Sunday, September 27, 2015

Haki na Ustawi wa watu wenye ulemavu baada ya uchaguzi mkuu Tanzania, 2015



 
Siku zote binadamu ili kupata mahitaji yake lazima adai haki ya mambo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Haki ya Mtanzania yeyote ndiyo haki ya mtu mwenye ulemavu. Ulinzi wa Mtanzania ni haki ya mtu mwenye ulemavu, haki ya mafanikio ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya Mtanzania yeyote ni ya mtu mwenye ulemavu pia! Naam, habari njema yoyote inayohubiriwa kwenye majukwaa ya siasa kwa Watanzania ni ya mtu mwenye ulemavu pia.

Nimejaribu kujiuliza mambo kadhaa kutokana na historia ya Tanzania kwa mapito ya watu wenye ulemavu.


1. Habari ya kuwaondoa watu wenye ulemavu Dar miaka ile kwa kisingizio cha kusafisha jiji haitaendelea?


2. Habari ya kuondoa biashara za watu wenye ulemavu kando ya barabara imeshakwisha?


3. Tabia ya kutuma sungusungu wahusike kuwatafuta albino wakitekwa imesitishwa?


4. Habari ya wanafunzi kadhaa wenye ulemavu kwenye mikoa ambayo haina shule maalum kwao imekwisha?


5. Mauaji ya wenzetu albino hayataendelea tena?


Kama maswali yote haya yatakuwa na majibu hasi, basi uchaguzi mkuu kwa watu wenye ulemavu utakuwa si wa furaha wala wenye ustawi kwao.

Tunapokuwa tunaongea habari za watu wenye ulemavu kwenye siasa tusidhani kuwa wao hawana vionjo vya moyo na hisia. You feel, they feel!


Hakika, ustawi wa Watanzania kwenye nyanja yoyote ya maisha ndio ustawi wa watu wenye ulemavu pia!

Ninatamani kuiona Tanzania yenye kuleta usawa kwa binadamu kwa nyanja zote za maisha na kwa ngazi zote kuanzia kaya, mtaa, kijiji, wilaya, mkoa na, taifa kwa ujumla wote. Nimesema haya kwa kuwa nimeshuhudia huduma hafifu kwa watu wenye ulemavu, hasa za kijamii. Tuijenge nchi yetu iwe mahali pa kutengeneza na kusambaza usawa kwa mataifa mengine.  






Fikiri Kijumuishi ~ Tenda Kijumuishi ~ Jenga Taifa Jumuishi!