Linda Haki Yako, Ukiaminiwa Jiamini!
Nimepita kwingi, nimeona mengi, mengine yanapendeza, yanashangaza, yanachekesha na hata mengine huleta machukizo na vitisho kwa maisha ya binadamu. Ni mchanganyiko wa matukio ya aina yake. Nimeshuhudia haki za watu zikiporwa kama vibaka waporavyo simu mtaani, hujiuliza maswali kuwa binadamu ni nani na ubinadamu ni nini? Hutamani nifanye kazi zangu kwa karibu na wanasheria watakatifu, wanaharakati wa kweli na watumishi thabiti wa Mwenyezi Mungu.
Leo nitumie uwanja huu kuleta mifano michache ya watu wenye ulemavu ambao wamepita kwenye magumu na wakashinda, kisha wameleta mitazamo mipya katika maisha ya mwanadamu.
NABII MUSSA
Nabii Musa akipiga mwamba ili utoe maji |
Musa akiwa ameshika amri 10 alizopewa na Mungu |
Huyu ndiye nabii pekee ambaye Mungu anasema alimpenda kupita manabii wote, na kwa kuthibitisha upendo kwa Musa, Mungu alimpa ofa ya kuonana nae uso kwa uso; Musa alifanikiwa kuona kisogo cha Mungu. Kwa mujibu maandiko ya Biblia takatifu, hakuna nabii yeyote aliyemwona Mungu isipokuwa huyu Musa. Huyu mtumishi wa Mungu alikuwa mlemavu wa kinywa (speech Impairment). Alipotumwa na Mungu kwenda kuwakombo wana wa Israel kutoka mikono ya chuma ya Farao ndipo ghafla akaubaini ulemavu wake na kurejesha ujumbe kwa Mungu kuwa hawezi. Mungu akampa msaidizi wa kwenda nae ambaye ni Haruni (kaka yake). Mwisho wa siku Mussa pamoja na ulemavu wake ndiye akawa rais wa wana wa Israel.
FRANKLINE DELANO ROOSEVELT
Rais wa Marekani 1933-1945 |
Huyu alikuwa rais wa Marekani mwaka 1933 hadi 1945. Alikuwa ni mlemavu wa viungo (miguu) uliotokana na polio. Ndiye rais aliyeijenga Marekani tunayoiona leo, sera na mipango mingi ya marekani bado ni ya wakati wa Roosevet. Alikuwa na rais wa pekee. Alikuwa anatumia misemo ya kutia nguvu kama "The only thing to fear is fear itself".
Hebu sasa tutoke huko turudi hapa kwetu Tanzania
Hapa Tanzania pia tuna watu wenye ulemavu ambao wanaweza kuwa "Role Model" kwa maisha yetu sote. Tuanze safari yetu kuwaangalia watu hawa:
SALUM KHALFAN BARWAN
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF) |
Huyu ni mlemavu wa ngozi, yaani albino. Mheshimiwa Salum Khalfan
Barwani ni mbunge wa Lindi Mjini kupitia Chama Cha Wananchi-CUF. Huyu ni mbunge wa kwanza albino katika historia ya Tanganyika hadi sasa Tanzania. Ni wazi kwamba huyu mheshimiwa Barwan anaweza hata akipewa nafasi nyingine kubwa zaidi ya hiyo. Ni wazi, kwa taratibu za uundaji wa baraza la mawaziri kwetu hapa Tanzania, mtu kupewa dhamana ya uwaziri ni lazima awe mbunge. Hivyo basi mheshimiwa Salum Khalifan Barwan anafaa kuwa waziri na hata kuwa rais wa nchi.
DR. EDWARD BAGANDANSHWA
Dr. Bagandanshwa (wa katikaki waliosimama |
Huyu ni mhadhiri mwandamizi (senior lecturer) wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (OUT) pamoja na SEKOMU. Yeye ni mlemavu wa macho (total blindness). Ana shahada za Uzamivu 2 na shahada za Uzamili 13, huku shahada zake mbili za uzamili (masters) zilipitishwa bila marekebisho ya aina yoyote. Ni Chief Editor katika Jarida la JIPE la The Open University of Tanzania.
Kwa sasa Dr. Bagandanshwa ni Dean Faculty of Education SEKOMU. Amebadilisha mtazamo wa taaluma hapo SEKOMU, pia sidhani kama wanaweza kumwacha aondoke kirahisi chuoni hapo.
Misemo yake: "Tunaweza kuona mbali tunaposimama juu ya mabega ya watu warefu"; "Kama vile watu walivyokusaidia mpaka ukapata mafanikio nawe huna kusaidia wengine".
Kwa hakika, kwa msomi kama huyu, jamii inafaidika kutokana na huduma zake. Ana mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa hili. Pia serikali ya Tanzania inatakiwa kuangalia mahali ambapo huyu 'giant' kukaa na kutumikia watu wengi zaidi kwa faida ya taifa kuliko kundi dogo la leo.
Hitimisho
Kwa muda mrefu jamii zetu na baadhi ya watawala wetu katika ngazi mbalimbali nchini wamekuwa hawaamini uwezo na mchango wa watu wenye ulemavu kwa taifa. Ukiona mtu mwenye ulemavu amepata hatua nzuri kielimu, kiuchumi na kisiasa ujue amepambana kwa kutumia nguvu nyingi sana. Amepambana na mazingira, binadamu wenzake pamoja na athari za ulemavu alionao.
Kazi sasa inaonekana, watu wenye ulemavu wanaweza, kilichobaki ni kujiamini na kuaminiwa na jamii zetu kwa kupewa nafasi stahili kwa maendeleao ya taifa hili la Tanzania. Ninaamini muda si mrefu tutashuhudia watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu wakienda pamoja kuchukua form za kugombea urais wa nchi hii na pia kwenye fursa zingine kwenye jamii.
"FIKIRI KIJUMUISHI ~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI"