"Dr. Aneth Munga mwenye FIKRA na VITENDO Jumuishi" |
Pichani hapo juu ni Mchungaji, Dr. Aneth Munga ambaye pia ni makamu mkuu wa chuo cha Sebastian Kolowa Memorial University (SEKOMU). Hapa pichani Dr. Aneth Munga anahutubia wanafunzi wa mwaka watatu wa SEKOMU kwa kutumia lugha ya alama. Dr. Aneth Munga ana mitazamo ya mbali sana kwa ajili ya kusaidia watu wenye mahitaji maalum. Anayo slogan moja nzuri ambayo imeandikwa kwenye ukumbi wa mihadhara usemao "Acquire Knowledge, Serve with Compasion". Kwa watu wenye mitazamo mizuri kama ya huyu mchungaji wakipatikana kwa wingi wanaweza wakabadilisha mitazamo ya watu kufikiri na hata kubadilisha mitazamo ya kielimu kwa nchi nzima. Uwepo wa watu hawa ni wasaa mzuri kwa jamii kuwatumia ili kujenga jamii jumuishi ambapo hakuna atakayeachwa katika hatua yoyote kwenye maendeleo na upataji wa mahitaji ya msingi ya binadamu kwa kisingizio cha ulemavu alionao mtu, kwa kuwa ulemavu si lazima umpelekee mtu kushindwa kujimudu (Disability is NOT Inability). Kuwatumikia watu wenye mahitaji maalum ni kama kuanzisha vita na jeshi kubwa la wapinzani, ni kujiingiza kwenye ulimwengu wa kudharauliwa, kupuuzwa na kutengwa. Wanathamani sana watu wenye mitazamo chanya juu ya jamii ya watu wenye ulemavu. Mara zote huwa nawahusisha na utume wa ki-Mungu watu wote wenye nia na utayari wa kuwatumikia watu wa kundi la chini kabisa kimaisha. Tujifunze kutoka kwake Dr. Aneth Munga. |
Hapa pichani juu ni Mwalimu Rose Yona ambaye ameshamaliza chuo mwaka wa masomo 2012/2013 SEKOMU. Anaipenda fani yake ya elimu maalum, ni mtaalam wa lugha ya alama kwa viziwi. Chuo cha SEKOMU kimemtumia sana kuandaa video mbalimbali za kutafsiri lugha ya alama na kuzipeleka Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA). Ni mtu muhimu sana kwa ajili ya ujenzi wa jamii jumuishi. Pichani hapo juu ni wakati alipokuwa kwenye mazoezi ya kufundisha kwa vitendo katika shule ya Viziwi Mwanga iliyoko mkoani Kilimanjaro.
Mtazamo wa mwalimu Rose Yona juu ya watu wenye mahitaji maalum, hususan watu ambao ni viziwi ni kutokana na ufahamu wake juu ya haki za watu viziwi kwenye mawasiliano. Anasema:
"Mawasiliano na taarifa mbalimbali kwenye jamii ni haki ya kila binadamu. Jukumu letu ni kujenga mazingira jumuishi yatakayomwezesha kila mwanajamii kupata taarifa kuwasiliana kwa uhuru wote".
Kwa mtazamo wa Mwalimu Yona ni kwamba; mawasiliano ni kila kitu kwa binadamu. Watu wote wenye mafanikio kwenye maisha ni lazima wawe na uwezo kuwasiliana kwa ufasaha.
Pichani hapa juu ni mwanachuo wa SEKOMU aitwae Jesca Mbotha. Hapa alikuwa katika mafuzo kwa vitendo katika shule ya msingi ya BUGURUNI VIZIWI Dar Es Salaam katika manispaa ya ILALA. Wanafunzi alionao pichani wako darasa la tatu. Katika mapinduzi ya kujenga kizazi kipya ambacho ni jumuishi ndipo tunaona ulazima wa kuwakuza watoto wadogo katika mazingira jumuishi pamoja na kuwaandaa walimu vijana watakaoweza kwenda sambamba na kasi ya uundaji wa jamii tuipendayo yenye utamaduni jumuishi.
Maneno ya mwalimu Jesca Mbotha kuhusu elimu maalum na wanafunzi wenye mahitaji maalum ni haya:
"Jukumu la kuwalea watoto wenye ulemavu ni letu sote. Tusiwanyanyapae na kusema hawana msaada, wakiwezeshwa wanaweza".
Huu ni mtazamo chanya juu ya watu wenye mahitaji maalum. Ndivyo wanajamii wote wanatakiwa kuwa na huu mtazamo wa kumpa binadamu awaye yote hadhi yake kwa kuwa amumbwa binadamu.
"Think Inclusively ~~~ Act Inclusively ~~~ Create an Inclusive Nation".
Mwandaaji: Sokime Philemon
Barua pepe: sokime2012@gmail.com
Simu: +255655410031