Sunday, March 13, 2016

Tupunguze viashiria vya ulemavu

Katika dunia ya leo, asilimia kumi ya kila idadi ya watu kadhaa ni watu wenye ulemavu.
Ulemavu upo wa makundi mawili,; wa kuzaliwa nao (congenital) na ule aupatao mtu akiwa amezaliwa (acquired). Pia ulemavu unaweza kuwa wa kurithi kutokana na vinasaba vya mtiririko wa kizazi husika.

(A) Namna ya Kupunguza ulemavu

Ulemavu wa kuzaliwa (ambao si wa kurithi)
1. Mama mjamzito fuata kanuni za kitabibu kwa kupata virutubisho sahihi kwa makuzi ya ujauzito wako
2. Baba epuka kuleta ghasia kwa mama mjamzito kama vile kumpiga mateke ya tumbo, kuwa mkali kwa mke wakati wa ujauzito wake.
3. Baba na mama mshirikiane ili kuhakikisha mimba inakua vizuri hadi hapo mtoto atakapozaliwa
4. Daktari awe wazi kuwataarifu wazazi watarjiwa wa mtoto pale anapobaini kuna dalili za ulemavu kwa mtoto ili kuona kama uwezekano wa kupunguza athari za ulemavu huo. Mfano, mtoto anayezaliwa na kifundo cha mguu (Club foot) anaweza kurekebishwa miguu yake angali mtoto mchanga.
5. Baba na mama muishi maisha ya furaha, hasa baba jitahidi kumjengea mama mjamzito furaha kubwa.

(B) Ulemavu baada ya kuzaliwa
Ulemavu wa aina hii ni matokeo ya ajali mbalimbali kwenye mazingira yetu
1. Epuka kugongeshagongesha kichwa cha mtoto mchanga ili kuepuka kuharibu ubongo wa mtoto (mtindio wa ubongo)
2. Epuka kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kwa tiba isiyo ya lazima kwa watoto. Kituo cha kwanza kwa matibabu yoyote ya mtoto iwe kwa madaktari waliosomea udaktari. Huko kwingine iwe ni ziada tu (hii itasaidia kitaalam kujua maendeleo ya afya ya mwanao.
3. Epuka kumpa mtoto wako vifaa vyenye ncha kali kama vile sindano, mouth sticks, kalamu za wino, visu nk. Vifaa hivi ni hatari kwa macho na masikio ya mtoto (upofu na ukiziwi au vyote kwa pamoja).
4. Epuka kumweka mwanao kwenye mchanga. Mara nyingi ni hatari kwa macho ya mtoto.
5. Epuka kumtishia mtoto mdogo kama vile tusemavyo kwa vitisho. Hii huweza kumsababishia mtoto kuwa na vurugu za maono, hasa hasira na woga uliopitiliza kiasi cha asili ya binadamu.
6. Epuka kumpiga makofi mwanao; unaweza ukamharibu masikio na mishipa ya macho na kumsababishia upofu na ukiziwi.
7. Epuka kuishi maeneo yenye kelele nyingi kama vile viwandani, migodini, vituo vya mazoezi ya kulenga shabaha kwa wanajeshi, karibu na viwanja vya ndege. Hii husababisha ukiziwi kwa mtoto.

(C) Ulemavu wa kurithi
Hapa sasa niongee na vijana ambao hawako kwenye ndoa.
Mara nyingi ulemavu wa kurithi ni matokeo ya kuwepo kwa vinasaba vya ulemavu husika kwa wana ndoa.
Ili kuepuka na/au kupunguza huu ulemavu ni jukumu lako kijana ambaye hujaoa au kuolewa kufanya uchunguzi wa kina juu ya mwezi wako mtarajiwa.
1. Uliza kama kwenye ukoo wao kuna ulemavu wa kurithi, na kama upo, je, unaweza ukaathiri kizazi chenu? Upo ulemavu wa kurithi ambao akiwa nao mmoja wa wana ndoa hauwezi kuathiri kizazi chenu.
2. Anza maandalizi ya uchunguzi wa huyo unayependa awe mwezi wako kabla ya kumdokezea kuwa unatamani awe mwezi wako. Hii itasaidia kuepuka maumivu ya kusiisha mahusiano yenu.
3. Pata uchunguzi wa kitabibu ili kuona kama kuna/hakuna dalili za vinasaba vya ulemavu.

Kwa ujumla, ulemavu si dhambi. Unaweza kumpata mtu yeyote. Kwa hakika hakuna mtu anayeweza kuepuka ulemavu kwa asilimia 100. Mtu akijaliwa kuufikia uzee wema lazima viungo kama macho na masikio vikose ufanisi wake. Ndio maana wazee wengi huanza kupata shida ya kuona na kusikia.

Ulemavu unahusika sana na mazingira matatu ya binadamu; yaani, kabla ya kuzaliwa, wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa. Na kila mazingira ya vihatarishi husika kwa aina moja au zaidi ya ulemavu.

Nihitimishe kwa kusema kuwa hizi ni baadhi ya tahadhari miongoni mwa nyingi. Nyingine unazifahamu mwenyewe kutokana na mazingira yako. Pia tunayazungumza haya kutokana na matokeo ya athari za ulemavu kwenye maisha yetu sisi binadamu. Kikubwa zaidi ni hizi tamaduni zetu zinazotugawa kwa kuangalia maumbile ya binadamu.

Tufikiri Kijumuishi.....Tutende Kijumuishi.....Tujenge Taifa Jumuishi