitabu cha Luka 14:12-14; Yesu anazungumza kuwa diakonia inatakiwa iwafikie watu wenye mahitaji maalumu, mathlani maskini, viwete na vipofu.
Mambo ya Walawi 19:14, Biblia imeandikwa hivi:
“Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; mimi ndimi Bwana”.
*Neno Usimlaani, lina maana usimkatae au usimtenge
*Usitie kikwazo, maana yake ni kwamba binadamu yeyote asimjengee mazingira magumu ya kuishi binadamu mwenzake mwenye ulemavu.

Yesu amponya kiziwi
Marko 7:32-37; Yesu anamponya mtu aliye kiziwi, anamwombea kwa kuugua, anatumia neno Efatha.

Hitimisho

Kama Biblia ambayo inaaminiwa na watu wengi kuwa ni kitabu cha maandiko matakatifu, na ndicho kitabu kinachounda madhehebu ya Kikristo yenye waumini wengi kuliko dini zingine dunia nzima, na iliyoathiri mtazamo wa dunia kwa kiasi kikubwa huelezea vizuri suala la ulemavu, kwanini sisi waumini wa hiyo imani tunaasi maagizo hayo? Kwa waumini wa dini zingine wanaoheshimu maandiko matakatifu ya Mungu, kwanini tunafanya mambo yanayoondoa ubinadamu wa watu wenye ulemavu?

Wote kwa ujumla, kama binadamu tunahitaji kuheshimiana, kutendeana mambo mazuri, kutobaguana, kutonyanyapaana, na kuepuka mengine mengi yenye kuondoa hadhi ya mtu kuitwa binadamu.

IMEANDALIWA NA  SOKIME PHILEMON