Tufundishe nafsi, roho na akili zetu
Awali ya yote,
napenda kukushukuru wewe msomaji wa makala hizi, na pia ninapenda na kufurahi sana
ninapoona mrejesho wenu wa maoni. Inaonyesha kuwa mnayaona haya kwenye jamii
zetu halisi yakitukia.
Sasa hebu
tujikite kwenye mada yetu hii “Je, ulemavu ni laana? Au ni mikosi? Au ni dhambi?
Maana ya ulemavu
Sera ya Taifa ya
Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (2004) inafafanua kuwa ulemavu
ni hali inayotokana na dosari mwilini au/na akilini ambayo inasababisha mtu
kushindwa kutenda mambo ambayo kwa kawaida angetegemewa kuyaweza na hivyo
kumletea mtu huyo kizuizi katika utekelezaji wa majukumu yake katika jamii.
Kizuizi katika utendaji kinatokana pia na mfumo wa mtizamo wa jamii dhidi ya
mtu huyo.
Ulemavu ni neno linalotumika kwa mapana
kuainisha maeneo matatu muhimu yafuatayo:
• Hali ya tatizo
kadri linavyoonekana (impairment)
• Upungufu wa
uwezo wa kutenda/kufanya jambo kwa njia ya kawaida kulingana na hali yake (Disability).
• Kizuizi katika
kutenda jambo (handicap) kutokana na hali ya ulemavu (Disability).
Maana ya mikosi (misfortune)
Ni hali ya
kukosa bahati, kukosa kupata mema kwa njia ya imani aliyonayo mtu. Kushindwa kufanikiwa
na/au kuandamwa na matukiomabaya ambayo chanzo chake ni laana.
Katika kitabu
cha 1Samweli 28: 6; tunaona mfalme Sauli akipatwa na majanga makubwa ya kupigwa
na Wafilisti, mkosi ambao ulitokana na dhambi yake ya kiburi mbele za Mungu
wake. Imeandikwa hivi katika mstari wa 6:
“Lakini
Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu,
wala kwa manabii”.
Maana ya Laana na Dhambi
Laana ni
kukataliwa na wanadamu au Mungu kutokana na kosa lisiloweza kusameheka. Neno Dhambi
(mistarget) inamaanisha ni UASI, kukosea lengo au shabaha ya kile ulichotegemea
kukitimiza. Umeamriwa kufanya hiki wewe ukafanya kile-hiyo ni dhambi.
Je, ulemavu ni
laana? Je, ni mikosi? Ni dhambi?
Mambo ya Walawi 19:14,
Biblia imeandikwa hivi:
“Usimlaani kiziwi, wala
usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; mimi ndimi Bwana”.
Maneno ya msingi katika
mstari huu:
Usimlaani, lina maana usimkatae au
usimtenge (mtu mwenye ulemavu).
…wala usitie kikwazo
(stumblingblock), maana yake ni kwamba binadamu yeyote asimjengee mazingira
magumu ya kuishi binadamu mwenzake mwenye ulemavu.
…bali umche Mungu wako;
Umche Mungu wako kwa lipi?
Umche Mungu wako kwa uumbaji wa aina yake,na wala usimkosoe
wala kumpinga Mungu kwa uumbaji huo.
…mimi ndimi Bwana.
Inamaanisha yeye Mungu
ndivyo alivyoamua na wala mtu mwingine asihoji hilo.
Pia katika kitabu cha Kutoka
4:10-17, tunasoma maneno haya:
“Bwana akamwambia, Ni nani
aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi,
au mwenye kuona, au kipofu? Si mimi Bwana?”
Haya maelezo yalitolewa na
Mungu wakati nabii Musa alipokuwa akikataa kwenda kuwakomboa wana wa Israel
katika nchi ya Misri. Musa alihofia kuwa angeshindwa kuongea mbele za Farao na
kwamba huenda na wana wa Israel wasingemsikiliza kwa sababu ya ulemavu wake wa
ugumu wa kuongea (speech impairment). Hii ilitokana na uzoefu wake kwenye jamii
yake. Yawezekana yalikuwa yanamkuta hayo aliyokuwa akijitetea kwa Mungu.
Katika kitabu cha Injili ya
Yohana 9: 2 & 3 (Yohana 9: 2, 3) tunasoma maneno haya:
“Wanafunzi wake wakamwuliza,
Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, hata mtu huyu azaliwe kipofu? Yesu akajibu,
Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani
yake”.
Ni swali zuri
sana na liko wazi likidokeza mtazamo wa jamii walimoishi kipindi hicho. Wanafunzi
wa Yesu hawakuwa na shida ya kujua ULEMAVU ni matokeo ya dhambi au la, kwani
tayari walikuwa wanafahamu hivyo kuwa mtu kupata ulemavu ni matokeo ya dhambi. Shida
yao kubwa ilikuwa kujua ni nani hasa aliyetenda dhabi kati ya aliyezaliwa
kipofu au wazazi waliomzaa huyo kipofu.
Yesu alikuja na
majibu yaliyowashangaza, pia majibu haya
yalibadilisha mtazamo wa wanafunzi wake. Majibu ya YESU yalikuwa hivi:
“Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake;
bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.
Kwa tafsiri
nyingine ya maneno ya Yesu ni kwamba si wazazi au mtoto aliyezaliwa akiwa na
ulemavu ni wenye dhambi, bali hayo ni matokeo na makusudi ya uumbaji wa Mungu. “…baki
kazi za Mungu zidhihirike (zionekane wazi, zitofautiane na kazi zingine zisizo
za ki-Mungu) ndani yake (ndani ya huo uumbaji)”.
Hitimisho
Ulemavu kwa
ukweli wake ni kwamba unaleta madhara katika utendaji kazi kwa maisha ya kila
siku ya mhusika mwenye ulemavu pamoja na kuleta ugumu wa mitazamo kwa familia
yenye mtu mwenye ulemavu. Pia tuweke kwenye fahamu zetu kuwa ulemavu, kwa elimu
ya kisayansi husababishwa na vigezo viwili tu ambavyo ni “mazingira na urithi”. Na kwa upande wa imani itokanayo na kitabu
kitakatifu kiitwacho “Biblia”, ulemavu umeelezwa kuwa ni sababu za kiuumbaji,
na pia tunaambiwa katika uumbaji huo kuna kusudio halisi. Si bahati mbaya wala
mikosi, si laana wala dhambi pia.
Watu wenye
ulemavu na wasio na ulemavu, wote kwa pamoja tujitambue, tujue kuwa na ulemavu
au la ni sehemu ya vionjo vya maisha ya binadamu. Wengine wamepata mafanikio
kutokana na misukumo ya ulemavu, na vilevile wapo watu ambao ulemavu ndio
umewafanya washindwe kufikia malengo yao katika maisha. Tena tusisahau kuwa
wapo watu ambao kutokuwa na ulemavu kumewafanya wakaona mazingira ni rafiki,
wakasahau kupambana na mazingira, na hatimaye wakashindwa kufikia malengo yao
kimaisha pia.
Hivyo, nionavyo
mimi, ulemavu unamfanya mtu kuwa makini na mazingira, humwezesha kuwafahamu
marafiki na maadui wa kweli katika maisha. Huweza kumwezesha mhusika kujua
asili ya binadamu na utofauti wa binadamu mmoja na mwingine. Hubainisha watu
wenye haiba dhaifu dhidi yao walio imaira, hututenganishia kati ya wenye fikra
potofu dhidi ya wale wabebao na kutemelea ukweli kwenye katika maisha yao.
"FIKIRI KIJUMUISHI ~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI"
REJEA
BIBLIA TAKATIFU
(1952)
Sera ya Taifa ya
Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (2004)