Ninapenda sana kuzungumza habari za ulemavu na watu wenye ulemavu. Hii si kwa sababu zinapendeza na kufurahisha mioyo ya wengi, bali ni habari ambazo zinahitajika sana kwa wakati uliopo kwa ukombozi wa fikra, nafsi na mitazamo ya watu kwenye jamii zetu. Huwezi kupata vionjo kamili vya moyo na hisia juu ya athari za ulemavu hadi uguswe na ulemavu; kwa maana ya kwamba wewe mwenyewe uwe na ulemavu na/au uwe na mwanafamilia mwenye ulemavu.
Nimesoma vitabu vingi, majarida mengi na magazeti pia. Nimeona jinsi jamii zetu zinavyojitahidi kuchambua habari ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Jambo moja kuu katika maandiko yote hayo waandishi huishia kuwajengea watu hisia za huruma bila kutaja wazi wazi na kwa ujasiri uthabiti wa watu wenye ulemavu kwenye jamii zao.
Ulemavu unaweza kumpata mtu yeyote kwenye maisha wakati wowote na mahali popote.
Biblia imemtaja mjukuu wa mfalme Sauli, yaani mtoto wa Yonathani kuwa alikuwa mlemavu.
2Samweli 4:4
"Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu.....Na jina lake aliitwa Mefiboshethi."
Makazi ya watu wenye ulemavu
1. Makazi katika ardhi
Mazingira mengi ya watu wenye ulemavu wanaishi kwenye mazingira mabaya na magumu, mazingira yasiyosadifu maisha ya maendeleo.
Mfano, mjukuu wa mfalme Sauli aliwekwa katika eneo lililoitwa Lo-Debari.
Lo-Debari- ni eneo lisilo na malisho, eneo lenye ugumu wa kuishi. Kwa mantiki hii watu wengi wenye ulemavu wanaishi Lo-Debari zao katika nchi zao.
2. Fahamu zetu zinawaweka mahali gani watu wenye ulemavu?
Hata wewe ni shahidi, watu wenye ulemavu wamefikiriwa kuwa ni watu wasio na faida kwenye jamii zetu. Adolf Hitler wa Ujerumani kwa kupitia dhana hii aliwaita watu wenye ulemavu kuwa ni USELESS EATERS (walaji wa rasilimali za jamii wasio na faida (see Eugenic Movement: The War Against the Weak).
3. Mamlaka za watu wenye ulemavu ziko wapi?
Kwa utamaduni wa binadamu Tanzania na dunia nzima kwa ujumla zinaonyesha kuwa watu wenye ulemavu wanatawaliwa na kila mtu. Hii ndiyo dhana ya watu wengi. Utamkuta mtu mwenye ulemavu msomi, ana pesa, ana ufahamu wa mambo mengi ambayo yangekuwa msaada kwa wengi. Kinyume chake utakuta kila mtu asiye mlemavu anahisi yeye ndiye mtawala wa mtu mwenye ulemavu. Ushahidi ni pale utakapoona mtu mwenye ulemavu akisemwa na kusimangwa na kila mtu, na hata pengine huwa na kuzushiwa na kusingiziwa tu.
4. Tujifunze kwa mfalme Daudi
"1 Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani?
2 Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba
ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme
akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye.
3 Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa
mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba
akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha
mguu.
4 Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba
akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa
Amieli, katika Lo-debari.
5 Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.
6 Basi Mefiboshethi, mwana wa
Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi,
akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa
wako!
7 Daudi akamwambia, Usiogope, maana
bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami
nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula
mezani pangu daima.
8 Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?"
MANENO MAGUMU HAYA
2Samweli 9:8
"Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?"
Siku zote ukitaka kujua mtu alikuwa na mazingira magumu kabla ya kusaidiwa fuatilia "SHUKRANI ZAKE". Huwa ni za kipekee sana. Soma 2Sameli 9:8 ujionee.
NIONAVYO
Watu wenye ulemavu wamepitia, naam, wanaendelea kupitia kwenye mazingira magumu. Shida za watu wenye ulemavu zinafanana kote duniani zikiwa kwenye vipengele vya Miundo mbinu, Mtazamo wa jamii na mawasiliano. Tujitahidi kujenga jamii jumuishi ili tuishi kwenye taifa ambalo halimtengi mtu kwa namna yoyote ile. Nikumbushe pia kuwa leo mtu ambaye ndiye kikwazo kwa mtu mwenye ulemavu ndiye pia anaweza akawa kwenye orodha ya watakaopata ulemavu muda mfupi ujao. Jumuisha ili ujumuishwe.
FIKIRI KIJUMUISHI~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI