Wednesday, March 19, 2014

Hotuba ya Warioba kuhusu rasimu ya katiba mpya


HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, MHE.
JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA, AKIWASILISHA RASIMU YA KATIBA YA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA
BUNGE MAALUM LA KATIBA,
MACHI 2014
________________
UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti na
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba,
1.  Kwa mujibu wa kifungu 20 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura  ya 83 na
Tangazo  la  Serikali  Na.  30  la  tarehe  14  Februari,  2014,  naomba  kuwasilisha
Rasimu  ya  Katiba  kwenye  Bunge  Maalum  la  Katiba.    Rasimu  ya  Katiba
ninayoiwasilisha  imeandaliwa  na  Tume  ya  Mabadiliko  ya  Katiba  baada  ya
kukamilisha  kazi  ya  kuratibu,  kukusanya,  kuchambua  na  kutathmini  maoni  ya
wananchi kuhusu Katiba Mpya.
2.  Mwanzo  kabisa,  nieleze  kwamba,  Maelezo  haya  ninayoyatoa,  ni  sehemu  ya
Randama (Memorandum) iliyoandaliwa na Tume kwa lengo la kufafanua kwa kina,
maudhui ya kila Ibara  iliyomo katika Rasimu ya Katiba na sababu za mapendekezo
ya  Ibara  hizo.   Hivyo,  naomba  maelezo  yote  yaliyomo  katika  Randama  yawe
sehemu ya maelezo yangu na yaingizwe katika kumbukumbu za Bunge hili.
3.    Rasimu  ya  Katiba  ni  miongoni  mwa  Nyaraka  zilizoambatanishwa  katika  Ripoti
ya Tume  kuhusu Mchakato  wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri  ya Muungano wa
Tanzania  tuliyowakabidhi  Waheshimiwa  Marais  tarehe  30  Desemba,  2013.
Nyaraka nyingine ni:
2
(a)  Taarifa  ya  Maoni  ya  Wananchi  kuhusu  Mabadiliko  ya  Katiba.     Taarifa  hii  ina
maoni ya Wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kikatiba ambayo ndio msingi
wa uandishi wa Rasimu ya Katiba;
(b)  Taarifa  ya  Mabaraza  ya  Katiba  ambayo  inaainisha  maoni  ya  Wananchi  kuhusu
Ibara  zilizokuwemo  katika  Toleo  la  Kwanza  la  Rasimu  ya  Katiba  na  jinsi
zilivyofanyiwa kazi;
(c)  Taarifa ya maoni ya Wananchi kuhusu Sera, Sheria na Utekelezaji. Taarifa hii
ina  maoni  ya  wananchi  kuhusu  mambo  ambayo  yanahitaji  kufanyiwa  uamuzi
wa kisera, kutunga au kurekebisha sheria zilizopo au utekelezaji wa kiutendaji;
(d)  Taarifa  ya  Utafiti  Kuhusu  Masuala  Mbalimbali  ya  Kikatiba,  ambayo  ina  taarifa
nne ambazo ni:
(i)  Utafiti  Kuhusu  Madaraka  ya  Rais  wa  Jamhuri  ya  Muungano  wa
Tanzania;
(ii)  Utafiti Kuhusu Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji;
(iii)  Utafiti Kuhusu Masuala Yanayohusu Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar; na
(iv)  Ushauri  Elekezi  Kuhusu  Mifumo  ya  Uchaguzi  na  Tume  ya
Uchaguzi,  Tanzania  (Final  Report  on  the  Review  of  Various
Aspects  of  Electoral  Systems  and  the  Electoral  Commission  in
Tanzania).
(e)  Taarifa  ya  Takwimu  za  Ukusanyaji  wa  maoni  ya  Wananchi  ambayo  inaainisha
maeneo makuu yaliyotolewa maoni, jinsi, elimu na kazi za watoaji maoni; na
(f)  Viambatisho  vya  Ripoti  ambavyo  vinaainisha  hatua  mbalimbali  za  mchakato,
uamuzi, hotuba za viongozi na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Tume.
4.  Ripoti  ya  Tume  na  baadhi  ya  Taarifa  zimegawiwa  kwa  kila  Mjumbe  na  Taarifa
nyingine zimewekwa katika Maktaba ya Bunge ili kuwawezesha Wajumbe kufanya
marejeo.   Tume  inaamini  kwamba  Ripoti  na  Taarifa  zinazowasilishwa  pamoja  na
maelezo  haya  zitawasaidia  Wajumbe  wa  Bunge  Maalum  la  Katiba  kujadili  na
kufanya  uamuzi  sahihi  kwa  kila  Ibara  iliyopendekezwa  kwa  kuzingatia  maslahi  ya
wananchi na Taifa kwa jumla.
3
Shukrani kwa Uteuzi na Kuchaguliwa
Mheshimiwa Mwenyekiti,
5.  Naomba kutumia fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha
Tume kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba na kuiwasilisha katika Bunge
lako.
6.  Mwenyezi  Mungu  alitulinda  katika  mchakato  mzima  wa  kuratibu  na  kukusanya
maoni ya  wananchi hadi kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu. Kwa huzuni kubwa
tulimpoteza mmoja wetu, Dkt. Adrian Sengondo Mvungi katika hatua za mwisho za
kazi  yetu.   Mchango  wa  Dkt.  Mvungi  ulikuwa  mkubwa  sana  na  ingawa  hatuko
naye,  Rasimu  ya  Katiba  ninayoiwasilisha  imesheheni  maoni  yake  mengi.   Kazi  ya
Mungu  haina  makosa  na  tunamuombea  kwa  Mwenyezi  Mungu  aiweke  roho  yake
mahali pema peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
7.  Napenda  kukupongeza  wewe  mwenyewe  na  Makamu  wako  kwa  kuchaguliwa
kwenu  ili  kuongoza  Bunge  hili  ambalo  lina  jukumu  kubwa  la  kujadili  na  kupitisha
masharti  ya  Rasimu  ya  Katiba  iliyotokana  na  maoni  ya  wananchi.  Bunge  hili
Maalum  la  Katiba  litapendekeza  Katiba  Mpya  itakayopigiwa  kura  ya  maoni  na
wananchi.  Kuchaguliwa  kwenu  ni  ishara  ya  imani  kubwa  waliyonayo  wajumbe  wa
Bunge  Maalum  juu  yenu.  Tunawaombea  kwa  Mwenyezi  Mungu  awawezeshe
kuifanya  kazi  hiyo  kwa  weledi,  hekima,  busara,  uzalendo  na  uadilifu  mkubwa  ili
kukamilisha  jukumu  la  Bunge  Maalum  la  Katiba.  Tunawapongeza  pia  wajumbe
wote  wa  Bunge  Maalum  la  Katiba  na  tunawatakia  kila  la  kheri  katika  kutimiza
jukumu ambalo taifa limewakabidhi.
4
Shukrani kwa Marais, Watendaji
Mheshimiwa Mwenyekiti,
8.  Kwa  niaba  ya  Wajumbe,  na  Watumishi  wa  Sekretarieti  ya  Tume  ya  Mabadiliko  ya
Katiba na kwa niaba yangu mwenyewe, ninawashukuru kwa dhati  kabisa Rais wa
Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania,  Mheshimiwa  Dkt.  Jakaya  Mrisho  Kikwete,  na
Rais  wa  Zanzibar  na  Mwenyekiti  wa  Baraza  la  Mapinduzi,  Mheshimiwa  Dkt.  Ali
Mohammed Shein, kwa mambo yafuatayo:
  Kwanza,  kwa  uamuzi  wao  wa  busara  wa  kusikiliza  matakwa  ya  Wananchi
ya kutaka Katiba Mpya.
  Pili,  kwa  kututeua  kuwa  Wajumbe  wa  Tume  ya  Mabadiliko  ya  Katiba  na
kutuwezesha  kuifanya  na  kuikamilisha  kazi  ya  kuandaa  Rasimu  ya  Katiba
kwa wakati uliowekwa kisheria.
  Tatu,  kwa  kuipatia  Tume,  Watumishi  wa  Sekretarieti  walio  makini,  wenye
ujuzi, utaalamu na uelewa katika fani zao walioiwezesha Tume kukamilisha
kazi yake kwa ufanisi.
  Nne  kuheshimu,  kuisimamia  na  kuipa  Tume  nyenzo  za  kutekeleza
majukumu yake kwa uwazi na bila ya kuiingilia.
  Mwisho  kwa  mujibu  wa  sheria,  kuunda  Bunge  Maalum  la  Katiba  lililojaa
wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali ya jamii za watanzania.
9.  Tunatoa  shukrani  zetu  za  dhati  kwa  Mawaziri  wa  Katiba  na  Sheria  wa  Serikali  ya
Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  na  Serikali  ya  Mapinduzi  ya  Zanzibar;
Wanasheria  Wakuu  wa  Serikali;  Makatibu  Wakuu  Viongozi,  Watendaji  Wakuu  wa
Wizara za Katiba na Sheria; Wakuu wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Wakurugenzi na
Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Watendaji wa Tarafa, Kata, Shehia,
5
Vijiji na Mitaa kwa ushirikiano mzuri waliotoa kwa Tume wakati wote wa mchakato
wa kupata maoni ya wananchi.
10.  Tume  pia  inatoa  shukrani  maalum  kwa  Jeshi  la  Polisi  la  Tanzania  na  vyombo
vingine  vya  Ulinzi  na  Usalama  kwa  kuhakikisha  mchakato  mzima  unaenda  kwa
usalama.  Aidha,  Tume  inatoa  shukrani  kwa  Vyama  vya  Siasa,  Jumuiya  za  Kidini,
Asasi  za  Kiraia,  Vyombo  vya  Habari,  Taasisi  na  Makundi  mengine  kwa  mchango
wao  mkubwa  wakati  wote  wa  mchakato  wa  kupata  maoni  ya  wananchi  kuhusu
Katiba Mpya.
Shukrani kwa Wananchi
Mheshimiwa Mwenyekiti,
11.  Kwa namna na kwa uzito wa pekee, Tume inawashukuru sana Wananchi wote
kwa ushiriki, na kwa mchango wao mkubwa wa mawazo, maoni na mapendekezo
yaliyowezesha  kupatikana  kwa  Rasimu  ya  Katiba.  Hii  ni  mara  ya  kwanza  katika
historia ya nchi yetu, kwa wananchi wa kawaida kushiriki katika kutoa maoni kwa
uhuru  na  uwazi  kuhusu  aina  ya  katiba  wanayoitaka,  na  wamefanya  hivyo  kwa
wingi, uhuru, uwazi, umakini na kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
12.  Baada  ya  kutoa  shukrani  sasa  naomba  nitoe  maelezo  marefu  kidogo  kuhusu
Rasimu  ya  Katiba.  Maeneo  yote  ya  Rasimu  ni  muhimu  lakini  kwanza
nitayazungumzia  machache  kwa  ujumla  kutokana  na  umuhimu  wake.   Baadaye
nitaizungumzia  Rasimu  ya  Katiba  kwa  kupitia  maudhui  ya  kila  Sura.  Maelezo  kwa
kina  ya  kila  Ibara  na  sababu  za  mapendekezo  zinaelezwa  kwenye  Randama
6
ambayo  tayari imekabidhiwa kwa Katibu wa Bunge  Maalum la Katiba na wabunge
wote watapata nakala.
Dhana ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti,
13.  Katika  nchi  yoyote,  msingi  wa  uendeshaji  wa  nchi  unategemea  Katiba.  Katiba  ni
sheria  kuu  au  sheria  mama  katika  nchi  yoyote.  Sheria  nyingine  zote  zinategemea
au  zinatungwa  kwa  mujibu  wa  Katiba.    Wakati  mwingine  Katiba  hutafsiriwa  kuwa
ni mkataba wa Kijamii kati ya Viongozi na Wananchi. Ni makubaliano ya wananchi
kuhusu utaratibu na kanuni  za uendeshaji wa mambo mbalimbali  katika nchi yao.
Katiba ni muafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya kuendesha nchi.
14.  Katiba ni Sheria  ya msingi ambayo inaweka mfumo wa uendeshaji wa nchi. Katiba
inafanya  hivyo  kwa  kuainisha  misingi  ya  taifa,  mgawanyo  wa  madaraka  na
majukumu  ya  mihimili  mikuu  ya  dola,  usimamizi  wake,  mgawanyo  na  ukomo  wa
mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
15.  Katika  nchi  ambazo  zimefanya  mabadiliko  ya  katiba,  njia  kuu  zifuatazo  huwa
zinatumika:
(i)    Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya kikatiba;
(ii)  Kuundwa Tume ya kuandaa Katiba kwa kupitia sheria zilizopo; na
(iii)  Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya Katiba.
7
16.  Nchi  yetu  imetumia  utaratibu  wa  Bunge  kutunga  Sheria  ya  Mabadiliko  ya  Katiba,
Sura  ya  83,  inayoelezea  utaratibu  wa  mchakato  mzima  wa  kupata  katiba  mpya
ambao  unawashirikisha  wananchi  kisheria  katika  hatua  zote  muhimu  za  uandikaji
wa katiba yao.
17.  Sheria  imeanzisha  Tume  ya  Mabadiliko  ya  Katiba,  ikaweka  Hadidu  za  Rejea  na
kuipa  Tume  jukumu  la  kuratibu,  kukusanya  maoni  ya  wananchi,  kuchambua  na
kutathmini  maoni  na  kuandaa  Ripoti  na  Rasimu  ya  Katiba.  Baadaye  wananchi,
kupitia  Mabaraza  ya  Katiba,  walipewa  fursa  tena  ya  kutoa  maoni  yao  kabla  ya
Tume  kufanya  maboresho  na  kuiwasilisha  katika  Bunge  Maalum  la  Katiba;  hatua
ambayo ndipo tulipofikia hivi sasa.
18.  Baada ya Bunge Maalum kutoa Katiba inayopendekezwa, wananchi watapata fursa
ya  kufanya  uamuzi  wa  mwisho  kuhusu  Katiba  Mpya  kupitia  kura  ya  maoni.  Si  nia
yangu  kutoa  maelezo  kuhusu  historia  ya  katiba  nchini,  kwa  kuonyesha  tumetoka
wapi,  tupo  wapi  na  tunakwenda  wapi.  Maelezo  ya  kina  kuhusu  suala  hilo  yamo
kwenye  Sura  ya  Tatu  ya  Ripoti  ya  Tume  kuhusu  Mchakato  wa    Mabadiliko  ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Utangulizi wa Rasimu ya Katiba
19.  Rasimu ya Katiba inaanza na utangulizi. Utangulizi ni sehemu muhimu ya Katiba ya
nchi.   Katika  hali  ya  sasa  ya  mwelekeo  wa  taaluma  ya  sheria  duniani,  na  kwa
mujibu wa Sheria ya Tafsiri  ya Sheria, Sura ya 1 ya Sheria za Tanzania, Utangulizi
ni sehemu ya Katiba. Utangulizi ndio kioo  kinachoonyesha  dhamira ya Katiba kwa
kutoa  tafsiri  ya  jumla  ya  Katiba.   Sehemu  hii  inatoa  taswira  na  picha  halisi  ya
8
Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  na  watu  wake,  historia  yao,  matarajio  yao,
misingi  na  masuala  muhimu  ambayo  wanataka  kuyaendeleza  katika  jamii,  kizazi
hadi kizazi.
20.  Utangulizi wa Rasimu ya Katiba unatamka  rasmi kwamba Katiba hii ya Jamhuri ya
Muungano  wa  Tanzania  imetungwa  na  wananchi  wa  Jamhuri  ya  Muungano  wa
Tanzania na kuthibitishwa na wananchi kupitia kura ya maoni.
Eneo la Jamhuri
21.  Tume  imependekeza  eneo  la  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  lijumuishe  eneo
lote  la  iliyokuwa  Jamhuri  ya  Tanganyika  ikijumuisha  sehemu  yake  ya  bahari  na
eneo  lote  la  iliyokuwa  Jamhuri  ya  Watu  wa  Zanzibar  ikijumuisha  sehemu  yake  ya
bahari, kama ilivyoainishwa katika Katiba za Uhuru za nchi mbili hizi.
22.  Madhumuni  ya  kubainisha  eneo  la  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  ni
kukubaliana na maoni ya wananchi waliotaka kuwepo kwa ufafanuzi thabiti kuhusu
eneo na mipaka ya nchi. Kufanya hivi, kutatunza historia ya Jamhuri ya Muungano
wa  Tanzania  na  kuondoa  utata  na  hisia  kwamba  mipaka  ya  nchi  hizi  mbili
inabadilika.
23.  Lengo pia la sehemu hii ni kuainisha mipaka ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inayotambulika na mikataba mbalimbali ya kimataifa  na Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Bahari wa mwaka 1982.
9
Misingi Mikuu ya Taifa
24.  Rasimu ya Katiba, kama ilivyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya  mwaka  1977,  imeorodhesha  misingi  mikuu  ya  Taifa  inayojenga  Taifa  la
Tanzania  na  kusimamia  ustawi  wa  wananchi  wake.  Katiba  ya  sasa  ina  misingi
mikuu  minne,  yaani,  uhuru,  haki,  udugu  na  amani.   Wananchi  walipendekeza
misingi mingine minne iongezwe, yaani  utu,  usawa, umoja na mshikamano.  Kwa
hiyo,  misingi inayopendekezwa ni  Utu, Uhuru, Haki, Udugu, Amani, Usawa, Umoja
na Mshikamano.
Tunu za Taifa
25.  Tunu  za  Taifa  ni  mambo  muhimu  ya  kujivunia  kwa  jamii  yoyote  ile.   Tunu  ndio
msingi  wa  maadili  na  utamaduni  wa  jamii.   Tume  inapendekeza  tunu  zifuatazo
zitajwe  ndani  ya  Katiba:   Utu,  Uzalendo,  Uadilifu,  Umoja,  Uwazi,  Uwajibikaji  na
Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa.
26.  Madhumuni  ya  kupendekeza  Tunu  hizi  kuingizwa  katika  Katiba  ni  kuheshimu  na
kuzingatia  maoni  na  mapendekezo  ya  wananchi  kuwa  Katiba  itaje  Tunu  za  Taifa  ili
kuifanya jamii kuzitambua, kuzithamini na kuzitekeleza.
Malengo Muhimu
27.  Sura  ya  Pili  ya  Rasimu  inaelezea  Malengo  Muhimu  na  Misingi  ya  Shughuli  za
Serikali  na  Sera  za  Kitaifa.   Wakati  wa  kukusanya  maoni,  wananchi  wengi,  hasa
wale wanaoishi vijijini, walizungumzia sana dira ya taifa kuhusu maendeleo yao.
10
28.  Moja  ya  mambo  ambayo  wananchi  waliyatolea  maoni  kwa  msisitizo  mkubwa  ni
ardhi.   Wananchi  wengi  walilalamika  kwamba  wanayo  matatizo  kutokana  na
ugumu wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo  na shughuli nyingine  lakini wawekezaji
wakubwa  wanapewa  upendeleo  wa  kupata  ardhi  kwa  urahisi.   Pia,  kuna
migongano  isiyokwisha  ya  makundi  mbalimbali,  wakulima  na  wafugaji,  wananchi
na  mamlaka  za  hifadhi  za  taifa  na  kadhalika.   Kuna  malalamiko  mengi  kuhusu
huduma za kilimo kama vile zana za kilimo, pembejeo na mizania ya bei.
29.  Mkulima  mmoja  wa  pamba,  wilaya  ya  Kahama,  alilalamika  kwamba  ingawa
wanaambiwa  na  Serikali  kwamba  watajiondoa  kwenye  lindi  la  umaskini  kupitia
kilimo  bora,  lakini  haoni  dalili  hizo.   Alisema  wakulima  wana  matatizo  ya  mbegu,
dawa  za  kuuwa  wadudu  na  bei  ndogo  ya  mazao.   Alisema  mwaka  2012  alikuwa
ametumia  shilingi  mia  nane  kupata  kilo  moja  ya  pamba,  lakini  bei  aliyopewa
ilikuwa  shilingi  mia  sita.   Katika  mazingira  haya,  badala  ya  kupata  maisha  bora,
anazidi kuwa maskini.
30.  Wakulima  wa  mazao  ya  chakula  wana  matatizo  ya  aina  hiyo,  na  hivyo  hivyo  kwa
wakulima  wa  mazao  ya  biashara.  Wafugaji  nao  wana  matatizo  ya  ardhi  ya
malisho, maji, madawa ya mifugo na bei ya mifugo yao. Wavuvi wana matatizo ya
maeneo ya uvuvi, zana za uvuvi bei na kadhalika.
31.  Wananchi  pia  walizumgumzia  hifadhi  ya  jamii,  hasa  kwa  wazee.   Wanasema
wafanyakazi  wana  mifumo  ya  hifadhi  ya  jamii  na  mishahara  yao  inaongezwa  kila
wakati.   Kwa  Wakulima,  mapato  yao  ni  madogo  na  wakizeeka  hawana  hifadhi
yoyote.   Hata  matibabu  ya  wazee  siyo  bure  kama  utaratibu  wa  Serikali
11
unavyoelekeza,  kwani  sharti  wanunue  dawa  wakati  uwezo  wao  wa  kifedha  ni
mdogo.
32.  Wananchi  pia  walizungumzia  elimu  na  huduma  za  afya.   Kwa  maoni  yao,  elimu
bora  na  huduma  za  afya  bora  zinatolewa  kwa  watu  wa  tabaka  la  juu.   Wao
wanabaki na shule zenye huduma hafifu na zahanati zenye kutoa huduma hafifu.
33.  Tume imezingatia maoni ya wananchi na imependekeza mambo kadhaa. Kubwa ni
kuweka dira ya taifa. Sura ya  Pili yote ya Rasimu ya Katiba inazungumzia dira ya
taifa.   Madhumuni  ya  kuweka  Malengo  Muhimu  na  Misingi  ya  Shughuli  za  Serikali
ni  kuhakikisha  kuwa  Serikali  na  mamlaka  zake  zinapewa  mwongozo  wa  kisera  na
mwelekeo  wa  kiutendaji.   Pamoja  na  mambo  mengine  malengo  yafuatayo
yamewekwa kwa ajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi:
(i)  Kuweka  mazingira  bora  kwa  ajili  ya  kuanzisha  na  kuendeleza  vyombo
vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi;
(ii)  Kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa
kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na
nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao;
(iii)  Kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji
na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya mazao yao;
(iv)  Kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji wa mizania ya bei za
mazao na pembejeo.
34.  Haki ya kumiliki mali imejumuishwa kwenye haki za binadamu, na vivyo hivyo, haki
ya elimu bora ya msingi ipatikanayo bila malipo.
12
Maadili
35.  Wananchi  walio  wengi  walionyesha  kufadhaishwa  sana  na  kuporomoka  kwa
maadili  ndani  ya  jamii  na  ndani  ya  Uongozi  wa  Umma  kwa  kiwango  kikubwa.
Aidha, wananchi walitoa maoni yao kuwa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi iliyopo
haina  mamlaka  ya  kutosha  ya  kuchukua  hatua  zinazostahiki  kwa  viongozi
wanaovunja na kukiuka maadili ya uongozi.
36.  Katika  kuchambua  na  kutathmini  maoni  ya  wananchi  kuhusu  maadili  ya  viongozi
wa umma na uwajibikaji, Tume ilifanya utafiti kuhusu dhana ya uwajibikaji.  Aidha,
Maoni  ya  Mabaraza  ya  Katiba  yamesisitiza  umuhimu  wa  kuwepo  kwa  Maadili  na
miiko ya Viongozi wa Umma ndani ya Katiba.
37.  Kwa  kuzingatia  maoni  ya  wananchi  na  Taarifa  ya  utafiti,  Tume  inapendekeza
Maadili ya Viongozi wa Umma na Miiko ya Uongozi yawekwe katika Katiba. Aidha,
inapendekezwa  Sekretariati  ya  Maadili  ya  Viongozi  ibadilishwe  kuwa  Tume  kamili
ya kikatiba yenye mamlaka na uwezo mkubwa wa kusimamia maadili ya viongozi.
Haki za Binadamu
38.  Kwa  kiwango  kikubwa  Haki  za  Binadamu  zilizoainishwa  kwenye  Rasimu  ya  Katiba
zinafanana  sana  na  namna  zilivyo  kwenye  katiba  ya  sasa.   Kwa  kuzingatia  maoni
ya  wananchi  ya  kutaka  kuimarishwa  kwa  Haki  za  Binadamu,  Tume  inapendekeza
kuimarishwa kwa Haki  hizo  kwa kuondoa  vikwazo visivyo  vya lazima. Kwa mfano,
kuimarisha  ushiriki  wa  wananchi  kwenye  uongozi  kwa  kuruhusu  mgombea  huru
kikatiba.
13
39.  Tume  kwa  kuzingatia  maoni  ya  wananchi  na  mikataba  ya  kimataifa  inapendekeza
kuongezwa  kwa  haki  mpya  kwa  kuzingatia  maadili  ya  watanzania.  Miongoni  mwa
haki  hizo  ni  Haki  za  Wafanyakazi,  Haki  ya  Mtoto,  Haki  za  Watu  wenye  Ulemavu,
Haki za Wanawake, Haki za Wazee, Haki za Vijana, Haki za Kupata Habari, Haki na
Uhuru  wa  Habari  na  Vyombo  vya  Habari.  Baadhi  ya  haki  hizi  zimo  kwenye  sheria
mahususi za nchi. Hata hivyo, Tume imeona ni vyema zikawekwa kwenye katiba ili
kuweka msingi wa wananchi kuweza kuhoji na kudai utekelezaji wake kikatiba.
40.  Pamoja  na  haki  hizo,  haki  ya  kumiliki  mali,  ilitolewa  maoni  na  wananchi  kwa
msisitizo  wa  kipekee.  Maoni  ya  wananchi  wengi  yanahusu  upungufu  katika
utekelezaji  na usimamizi wa sheria za  ardhi  kuhusu  umiliki, uchukuaji wa maeneo
ya ardhi yao na ulipaji wa fidia stahiki. Aidha, wananchi walilalamika kuwa Serikali
imekuwa  ikichukua  mali  zao  bila  fidia  stahiki.   Hivyo,  Tume  inapendekeza  kuwa
mtu  yeyote  ana  haki  ya  kumiliki na  kupata  hifadhi  ya  mali  ambayo  ameipata  kwa
njia  ya  halali  na  kwamba,  asinyang’anywe  mali  hiyo  kwa  madhumuni  yoyote,  bila
ya kupata malipo stahiki yanayolingana na thamani halisi ya mali hiyo kwa wakati.
Uraia
41.  Rasimu  imetamka  Uraia  kuwa  ni  mmoja  ambao  ni  wa  Jamhuri  ya  Muungano  wa
Tanzania. Moja ya masuala  makuu ya kidola (sovereign functions) ni uraia.  Suala
la uraia limeorodheshwa kuwa ni miongoni mwa Mambo ya Muungano.
42.  Uraia  ni  msingi  wa  utambulisho  (identity)  unaompa  raia  haki  ya  kulindwa  na  nchi
yake,  ikiwa  ni  pamoja  na  haki  zake  za  binadamu  za  asili  na  zisizoondosheka
(inherrent  and  inalienable  rights)  kama  zilivyotambuliwa  au  zitakavyotambuliwa
14
katika Katiba ya Jamhuri  ya Muungano  wa  Tanzania, Katiba za Nchi  Washirika na
Mikataba ya Kimataifa.
43.  Uraia  kama  ulivyowekwa  katika  Rasimu  ya  Katiba,  umejengwa  katika  msingi  wa
uzalendo usiotiliwa shaka (patriotism) unaompatia raia wajibu wa kuitetea, kuilinda
na  kuifia  nchi  yake  bila  ya  mashaka.   Kwa  hiyo,  Uraia  ndiyo  kigezo  na  sifa  ya
kupewa  dhamana  ya  uongozi  wa  Taifa  na  kuajiriwa  katika  mihimili  ya  Serikali  na
vyombo  vya  Ulinzi na Usalama. Rasimu inapendekeza kutambuliwa kwa uraia wa
kuzaliwa  na  uraia  wa  kujiandikisha  ambao,  katika  kujidhihirisha  kwake,  ni    uraia
wa  nchi  moja  usiojenga  au  kuleta  hisia  za  kuwabagua  au  kuwatenga  raia  katika
matabaka na madaraja yanayotokana na tofauti ya hali au fursa zao.
44.  Rasimu ya Katiba pia inapendekeza kuwapatia hadhi mahsusi watu wenye asili au
nasaba  ya  Utanzania  ambao  wameacha  kuwa  raia  wa  Tanzania  kwa  kuchukua
Uraia wa nchi nyingine.
45.  Lengo  ni  kuwarahisishia  watu  wenye  asili  ya  Tanzania  waliochukua  uraia  wa  nchi
nyingine  wakija  hapa  nyumbani  wasipate  usumbufu  usio  wa  lazima  na  pia  ili
warahisishiwe  ushiriki  wao  katika  ujenzi  wa  taifa  kwa  kuwawezesha  kuchangia
ipasavyo  katika  maendeleo  ya  uchumi  wa  Tanzania.   Utaratibu  kama  huu
unafuatwa  katika  nchi  kadhaa,  kwa  mfano  Ethiopia,  India  na  Ujerumani  ambako
umeonyesha mafanikio.
15
Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa Mwenyekiti;
46.  Sura  ya  Saba  hadi  Sura  ya  Kumi  zinahusu  Mihimili  ya  Serikali.   Katika  sehemu  hii
kuna mapendekezo ambayo yataleta mabadiliko makubwa.
47.  Tukianza na taasisi ya Urais,  kuna mapendekezo manne makubwa. Pendekezo la
kwanza ni kumuondoa Rais kutoka kwenye Bunge.
Hali ilivyo sasa, Rais ni  sehemu ya Bunge na Mawaziri wake ni  Wabunge. Nia ya
pendekezo  hili  ni  kutenganisha  mamlaka  na  madaraka  ya  mihimili  (separation  of
powers). Kazi kubwa ya Bunge ni kuisimamia Serikali. Bunge haliwezi kuisimamia
Serikali kwa uhuru kama Serikali nayo ni  sehemu ya Bunge. Kwa kifupi, lengo la
pendekezo hili ni kuongeza mamlaka na madaraka ya Bunge.
48.  Katika pendekezo la pili, mtu atakuwa amechaguliwa kuwa Rais kama atapata kura
za wapiga kura zaidi ya nusu (absolute majority), badala ya utaratibu wa sasa wa
kupata wingi wa kura (simple majority).  Msingi wa pendekezo hili ni kwamba, Rais
si  kiongozi  wa  Serikali  tu  bali  pia  ni  Mkuu  wa  Nchi  na  Amri  Jeshi  Mkuu.   Kwa
sababu  hiyo,  Rais  ndiye  alama  na  taswira  ya  nchi  na  watu  wake,  na  Rais  ndiye
alama  ya  umoja  na  uhuru  wa  nchi  na  mamlaka  ya  nchi.   Kwa  maana  hiyo,  ni
muhimu Rais kuonekana anakubalika kwa wananchi walio wengi.
49.  Pendekezo  la  tatu  ni  kuruhusu  matokeo  ya  uchaguzi  wa  Rais  kuhojiwa
Mahakamani. Kwa hali ya sasa, matokeo ya uchaguzi wa Rais yakishatangazwa na
Tume ya Uchaguzi, hakuna ruhusa ya kuyahoji matokeo hayo.
16
50.  Katika  uchaguzi  wa  Rais,  inawezekana  kutakuwa  na  sababu  za  msingi  kuamini
kwamba  uchaguzi  huo  haukuwa  halali.   Ni  jambo  la  msingi  kuhakikisha  kwamba
Rais  amechaguliwa  kihalali.   Hata  hivyo,  tahadhari  imewekwa  ili  kuhakikisha
kwamba  ruhusa  hii  isitumiwe  vibaya.   Kwanza,  mtu  anayeweza  kuhoji  ni  yule  tu
aliyekuwa  mgombea  nafasi  ya  Urais.   Sharti  hili  litazuia  watu  kutumia  vibaya
ruhusa ya kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais. Pili, ni Mahakama ya Juu tu ndiyo
yenye  madaraka  ya  kusikiliza  shauri  la  aina  hii  na  ni  lazima  uamuzi  juu  ya  shauri
hilo  utolewe  ndani  ya  muda  wa  mwezi  mmoja.   Wenzetu  wa  Kenya  na  mataifa
mengine duniani wanao utaratibu kama huu.
51.  Pendekezo  la  nne  linahusu  madaraka  ya  Rais.    Suala  la  madaraka  ya  Rais
limezungumziwa kwa uzito sana katika kipindi hiki. Wakati wa kutunga Sheria ya
Mabadiliko  ya  Katiba,  suala  la  madaraka  ya  Rais  lilijitokeza  sana.   Wakati  wa
kukusanya maoni wananchi nao walilitolea maoni mengi.
52.  Baada  ya  uchambuzi  na  tathmini  ya  maoni  yote  na  Taarifa  ya  Utafiti,  Tume
imependekeza  kwamba  Rais  abaki  na  madaraka  ya  msingi  kama  Mkuu  wa  Nchi,
Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Serikali. Madaraka hayo yameainishwa katika  Ibara
ya 72 ya Rasimu. Hata hivyo, madaraka ya Rais  akiwa Mkuu wa Serikali na hasa
kwa  upande  wa  uteuzi  wa  viongozi,  ama  yamepunguzwa  au  yamewekewa
utaratibu. Rais amepunguziwa madaraka ya kuteua watumishi wa umma wa ngazi
za  kati  na  ngazi  za  chini.   Watumishi  hao  uteuzi  wao  utakuwa  kwenye  madaraka
ya Tume za Utumishi.
17
53.  Rais,  atabaki  na  madaraka  ya  kuwateua  viongozi  wa  kitaifa,  kama  vile  Mawaziri,
Majaji, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu wa Wizara na
Wenyeviti na Wajumbe wa Tume za kitaifa. Pamoja na kubaki na madaraka hayo,
Rais  amewekewa  utaratibu  wa  uteuzi.   Baadhi  ya  viongozi  watateuliwa  moja  kwa
moja  na  Rais  na  baadaye  watathibitishwa  na  Bunge,  kwa  mfano,  Mawaziri.
Wengine  watapendekezwa  na  Kamati  ya  Uteuzi  na  baada  ya  kuteuliwa,
watathibitishwa na Bunge, kwa mfano, Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya
Uchaguzi.  Wakuu  wa  Vyombo  vya  Ulinzi  na  Usalama  watateuliwa  na  Rais  kwa
kushauriana  na  Baraza  la  Ulinzi  na  Usalama  la  Taifa.   Wengine  watateuliwa
kutokana na ushauri wa Tume za Utumishi, kama vile Majaji na Makatibu Wakuu.
Bunge
Mheshimiwa Mwenyekiti;
54.  Kwa Bunge la Muungano, madaraka yake na mamlaka yatabaki kusimamia mambo
ya  Muungano.   Kinachobadilika  sasa  ni  Bunge  kutokuwa  na  mamlaka  juu  ya
mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika kama ambavyo imekuwa kwa upande
wa  Zanzibar.   Hata  hivyo,  Bunge  la  Muungano  litapata  taarifa  ya  uratibu  na
utekelezaji  wa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar kupitia
Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali.
55.  Imependekezwa pia  kwamba Spika na  Naibu Spika wasitokane na Mawaziri, Naibu
Mawaziri  au  Wabunge.   Lengo  la  pendekezo  hili  ni  kupata  viongozi  ambao
wataonekana  hawaegemei  upande  wowote.   Imependekezwa  pia  kwamba
Wabunge  wasiwe  Mawaziri.   Pendekezo  hili  limetokana  na  maoni  ya  wananchi
18
kwamba  wanahitaji  Wabunge  kuwa  karibu  na  wapiga  kura  wao.   Wengine
wanaamini  kwamba  wabunge  ambao  ni  Mawaziri  wanapendelea  majimbo  yao  ya
uchaguzi badala ya kutumikia taifa kwa ujumla kwa usawa.
56.  Lakini  lengo  jingine  la  pendekezo  hili,  ni  kutenganisha  madaraka  ya  mihimili.
Kama  Bunge  likiwa  na  madaraka  ya  kuthibitisha  Mawaziri  itakuwa  vigumu  kwa
Wabunge  kuwakataa  Wabunge  wenzao  watakaoteuliwa  kuwa  Mawaziri,  kisha
kuendelea kukaa pamoja kwa utulivu ndani ya Bunge.
57.  Tume  imependekeza  ukomo  wa  ubunge  kuwa  vipindi  vitatu  vya  miaka  mitano
mitano.   Hata  hivyo,  wananchi  wanaweza  kumwondoa  Mbunge  wao  kabla  ya
kumaliza muda wa kipindi chake  cha miaka  mitano. Pendekezo hili linatokana na
maoni  ya  wananchi  waliotaka  kuwepo  ukomo  wa  ubunge  ili  kuondoa  dhana  ya
umiliki  wa  jimbo  la  uchaguzi,  kutoa  fursa  kwa  wananchi  wengine  wenye  uwezo
kugombea nafasi ya ubunge, kuongeza uwajibikaji wa wabunge katika majimbo ya
uchaguzi na kuongeza mamlaka ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao.
58.  Pia, ni maoni ya wananchi kuwa kusiwepo uchaguzi mdogo ili kupunguza gharama.
Endapo nafasi ya ubunge itaachwa wazi kutokana na mbunge wa chama cha siasa
kupoteza  Ubunge,  basi  Tume  Huru  ya  Uchaguzi  itajaza  nafasi  hiyo  kutokana  na
orodha ya majina yaliyowasilishwa na chama cha siasa husika na kwa kushirikiana
na  chama  hicho.  Uchaguzi  mdogo  utafanyika  tu  pale  ambapo  nafasi  ya  ubunge
iliyo wazi imetokana na mbunge huru.
19
Mahakama
59.  Kuhusu  Mahakama,  pendekezo  kubwa  ni  kuundwa  kwa  Mahakama  ya  Juu  na
kwamba  Mahakama  hiyo  na  Mahakama  ya  Rufani  ndizo  ziwe  Mahakama  za
Muungano.   Mahakama Kuu ziendelee kutokuwa za Muungano kama ilivyo sasa.
Hata  hivyo,  inapendekezwa  kuwa  Mahakama  Kuu  ya  Tanganyika  na  Mahakama
Kuu  ya  Zanzibar  ziwe  na  mamlaka  sawa  katika  kusikiliza  na  kuamua  mashauri
yanayohusu  masuala  ya  Muungano  na  yasiyo  ya  Muungano  (concurrent
jurisdiction).  Hivi  ndivyo  ilivyo  hivi  sasa  kwa  upande  mmoja,  ambapo  Mahakama
Kuu  ya  Zanzibar,  japokuwa  si  sehemu  ya  Mahakama  za  Jamhuri  ya  Muungano,
lakini imepewa mamlaka na Katiba ya Jamhuri ya  Muungano kusikiliza na kuamua
kuhusu  mashauri  ya  kesi  za  madai  na  jinai  yanayohusu  sheria  za  muungano.
Pendekezo jingine ni kuuweka Mfuko wa Mahakama ndani ya Katiba.
Vyombo vya Kikatiba
Mheshimiwa Mwenyekiti,
60.  Masuala  mengine  ambayo  yameainishwa  na  kuwekewa  masharti  ya  Kikatiba  ni
Utumishi  wa Umma katika Jamhuri  ya Muungano, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume
ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji na Tume ya Haki za Binadamu.
Tume ya Utumishi wa Umma
61.  Rasimu  ya  Katiba  inaweka  utumishi  wa  umma  wa  Jamhuri  ya  Muungano  wa
Tanzania  ndani  ya  Katiba.  Sura  ya  Kumi  na  Moja  inaainisha  misingi  na  kanuni
kwamba utumishi wa umma ni dhamana kutoka kwa wananchi na hivyo,  mtumishi
anatakiwa  kutumikia  wananchi  kwa  uadilifu  na  uaminifu.  Misingi  mingine  ni
kudumisha  na  kukuza  viwango  vya  juu  vya  maadili  ya  kitaaluma,  na  kuhakikisha
20
kwamba uteuzi na uajiri katika nafasi mbalimbali unazingatia uwezo wa kitaaluma,
uweledi, maarifa, ujuzi, umakini na uzoefu katika eneo husika. Msingi mwingine ni
kutoa  huduma  kwa  umma  kwa  njia  ya  haki,  usawa  na  bila  upendeleo.  Misingi  hii
itatumika  katika  mihimili  yote  ya  dola,  taasisi  na  idara  zote  za  Serikali,  mashirika,
makampuni na wakala wa Serikali.
62.  Ili  kuweka  mfumo  madhubuti  wa  usimamizi  wa  utumishi  wa  umma,  Rasimu  ya
Katiba inaanzisha Tume ya Utumishi  ya Umma wa Jamhuri  ya Muungano ambayo
itaongozwa  na  Mwenyekiti  na  wajumbe  wengine  sita  watakaoteuliwa  na  Rais  na
kuidhinishwa na Bunge.  Tume ya Utumishi wa Umma itakuwa ni chombo cha juu
katika Utumishi wa Umma chenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu mambo yote
ya utumishi wa umma.
63.  Ibara  ya  188  inaainisha  majukumu  ya  Tume  ya  Utumishi  wa  Umma  ambayo  ni
pamoja  na  kumshauri  Rais  juu  ya  uteuzi  wa  viongozi  katika  nafasi  mbalimbali  za
utumishi  wa  umma,  kutoa  miongozo  mbalimbali  ya  kusimamia  mchakato  wa  ajira
katika  utumishi  wa  umma  na  kuhamasisha  utekelezaji  wa  misingi  na  kanuni  za
utumishi katika Sekta zote za Utumishi wa Umma.  Tume pia itakuwa na mamlaka
ya  kuunda  na  kupanga  mishahara  na  marupurupu  ya  watumishi  wote,  wakiwemo
viongozi wa kisiasa.
Tume Huru ya Uchaguzi
Mheshimiwa Mwenyekiti,
64.  Rasimu  ya  Katiba,  kama  ilivyo  Katiba  ya  Jamhuri  ya  Muungano  ya  mwaka  1977,
imetambua  haki  ya  kupiga  kura  kuwa  ni  haki  ya  msingi  ya  raia  ambayo  ni  lazima
21
itambuliwe  na  kulindwa  na  Katiba.  Kwa  umuhimu  huo,  inapendekezwa  kuwepo
kwa mfumo wa wazi wa utaratibu wa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi na kura
ya maoni.
65.  Ili kusimamia taratibu za uchaguzi, Rasimu ya Katiba inapendekeza Tume Huru ya
Uchaguzi  ya  Jamhuri  ya  Muungano.  Tume  ndiyo  itakayosimamia  masuala  ya
uchaguzi  na  kura  za  maoni.  Yapo  masharti  kuhusu  upatikanaji  wa  wajumbe  kwa
uwazi kupitia utaratibu wa kuomba nafasi na kuchujwa na Kamati ya Uteuzi kabla
ya kuteuliwa rasmi na Rais.
66.  Rasimu ya Katiba inaanzisha Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti
na Wajumbe wa  Tume Huru ya Uchaguzi. Wajumbe hao ni  Jaji Mkuu wa Jamhuri
ya  Muungano  ambaye  atakuwa  Mwenyekiti,  Spika  wa  Bunge  la  Jamhuri  ya
Muungano,  Spika  wa  Bunge  la  Tanganyika,  Spika  wa  Baraza  la  Wawakilishi,  Jaji
Mkuu  wa  Tanganyika,  Jaji  Mkuu  wa  Zanzibar  na  Mwenyekiti  wa  Tume  ya  Maadili
ya Viongozi na Uwajibikaji.
67.  Inapendekezwa  Mwenyekiti,  Makamu  Mwenyekiti  na  Wajumbe  wa  Tume
wathibitishwe na Bunge. Rasimu pia inaweka sifa za watu wanaoweza kuchaguliwa
kuwa  Mwenyekiti,  Makamu  Mwenyekiti  na  Wajumbe  wa  Tume.   Tume  Huru  ya
Uchaguzi  ni  chombo  muhimu  katika  mfumo  wa  utawala  wa  kidemokrasia  kupitia
uchaguzi huru na wa haki.  Mapendekezo haya yamezingatia misingi inayokubalika
duniani  kuhusu  umuhimu  wa  kuwepo  vyombo  huru  vya  usimamizi  wa  uchaguzi.
Misingi hiyo ni uhuru, uadilifu, uwajibikaji na uwazi.
22
Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji
Mheshimiwa Mwenyekiti,
68.  Kwa kuzingatia masharti yaliyomo katika Sura ya Tatu kuhusu Maadili na Miiko ya
Uongozi  na  Utumishi  wa  Umma,  Rasimu  ya  Katiba  inapendekeza  kuanzishwa  kwa
Tume  ya  Maadili  ya  Uongozi  na  Uwajibikaji  na  kutaja  sifa  za  mtu  kuteuliwa  kuwa
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume na kuthibitishwa na Bunge. Tume ya
Maadili  itakuwa  ni  chombo  cha  kikatiba  kitakachokuwa  na  nguvu  ya  kusimamia
maadili ya Viongozi wa Umma.
69.  Majukumu ya Tume ya Maadili ni kusimamia maadili na uwajibikaji katika utumishi
wa umma, kuchunguza tabia na mwenendo wa mtumishi au kiongozi na kuchukua
hatua pale inapostahili. Uhuru wa Tume katika utekelezaji wa majukumu yake ni
muhimu  ili  kuhakikisha  kuwa  haitaingiliwa  na  mtu  au  mamlaka  yoyote  katika
utekelezaji wa majukumu hayo.
Tume ya Haki za Binadamu
Mheshimiwa Mwenyekiti,
70.  Tume  ya  Haki  za  Binadamu  ni  taasisi  ambayo  inapendekezwa  iendelee  kuwepo
ndani  ya  Katiba.  Rasimu  ya  Katiba  imeainisha  muundo  wake  na  utaratibu  wa
kuwateua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna.
71.  Majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyopo hivi sasa kuhusu
masuala  ya  utawala  bora,  yamewekwa  katika  Tume  ya  Maadili  ya  Uongozi  na
Uwajibikaji,  hasa  yanayohusu  matumizi  mabaya  ya  madaraka.   Vile  vile,
23
mapendekezo  haya  yanakubaliana  na  maoni  ya  wananchi  waliotaka  kuwepo  kwa
utaratibu utakaokuza, kuhifadhi na kulinda haki za binadamu.
72.  Rasimu  ya  Katiba  inapendekeza  kuendelea  kuwepo  kwa  uhuru  wa  Tume  katika
utekelezaji wa majukumu yake ili kuhakikisha kuwa haiingiliwi na mtu au mamlaka
yoyote. Masharti haya ya kikatiba yataiwezesha Tume kufanya kazi kwa uhuru na
kuwawezesha  Makamishna  kutekeleza  majukumu  yao  kwa  uaminifu,  uadilifu  na
bila  ya  woga  au  upendeleo.   Hali  hii  itaendeleza  imani  ya  wananchi  kuwa;
maamuzi  yatakayofanywa  na  Tume  hayatokani  na  maelekezo,  shinikizo  au
matakwa ya mtu, kikundi cha watu au chombo kingine chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
73.  Baada  ya  maelezo  hayo  ya  jumla  kuhusu  Rasimu  ya  Katiba,  sasa  naomba
nizungumzie  Rasimu  ya  Katiba  kwa  kupitia  maudhui  ya  kila  Sura.  Kama
nilivyoeleza  hapo  awali,  maelezo  ya  kina  kuhusu  kila  Ibara  na  sababu  za
mapendekezo  zimeelezwa  kwenye  Randama  ambayo  waheshimiwa  wajumbe
watapatiwa pamoja na nakala ya Hotuba hii.
74.  Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ni ndefu kidogo, ina  Ibara  271, ikilinganishwa
na  Katiba  ya  sasa  yenye  Ibara  152.  Rasimu  hii  imeganywa  katika  Sura  Kumi  na
Saba.  Ongezeko  la  Ibara,  kwa  kiwango  kikubwa,  limetokana  na  Tume  kuzingatia
maoni ya wananchi ambao walitaka mambo mengi zaidi yaingizwe kwenye Katiba.
24
Mheshimiwa Mwenyekiti;
75.  Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba imegawika katika Sehemu mbili. Sehemu ya
Kwanza  inaanzia  Ibara  ya  1  hadi  5  na  zinahusu  Jina,  Eneo  la  Jamhuri  ya
Muungano,  Alama,  Lugha  na  Tunu  za  Taifa.  Sehemu  ya  Pili  inaanzia  Ibara  ya  6
hadi 9 zinazopendekeza masharti kuhusu Mamlaka ya Wananchi, Watu na Serikali,
Ukuu na Utii wa Katiba na Hifadhi ya Utawala na Katiba.
76.  Sura ya Pili ya Rasimu ina Ibara ya 10 hadi 12. Sehemu hii inapendekeza masharti
yanayohusu Malengo Makuu, Utekelezaji wa Malengo ya  Taifa na  Sera ya Mambo
ya Nje.
77.  Sura  ya  Tatu  ya  Rasimu  imegawika  katika  Sehemu  mbili.  Sehemu  ya  Kwanza
inaanzia  Ibara  ya  13  hadi  20  zinazopendekeza  masharti  kuhusu  Dhamana  ya
Uongozi  wa  Umma,  Kanuni  za  Uongozi  wa  Umma,  Zawadi  katika  Utumishi  wa
Umma,  Akaunti  Nje  ya  Nchi  na  Mikopo,  Wajibu  wa  Kutangaza  Mali  na  Madeni,
Mgongano  wa  Maslahi,  Matumizi  ya  Mali  ya  Umma  na  Utekelezaji  wa  Masharti  ya
Maadili.
78.  Sehemu  ya  Pili  ya  Sura  ya  Tatu  inaanzia  Ibara  ya  21  hadi  22  zinazopendekeza
masharti  kuhusu  Utii  wa  Miiko  ya  Uongozi  wa  Umma  na  Marufuku  ya  Baadhi  ya
Vitendo kwa Watumishi wa Umma.
25
79.  Sura ya Nne ya Rasimu ina sehemu mbili. Sehemu ya Kwanza inayoanzia  Ibara  ya
23 hadi 48 inahusu Haki za Binadamu. Haki hizo kwa sasa zimeainishwa vizuri zaidi
na kuongeza haki za makundi mbalimbali katika jamii.
