Sunday, January 24, 2016

Ukishindwa Kuwajengea furaha, basi angalau usiwe sehemu ya Maumivu yao

Katika maisha kwenye jamii zetu jukumu letu kuu ni kusaidiana. Tunapaswa kuwa wajenzi wa furaha kwa watu wenye ulemavu, na kwa watu wote ambao wanaonekana kwa namna moja ama nyingine wamekandamizwa na mifumo ya jamii zetu. Hii ni kwasababu tayari asili (nature) imeshaharibu furaha yao ya asili.

Kama tumeshindwa kuijenga furaha yao, tumeshindwa kuwasaidia kwa hili au kwa lile; basi angalau tujitahidi tusiwaumize, na wala tusiwe sehemu ya watu wajengao maumivu kwenye maisha yao.

 

Tuishi kijumuishi... Tutende kijumuishi.... Tujenge taifa jumuishi

Tuweke Mkazo wa Kuwajengea Uwezo Kijamii Watu Wenye Ulemavu

Nimeona utofauti mkubwa wa mtu aliyepata ulemavu wa kuzaliwa na ule wa ukubwani kwenye maisha. Dhana ya ulemavu inaogopwa kuliko hata ulemavu wenyewe. Watu hawataki kusikia habari za ulemavu kwenye masikio yao. Nimeshuhudia watu wenye ulemavu wakihojiwa na media, wengi wetu ambao tumezaliwa na ulemavu tunaonyesha kuwa tumeendelea kuishi kwa sababu tu ya ubishi wetu juu ya kukataliwa kwetu, tunapuuza kukataliwa kwetu. Wenye machungu na magumu zaidi ni hawa wenzetu wanaoendelea kupata ulemavu ukubwani. Hawa wanajua jinsi walivyouogopa ulemavu, wakajitenga mbali na watu wenye ulemavu, wakaenda mbali zaidi kwa kudhani watu wenye ulemavu ni jamii ya pembezoni ukilinganisha na jamii ya watu wasio na ulemavu. Hii ni sababu tosha kuwa kundi hili la pili lipatapo ulemavu huyaona maisha magumu kana kwamba wameibeba dunia nzima kwa uzito.

Hakika, makundi yote haya yenye ulemavu (congenital and Acquired Disabilities) kwa pamoja yanahitaji huduma fulani ya Kisaikolojia ili kuwapumzisha mizigo ya fikra zao za muda mrefu. Ingekuwa vema tukawa na vituo vya kisaikolojia kwenye media zetu; mathalan magazeti, TV na redio ziweke programu kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya ulemavu. Hii itasaidia kuweka ufahamu wa jumla juu ya ulemavu, kuwaweka sawa kisaikolojia wanaoathiriwa na ulemavu na, pia kuweka akiba ya maarifa na kisaikolojia kwa wote ambao wanaweza kupata ulemavu ukubwani.

Fikiri Kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi