Saturday, November 2, 2013

Hali ya Elimu Tanzania Iko ICU


Hali ya elimu Tanzania inaendelea kukaa vibaya na itazidi kuwa mbaya hadi hapo wavamizi wa elimu watakapoiacha huru tena ikiwa kwenye mikono salama ya wanaelimu.

Tatizo kubwa hapa Tanzania ni kwamba kila mtu anadhani anaifahamu vizuri elimu. Wanasiasa wasio na utaalam wa elimu wanafanya maamuzi ya kitaalam kuhusu elimu bila kuwashirikisha wataalam wa elimu. Walimu wamepuuzwa, wamebezwa, wameonekana hawafai. Inafika mahali watu wenye madaraka katika nchi hii wanasema kama walimu wameona ualimu haulipi waende wakatafute kazi nyingine. Kauli hizi ni za watu wasioitakia mema nchi yetu.

“Big Result Now” nasema haiwezekani mpaka walimu waheshimiwe, warudishiwe utu wao, waachiwe wafanye mambo ya kitaalam kuhusu elimu. Kila mwanasiasa anaongea anachoweza kuhusu elimu, waende wakafundishe tuone kama wanaweza. Majina mazuri, slogan nzuri na misemo mizuri si utendaji.

Division Five nayo iko mbioni na ni lazima ilete majanga. Naionea huruma sana sekta ya elimu, itakaa utumwani kwa miaka mingi kama wana wa Israel hadi hapo mkombozi wake atakapokuja. Huyu mkombozi bado hata hajatabiriwa, na haijulikani atatokea kona ipi.

Nasisitiza, mambo ya elimu waachiwe wanaelimu, maslahi ya walimu ni haki yao, waachiwe kilicho chao. Siasa itatuliwe na wanasiasa na mambo ya elimu yatatuliwe na wanaelimu. Nchi bila elimu iko gizani kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.


Pole Elimu, Poleni wanaelimu, Poleni wanafunzi, Pole nchi yangu. Japo nchi yangu iko ICU kielimu lakini hakuna juhudi yoyote kuinusuru na kifo kilichoikaribia. Elimu inaendelea kupambwa majina mazuri sana japo uhai wake umefikia mwisho. Salaam Big Result Now, Karibu Division Five. Na walimu wengi sasa watatoka hapa Division Five. 

Siko Tayari Kushuhudia Umauti wako Elimu, Nitafumba Macho yangu nisione ukitoa pumzi yako ya mwisho. Sitahudhuria mazishi yako wala kuja kuanua matanga. Ni msiba ambao haujawahi tokea kwa nchi hii tangu hayati baba wa taifa aanze kuiongoza Tanganyika hadi kufikia Tanzania. Si kwamba sikupendi elimu, bali waliokuteka ni hatari hata kwa maisha yangu pia.

Kwaheri Elimu, Kwaheri ya kuonana!