Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo ametoa muda wa siku
tano kwa wakazi wa kijiji cha Ndami na jeshi la jadi Sungusungu wilayani
kwimba, kuhakikisha wanampata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi – Alibinism, Pendo
Emanuel akiwa hai au amekufa ikiwa ni pamoja na wahusika wa tukio hilo
kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Agizo hili la mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo,
linakuja kufuatia watu wasiojulikana kumuiba mtoto Pendo Emanuel mwenye ulemavu
wa ngozi majira ya saa 4 usiku Desemba 27 mwaka jana nyumbani kwao katika
kijiji cha Ndami na kutoweka naye kusikojulikana, mkasa ambao umeilazimu kamati
ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mwanza kuapa kuwa serikali haitalala usingizi
mpaka mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne apatikane.
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoa wa
Mwanza Alfred Kapole amesema kuwa miongoni mwa kesi 72 zilizokuwa mahakamani
zikihusu mauaji ya walemavu wa ngozi, ni kesi tatu ndizo zilizotolewa hukumu
mpaka sasa, huku akiilaumu ofisi ya mkemia mkuu wa serikali pamoja na mahakama
kwa kuchelewesha kesi hizo.
Mama mzazi wa mtoto Pendo, Bi. Sophia Juma pamoja na
mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Chiriko Bi. Specioza Kasoli
wamesema kila mtu ana haki ya kuishi na kulindwa na kuongeza kwamba mtoto huyo
ni kati ya watu 74 wenye ulemavu wa ngozi wilayani kwimba na alikuwa ni mtu wa
9 kwa kupatiwa ulinzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Valentino Mlowola amesema
tayari askari polisi wamepiga kambi katika kijiji hicho kwa kazi moja tu ya
kuhakikisha mtoto huyo anapatikana, lakini pia watuhumiwa wanasakwa kwa udi na
uvumba ili wafikishwe mahakamani kwa kosa la jinai.
Chanzo: ITV Tanzania
No comments:
Post a Comment