80.  Sehemu ya Pili ya Sura ya Nne inayoanzia  Ibara  ya 49 hadi  55 inahusu mipaka ya
matumizi  ya  haki  za  binadamu  na  wajibu  wa  raia  na  Serikali  ambazo  zimewekwa
kwa  upana  na  uwazi  zaidi  ikiwemo  Wajibu  wa  Raia  kwa  Ujumla,  Wajibu  wa
Kushiriki  Kazi,  Wajibu  wa  Kulinda  Mali  ya  Umma,  Haki  na  Wajibu  Muhimu  kwa
Raia, Hifadhi ya Haki za Binadamu, Usimamizi wa Haki za Binadamu na Mipaka  ya
Hifadhi ya Haki za Binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
81.  Sura ya Tano ya Rasimu  ya Katiba inaanzia  Ibara  ya 56 hadi 59 na inapendekeza
masharti kuhusu Uraia wa Jamhuri ya Muungano. Rasimu inapendekeza aina mbili
za  uraia;  wa  kuzaliwa  na  kujiandikisha.   Ibara  59  inapendekeza  kuwapa  hadhi
maalum  watu  walioacha  kuwa  raia  wa  Jamhuri  ya  Muungano  tofauti  na  raia  wa
nchi nyingine ambao hawana asili au nasaba ya Tanzania.
82.  Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba inaanzia Ibara ya 60 hadi 69 na inahusu Muundo
wa  Jamhuri  ya  Muungano.  Rasimu  inapendekeza  masharti  kuhusu  Muundo  wa
Muungano,  Vyombo  vya  Utendaji  vya  Jamhuri  ya  Muungano,  Mamlaka  ya  Serikali
ya Muungano, Mambo ya Muungano, Nchi Washirika, Mamlaka ya Nchi Washirika,
Mahusiano  kati  ya  Nchi  Washirika,  Mawaziri  Wakaazi,  Mamlaka  ya  Wananchi  na
wajibu wa Kuhifadhi Muungano.
26
83.  Sehemu  hii  inapendekeza  muundo  wa  Muungano  wa  Shirikisho  la  Serikali  tatu,
ambazo  ni  Serikali  ya  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania,  Serikali  ya  Tanganyika
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia inaainisha mihimili mikuu ya dola ambayo
ni  Serikali,  Bunge  na  Mahakama  ya  Jamhuri  ya  Muungano.   Sehemu  hii  pia
inatambua  kwamba  mambo  mengine  ya  kiutendaji  yasio  ya  Muungano
yataainishwa katika Katiba za Nchi Washirika
84.  Sura  ya  Saba  inahusu  Serikali  ya  Jamhuri  ya  Muungano  na  imegawanyika  katika
sehemu  mbili.  Sehemu  ya  Kwanza  inaanzia  Ibara  ya  70  hadi  96  zinazopendekeza
masharti  kuhusu  Rais  wa  Jamhuri  ya  Muungano,  Uchaguzi  wa  Rais,  Masharti
Mahsusi kuhusu Mamlaka ya Rais na nafasi ya Makamu wa Rais.
85.  Sehemu  ya  Pili  ya  Rasimu  ya  Katiba  inanzia  Ibara  ya  97  hadi  108  zinazohusu
Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri  ya Muungano. Sehemu hii inapendekeza
Masharti  kuhusu  Kuundwa  kwa  Baraza  la  Mawaziri,  uteuzi  wa  Mwanasheria  Mkuu
wa  Serikali,  Katibu  Mkuu  Kiongozi  na  Makatibu  Wakuu  pamoja  na  sifa  za  uteuzi.
Aidha,  masharti  ya  Utekelezaji  wa  shughuli  za  Baraza  la  Mawaziri
yanapendekezwa.
86.  Sura ya Nane inaanzia  Ibara  ya 109 hadi 112 na inahusu Uhusiano na Uratibu wa
Serikali.  Ili  kuzuia  uwezekano  wa  mgongano,  na  kwa  lengo  la  kuwianisha  sera,
sheria,  mipango  na  mikakati,  Rasimu  inapendekeza  kuundwa  Tume  ya  Uhusiano
na Uratibu wa Serikali. Tume hii ni  muhimu katika Muungano wowote kwa kuwa
27
mambo yasiyo ya Muungano mara nyingi ndio husababisha tofauti na mgawanyiko
mkubwa  katika  nchi.   Kwa  lengo  hilo  hilo,  Rasimu  ya  Katiba  inapendekeza
kuanzishwa  kikatiba,  Baraza  la  Ulinzi  na  Usalama  la  Taifa.   Baraza  hilo  litakuwa
chini  ya  Uwenyekiti  wa  Rais  na  Wajumbe  wake  watakuwa  ni  pamoja  na  Rais  wa
Tanganyika na Rais wa Zanzibar.
87.  Sura ya Tisa ya Rasimu inahusu Bunge la Jamhuri ya Muungano. Sura hii inaanzia
Ibara  ya  113  hadi  149  na  imegawika  katika  sehemu  Sita.  Katika  Sura  hii,  Rasimu
inapendekeza  masharti  kuhusu  Muundo  na  Madaraka  ya  Bunge,  Uchaguzi  wa
Wabunge, Uongozi wa Bunge, Utaratibu  wa Shughuli za Bunge, Madaraka na Haki
za  Bunge.  Aidha,  Rasimu  inapendekeza  masharti  kuhusu  Tume  ya  Utumishi  na
Mfuko wa Bunge.
88.  Sura ya Kumi inahusu Mahakama ya Jamhuri ya Muungano. Sura hii inaanzia Ibara
ya  150  hadi  183  na  imegawanyika  katika  Sehemu  Tatu.  Sura  hii  inapendekeza
masharti  kuhusu  Kuanzishwa  kwa  Mahakama  ya  Jamhuri  ya  Muungano,  Muundo
wa  Mahakama,  Uanzishwaji  wa  Mahakama  ya  Juu  na  Mahakama  ya  Rufani  na
Uteuzi  wa  Majaji.  Aidha,  masharti  ya  Usimamizi  wa  Shughuli  za  Mahakama,
Uanzishwaji wa Tume ya Utumishi na Mfuko wa Mahakama yanaainishwa.
89.  Sura  ya  Kumi  na  Moja  inahusu  Utumishi  wa  Umma  katika  Jamhuri  ya  Muungano.
Sura  hii  inaanzia  Ibara  ya  184  hadi  188  ambazo  zinapendekeza  masharti  kuhusu
Misingi Mikuu ya Utumishi wa Umma na Ajira na Uteuzi wa Viongozi wa Taasisi za
28
Serikali.  Aidha,  Rasimu  inapendekeza  masharti  ya  uanzishwaji  wa  Tume  ya
Utumishi wa Umma pamoja na Mamlaka na Majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
90.  Sura ya Kumi na Mbili inayohusu masuala ya uchaguzi,  inaanzia  Ibara  ya 189 hadi
199.  Sura  hii  inapendekeza  masharti  kuhusu  Kuundwa  na  Majukumu  ya  Tume
Huru  ya  Uchaguzi,  Uteuzi  wa  Wajumbe  wa  Tume,  Uteuzi  na  Majukumu  ya
Mkurugenzi  wa  Tume  ya  Uchaguzi  na  Uteuzi  na  Majukumu  ya  Msajili  wa  Vyama
vya Siasa.
91.  Sura ya Kumi na Tatu inahusu taasisi za uwajibikaji. Sura hii inaanzia Ibara ya 200
hadi 220. Sehemu hii inapendekeza masharti kuhusu uanzishwaji na majukumu ya
Tume  ya  Maadili  ya  Viongozi  na  Uwajibikaji,  Tume  ya  Haki  za  Binaadamu  na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Seikali.
92.  Sura  ya  Kumi  na  Nne  inahusu  fedha  za  Jamhuri  ya  Muungano.  Sura  hii  inaanzia
Ibara  ya  221  hadi  234  na  inapendekeza  masharti  kuhusu  Mfuko  Mkuu  wa  Hazina
na  Fedha  za  Jamhuri  ya  Muungano,  Deni  la  Taifa  na  Mikopo,  Vyanzo  vya  Mapato
ya  Serikali  ya  Jamhuri  ya  Muungano  na  uanzishwaji  wa  Benki  Kuu  ya  Jamhuri  ya
Muungano.
93.  Sura  ya  Kumi  na  Tano  inaanzia  Ibara  ya  235  hadi  250  na  inahusu  ulinzi  na
usalama  wa  Jamhuri  ya  Muungano.  Sura  hii  inapendekeza  masharti  ya  Vyombo
vya Ulinzi na Usalama wa Taifa,  pamoja na kulitambua kikatiba  Baraza la Ulinzi na
Usalama wa Taifa.
29
94.  Sura  ya  Kumi  na  Sita  inaanzia  Ibara  ya  251  hadi  256.  Rasimu  katika  Sura  hii
inapendekeza  masharti  ya  Kujiuzulu  katika  Utumishi  wa  Umma,  Kukabidhi
Madaraka,  Ufafanuzi  wa  Maneno  yaliyotumika  katika  Rasimu  ya  Katiba,  Jina  la
Katiba na Kuanza Kutumika kwa Katiba Mpya.
95.  Sura ya Kumi na Saba ndio Sura ya Mwisho na imegawanyika katika Sehemu Sita
na  ina  Ibara  kuanzia  257  hadi  271.  Sura  hii  inahusu  Masharti  ya  Yatokanayo  na
Masharti ya Mpito. Rasimu inapendekeza masharti kuhusu matumizi ya masharti
ya  kipindi  cha  mpito  na  ukomo  wa  Katiba  ya  mwaka  1977  ili  kuhakikisha  kuwa
mabadiliko  ya  Katiba  hayafuti  uhalali  wa  sheria  za  nchi  zilizopo  na  maamuzi
yaliyofanywa  chini  ya  Katiba  iliyofutwa  au  Katiba  za  awali  zilizopita  na  ambazo
masharti yake yanatumika hadi sasa.
96.  Aidha, Rasimu inapendekeza masharti kuhusu kuendelea kuwepo madarakani kwa
Rais,  Makamu  wa  Rais,  Waziri  Mkuu,  Mawaziri  na  Manaibu  waziri.   Pia  masharti
kuhusu  kuendelea  kuwepo  Bunge  la  Jamhuri  ya  Muungano  na  Mahakama  ya
Rufani ya Jamhuri ya Muungano.
97.  Inapendekeza  kuanzishwa  kwa  Kamati  ya  kusimamia  utekelezaji  wa  mambo  yote
yanayopaswa  kutekelezwa  katika  kipindi  cha  mpito,  muundo  wake,  majukumu
yake  na  masharti  ya  uteuzi  wa  Mwenyekiti  na  wajumbe,  Katibu  na  Watumishi  wa
Sekretarieti ya Kamati.
30
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
98.  Suala  la  Muundo  wa  Serikali  Tatu  limechukua  nafasi  kubwa  sana  katika  mjadala
tangu  Tume  ilipozindua  Rasimu  ya  Kwanza  ya  Katiba.   Mjadala  wa  Muundo  wa
Muungano  umekuwa  mkubwa  kwa  kiasi  cha  kufunika  mapendekezo  mengine
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
99.  Kwa  kuwa  jambo  hili  lina  umuhimu  wa  pekee  katika  mstakabali  wa  nchi  yetu,
naomba nitumie nafasi hii kutoa maelezo ya kutosha ili Waheshimiwa Wabunge na
wananchi kwa jumla wafahamu msingi ulioifanya Tume kutoa pendekezo hili.
100.  Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika  kifungu cha  9(2)  imetoa mwongozo kwa
Tume  kuzingatia  mambo  kadhaa  ya  msingi.   Kati  ya  mambo  hayo  ni  kuendelea
kuwepo  kwa  Jamhuri  ya  Muungano,  uwepo  wa  Serikali,  Bunge  na  Mahakama  na
kuendelea kuwepo kwa Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tafsiri ya Tume ilikuwa
kwamba mwongozo huu ulikuwa kwa Tume tu, siyo kwa wananchi. Tume iliamini
sheria  haikukusudia  kuwazuia  wananchi  kutoa  mawazo  yao  kwa  uhuru  bila  ya
kizuizi wala mipaka. Hivyo, Tume ilipokea mawazo ya kila aina.
101.  Pia,  Tume ilijadili njia bora ya kupata maoni. Tume ilifikiria kuandaa dodoso ili
wananchi  wajibu  maswali  kuhusu  mambo  mbalimbali  kuhusu  Katiba.   Hata  hivyo,
Tume iliamua wananchi wasipewe mwongozo  ili  wawe na uhuru kusema chochote
wanachoamini. Msingi huu ndio uliofuatwa na Tume ili kupata maoni ya wananchi
kuhusu maeneo yote, ikiwa ni pamoja na suala la Muungano.
31
102.  Tume ilianza kazi kwa madhumuni ya kupata maoni ya  wananchi ili  kuboresha
Muungano.  Wananchi wengi waliotoa maoni kuhusu  Muungano,  walijikita kwenye
Muundo wake  kama njia ya kuondoa kero. Kwa Tanzania Bara,  wananchi zaidi ya
39,000  walitoa  maoni  kuhusu  Muungano  na  kati  ya  hao,  karibu  27,000
walizungumzia  muundo.   Kwa  Zanzibar,  wananchi  karibu  wote  waliotoa  maoni
walijikita  kwenye  suala  la  Muungano.   Kati  ya  wananchi  karibu  38,000  waliotoa
maoni  kuhusu  Muungano,  wananchi  19,000  walitoa  maoni  kuhusu  muundo  wa
Muungano.  Mchanganuo  wa  takwimu  hizi  unaonyesha  kuwa  wananchi  waliotoa
maoni  kuhusu  muundo  wa  Muungano  kwa  upande  wa  Tanzania  Bara,  13%
walipendelea  Serikali  Moja,  24%  walipendekeza  Serikali  Mbili  na  61%
walipendekeza  Serikali  Tatu.   Kwa  upande  wa  Zanzibar,  34%  walipendekeza
Serikali  mbili  na  60%  walipendekeza  Muungano  wa  Mkataba,  na  0.1%  (watu  25)
walipendekeza  Serikali  Moja.  Aidha,  taasisi  nyingi  kama  vile  vyama  vya  siasa,
asasi za kiraia na jumuia za kidini zilipendekeza Muundo wa Serikali Tatu.
103.   Baadhi  ya  taasisi  za  kiserikali,  ama  moja  kwa  moja  au  kwa  tafsiri  ya
mapendekezo  yao,  pia  zilipendekeza  au  kukubali  muundo  wa  Serikali  Tatu.   Kwa
mfano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipendekeza kuwepo kwa mamlaka huru ya
Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano na iwekwe wazi
maeneo,  uwezo,  nguvu,  utendaji  na  mipaka  ya  kila  mamlaka.    Baraza  la  Ofisi  ya
Makamu  wa  Rais  lilipendekeza,  kuhusu  Muundo  wa  Serikali  kwamba,  nanukuu
“kuwe na Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  Wakuu
wa  Serikali  za  Washirika  wa  Muungano  wapewe  vyeo  vingine
32
vinavyoendana na hadhi na mamlaka zao. Pia katika kutaja hizo serikali
tatu  inabidi  zitenganishwe  ili  Serikali  ya  Muungano  ionekane  ndio  ya
juu”
104.  Baraza la Ofisi ya Waziri Mkuu lilipendekeza, kuhusu  uongozi wa taifa kwamba
kuwe,  na  “Rais  wa  Jamhuri  ya  Muungano,  Waziri  Mkuu  wa  Jamhuri  ya
Muungano,    Waziri Mkuu wa Serikali ya Tanganyika na Waziri Mkuu wa
Serikali  ya  Zanzibar.   Mapendekezo  hayo  ni  kwa  sababu  hakuna
umuhimu wa kuwa na marais watatu (3)  katika nchi moja  na wala neno
Rais  halimuongezei  hadhi  kiongozi  yeyote.  Pia  kutoa  nafasi  kwa
Mawaziri  Wakuu  kuwa  watendaji  zaidi  na  hivyo  kusimamia  Serikali  za
Washirika.”    Aidha,  Bunge  la  Jamhuri  ya  Muungano  katika  maoni  yake
lilipendekeza  kuwepo  kwa  Tume  ya  Utumishi  wa  Bunge  ambayo  inajumuisha,
katika Wajumbe, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano (Mwenyekiti), Spika wa
Bunge la Tanzania Bara na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
105.  Baada ya kuona takwimu hizi na  kuchanganua sababu zilizotolewa na makundi
mbali  mbali,  Tume  iliamua  kufanya  utafiti  wa  kina  kuhusu  Muundo  wa  Muungano
na matatizo yake tangu  Muungano ulipoundwa.  Katika utafiti  huo    mambo kadhaa
yamejitokeza.
106.  Kwanza,  kulikuwa  na  changamoto  nyingi  baada  ya  Tanganyika  na  Zanzibar
kuungana  mwaka  1964.   Ujenzi  wa  taasisi  ili  kuendesha  mambo  ya  muungano
ulikuwa ni changamoto kubwa. Serikali ya Muungano haikuwa na taasisi zake, kwa
33
hiyo  ilianza  kwa  kutumia  taasisi  zilizokuwapo  katika  sehemu  zote  mbili  za
muungano.   Kwa  upande  wa  sheria,  hali  ilikuwa  hivyo  hivyo.   Hata  uamuzi  wa
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya demokrasia ya chama kimoja ulichukuliwa wakati
nchi  ikiwa  na  vyama  viwili;  TANU  na  ASP.    Kwa  hiyo,  kila  upande  uliendesha
mambo yake kutumia itikadi na sera zake.
107.  Changamoto  hizi  hazikuzuia  kuimarika  kwa  muungano  kwa  sababu  utashi  wa
kisiasa wa Waasisi wa Muungano ulikuwa mkubwa. Mwaka 1977, vyama vya siasa
vya TANU na  ASP viliunganishwa  na Chama Cha Mapinduzi kilizaliwa na Katiba  ya
kudumu  ilitungwa.   Baada  ya  Jumuiya  ya  Afrika  Mashariki  kuvunjika,  baadhi  ya
mambo yaliyokuwa chini ya Jumuiya hiyo yaliwekwa kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Matokeo yake, nchi ilionekana ni moja, yenye mshikamano, utulivu na
amani.
108.  Wakati  huo,  viongozi  na  watumishi  wa  umma  na  kwenye  Chama  cha  siasa
walipangiwa  kazi  sehemu  yoyote  ya  nchi  bila  kujali  sehemu  wanayotoka.   Kwa
muda mfupi nchi ilionekana kuwa kweli ni taifa  moja. Lakini  hali hiyo haikudumu
kwa muda mrefu. Utaifa wa nchi mbili ukaanza kujitokeza.  Viongozi na watumishi
wa umma kutoka upande mmoja  wa Muungano wakaonekana  hawapendi  kwenda
kufanya kazi upande wa pili wa Muungano.
109.  Pia  majina ya sehemu mbili za Muungano  yakabadilishwa. Badala ya Tanzania
Bara na Tanzania Visiwani tukaanza kutumia Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar,
ili  kulinda  Zanzibar  isionekane  imemezwa.   Ni  wakati  huo,  lugha  ya  Tanganyika
kuvaa Koti la Muungano ilianza kusikika.
34
110.  Mwaka 1984,  kulitokea  kile kilichoitwa  “kuchafuka kwa hali ya hewa  ya  kisiasa
Zanzibar”.   Msingi  wake  ilikuwa  ni  mpango  wa  baadhi  ya  viongozi  wa  Zanzibar
kutaka  Serikali  Tatu.   Ingawa  jaribio  hili  halikufanikiwa,  Zanzibar  ilitunga  Katiba
Mpya mwaka huo huo.
111.    Katika  Katiba  hiyo,  Zanzibar  iliondoa  madaraka  ya  sheria  zinazotungwa  na
Bunge  kutumika  moja  kwa  moja  Zanzibar.   Katiba  ya  Zanzibar  iliweka  masharti
kwamba  sheria  za  muungano  zipelekwe  kwenye  Baraza  la  Wawakilishi  kabla  ya
kutumika Zanzibar.
112.  Mwaka  1991,  Tume  ya  Jaji  Nyalali  ilipendekeza  muundo  wa  Serikali  Tatu.
Ingawa  pendekezo  hili  halikukubalika,  Zanzibar  iliamua  kuwa  na  bendera  na
nembo  yake  na  baadaye  sharti  likawekwa  kwamba  meli  zinazoingia  kwenye
bandari za Zanzibar ni  lazima zitumie  bendera ya  taifa yenye  nembo ya Zanzibar.
Kwa maana nyingine, Zanzibar ikaanza kutumia Bendera ya Taifa iliyo tofauti.
113.  Mwaka  1992,  Zanzibar  ilijiunga  na  Organisation  of  Islamic  Conferece  (OIC)  na
Bunge  lilipitisha  Azimio  la  kuzitaka  Serikali  zote  mbili  kushirikiana  katika  kutafuta
ufumbuzi  wa  tatizo  hilo  na  matatizo  mengine  ya  Muungano  na  kutoa  taarifa
Bungeni katika kipindi cha mwaka mmoja.
114.  Mwaka 1993, wakati wa Mkutano wa Bajeti, Wabunge kutoka Tanzania Bara (G
55)  walipeleka  Bungeni  hoja  ya  kuundwa  kwa  Serikali  ya  Tanganyika.  Hoja  hiyo
ilipitishwa.
35
115.  Mwezi  Novemba  mwaka  1993,  Kikao  Maalum  cha  CCM  na  Serikali  zote  mbili
kilifanyika  Dodoma  ili  kutafuta  maelewano  kuhusu  Azimio  la  Bunge.  Muafaka
ulifikiwa kwamba Azimio hili lisitekelezwe, yaani Serikali ya Tanganyika isiundwe.
116.  Mwaka  1994,  Halmashauri  Kuu  ya  CCM  ilipitisha  azimio  kuhusu  haja  ya
kuendelea  na  muundo  wa  Serikali  Mbili  kwa  lengo  la  kufikia  Muundo  wa  Serikali
Moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
117.  Baada  ya  Tume  ya  Jaji  Nyalali,  Serikali  iliunda  Kamati  ya  Shellukindo
ikijumuisha  wajumbe  kutoka  Serikali  zote  mbili.   Serikali  ya  Zanzibar  nayo  iliunda
Kamati  ya  Amina  Salum  Ali.   Kamati  ya  Shellukindo  ilichambua  Mambo  yote  ya
Muungano  na  kutoa  mapendekezo  ya  kuboresha  utekelezaji.   Lakini  pia  ilitoa
mapendekezo  ya  baadhi  ya  mambo  kuondolewa  kwenye  Orodha  ya  Mambo  ya
Muungano,  kwa mfano bandari. Kwa  upande mwingine  Kamati ya Amina, pamoja
na  mambo  mengine,  ilipendekeza  mambo  kumi  na  mbili  yaondolewe  kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo yalihusu uchumi.
118.  Mwaka  1994,  Serikali  zote  mbili  zilikutana  kutafakari  mapendekezo  ya  Kamati
ya  Shellukindo.   Pamoja  na  mambo  mengine  muafaka  ulifikiwa  kuondoa  au
kubadili baadhi ya mambo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
119.  Kwa  kuwa  mjadala  juu  ya  Muundo  wa  Muungano  ulikuwa  unaendelea  wakati
wote,  Serikali ikaona ni busara kuunda Kamati ya  Jaji Kisanga  ambayo, pamoja na
mambo  mengine,  ilitakiwa  kupendekeza  aina  ya  Muundo  wa  Muungano.   Kamati
ya  Kisanga  ilipendekeza  muundo  wa  Serikali  tatu.   Pendekezo  hili  halikukubalika
36
lakini  Muafaka  wa 1994,  kati ya Serikali zote mbili,  uliendelea kutekelezwa bila ya
kufanya mabadiliko kwenye Katiba.
120.  Katika  kipindi  chote  hiki,  kulikuwa  na  malalamiko  kutoka  kila  upande.  Kwa
upande wa Zanzibar baadhi ya malalamiko yalikuwa yafuatayo:
(i)  Serikali  ya  Tanganyika  imevaa  koti  la  Serikali  ya  Muungano  ambalo
linaisaidia  Tanganyika  zaidi  kuliko  Zanzibar.   Taswira  hiyo  imeifanya
Tanganyika  kuwa  ndiyo  Tanzania  na  Watanganyika  ndiyo  waamekuwa
Watanzania; na Wazanzibari wamebaki kuwa Wazanzibari.
(ii)  Mambo  ya  Muungano  yamekuwa  yakizidi  kuongezeka  na  hivyo  kuathiri
uhuru wa Zanzibar (Autonomy) na kufifisha hadhi ya Zanzibar (Identity);
(iii)  Kuvunjwa  kwa  makubaliano  ya  Hati  ya  Muungano  kwa  kuificha  sura  ya
Tanganyika katika Muundo wa Serikali ya Muungano;
(iv)  Kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano;
(v)  Kutokuwepo  kwa  uwazi  wa  mapato  na  matumizi  ya  fedha  za  Serikali  ya
Muungano;
(vi)  Kutokuanzishwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja;
(vii)  Kuwepo  kwa  mkanganyiko  wa  ugawaji  wa  mapato  na  jinsi  ya  kuchangia
gharama  za  uendeshaji  wa  shughuli  za  Muungano  baina  ya  Serikali  ya
Muungano na Serikali ya Zanzibar;
(viii)  Kuwepo kwa chumi mbili tofauti zinazoshindana katika nchi moja;
(ix)  Zanzibar  kutoshirikishwa  kikamilifu  na  Serikali  ya  Jamhuri  ya  Muungano
katika masuala ya kupata misaada na mikopo kutoka nje ya nchi;
37
(x)  Malalamiko  kuwa  viongozi  wakuu  wa  Zanzibar  wanachaguliwa  Dodoma  na
sio Zanzibar kwenyewe;
(xi)  Zanzibar  kulalamika  kuwa  kuna  baadhi  ya  mambo  yamefanywa  kuwa  ya
Muungano kupitia kutungwa kwa sheria na Bunge  la Jamhuri ya Muungano
kwa  mambo  yasio  ya  Muungano  na  baada  ya  hapo  mambo  hayo  kupata
hadhi ya Muungano;
121.  Kwa upande wa Tanzania Bara, baadhi ya malalamiko yalikuwa yafuatayo:
(i)  Zanzibar  imekuwa  nchi  huru,  ina  bendera  yake,  ina  wimbo  wake  wa  Taifa,
ina Serikali yake na imebadili Katiba yake ili kujitambua kuwa ni nchi;
(ii)  Zanzibar  imebadili  masharti  ya  Katiba  ya  Jamhuri  ya  Muungano  ambayo
inasema  sheria  za  Muungano  zinazotungwa  na  Bunge  la  Jamhuri  ya
Muungano  zitumike  sehemu  zote  za  Muungano,  badala  yake  Katiba  ya
Zanzibar  inaelekeza  kuwa  ili  Sheria  itumike  Zanzibar  ni  sharti  ipelekwe
mbele  ya  Baraza  la  Wawakilishi.   Maana  yake  ni  kuwa,  Katiba  ya  Zanzibar
ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano;
(iii)  Zanzibar  imetunga  sheria  kuhusu  fedha  ambalo  ni  suala  lililo  kwenye
madaraka ya Muungano;
(iv)  Zanzibar  imetunga  Katiba  ambayo  imechukua  madaraka  ya  Rais  yaliyomo
katika  Katiba  ya  Jamhuri  ya  Muungano  yanayoeleza  kwamba  Rais  wa
Jamhuri  ya  Muungano  ana  madaraka  ya  kugawa  nchi  katika  maeneo  ya
kiutawala.   Mabadiliko  ya  Kumi  ya  Katiba  ya  Zanzibar  ya  mwaka  1984
yameitambua  Zanzibar  kuwa  ni  nchi  na  yanampatia    mamlaka  Rais  wa
Zanzibar kuigawa nchi katika maeneo ya kiutawala;
38
(v)  Katiba ya Zanzibar inaeleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mbili
lakini  Katiba  ya  Jamhuri  ya  Muungano  inaeleza  kwamba,  Tanzania  ni  nchi
moja;
(vi)  Masharti  ya  kikatiba  yaliyowekwa  na  Katiba  ya  Zanzibar  kuhusu  mchango
wa  Zanzibar  katika  uendeshaji  wa  Mambo  ya  Muungano  yanapingana  na
masharti ya Katiba ya Muungano.
(vii)  Muundo  wa  Muungano  uliopo  umepoteza  utambulisho  wa  kihistoria  wa
Tanganyika na fursa ya watu wa Tanganyika kutetea maslahi  yao ndani  ya
Muungano;
(viii)  Wananchi  wa  Tanzania  Bara  kutokuwa  na  haki  ya  kumiliki  ardhi  Zanzibar
wakati  wenzao  wa  upande  wa  Zanzibar  wana  haki  ya  kumiliki  ardhi
Tanzania Bara;
(ix)  Wabunge wa Zanzibar huchangia mijadala kwa mambo yasiyo ya Muungano
na  ambayo  kwa  uhakika  wake  ni  mambo  ya  Tanganyika  na  kwamba
Wabunge  wa  Tanganyika  hawana  nafasi  ya  kuchangia  katika  Baraza  la
Wawakilishi kwa mambo yasio ya Muungano yanayohusu Zanzibar; na
(x)  Kwa  mujibu  wa  Sheria  ya  Mzanzibari,  1985,  Watanzania  ambao  ni
Watanzania  wa Bara  hutakiwa kutimiza sifa  maalum  ili  kuweza kupata haki
za kiraia huko Zanzibar ilhali Mzanzibari huweza kupata haki ya kiraia wakati
wowote  na  popote  katika  ardhi  ya  Tanganyika.   Haki  hizo  za  kiraia  ni
pamoja na kugombea uongozi na kupiga kura.
39
Tanganyika kuvaa Koti la Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
122.  Tume iliamua kufanya uchambuzi wa  kina kuhusu baadhi ya malalamiko, hasa
malalamiko  ya  Zanzibar.   Malalamiko  ya  Tanzania  Bara  yanatokana,  kwa  kiwango
kikubwa, na hatua  zilizochukuliwa kwa upande wa Zanzibar. Kama malalamiko ya
Zanzibar  yakipatiwa  ufumbuzi,  malalamiko  ya  Tanzania  Bara  nayo  yatakuwa
yamepatiwa ufumbuzi.
123.  Katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar kwamba  Tanganyika imevaa koti la
Muungano,  Tume  imebaini  kwamba  muundo  wa  Muungano  wa  Serikali  mbili
umeifanya  Serikali  ya  Muungano,  kwa  kiwango  kikubwa,  kushughulikia  zaidi
mambo  ya  Tanzania  Bara,  hasa  mambo  ya  maendeleo.  Kwa  mujibu  wa  Katiba  ya
Jamhuri  ya  Muungano  ya  mwaka  1977,  Serikali  ya  Muungano  ina  mamlaka  ya
kusimamia mambo ya muungano na mambo yasiyo ya muungano kwa upande wa
Tanzania Bara. Kwa msingi huo, Serikali ya Muungano inashughulikia sana mambo
ya  kilimo,  elimu,  afya,  maji,  nishati  na  madini,  ujenzi,  uchukuzi,  maliasili  na  utalii
na mengine ya Tanzania Bara ambayo siyo mambo ya Muungano.
124.  Wakati wa kikao cha Bajeti,  Bunge  la Muungano  hutenga siku mbili au tatu za
majadiliano  kwa  Wizara  zinazosimamia  mambo  haya  ya  Tanzania  Bara  wakati
mambo  ya  Muungano  kama  vile  ulinzi,  mambo  ya  nje  na  mambo  ya  ndani
hutengewa siku moja au nusu siku. Sheria nyingi zinazotungwa na Bunge zinahusu
mambo ya Tanzania Bara.  Maswali ya Wabunge kuhusu mambo ya maendeleo pia
yanahusu  Tanzania  Bara  na  ziara  za  Wabunge  kukagua  miradi  ya  maendeleo
40
zinahusu  Tanzania  Bara  katika  mambo  yasiyo  ya  Muungano.  Ndani  ya  Bunge,
Mambo  haya  yanasimamiwa  na  Waziri  Mkuu  wa  Jamhuri  ya  Muungano  ambaye,
kiuhalisia hana mamlaka wala  madaraka yoyote kuhusu Zanzibar na huwa hafanyi
ziara  Zanzibar  kukagua  shughuli  za  maendeleo.  Hali  hii  ndiyo  imeifanya
Tanganyika kuonekana imevaa koti la muungano.
125.  Hata Rais wa Jamhuri hafanyi ziara za kukagua miradi  ya maendeleo na kutoa
ahadi  kwa  upande  wa  Zanzibar.   Sura  ya  Serikali  ya  Muungano  inaonyesha
kuegemea  zaidi  upande  wa  Tanzania  Bara.   Kati  ya  Wizara  24  ni  wizara  mbili  tu
ndizo  zinashughulikia  mambo  ya  Muungano  pekee.  Wizara  kumi  zinashughulikia
mambo  ya  Tanzania  Bara  na  Wizara  kumi  na  mbili  zinashughulikia  mambo
mchanganyiko  ambayo  mengi  ya  mambo  hayo  yanahusu  Tanzania  Bara.  Kwenye
utawala,  viongozi  wakuu  wengi  wa  Wizara  wanatoka  Tanzania  Bara.   Hivi  sasa  ni
Katibu  Mkuu  mmoja  tu  ndiye  anayetoka  Zanzibar.   Hali  hii  inatokana  na  ukweli
kwamba Serikali ya Muungano inashughulikia zaidi mambo yasiyo ya Muungano na
ndiyo imeifanya Tanganyika kuonekana imevaa koti la Muungano.
126.  Tume imeona hakuna njia ya kubadili hali hii kwa sababu Serikali ya Muungano
haina mamlaka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar.
Mawaziri  na  Serikali  kwa  ujumla,  wanalazimika  kupanga  maendeleo  na  kutafuta
rasilimali  kwa  ajili  ya  Tanzania  Bara  kuliko  kwa  Zanzibar.  Zanzibar  hufanya
mipango yake ya maendeleo,  lakini,  ili kupata rasilimali kama mikopo na misaada,
ni  lazima  Serikali  ya  Zanzibar  ipitie  Serikali  ya  Muungano,  jambo  ambalo
utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi.
41
127.  Njia  pekee  ambayo  ingefanya  maendeleo  ya  Zanzibar  yapewe  uzito  sawa  na
mambo ya Tanzania Bara ni kuyaweka mambo yote ya Zanzibar chini ya Serikali ya
Muungano,  yaani  kuwa  na  Serikali  Moja.  Lakini  kama  nilivyosema,  wakati  wa
kukabidhi  Rasimu  kwa  Marais  wetu,  Muundo  wa  Serikali  Moja  una  changamoto
nzito.   Waasisi  waliona  matokeo  ya  Muundo  huo  ni  Zanzibar  kumezwa  na
Tanganyika.   Tume  ilipokuwa  inakusanya  maoni,  wananchi  wengi,  hasa  Zanzibar,
walionyesha  hofu  hiyo  ni  kubwa  sana  hivi  sasa  kuliko  ilivyokuwa  mwanzoni.  Kwa
hiyo, tathmini ya Tume ni kwamba Muundo wa Serikali moja hauna uhalisia.
Kuongezeka kwa Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
128.  Kwa  muda  mrefu  kumekuwa  na  malalamiko  kutoka  Zanzibar  kwamba
kuongezeka kwa mambo ya Muungano kunapunguza mamlaka ya Zanzibar. Katika
mihadhara mingi iliyofanywa Zanzibar muda mfupi kabla Tume kuanza kazi, baadhi
ya  watoa  mada  walitumia  mizani  kuonyesha  jinsi  ongezeko  la  mambo  ya
Muungano linavyoathiri mamlaka na hadhi ya Zanzibar.
129.  Tume  imefanya  uchambuzi  wa  kina  kuhusu  malalamiko  haya.  Tangu  mwanzo
wa  Muungano,  ilikubalika  kwamba  Zanzibar  ibaki  na  hadhi  yake  na  iwe  na
madaraka  kuhusu  Mambo  yasiyo  ya  Muungano.  Tume  ilifanya  uchambuzi  wa
Mambo  ya  Muungano  ili  kubaini  kama  yanaingilia  hadhi  na  mamlaka  ya  Zanzibar.
Kati  ya  Mambo  22  ya  Muungano,  Tume  imebaini  kuwa  siyo  mambo  yote
yanatekelezwa  kikamilifu  kimuungano.  Mambo  mengi  yamebadilishwa  bila  ya
kubadili  katiba,  ama  kwa  makubaliano  kati  ya  pande  zote  mbili  za  Muungano  au
kwa  hatua  zilizochukuliwa  na  upande  mmoja.  Mambo  ambayo  hayatekelezwi
42
kimuungano  ni  bandari,  leseni  za  viwanda,  utafiti,  takwimu,  biashara  ya  nje  na
maliasili  ya  mafuta  na  gesi.   Lakini  kuna  mambo  mengine  mengi  ambayo
hayatekelezwi kikamilifu. Kwa mfano, mambo yanayohusu uhusiano wa kimataifa,
ulinzi, uchukuzi, Mahakama ya rufani, usafiri wa anga, kodi, posta, simu na uraia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
130.  Katika  kipindi  cha  miaka  ishirini  iliyopita,  kamati  nyingi  zimeundwa
kushughulikia  matatizo  ya  muungano  na  baadhi  yake  zilipendekeza  kuondoa
mambo mengi zaidi kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwa mfano,
Kamati  ya  Amina    ilipendekeza  mambo  yafuatayo  yaondolewe  kwenye  Orodha  ya
Mambo ya Muungano:
(i)  Kodi ya mapato;
(ii)  Mikopo;
(iii)  Misaada;
(iv)  Uhusiano wa Kimataifa;
(v)  Fedha  za  kigeni  na  usimamizi  juu  ya  mambo  yanayohusika  na  fedha  za
kigeni;
(vi)  Mabenki  (pamoja  na  mabenki  ya  kuweka  akiba)  na  shughuli  zote  za
mabenki isipokuwa Benki Kuu ya Tanzania);
(vii)  “off-shore  Banking”  na  utanganzaji  wa  maeneo  huru  ya  uchumi  na
mambo yanayohusiana nayo;
(viii)  Leseni za viwanda;
(ix)  Bandari;
(x)  Usafiri wa Anga;
(xi)  Tawimu (isipokuwa Sensa); na
43
(xii)  Biasahara ya nje (isipokuwa Bodi ya Biashara ya Nje).
131.   Mwaka  2003,  Serikali  ya  Mapinduzi  ya  Zanzibar  iliunda  kamati  nyingine
Kuchambua  Matatizo  na  Kero  za  Muungano  na  Taratibu  za  Kuziondoa.”  Kamati
hiyo  ilipendekeza  mambo  yafuatayo  yaondolewe  kwenye  Orodha  ya  Mambo  ya
Muungano:
(i)  Mafuta na gesi asilia;
(ii)  Elimu ya Juu;
(iii)  Posta;
(iv)  Simu (mawasiliano);
(v)  Biashara ya nje;
(vi)  Kodi ya mapato;
(vii)  Ushuru wa bidhaa;
(viii)  Usafiri wa anga;
(ix)  Takwimu;
(x)  Utafiti;
(xi)  Ushirikiano wa kimataifa;
(xii)  Leseni za viwanda;
(xiii)  Polisi; na
(xiv)  Usalama.
132.  Kama  mambo  haya  yote  yataondolewa  kwenye  Orodha  ya  Mambo  ya
Muungano  basi  Serikali  ya  Muungano  itakuwa  imebaki  na  mambo  ya  Tanzania
Bara tu kwa upande wa maendeleo.
44
133.   Tume  ilitafakari  kama  kuna  uwezekano  wa  kuyarudisha  mambo
yaliyoondolewa  kwenye  orodha  kufuatia  muafaka  wa  1994,  lakini  tathmini  ya
Tume  ni  kwamba  kufanya  hivyo  ni  kuzua  mgogoro  upya  kwani  itaonekana
mamlaka  (autonomy)  ya  Zanzibar  yanaingiliwa.   Wakati  Tume  ilipokuwa
inakusanya  maoni,  wananchi  wengi  wa  Zanzibar  kutoka  makundi  yote  mawili,
yaani wale waliotaka  Muungano wa  Serikali  Mbili na wale waliotaka  Muungano wa
Mkataba,  wote  walipendekeza  mambo  mengi  yaondolewe  kwenye  Orodha  ya
Muungano.  Wale  waliotaka  Muungano  wa  Mkataba  walitaka  mambo  yote
yaondolewe  kwenye  Orodha  ya  Mambo  ya  Muungano  isipokuwa  suala  la  ulinzi.
Wale  waliotaka  Muundo  wa  Serikali  mbili  walitaka  mambo  yote  ya  uchumi
yaondolewe  kwenye  Orodha  ya  Mambo  ya  Muungano.  Katika  hali  hiyo,
kuyarudisha  mambo  ambayo  hivi  sasa  yako  chini  ya  Serikali  ya  Mapinduzi  ya
Zanzibar, hata kama siyo kikatiba, kunaweza kuleta mgogoro wa kisiasa.
Mgongano wa Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti
134.  Eneo  jingine  lenye  matatizo  ni  mgongano  kati  ya  Katiba  ya  Muungano  na
Katiba ya Zanzibar.  Ibara  ya 132 ya  Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka
masharti  kwamba  sheria  zinazotungwa  na  Bunge  la  Jamhuri  ya  Muungano
hazitatumika Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.
135.   Jambo  hili  limeleta  mgongano  wa  Katiba.   Juhudi  zilizofanywa  na  pande  zote
mbili  hazikufanikiwa  kuondoa  mgongano  huo.   Katika  muafaka  wa  mwaka  1994
Serikali zote zilikubaliana kwamba  Zanzibar ifanye mabadiliko kwenye Katiba yake
45
ili  mgongano  huu  wa  Katiba  uondolewe.   Lakini  hadi  sasa  muafaka
haujatekelezwa.  Zaidi  ya  hapo,  mabadiliko  ya  Katiba  ya  Zanzibar  katika  Ibara  ya
kwanza  yaliyofanywa mwaka 2010 yametamka  wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati
ya nchi mbili  zinazounda  Muungano  wakati Katiba ya Jamhuri  inaelekeza  kwamba
Tanzania ni Nchi moja.
136.   Mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya madaraka ya
Serikali  ya  Muungano  kwenda  Zanzibar.  Kwa  mfano,  Katiba  ya  Jamhuri  inampa
Rais  wa  Jamhuri  madaraka  ya  kuigawa  nchi  katika  maeneo.   Lakini  Katiba  ya
Zanzibar imeyahamisha madaraka hayo kwenda kwa Rais wa Zanzibar.
137.   Wakati  wa  kukusanya  maoni  ya  wananchi,  Tume  ilibaini  kwamba  haitakuwa
rahisi  kubadili  Katiba  ya  Zanzibar  kuifanya  Zanzibar  kuonekana  kuwa  sehemu  ya
Jamhuri  ya  Muungano  badala  ya  kuwa  na  sura  ya  nchi.  Mabadiliko  ya  aina  hiyo
yatahitaji kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza. Kwa tathmini ya
Tume, baada ya kuwasikiliza wananchi wa Zanzibar, ni dhahiri kwamba uwezekano
wa kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ili Zanzibar iwe sehemu ya nchi
moja badala ya kuwa nchi, ni mdogo sana.
Michango, Gharama za Muungano na Mgao wa Mapato
Mheshimiwa Mwenyekiti
138.  Matumizi  ya  fedha  na  rasilimali  za  Muungano,  mchango  wa  pande  zote  mbili
kwa  shughuli  za  Muungano  na  mgao  wa  mapato  ya  muungano  yamekuwa  ni
masuala  yenye  utata  kwa  muda  mrefu.   Katika  jitihada  za  kupata  ufumbuzi  wa
46
tatizo hili, mwaka 1977 Halmashauri Kuu ya CCM  ilitoa uamuzi kwamba mapato ya
kodi  za  muungano  yabaki  upande  wa  muungano  yanapokusanywa.  Kwa  msingi
huo,  mapato  ya  kodi  za  muungano  yanayokusanywa  Zanzibar  yabaki  kwenye
Hazina  ya  Serikali  ya  Mapinduzi  ya  Zanzibar  na  yatumike  Zanzibar  badala  ya
kupelekwa kwenye Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na yale mapato ya
kodi  za  Muungano  yanayokusanywa  Tanzania  Bara  yabaki  kwenye  Hazina  ya
serikali  ya  Jamhuri  ya  Muungano  na  yatumike  Tanzania  Bara.   Halmashauri  Kuu
pia ilibadili utaratibu wa kuchangia. Hata hivyo uamuzi huu haukumaliza matatizo.
139.  Zanzibar  kwa  upande  wake  imekuwa  ikidai  kwamba  fedha  na  rasilimali  za
Muungano zinatumika na kuinufaisha Tanzania Bara chini ya kivuli cha muungano.
Aidha,  kwa  upande  wa  Serikali  ya  Muungano  inadaiwa  kwamba  Tanzania  Bara
ndiyo inayochangia fedha na rasilimali nyingi katika muungano hivyo inayo haki ya
kutumia  fedha  na  rasilimali  hizo  kwani  Zanzibar  kwa  muda  mrefu  imekuwa
haichangii katika fedha na rasilimali hizo za muungano.
140.   Kutokana  na  matatizo  hayo,  chombo  maalum  cha  kikatiba  (Tume  ya  Pamoja
ya Fedha) kilianzishwa ili  kushughulikia masuala ya uhusiano wa kifedha baina ya
Serikali ya Muungao na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
141.   Tume  ya  Pamoja  ya  Fedha  ilianzishwa  chini  ya  Ibara  ya  134  ya  Katiba  ya
Jamhuri  ya  Muungano  ya  mwaka  1977  kufuatia  marekebisho  ya  Katiba
yaliyofanywa mwaka 1984. Kwa mujibu wa Katiba  majukumu makubwa ya Tume
ni:
47
(i)  Kuchambua  mapato  na  matumizi  yanayotokana  na,  au  yanayohusu
utekelezaji  wa  Mambo  ya  Muungano  na  kutoa  mapendekezo  kwa  Serikali
mbili kuhusu mchango na mgawo wa kila mojawapo ya Serikali hizo;
(ii)  Kuchunguza  kwa  wakati  wote  mfumo  wa  shughuli  za  fedha  za  Jamhuri  ya
Muungano  na  pia  uhusiano  katika  mambo  ya  kifedha  kati  ya  Serikali  mbili;
na
(iii)  Kutekeleza  majukumu  mengine  ambayo  Rais  ataipatia  Tume  au  kama  Rais
atakavyoagiza, na kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.
142.   Ibara  ya  134  inaelekeza  pamoja  na  mambo  mengine,  kutungwa  kwa  sheria
itakayoweka  utaratibu  juu  ya  uteuzi  wa  Wajumbe  wa  Tume  na  namna  Tume
itakavyotekeleza majukumu yake. Baada ya takriban miaka kumi na mbili kupita,
yaani mwaka 1996, ndipo ilipotungwa Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha.
143.   Miaka saba baada ya kupitishwa Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha au kwa
maana  nyingine  miaka  kumi  na  tisa  baada  ya  Katiba  kuianzisha  Tume  hiyo,
Wajumbe wa kwanza wa Tume waliteuliwa mwaka 2003.
144.  Ripoti ya kwanza ya Tume ya Pamoja ya Fedha ilitolewa mwaka 2006 ambayo
ilihusu  mchango  wa  gharama  za  matumizi  na  mgao  wa  mapato  ya  muungano.
Katika  Ripoti  hiyo,  Tume  ilipendekeza  kiwango  cha  uchangiaji,  utaratibu  wa  kila
Serikali  kuchangia  gharama  za  muungano  na  kiwango  cha  mgao  na  utaratibu  wa
mgawanyo  wa  mapato  ya  muungano  baina  ya  Serikali  hizo.   Aidha,  Tume  ya
Pamoja  ya  Fedha  ilipendekeza  kwamba  masharti  ya  Katiba  yatekelezwe  kwa
48
kuanzishwa  kwa  Akaunti  ya  Fedha  ya  Pamoja  ambapo  fedha  yote  inayohusu
gharama za muungano zitawekwa.
145.   Hadi sasa, huu ni mwaka wa nane tokea mapendekezo hayo kutolewa, hakuna
hata  moja  kati  ya  mapendekezo  hayo  lililotekelezwa  au  kuchukuliwa  hatua.   Kwa
taarifa  ambazo  Tume  ilipewa,  Serikali  ya  Mapinduzi  ya  Zanzibar  imeshayajadili
mapendekezo  hayo  na  kutoa  msimamo  wake.   Serikali  ya  Muungano  imekuwa
ikieleza  kwamba  imo  katika  hatua  ya  kuyafanyia  kazi  na  kutafuta  namna  bora  ya
kuyatekeleza  mapendekezo  hayo  lakini  bado  haijatoa  maoni  yake  kuhusu
mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha.
146.  Tatizo  hili  ni  kubwa  sana.    Serikali  ya  muungano  ndiyo  ina  uwezo  wa
kushughulikia  mambo  ya  fedha  kwa  nchi.   Serikali  hiyo  ina  madaraka  ya  kutoza
kodi  na  kutafuta  mikopo  na  misaada  kutoka  nje.   Serikali  ya  Zanzibar  haina
madaraka hayo bali ni lazima ipitie kwenye Serikali ya muungano. Mgao sahihi wa
mapato  ya  kodi,  mikopo  na  misaada  ungeleta  nafuu  kubwa  kwa  Zanzibar  katika
kuendesha mambo yake na Akaunti ya Fedha ya Pamoja ingeweka wazi mapato na
matumizi kwa mambo ya muungano.
147.  Hivi  sasa,  ni  miaka  thelathini  tangu  Katiba  ilipoianzisha  Tume  ya  Pamoja  ya
Fedha,  ni  miaka  kumi  na  nane  tangu  Sheria  ya  Kuanzisha  Tume  ya  Pamoja  ya
Fedha  ilipotungwa,  na  ni  miaka  kumi  na  moja  tangu  Tume  hiyo  ilipoundwa.   Ni
miaka minane tangu Tume ya Pamoja ya Fedha ilipotoa mapendekezo ya kiwango
cha  uchangiaji,  utaratibu  wa  kuchangia,  kiwango  cha  mgao  na  utaratibu  wa
49
mgawanyo  wa  mapato  ya  muungano.   Zaidi  ya  hapo  hadi  sasa  Akaunti  ya  Fedha
ya Pamoja haijaanzishwa.
148.  Tathmini  ya  Tume  ni  kwamba  siyo  rahisi  mambo  haya  kutekelezwa  chini  ya
muundo  wa  Serikali  mbili.  Hii  ni  kwa  sababu,  Wizara  za  Serikali  ya  Muungano  ni
mchanganyiko.  Zipo  wizara  ambazo  zinashughulikia  mambo  ya  Muungano  tu  na
zipo  wizara zinazoshughulikia  mambo ya  Tanzania Bara  pekee. Aidha,  zipo  wizara
zinazoshughulikia  mambo  mchanganyiko,  yaani  mambo  ya  Muungano  na  Mambo
yasiyo  ya  Muungano  kwa  upande  wa  Tanzania  Bara.  Katika  mazingira  hayo,
haiwezekani kujua kwa uhakika gharama zipi ni za Mambo ya Muungano  na zipi ni
za Mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara.
149.  Wizara  zinazoshughulikia  mambo  mchanganyiko  ni  pamoja  na  Ofisi  ya  Rais,
Ofisi  ya  Makamu  wa  Rais,  Ofisi  ya  Waziri  Mkuu,  Wizara  ya  Ulinzi  na  Jeshi  la
Kujenga  Taifa,  Wizara  ya  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi,  Wizara  ya  Katiba  na  Sheria,
Wizara  ya  Fedha,  Wizara  ya  Elimu  na  Vyuo  vya  Ufundi,  Wizara  ya  Mawasiliano,
Wizara  ya  Biashara  na  Viwanda,  Wizara  ya  Nishati  na  Madini  Wizara  ya  Uchukuzi
na  Wizara  ya  Ushirikiano  wa  Afrika  Mashariki.    Katika  hali  hiyo  ni  vigumu  kujua
kwa  mfano  ni  gharama  zipi  za  shughuli  za  Rais  ni  za  Muungano  na  zipi  ni  za
Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
150.  Mambo manne niliyoyaeleza ndiyo msingi wa kupendekeza muundo wa Serikali
tatu.   Kwa  muda  mrefu  Zanzibar  imelalamika  kwamba  Tanganyika  imejificha
50
kwenye koti la Muungano na ndiyo inafaidi. Pamoja na  kwamba kuna mawaziri na
wabunge  wanaotoka  Zanzibar,  Serikali  ya  Zanzibar  imekuwa  inalalamika  kwamba
haishirikishwi kwenye maamuzi ya  Muungano. Hata wakati ambapo Rais ametoka
Zanzibar haitoshi kuona kama Zanzibar ni sehemu ya Serikali ya Muungano.
151.  Wakati  Tume  ilipokuwa  inakusanya  maoni  ilikuwa  jambo  la  kawaida  kusikia
wananchi  wa  Zanzibar,  na  hata  viongozi  wao,  wakizungumzia  Serikali  ya  Bara
badala ya Serikali ya Muungano.
152.  Orodha ya mambo ya Muungano ni suala ambalo  pia  limelalamikiwa kwa muda
mrefu  na  hatua  zilizochukuliwa  ni  kuyapunguza  mambo  ya  Muungano,  ikiwa  ni
pamoja  na  yaliyoorodheshwa  kwenye  makubaliano  ya  Muungano  (Articles  of
Union).  Kwa  mfano  Bandari  na  Biashara  ya  Nje.  Suala  la  mahusiano  ya  kifedha
nalo  limekuwa  na  utata  kwa  muda  wa  karibu  miaka  arobaini.   Kiini  chake  ni
malalamiko ya kutoka kila upande kuhusu nani anafaidi rasilimali za taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
153.   Azimio  la  Halmashauri  Kuu  ya  CCM  la  1994,  lililenga  kubaki  na  Muundo  wa
Serikali  mbili  kwa  lengo  la  kwenda  kwenye  Muundo  wa  Serikali  moja.  Lengo  la
uamuzi huu ilikuwa kuzuia madai ya Serikali tatu ambayo yalikuwa yanatolewa na
pande  zote  mbili.  Lakini  hatua  zilizochukuliwa,  tena  kuanzia  mwaka  huo  huo,
zilikuwa zinaelekea kwenye muundo wa Serikali tatu.
154.  Mwaka 1994, Serikali zote mbili zilifikia muafaka kuondoa mambo mengi kutoka
kwenye  orodha  ya  Muungano.   Katiba  ya  Zanzibar  imebadilishwa  kwa  msingi  wa
51
kutambua nchi mbili zinazounda Muungano. Mwelekeo wa hatua hizo siyo kwenda
kwenye Muundo wa Serikali moja bali kwenda Serikali tatu.
155.  Ripoti  ya  2003  iliyotayarishwa  na  Kamati  ya  kuchambua  “Matatizo  na  Kero  za
Muungano  na  Taratibu  za  Kuziondoa,”  iliyoundwa  na  Serikali  ya  Mapinduzi  ya
Zanzibar, inaeleza kwamba;
“Matatizo  makubwa  yaliopo  kwa  upande  wa  sheria  ni  kuwa  Zanzibar
haina kauli juu ya Sheria zinazohusu mambo ya Muungano. Kwa mujibu
wa  Katiba  ya  Muungano,  sheria  zote  hupitishwa  kwa  wingi  wa  kura
isipokuwa  sheria  ya  marekebisho  ya  Katiba  na  sheria  kuhusu  mambo
yaliyoelezwa katika Jedwali la Pili, Orodha ya pili. Mambo hayo ni 8 tu
na kati ya hayo 5 tu ndio mambo ya Muungano.
Kutokana na kasoro hii, wananchi wa Zanzibar wamekosa haki ya msingi
ya kujitawala nayo ni ya kupitisha sheria kwa ridhaa yao. Hii ni  kasoro
kubwa  sana  katika  mfumo  wowote  ule  wa  utawala.   Kwa  upande
mwingine,  wananchi  wa  Tanzania  Bara  nao  wanalalamika  kwamba
Wabunge  wa  Zanzibar  wanashiriki  katika  kuamua  mambo  ya  Bara
ambayo  si  ya  Muungano.   Ni  ukweli  ulio  wazi  kwamba  mchango  wa
Wabunge  wa Zanzibar katika mambo ambayo si ya Muungano ni mdogo
mno kama upo.
Kwa  sababu  zilizoelezwa  hapo  juu  Kamati  inapendekeza  njia  mbili
muhimu zifuatazo:-
52
1)  Bunge  la  Jamhuri  ya  Muungano  lipitishe  mambo  yake  kwa
utaratibu wa idadi maalum ya Wabunge kutoka pande zote mbili.
Kama ni  sheria inayohitaji  kupitishwa kwa “simple majority” iwe
ni ya kila upande au  sheria  inayohitaji  masharti ya theluthi mbili
iwe ni kwa kila upande.
2)  Bunge la Jamhuri ya Muungano liwe na mabaraza mawili: Baraza
la  Juu  na  Baraza  la  Chini.   Baraza  la  Juu  lipitishe  mambo  ya
Muungano na Baraza la Chini lipitishe masuala ya Tanzania Bara.”
156.   Baraza  la  Wawakilishi  la  Zanzibar  nalo  limetoa  mapendekezo  ambayo  kwa
tafsiri  yake  yanaelekea  kupendekeza  muundo  wa  Serikali  Tatu.   Katika  Waraka
uliowasilishwa  kwenye  Tume  mwezi  Februari  2013,  pamoja  na  mambo  mengine,
Baraza la Wawakilishi lilitoa maoni  yafuatayo:
“Kwa sababu Wazanzibari ni waumini wa Muungano ambao haukuondoa na
hautoondoa uwepo wa Zanzibar kama nchi, ni vyema Katiba ya Jamhuri ya
Muungano  wa  Tanzania  ijayo  iweke  wazi  kuwa  Tanzania  ni  Jamhuri  ya
Muungano inayotokana na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar.   Hali  hii  itahakikisha  kuwepo  na  maeneo  maalum  ya  mamlaka
ambayo  Zanzibar  ina  uwezo  nayo  kama  nchi  (yaani,  Mamlaka  ya  Dola  ya
Zanzibar).
Kwa  sababu  inapendekezwa  kuwepo  na  Mamlaka  ya  Zanzibar  huru  na
Mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Jamhuri ya Muungano, Mamlaka ya
Muungano iwekwe wazi –  maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji
wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake.
53
Uwepo wa Muungano uonekane katika hali zote – uundwaji wa Mamlaka za
Muungano,  ufanyaji  kazi  katika  Mamlaka  za  Muungano,  ufanyaji  wa
maamuzi  katika  Mamlaka  za  Muungano,  na  uingizwaji  na  upunguzwaji
katika orodha wa mambo ya Muungano.
Kwa  mfano,  maamrisho  kama  yaliyopo  sasa  kwenye  Ibara  ya  64(4)  ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, ambayo yanawezesha
jambo  kufanywa  la  Muungano  bila  ya  kuishirikisha  katika  maamuzi
Mamlaka  ya  Zanzibar,  yasiwe  na  nafasi  tena  ya  kutokea  kwa  mujibu  wa
Katiba ijayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Utungaji wa sera na sheria za Muungano isiwe ni jambo la kuzingatiwa na
kutekelezwa  na  Mamlaka  za  Muungano  pekee.   Kama  tulivyoelezea  hapo
awali  kuwa  uwepo  ushirikishwaji  wa  sehemu  (Dola)  mbili  huru  katika
kufanya maamuzi na uendeshaji wa Mamlaka ya Muungano. Ushirikishwaji
huo  ni  lazima  udhihirike  katika  maamuzi  yatakayopelekea  kuundwa  kwa
sera na sheria zote za mambo ya Muungano.
Jambo  kubwa  zaidi  ya  yote  linalohitajika  lionekane  kwa  maneno
(maamrisho ya Katiba) na vitendo ni haja ya kuwa na Muungano wa kweli,
hata  kama  ni  kwa  maeneo  machache,  kwa  dhati  ya  wanasiasa  na
watanzania kwa jumla. Hali hii inaweza kupatikana kwa kuzingatia Misingi
ya Katiba iliyoainishwa hapo juu ambayo yanaweka mkazo juu ya haki na
maslahi ya  pande mbili za  Muungano ya  kujiamulia  hatma  za  mambo  yao
yote, ya kiuchumi, ya kijamii na ya kisiasa.
54
Kuhusu muundo unaohitajika katika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano,
Baraza  la  wawakilishi  halikufikia  maamuzi  maalum.   Katika  mtazamo  wa
Baraza  kama  taasisi,  Muungano  wa  Tanzania  unaweza  kuchukua  muundo
wowote kwa kuzingatia misingi ya Katiba iliyoelezewa hapo juu”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
157.   Kwa  Tahmini  ya  Tume,  Muundo  wa  Serikali  mbili  hauwezi  kubaki  kwa  hali  ya
sasa.  Muungano  wa  Serikali  mbili  waliotuachia  waasisi  siyo  uliopo  sasa.
Umebadilishwa  mara  nyingi,  wakati  mwingine  bila  ya  kufanya  mabadiliko  kwenye
Katiba.  Waasisi  walituachia  Muungano  wa  Nchi  Moja  yenye  Serikali  Mbili,  na  siyo
Nchi Mbili zenye  Serikali Mbili.    Muundo wa  Serikali Mbili unaweza kubaki  tu kama
orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali itaongezwa. La sivyo, Serikali
ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu. Katika hali hiyo,
pande zote mbili zitaendelea kulalamika.  Kwa upande, mmoja Zanzibar itaendelea
kulalamika  kwamba  Tanzania  Bara  imevaa  koti  la  Muungano  kwa  faida  yake,  na
kwa  upande  mwingine,  Tanzania  Bara  itaendelea  kulalamika  kwamba  mambo
yasiyo  ya  Muungano  ya  Tanzania  Bara  na  rasilimali  zake  ndizo  zimekuwa
Muungano.
158.  Kwa  kipindi  cha  miaka  thelathini,  kumekuwepo  hoja  za  muundo  wa  Serikali
tatu. Chanzo cha kuchafuka kwa hali ya hewa  ya  kisiasa Zanzibar ilikuwa ni hoja
ya muundo wa Serikali tatu. Tume ya Jaji Nyalali ilikuwa na hoja hiyo. Hoja ya G
55  ilikuwa  ni  kuundwa  kwa  Serikali  ya  Tanganyika.  Kamati  ya  Jaji  Kisanga  nayo
ilipendekeza  muundo  wa  Serikali  tatu.   Tume  pia  imepata  hoja  hiyo  kutoka  kwa
wananchi wakati wa kuratibu na kukusanya maoni.
55
159.   Lakini  la  muhimu  zaidi  ni  kwamba  matendo  katika  kipindi  hicho  cha  miaka
thelathini.   Hatua  ambazo  zimechukuliwa  zimefanya  mamlaka  na  madaraka  ya
Serikali  ya  Muungano  yapungue  sana  na  mamlaka  na  madaraka  ya  Zanzibar
kuongezeka.   Vivyo  hivyo,  mamlaka  ya  Zanzibar  yameongezeka  kiasi  kwamba
Serikali  ya  Muungano  imebaki  ikishughulikia  mambo  ya  Tanzania  Bara  tu  kwa
upande wa maendeleo.
160.   Jambo  kubwa  zaidi  katika  kuchukua  hatua  hizi  ni  kuvunjwa  kwa  Katiba.   Hili
siyo  jambo  dogo.   Kama  Katiba  haitaheshimiwa  nchi  haitakuwa  salama.
Mapendekezo  ya  Tume  yanalenga  kuondoa  matatizo  yanayohatarisha  kuyumba
kwa muungano,  ili kuzuia pande zote mbili  kuendelea kuchukua hatua  zinazovunja
Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
161.   Muundo  wa  Serikali  tatu  haupunguzi  uimara  wa  Muungano.   Muungano  huu
siyo  Muungano  wa  Serikali  ama  Viongozi  bali  ni  muungano  wa  nchi  mbili  kwa
manufaa ya wananchi. Faida kubwa iliyopatikana katika miaka hamsini iliyopita ni
kuungana kwa wananchi.
162.   Njia  kuu  ya  kuimarisha  muungano  ni  kuzingatia  haki  za  raia.   Kudumu  na
kuimarika  kwa  muungano  kunategemea  jinsi  wananchi  wanavyofaidika  katika
juhudi zao za kujiletea maendeleo.
56
163.   Rasimu  imependekeza uraia mmoja. Rasimu  pia imependekeza orodha ndefu
ya  haki  za  binadamu.   Lengo  la  mapendekezo  haya  ni  kumwezesha  mwananchi
kupata  haki  zake  kama  raia  bila  vikwazo.   Kisiasa  atakuwa  na  haki  ya  kwenda
mahali  popote  katika  nchi  na  kushiriki  katika  shughuli  za  utawala  bila  kujali  asili
yake  ni  upande  upi  wa  nchi.   Kama  anataka  kugombea  nafasi  yoyote  mahali
anapoishi  awe  na  haki  hiyo.   Awe  pia  na  haki  ya  kupiga  kura  ya  kumchagua
mwenyekiti wa kijiji, au mtaa, diwani, mbunge na rais.
164.  Kiuchumi,  bila  kujali  orodha  ya  Mambo  ya  Muungano,  raia  awe  na  haki  ya
kufanya  shughuli  zake  bila  ubaguzi.   Kama  anahitaji  ardhi  apewe  kama  raia  bila
kikwazo  cha  asili  yake.   Hivyo  hivyo,  katika  kufanya  biashara  na  katika  kupata
ajira,  mwananchi  asizuiwe  kufanya  kazi  mahali  popote  alipo  kwa  sababu  ya  asili
yake.
165.  Kijamii,  mwananchi  ana  haki  ya  kupata  huduma  popote  alipo  bila  kujali  asili
yake. Kwa mfano,  ingawa elimu siyo suala la  Muungano, mwananchi awe na haki
yake  kama  raia  kupata  elimu  mahali  popote  na  kwa  ngazi  yoyote.    Huduma  ya
afya  nayo  iwe  hivyo  hivyo.   Kama  kuna  ulazima  wa  mwananchi  kuhamishiwa
hospitali  ya  upande  mmoja  wa  muungano  kwenda  hopitali  ya  upande  mwingine
wa  muungano,  mwananchi  huyo  apewe  haki  yake  kama  raia.   Kama  kukitokea
ubaguzi  wa  raia  kinyume  na  haki  za  uraia  wananchi  wataanza  kulalamika  na
kubaguana  wenyewe  kwa  wenyewe.   Likitokea  hilo,  muungano  wa  muundo
57
wowote  ule  utayumba.   Hivyo,  ni  jambo  la  lazima  Serikali  zote  kulinda  kikamilifu
haki za raia.
Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
166.  Muundo  wowote  wa  Serikali  utakuwa  na  changamoto  zake.   Waasisi  waliona
changamoto za Serikali moja, yaani Zanzibar kumezwa na Tanganyika. Hali ni hiyo
hadi  sasa.   Muundo  wa  Serikali  Mbili  umekuwa  na  changamoto  nyingi  ambazo
zimekuwa kero na msingi wa malalamiko mengi kuhusu muungano, na hata Katiba
kuvunjwa.
167.  Kwa maana hiyo, Muundo wa Serikali tatu utakuwa na changamoto zake. Moja
ni  gharama  kuongezeka.   Ongezeko  hilo  halitakuwa  kubwa  sana  kama
inavyofikiriwa.  Gharama kubwa kwa shughuli za Muungano ni katika eneo la ulinzi
na  usalama,  yaani  jeshi  la  wananchi,  polisi,  usalama  wa  taifa  na  mambo  ya  nje.
Gharama hizo hazibadiliki, zinabaki   zile zile bila kujali kama ni Muundo wa Serikali
Mbili au  Serikali  Tatu. Gharama zitaongezeka kwenye utawala. Tume ililiona hilo
na ndiyo maana imependekeza Serikali ndogo.
