Thursday, September 18, 2014

UKWELI HUU UNAFANYIWA KAZI KWA WATU WENYE ULEMAVU KIELIMU?



SEHEMU YA 1.2.5:  Elimu

Imedhihirika kwamba watoto  wenye ulemavu wanakabiliwa na  mtizamo hasi wa watu wanaowazunguka (negative attitude). Hivyo kuwa na msimamo wa kiakili unaowanya washindwe kukabiliana na mazingira yao kiukweli.

Elimu ni muhimu kwa maisha na maendeleo ya binadamu, hata hivyo elimu peke yake huwa ndio uwezo (faculty) anaotegemea mtu mwenyeulemavu katika kutawala mazingira kwa maendeleo yake baada ya uwezo mwingine kuzuiwa na ama kupunguzwa na ulemavu. Mtizamo hasi wa jamii dhidi ya watu wenye ulemavu huchangia watoto wenye ulemavu kutopata elimu ambapo baadhi ya wazazi na ndugu huwaona watoto hao kama mzigo na hivyo kuamua kutowapeleka shule. Mfumo wa elimu nchini pia hautoi fursa na nafasi sawa kwa watoto wenye ulemavu wa aina  mbalimbali. Kutokana na hali zao watoto wenye ulemavu wanashindwa kumudu mazingira ya shule hivyo kushindwa kuandikishwa kujiunga na darasa la awali/kwanza.


Shule takriban zote za awali/msingi/sekondari na vyuo vya elimu ya juu  vimejengwa bila kuzingatiamahitaji maalumu ya watoto wenye ulemavu. Mafunzo ya waalimu na mitaala ya shule kadhalika haizingatii mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu, kwa mfano matumizi ya lugha ya alama na maandishi yanukta nundu. Kutokana na mazingira haya idadi ya watoto wenye ulemavu wanaoandikishwa darasa la kwanza ni chini ya asilimia moja.  Idadi ni ndogo zaidi katikashule za sekondari na vyuo.


REJEA: SERA YA TAIFA YA MAENDELEO NA HUDUMA KWA WATU WENYE  ULEMAVU
              (2004)

Wanafunzi walemavu waomba kuboreshewa miundombinu

Kutoka mkoani Tanga

WANAFUNZI walemavu wa shule ya Msingi Kisosora mkoani hapa, wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya mazingira ya shule hiyo iwe rafiki kulingana na uhitaji wao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.
Wanafunzi wenye ulemavu, Lucy Apolinali na Nyamkala Egness, waliiambia Tanzania Daima kuwa, kilio chao kikubwa ni ukosefu wa vitabu vya maandishi makubwa, miwani ya kusomea na usafiri.
"Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya vitu hivi ambayo inatupelekea kushindwa kufanya vizuri katika masomo yetu, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea," alisema Nyamkala.
Awali, mwalimu wa walemavu shule ya Kisosora ambaye naye ni mlemavu, Selina Mremba, alisema shule yake inakabiliwa na upungufu wa walimu wenye taaluma ya kufundisha makundi maalumu, hali ambayo huathiri kiwango cha ufaulu wa wanafunzi walemavu.
Naye Ofisa Utetezi wa Haki za Walemavu Kituo cha Kutolea Mazoezi ya Viungo kwa Walemavu (YDCP), Prisca Mwakasindile, aliwataka wanafunzi wasiwabague walemavu, badala yake washirikiane nao katika masomo, stadi za kazi na michezo kwa lengo la kuwajengea elimu shirikishi ili wanapomaliza shule wawe na cha kujivunia.


Shule ya Msingi Kisosora, ina wanafunzi walemavu 25 katika madarasa tofauti, licha ya kukabiliwa na tatizo la upungufu wa vifaa, miundombinu ya vyoo  na majengo si rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Chanzo: Tanzania Daima