Saturday, December 10, 2016

Tengeneza Maana kwenye uwanja wa fujo






Utamaduni una nguvu kwenye maisha ya binadamu, naam, ndiyo maisha yenyewe! Tunaishi kutokana na utamaduni tuliojiwekea.

Jamii nyingi za Kitanzania hazipendi kufanya mijadala juu ya watu wenye ulemavu. Huu ni utamaduni wa jamii zetu katika ngazi za kaya, ukoo, kabila na hata kuakisi taifa zima.

Kutokana na utamaduni huu wa kutokufanya mijadala mingi juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu kuwa ni mwiko (taboo) kuongelea masuala ya ulemavu. Kutoka hapa ndipo pamezaliwa, kukua na kukomaa kwa mizizi ya unyanyapaa kwa watu wenye mahitaji maalum.

Kama taifa, tunahitaji watu wenye roho ngumu za kutengeneza maana ya maisha kwa watu wenye mahitaji maalum na kwa watu wote ambao kwa namna hii au ile wameathiriwa na ulemavu (mfano: wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu). Tunahitaji watu watakaotoa huduma ya kuwawezesha wahanga hawa kupumzika kisaikolojia (psychological comfort). Huduma hii ni adimu sana hapa nchini.

Kama kwenye vita za risasi na mabomu wapo watu wenye kujipatia ajira kwa vita hizo (mfano waandishi wa habari), je, si rahisi sana kupata ajira ya kutangaza habari za amani, mshikamano na upendo ndani ya nchi yetu wenyewe? Naam, inawezekana!

Wapo watu wengi wenye mahitaji maalum ambao wanatafuta neno la kuambiwa 'unaweza' na hawapati. Wapo wazazi na walezi ambao wanataabika kisaikolojia kwa kutokujua namna ya kukaa na watoto wao wenye mahitaji maalum- wanashindwa kupata mtu wa kusema 'mwanao ni mzuri na anaweza kufanya abcs'.

Sote tufikiri juu ya hilo!



No comments: