Saturday, December 10, 2016

Kamata sana hii elimu

Katika elimu ambazo zinaogopwa ni hizi zinzohusu masuala ya ulemavu. Mtu anahisi akiifuatilia anaweza akaupata ulemavu. Hakika ulemavu unawapata watu, lakini si wote wanaweza kuathiriwa na ulemavu kwa kiwango kinachofanana. Ugumu unakuja kuwa "ni nani anayefuata kwa kupata ulemavu (kwa wasio na ulemavu)?"

Umuhimu wa elimu hii upo hapa:
1. Hii ni elimu ihusuyo afya ya mwili wako
2. Elimu hii inasaidia kuepuka mazingira hatarishi ya kupata ulemavu wa aina fulani fulani (mfano: ulemavu unaotokea kwa kutozingatia lishe bora).
3. Elimu hii juu ya ulemavu inasaidia kuwa na mtazamo chanya juu ya binadamu wengine wenye ulemavu.
4. Elimu hii ni sawa na huduma ya kuganga mioyo ya watu walioathiriwa na ulemavu kwa namna moja ama nyingine. Nimejifunza mambo mengi juu ya jamii ya watu wenye ulemavu na familia zao.

Ushuhuda wa kweli:
Kuna siku nikiwa natembea mtaani nilisimama kusalimiana na jamaa zangu. Mtu mmoja akasema "mtu yule mbona anaachwa kutambaa mtaani kwa shida"?. Huyu jamaa yangu alimaanisha kuwa ni kitendo cha aibu sana kwa mtu mwenye ulemavu kuonekana mtaani. Mimi nilianza kwa kusema: Hawa watu wanaokaa na huyu mtu wana akili sana, wana utu na wanampenda mtu wao. Nikamalizia kwa kusema: "Ulemavu ukiupokea vibaya unaweza ukawa masikini".
Katika kundi lile alikuwepo jamaa ambaye alishaathiriwa na ulemavu wa mwanae kwa miaka kadhaa. Akanishika mkono akanipeleka pembeni na kuanza kunihoji.

Miongoni mwa mambo aliyoniambia ni kuwa amehangaika na huyo mwanae kwa waganga hadi akafilisika, amekimbia kutoka Arusha na kwenda Morogoro kwa kuogopa aibu kwa marafiki zake. Akaongeza kusema kuwa mwanae huwa anamfungia ndani akienda kufanya shughuli zake. Nilipomwelekeza namna ya kuishi na huyo mwanae mwenye ulemavu alinielewa na kuishia kusema "mzigo nimeutua sasa".

Wapo watu wengi waliokosa huduma kama hizi, wanapata shida kwa kutokujua jinsi ya kuishi na jamii za watu wenye ulemavu na pia kupata shida ya kujifikiri juu ya ulemavu wao.
5. Ni elimu inayomhusu mtu mwenye ulemavu ajikubali jinsi alivyo, watu wanaotunza wenzao wenye ulemavu wasijisikie vibaya na kuwajengea utamaduni watu wasio na ulemavu jinsi ya kufikiri kivingine bila kuzingatia mapokeo mabaya juu ya watu wenye ulemavu. Ni kweli kila apataye ulemavu amelaaniwa? Amefanya kosa? Kwanini atengwe? Kwanini aonekane si binadamu? Ndiyo aonekane hawezi? (Haya ndiyo ya kujirekebisha).

Naendelea kukutia moyo wa kusoma maandiko haya kila upatapo nafasi ya kufanya hivyo.


Tengeneza Maana kwenye uwanja wa fujo






Utamaduni una nguvu kwenye maisha ya binadamu, naam, ndiyo maisha yenyewe! Tunaishi kutokana na utamaduni tuliojiwekea.

Jamii nyingi za Kitanzania hazipendi kufanya mijadala juu ya watu wenye ulemavu. Huu ni utamaduni wa jamii zetu katika ngazi za kaya, ukoo, kabila na hata kuakisi taifa zima.

Kutokana na utamaduni huu wa kutokufanya mijadala mingi juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu kuwa ni mwiko (taboo) kuongelea masuala ya ulemavu. Kutoka hapa ndipo pamezaliwa, kukua na kukomaa kwa mizizi ya unyanyapaa kwa watu wenye mahitaji maalum.

Kama taifa, tunahitaji watu wenye roho ngumu za kutengeneza maana ya maisha kwa watu wenye mahitaji maalum na kwa watu wote ambao kwa namna hii au ile wameathiriwa na ulemavu (mfano: wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu). Tunahitaji watu watakaotoa huduma ya kuwawezesha wahanga hawa kupumzika kisaikolojia (psychological comfort). Huduma hii ni adimu sana hapa nchini.

Kama kwenye vita za risasi na mabomu wapo watu wenye kujipatia ajira kwa vita hizo (mfano waandishi wa habari), je, si rahisi sana kupata ajira ya kutangaza habari za amani, mshikamano na upendo ndani ya nchi yetu wenyewe? Naam, inawezekana!

Wapo watu wengi wenye mahitaji maalum ambao wanatafuta neno la kuambiwa 'unaweza' na hawapati. Wapo wazazi na walezi ambao wanataabika kisaikolojia kwa kutokujua namna ya kukaa na watoto wao wenye mahitaji maalum- wanashindwa kupata mtu wa kusema 'mwanao ni mzuri na anaweza kufanya abcs'.

Sote tufikiri juu ya hilo!