Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu duniani. Miongoni mwa haki za watu wenye ulemavu ni ile inayohusu elimu. Ibara ya 24 ya mkataba huu imeongelea kwa undani habari za elimu kwa watu wenye ulemavu. Tuusome huu mkataba kisha tujitathmini wenyewe kama taifa na kujiuliza swali moja tu;
"Je, tumeweza kuitimiza hii haki ya watu wenye ulemavu kujipatia elimu yao ipasavyo?"
Ibara ya
24
Elimu
"1. Waliouridhia Mkataba huu, wanatambua
haki za watu wenye ulemavu kupata elimu. Ili haki hii ipatikane bila ya ubaguzi
na kwa misingi ya usawa wa fursa, Waliouridhia Mkataba, watahakikisha
kuwepo kwa mfumo wa elimu jumuishi katika ngazi zote na mfumo wa ujifunzaji kwa
maisha yote ukijielekeza kwenye:
(a) Uendelezaji kamili wa uwezo wa binadamu na
uzingatiaji wa hadhi na kujithamini, kuimarisha hali ya kuheshimu haki za
binadamu, uhuru wa kujiamulia na uanuwai miongoni mwa binadamu.
(b) Watu wenye ulemavu kujiendeleza kadri
wawezavyo kihaiba, kivipawa na kiubunifu, kadhalika na uwezo wao kiakili na
kimwili;
(c)
Kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki ipasavyo katika jamii iliyo huru.
2. Ili haki
hii ipatikane, Waliouridhia Mkataba huu watahakisha kwamba:
(a) Mfumo wa elimu
hauwatengi watu wenye ulemavu na
kwamba
watoto wenye ulemavu hawabaguliwi kwenye elimu ya msingi ambayo ni ya lazima au
ile ya sekondari kwa misingi ya ulemavu;
(b) Watu wenye ulemavu
wanaweza kuipata elimu ya msingi na ya sekondari katika mfumo jumuishi, bora na
bila ya malipo kwa misingi ya usawa na wengine katika jamii waishimo.
(c) Marekebisho stahili
yanafanyika kulingana na mahitaji binafsi;
(d) Watu wenye ulemavu
wanapata usaidizi unaohitajika ndani ya mfumo wa elimu, ili kuwawezesha
kuelimika vilivyo;
(e) Hatua za makusudi za
kumuwezesha mtu binafsi mwenye ulemavu zinachukuliwa katika mazingira
yanayomuwezesha kufikia upeo wa maendeleo ya kitaaluma na kijamii kama lilivyo lengo la ujumuishaji kamilifu;
3. Nchi zilzoridhia
Mkataba huu, zitawawezesha watu wenye ulemavu kujifunza maishani na stadi za
kimaendeleo katika jamii ili kurahisisha ushiriki wao ulio kamilifu katika nyanja
ya elimu na kama wanajamii wengine. Ili kufikia lengo hili, Waliouridhia Mkataba
huu watachukua hatua zinazofaa, zikijumuisha:
a) Kuwezesha mafunzo
ya maandishi ya nukta nundu, maandishi mbadala na njia za kukuza mawimbi
ya sauti na nyinginezo za kuboresha mawasiliano, mbinu kabilifu za ujongeaji,
na kuwezesha huduma za makundi rika na ushauri;
b) Kuwezesha mafunzo ya
lugha ya alama na kukuza utambulisho wa kiisimu wa jamii ya viziwi;
c) Kuhakikisha kwamba
elimu kwa watu wenye ulemavu, hususan watoto wasioona, viziwi au viziwi
wasioona, inatolewa kwa lugha, mfumo na njia sadifu za kimawasiliano, na katika
mazingira yatakayotoa nafasi kubwa ya maendeleo kitaaluma na kijamii.
4. Ili
kusaidia katika kuhakikisha upatikanaji wa haki hii, Waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua madhubuti katika, kuajiri walimu, wakiwemo
walimu wenye ulemavu, walio na utaalamu wa lugha ya alama na/au nukta nundu na
pia kuwafundisha wataalamu na watumishi katika ngazi zote za elimu. Mafunzo
kama hayo yatajumuisha mwamko kuhusu ulemavu na kutumia njia za kukuzia mawimbi
ya sauti na zile mbadala kimawasiliano, mbinu na vifaa vya kimafunzo
vitakavyowasaidia watu wenye ulemavu.
5. Waliouridhia Mkataba huu, watahakikisha
kwamba watu wenye ulemavu wanapata elimu ya juu, mafunzo ya ufundi, elimu ya
watu wazima na mafunzo wakati wote wa maisha yao bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kuipata
kwa misingi sawa na watu wengine. Ili kufikia hatua hii, Waliouridhia
Mkataba huu watahakikisha kwamba marekebisho stahiki yanafanyika kwa ajili ya
watu wenye ulemavu."
NB:
Elimu Jumuishi Tanzania bado ina kasoro kadhaa ambazo sote kwa pamoja kama taifa tunahitaji kuzirekebisha:
1. Upungufu wa walimu wenye utalamu wa elimu maalum
2. Upungufu na/au ukosefu wa vifaa saidizi kwa watoto wenye mahitaji maalum
3. Mtazamo juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu bado haujaeleweka vizuri
4. Mazingira ya kielimu kwenye shule jumuishi si rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum