Tuesday, January 6, 2015

Jifunze chanzo cha ualbino


By Neristera Kihoza

Albino ni watu wenye ulemavu wa ngozi unaosababishwa na ukosefu wa madini aina ya melanin mwilini ambapo madini haya husababisha kutokuwepo kwa rangi nyeusi kwenye ngozi na nywele pia, hivo basi wanandoa wanapokutana kimwili kwa lengo la kutafuta mtoto, kama mmoja wao ana madini haya, haijalishi ni albino au sio, kuna uwezekano mkubwa wa kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino).

Kwa hiyo mtu yeyote akijifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi sio laana, mikosi, wala balaa n.k kwa mtu huyo kama jamii kubwa ya kitanzania inavyoamini. Naomba tufunguke sasa ili tuwaone kuwa nao ni watu wa kawaida kama wewe na mimi, tofauti tu ni ngozi ila shughuli zote anaweza kuzifanya.

Nanyi washirikina mnaotaka utajiri wa haraka haraka kwa kutumia viungo vya binadamu wenzenu hivi hiyo dhambi mtaitubu wapi? Mmewafanya wenzetu kuwa wakimbizi kwenye nchi yao wenyewe kweli! na hata kutengana na familia zao! Naomba tutoke mapangoni jamani! Kwanini wenzetu wa nchi za nje hawana haya mauzauza?

Leo hii nimepata taarifa kuwa kuna mtoto mwenye ulemavu wa ngozi aitwaye Upendo Emanuel wa Mkoa wa Mwanza wilaya ya Kwimba ametoroshwa na wajinga wachache wasiowatakia heri wenzetu, cha ajabu sasa eti hata watu wanaojiita eti ni wasomi bado wana dhana potofu dhidi ya albino.

Naomba wewe mwenye upendo na hawa wenzetu tuungane pamoja ili tuwaelimishe watu waweze kuondokana na ubaya huu pengine shetani amewakamata pasipo kujitambua. Mwisho nawaomba watanzania wote tujenge hali ya upendo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi tule nao, tucheze nao na hata kushirikiana kwa mambo yote, kwani wengine huogopa hata kuwagusa jamani! Tusiwatenge kwa sababu we are under the same sun, mimi nawapenda sana hawa ndugu zangu.


Ubarikiwe sana kwa ushirikiano wako!

Nelistera Kihoza aonya juu ya dhana potofu ya ulemavu




Huyu ni mwalimu wa Elimu Maalum Kanda ya Ziwa. Anajua ugumu wa kumwelimisha mtu kuhusu dhana ya ulemavu. Anachotamani ni watu wote kuona umuhimu wa haki za binadamu kuzingatiwa ili kutoa fursa sawa kwa binadamu wote.
Haya ndiyo maneno yake:

"Ewe Mtanzania, uwe Mkristo, Muislam au Mpagani; unapaswa kutambua kwamba walemavu wa aina zote nao wanathamani kubwa mbinguni na duniani kama wewe ulivyo. Shida tu ni ule mtazamo potofu juu ya watu hawa; lakini wanao uwezo wa kufanya kila kitu unachoweza kufanya wewe, Ewe mzazi mpeleke shule mtoto wako ambaye ni mlemavu,  kwani naye anayo haki ya kusoma kama watoto wengine. Achana na mtazamo potofu hiyo ambayo haijengi bali inabomoa. Napenda kuishauri serikali nayo pia isiwe na mtazamo potofu juu ya watu wenye ulemavu kwamba wanaweza kuajiriwa ktk sekta baadhi na sekta na sekta zingine hawawezi, sio hivo, Nao wapewe fursa  mbalimbali ilimradi tu wana sifa za kitaaluma husika, Lakini pia walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wana kazi kubwa sana kuliko tunavyofikiria, hivyo nashauri wapewe motisha ya kutosha



Mwisho Biblia inasema 'huyu na wazazi wake wote hawana dhambi bali kazi ya Mungu idhihirishwe ndani yake'. Kwa hiyo tusiwanyanyase."

Wanafunzi wa shule ya msingi ya wasioona Furaha, Tabora.

Mkuu wa mkoa Mwanza atoa siku tano kwa wanakijiji kwimba kuhakikisha wanampata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi.




Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo ametoa muda wa siku tano kwa wakazi wa kijiji cha Ndami na jeshi la jadi Sungusungu wilayani kwimba, kuhakikisha wanampata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi – Alibinism, Pendo Emanuel akiwa hai au amekufa ikiwa ni pamoja na wahusika wa tukio hilo kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Agizo hili la mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo, linakuja kufuatia watu wasiojulikana kumuiba mtoto Pendo Emanuel mwenye ulemavu wa ngozi majira ya saa 4 usiku Desemba 27 mwaka jana nyumbani kwao katika kijiji cha Ndami na kutoweka naye kusikojulikana, mkasa ambao umeilazimu kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mwanza kuapa kuwa serikali haitalala usingizi mpaka mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne apatikane.

Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoa wa Mwanza Alfred Kapole amesema kuwa miongoni mwa kesi 72 zilizokuwa mahakamani zikihusu mauaji ya walemavu wa ngozi, ni kesi tatu ndizo zilizotolewa hukumu mpaka sasa, huku akiilaumu ofisi ya mkemia mkuu wa serikali pamoja na mahakama kwa kuchelewesha kesi hizo.

Mama mzazi wa mtoto Pendo, Bi. Sophia Juma pamoja na mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Chiriko Bi. Specioza Kasoli wamesema kila mtu ana haki ya kuishi na kulindwa na kuongeza kwamba mtoto huyo ni kati ya watu 74 wenye ulemavu wa ngozi wilayani kwimba na alikuwa ni mtu wa 9 kwa kupatiwa ulinzi.


Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Valentino Mlowola amesema tayari askari polisi wamepiga kambi katika kijiji hicho kwa kazi moja tu ya kuhakikisha mtoto huyo anapatikana, lakini pia watuhumiwa wanasakwa kwa udi na uvumba ili wafikishwe mahakamani kwa kosa la jinai.


Chanzo: ITV Tanzania