168.   Bunge  lililopendekezwa  katika  Rasimu  ya  Katiba  nalo  ni  dogo.   Hivi  sasa,
Bunge  la  Muungano  lina  wabunge  357  na  Baraza  la  Wawakilishi  Zanzibar  lina
Wawakilishi  81,  jumla  ni  438.  Wabunge  wanaotoka  Zanzibar  ni  77  ambao
wasipokuwepo  kwenye  Bunge  la  Muungano  watabaki  wabunge  280  wa
Tanganyika.   Wabunge  wa  mabunge  matatu  watakuwa  ni  wachache  kuliko
wajumbe  wa  mabunge  mawili  ya  sasa.   Tume  inategemea  mabunge  ya  Nchi
58
Washirika yatapunguza wabunge wake ili  kupunguza gharama, hasa wabunge wa
kuteuliwa. Hivi sasa, Wabunge wa kuteuliwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
ni  10,  ukiongeza  na  Wajumbe  5  wa  Baraza  la  Wawakilishi  wanakuwa  jumla  15.
Wajumbe  wa  kuteuliwa  katika  Baraza  la  Wawakilishi  nao  ni  10.  Hivyo,  jumla  ya
Wajumbe  wote  hao  ni  25.  Kwa  kufuata  mapendekezo  ya  Rasimu  ya  Katiba,  upo
uwezekano  mkubwa  kupunguza  idadi  wa  Wabunge  katika  Mabunge  ya  Nchi
Washirika na hatimaye kupunguza gharama za kuendesha Mabunge hayo.
169.  Gharama  zitakazoongezeka  ni  za  kawaida  ambazo  haziwezi  kuepukika
inapokuwa  ni  lazima  kuleta  ufanisi  wa  mfumo  wa  utawala  katika  mazingira  ya
muungano wa  nchi zilizokuwa huru hapo mwanzoni. Lakini  pia,  tangu Muungano
uundwe,  kila  Serikali  kati  ya  Serikali  zetu  mbili,  zimekuwa  zikiongeza  wizara,
mikoa,  wilaya  na  taasisi  mbali  mbali  za  kiutawala  ili  kuleta  ufanisi  na  hivyo
kuongeza matumizi ya Serikali. Hivyo,  suala la kuongezeka kwa matumizi ni suala
la  lazima  katika  kuongeza  ufanisi  hasa  katika  enzi  hizi  za  ushiriki  zaidi  wa
wananchi.   Vilevile,  ni  suala  la  kawaida  kuendana  na  kukua  kwa  majukumu,
dhamana na ukubwa wa nchi.
170.   Suala  la  matumizi  katika  mfumo  wa  Serikali  zetu  ni  suala  la  utamaduni  wa
matumizi  kuliko  kuwa  suala  la  muundo  wa  muungano.   Katika  Rasimu,  Tume
imependekeza  mfumo ambao utaweza kudhibiti na kujenga nidhamu ya matumizi
ya  fedha  na  mali  za  umma.   Kwa  kuwa  Katiba  za  Nchi  Washirika  zinapaswa
kufuata misingi  iliyomo katika  Katiba ya Muungano, basi ni  wazi mfumo mpya wa
kikatiba  utajenga  mazingira  yatakayowezesha  kupunguza  matumizi  yasiyo  ya
lazima  kwa Serikali zote tatu  pamoja na  kuziba mianya ya matumizi yasiyo na tija
59
kwa  taifa,  ambayo  ndiyo  chanzo  kikubwa  cha  matumizi  makubwa  katika
kuendesha Serikali zetu.
171.   Changamoto  ya  pili  ni  uhakika  wa  mapato  kwa  Serikali  ya  muungano.   Tume
imependekeza  kodi  ya  bidhaa  iwe  ya  muungano,  na  pia  mapato  yasiyo  ya  kodi,
mikopo na michango ya Nchi Washirika.
172.   Ushuru  wa  bidhaa  utakidhi  sehemu  kubwa  ya  gharama  za  muungano.
Sehemu  inayobaki  itachangiwa  na  nchi  washirika.   Utaratibu  na  viwango  vya
michango  utawekwa  na  bila  shaka  utaratibu  huo  utazingatia  ukubwa  wa  uchumi,
idadi  ya  watu  na  ukubwa  wa  eneo.  Katika  muungano  wowote  ule,  mchango
unategemea, pamoja na mambo mengine, uwezo na wakati wote uchumi mkubwa
unaubeba uchumi mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
173.  Changamoto  nyingine  ni  nchi  mojawapo  kutenda  kinyume  na  Katiba  ya
muungano.   Lakini  hili  halitokani  na  muundo.   Chini  ya  muundo  huu  wa  Serikali
mbili,  Katiba  imevunjwa.   Tume  imeona  hilo  na  ndiyo  maana  imependekeza
utaratibu  wa  kuzuia  hilo,  ikiwa  ni  pamoja  na  kuanzisha  Tume  ya  Uhusiano  na
Uratibu pamoja na kuipa madaraka Mahakama ya Juu kuamua migogoro.
174.  Kwa  upande  wa  matatizo  ya  kiutendaji  Tume  imependekeza  muundo  wa
Serikali tatu ujengwe kwenye misingi minne ya utendaji. Misingi hiyo ni muungano
wa hiyari, ushirikiano, mshikamano na kutegemeana.
60
175.  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  ni  Muungano  wa  iliyokuwa  Jamhuri  ya
Tanganyika na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Msingi wa Muungano huu
ni Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ya mwaka 1964 yaliyofikiwa baina
ya  mataifa  haya  mawili.   Chini  ya  makubaliano  hayo,  mataifa  hayo  yalikubaliana
kwa  hiyari  kuachia  baadhi  ya  mamlaka  na  kuyapeleka  mamlaka  hayo  kwenye
Serikali  ya  Muungano.   Uhiyari  huu  wa  kukubali  kuungana  kwa  mataifa  haya
mawili  ni  moja  ya  misingi  ya  utekelezaji  wa  muundo  wa  Muungano
unaopendekezwa  wa  Serikali  Tatu.   Ibara  ya  1  (3)  ya  Rasimu  ya  Katiba
inapendekeza, pamoja na mambo mengine, Hati ya Muungano iwe ni msingi mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
176.   Msingi  mwingine  wa  utendaji  katika  muundo  wa  Serikali  Tatu  ni  Ushirikiano.
Chini ya msingi huu, Serikali ya Muungano na  Serikali za Nchi Washirika zitakuwa
na ushirikiano baina yao katika shughuli zote za utendaji na uendeshaji wa nchi ili
mradi  ushirikiano  huo  haukiuki  Katiba.   Ibara  ya  65(1)  inapendekeza  kuwa  Nchi
Mshirika inaweza kuomba ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa
ajili  ya  kufanikisha  uhusiano  wake  wa  kikanda  na  kimataifa.   Aidha,  Ibara  ya  66
inapendekeza  masharti  kuhusu  ushirikiano  kati  ya  Nchi  Washirika  zenyewe  na
baina  ya  Nchi  hizo  na  Serikali  ya  Muungano  kwa  lengo  la  kukuza  na  kulinda
maslahi ya Taifa na kukuza maendeleo ya wananchi.
177.  Katika  mfumo  wa  Serikali  Tatu,  uratibu  wa  uhusiano  baina  ya  Serikali  hizo  ni
moja  ya  misingi  muhimu.   Ibara  ya  67  inapendekeza  kuwepo  kwa  Waziri  Mkaazi
atakayeteuliwa  na  kila  Nchi  Mshirika  atakayefanya  kazi  akiwa  Makao  Makuu  ya
Serikali ya Muungano. Moja ya majukumu ya msingi ya Waziri Mkaazi ni kuratibu
61
uhusiano  baina  ya  Serikali  yake  na  Serikali  ya  Muungano.   Aidha,  Ibara  ya  109
inapendekeza  kuanzishwa  kwa  Tume  ya  Uhusiano  na  Uratibu  wa  Serikali  chini  ya
uenyekiti  wa  Makamu  wa  Rais.   Kuwepo  kwa  uratibu  kutaimarisha  uhusiano  wa
kiutendaji baina ya Serikali na hivyo kuimarisha Muungano.
178.   Mshikamano (Solidarity) ni  moja ya misingi muhimu ya utendaji katika mfumo
wa  shirikisho.   Msingi  huu  umezingatiwa  katika  Rasimu  inayopendezwa  ili
kuhakikisha  kuwa  Serikali  zote  tatu  zinashikamana  na  kusaidiana  katika  kila  hali
inayoweza  kujitokeza.   Mathalani,  Ibara  ya  62(3)  inapendekeza  kuipa  Serikali  ya
Muungano,  kwa  makubaliano  na  masharti  maalum  na  Serikali  ya  Nchi  Mshirika,
madaraka  ya  kutekeleza  jambo  lolote  lililo  chini  ya  mamlaka  ya  Serikali  ya  Nchi
Mshirika. Aidha,  Ibara  ya  65 na  66 zinapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina
ya  Serikali  za  Nchi  Washirika  na  kati  ya  Serikali  hizo  na  Serikali  ya  Muungano.
Msingi  huu  ni  muhimu  katika  kuhakikisha  kuwa  wananchi  wa  pande  zote  mbili  za
Muungano wananufaika kwa usawa na mshikamano baina ya Nchi Washirika.
179.   Msingi  wa  kutegemeana  unakusudia  kuweka  utaratibu  wa  mamlaka  za  chini
kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya uwezo wake ikiwa mamlaka hizo zina uwezo
wa  kutekeleza  majukumu  hayo  kwa  ukamilifu.   Msingi  huu  wa  kutegemeana
unaruhusu mamlaka ya juu kutekeleza jambo ambalo kwa kawaida hutekelezwa na
mamlaka  ya  chini  iwapo  mamlaka  ya  juu  ina  uwezo  wa  kutekeleza  jambo  husika
kwa ufanisi au vinginevyo.  Ibara  ya 65 na  66 zimeweka msingi kwamba, ingawa
Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kushughulikia Mambo ya Muungano,
Serikali  hiyo,  kwa  ridhaa  ya  Serikali  ya  Nchi  Mshirika,  itakuwa  na  mamlaka  ya
62
kushughulikia  masuala  yasiyo  ya  Muungano  katika  Nchi  Mshirika.   Msingi  huu
utasaidia kuimarisha utendaji katika muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
180.   Muungano,  pamoja  na  matatizo  yote  tuliyonayo,  umedumu  kwa  miaka
hamsini. Kuna hofu kwamba muundo wa Serikali tatu utavunja Muungano. Baada
ya kutafakari kwa kina Tume inaamini hakuna msingi wa hofu hii.
181.  Waasisi  walikubaliana  orodha  fupi  ya  mambo  ya  Muungano,  hasa  yale  ya
kidola. Hakukuwa na sharti kwamba Muungano utakuwepo tu kama mambo yote
ya  Tanganyika  yatawekwa  chini  ya  Muungano.   Ni  Tanganyika  kwa  hiyari  yake
ilikubali  mambo  yake  yote  yawe  kwenye  mamlaka  ya  Serikali  ya  Muungano.
Sababu  za  kufanya  hivyo  zilikuwa  mbili.   Sababu  ya  kwanza  ilikuwa  kupunguza
gharama  na  sababu  ya  pili  ilikuwa  matumaini  kwamba  siku  ambayo  hakutakuwa
na  hofu  ya  Zanzibar  kumezwa  na  Tanganyika,  basi  tungekuwa  na  Serikali  moja
badala ya Serikali mbili. Hali  halisi  ilivyo hivi sasa  inaonyesha kwamba hatutafikia
azma ya kuwa na Serikali moja.
182.  Kuingiza  mambo  ya  Tanganyika  kwenye  Serikali  ya  Muungano  ndicho  chanzo
kikubwa  cha  matatizo  tuliyonayo.   Sababu  kubwa  ya  Zanzibar  kudai  mambo  ya
Muungano  yapunguzwe  ni  kutokana  na  hisia  kwamba  Serikali  ya  Muungano
inaonekana ni Serikali ya Tanganyika.
183.   Hali  hii  inapunguza  uzalendo  na  kuchochea  utaifa.   Kwa  miaka  hamsini
wananchi  wameungana  na  wameimarisha  udugu,  umoja  na  mshikamano  wao.
Nchi  imejenga  taasisi  ambazo  zimezoea  kufanya  kazi  kwa  pamoja  na  viongozi  pia
63
wamejenga  utamaduni  wa  kufanya  kazi  kwa  pamoja.   Mambo  yote  haya
yamejenga utamaduni wa  taifa na kukuza uzalendo. Madhumuni ya kupendekeza
muundo  wa  Serikali  tatu  ni  kuondoa  kero  ambazo  zinahatarisha  umoja,  uzalendo
na mshikamano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
184.   Mwisho  naomba  kutoa  shukrani  zangu  binafsi  kwa  Watumishi  wa  Sekretarieti
ya  Tume  na  Wajumbe  wenzangu.   Tume  imekamilisha  kazi  yake  kwa  muda
ulipangwa  kutokana  na  kazi  nzuri  ya  Sekretarieti.  Wakati  Wajumbe  wa  Tume
walipokuwa  wanakusanya maoni mikoani,  Watumishi  wa Sekretarieti waliofuatana
na  Wajumbe,  walifanya  kazi  kwa  muda  mrefu  sana,  hata  siku  za  mapumziko.
Walikuwa  wa  kwanza  kuamka  na  wa  mwisho  kwenda  kulala.   Walihakikisha
kwamba  kila  neno  lililosemwa  na  mtoa  maoni  limewekwa  kwenye  kumbuk umbu.
Madereva nao walifanya kazi za ziada hata wakati walipokuwa wamechoka.
185.  Watumishi  waliobaki  Ofisini,  kila  mmoja  wao  na  kwa  ujumla  wao,  walifanya
kazi  kwa  kujituma  sana  na  waliweza  kuziweka  pamoja  kumbukumbu  zilizotoka
mikoani  na  kufanya  maandalizi  ya  vikao  vya  wajumbe  wa  Tume.   Kazi  hii
waliifanya kwa haraka lakini kwa umakini mkubwa. Nawashukuru sana.
186.  Nawashukuru sana Wajumbe wenzangu wa Tume, ikiwa ni pamoja na  Makamu
Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa Tume. Baada ya kuteuliwa na kuapishwa
na Mheshimiwa Rais, mimi kama Mwenyekiti, nilikuwa na wasiwasi mkubwa kama
tungeifanya kazi yetu kwa ufanisi na kwa wakati.
64
187.    Tulikuwa  katika  makundi  ya  kutoka  Tanzania  Bara  na  Tanzania  Zanzibar.
Tulikuwa tumeteuliwa kutokana na mapendekezo ya makundi mbali mbali,  Vyama
vya  Siasa,  Jumuiya  za  Dini,  Asasi  za  Kiraia,  Wanaharakati,  Wanauamsho  na
kadhalika.   Tulikuwa  na  muono  tofauti,  itikadi  tofauti,  misimamo  tofauti  na  imani
tofauti. Ilionekana dhahiri kuwa kazi yetu ingekuwa ngumu.
188.   Bahati  nzuri  wenzangu  wote  walitambua  changamoto  hiyo.   Mapema  kabisa
tulitambua  kwamba  jukumu  letu  ni  kulitumikia  taifa,  siyo  makundi
yaliyotupendekeza  au nafsi zetu. Tulikusanya maoni ya wananchi kwa msingi huo
bila kuchakachua. Mijadala yetu ilikuwa ya uwazi na ukweli.
189.  Hata  tulipopata  matatizo  ya  kufikia  uamuzi  kwa  suala  lolote  hatukukimbilia
kupiga  kura.   Tulijifungia  kwenye  vikundi  vya  watu  wenye  mawazo  kinzani  na
mwisho  tukafikia  maridhiano  na  muafaka.   Dira  yetu  ilikuwa  Maslahi  ya  Taifa.
Hatukupiga  kura  hata  mara  moja  kwa  jambo  lolote  wala  kuwa  na  mawazo
mbadala.   Kila  Ibara  iliyomo  kwenye  Rasimu  ya  Katiba  ambayo  ninaiwasilisha
katika Bunge Maalum la Katiba, inaungwa mkono na kila mmoja wetu.
190.  Hiyo haina maana  kwamba  kila mmoja wetu ameacha  imani  yake, itikadi yake
na  msimamo  wake.   Kuna  mambo  ambayo  kila  mmoja  wetu  amebaki  na  imani
yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini
muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini  Muundo wa Serikali  Mbili, tupo
tunaoamini  Serikali  Tatu  na  tupo  tunaoamini  Muungano  wa  Mkataba.
Tunachoamini  wote  kwa  pamoja  ni  umuhimu  wa  kuendelea  kuwepo  na  kudumu
kwa Muungano. Baada ya kuwasikiliza wananchi, dira yetu imekuwa ni maslahi ya
Taifa na siyo maslahi ya makundi yetu au nafsi zetu. Nawashukuru sana wajumbe
65
wenzangu  wa  Tume  kwa  kusimamia  misingi  ya  kiutendaji  ambayo  imetuwezesha
kukamilisha kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
191.  Baada  ya  kusema  hayo  nimalizie,  kwa  niaba  ya  Tume,  kukutakia  wewe  na
Waheshimiwa Wabunge kheri na fanaka katika kazi yenu muhimu.  Jukumu lenu ni
kubwa na lina ugumu wake. Lakini,  tunaamini  mnao uwezo wa  kufanya kazi yenu
kwa  ufanisi,  na  mwisho,  mtakubaliana  kupendekeza  Katiba  ambayo  itakidhi
matakwa ya wananchi na kuendelea kuliunganisha taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Naomba kuwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.