Saturday, August 31, 2013

UNGEJISIKIAJE KAMA UNGEKUWA MWENYE ULEMAVU?


"Ungejisikiaje kama wewe ungekuwa mtu mwenye ulemavu halafu wenzako wakakuona hufai kuishi, hufai kupata elimu, huna hadhi ya kula nao chakula, huna hadhi ya kuongozana nao na pia wakaona huna hata sifa ya kupata mwenzi wa kuishi naye kutokana na ulemavu ulio nao, na hata wakati mwingine unaona mazingira ya kukufanya kitega uchumi kuwa utolewe viungo vyako au uwe kafara kwa jamii????".

Tujifunze nyakati zote kwa faida, wakati wa kutosheka na wakati wa kupungukiwa, wakati wa kushiba na wakati wa njaa, wakati wa kuwa jangwani na wakati wa kujilaza kwenye mito ya baraka.


Pichani juu ni wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2012 wa shule ya viziwi ya Mwanga wakiimba wimbo wa kuwaaga wenzao kwa kutumia lugha ya alama. Kwa hakika, lugha ya alama imepunguza athari zitokanazo na ulemavu wa kutosikia (ukiziwi). Tunatakiwa kuwa na msimamo chanya juu ya watu wenye ulemavu kwa kujifunza na kuiendeleza lugha hii ya alama ili kujenga taifa jumuishi.


Binadamu ni kiumbe mwenye utashi, pia ni miongoni mwa wanyama wenye hulka ya kuambatana kimakundi. Binadamu anafundishika na anaweza akaumbika na kuumbiwa taaluma yeyote ile. Pia huyu binadamu anaweza umbiwa tabia zisizoridhisha kwenye jamii, lakini yote haya, yawe mazuri au mabaya mtu anahesabika kuwa anaweza akajifunza kitu kwa ajili yake mwenyewe na jamii kwa ujumla.

Watu wenye ulemavu na/au mahitaji maalum wanaweza wakajifunza kitu chochote kwenye jamii pale wanapokuwa wamewekewa misingi yote yenye kuwafaa na kuwawezesha binadamu. Mara nyingi haya hayawezi kuonekana sana mahali ambpo hakuna watu wengi wenye mahitaji maalum. Ukitaka kuona haya tembelea maeneo yenye shule za watu wenye mahitaji maalum, watoto viziwi wanafanya shughuli zote za kijamii na kiuchumi, watoto wasioona wanawajibika sawasawa na mtu mwingine yeyote kwenye jamii. Watoto wasioona wanaweza kucheza mpira wa miguu, wanaweza kupika chakula bila kusaidiwa, wanatumia simu na kompyuta pamoja na vifaa vingine vya kielektroniki kama wafanyavyo wengine.

Kwa miaka mingi sasa tumekosa sana utaalam na weledi kutoka  kwa watu wenye mahitaji maalum. Nilishangaa kuona mtu asiyeona anaweza kukariri namba za simu zaidi ya 300, anaweza akafundisha darasani kama mwalimu kupita walimu wengine, anaweza kuongoza familia yake na taasisi kuzidi huyu tunayemwita hana ulemavu, anaweza akawa na uchumi mzuri kupita wengine. Pia nimeona wasomi wengi wa uhakika tofauti na wengine wanaoghushi vyeti vya taaluma, wana mchango mzuri wa kimawazo hata zaidi viongozi wengine ambao tunaamini wamebobea kiuongozi.

Ni wakati mzuri sasa kwa watu wote kujenga tabia ya kuthaminiana kama binadamu. Kwa kufanya hivi itasaidia hata inapotokea mtu amepata ulemavu ukubwani aweze kumudu maisha mwenyewe, kwa wazazi ambao wanaweza wakazaa mtoto mwenye ulemavu waweze kuwa na utaalam wa kumlea mtoto wao kwa misingi ya kibinadamu.

Ukweli ni kwamba, binadamu yeyote yule lazima ana ulemavu ambao waweza kuwa mdogo sana, wa kujificha, wa kuonekana, unaoonyesha athari kwenye maisha yake au usioonyesha athari kwenye maisha. Upo usemi unaosema "ukimcheka kilema yawezekana na wewe ukazaa mtoto mlemavu au wewe mwenyewe ukapata ulemavu". Pia ipo methali isemayo "Hujafa hujaumbika" ikimaanisha, madam bado unaishi-unaweza ukapata ulemavu wa aina yoyote ile.

Kwa taarifa tu, ni kwamba kasi ya kuongezeka ulemavu kwa sasa ni kubwa kuliko hapo zamani. Mfano, ni watoto wangapi wanaanza kuvaa miwani wakiwa darasa la tatu hadi la saba? Ni ajali ngapi za gari na pikipiki zinatokea kwenye jamii zetu? Ni shehena ngapi za vyakula kutoka nje vikiwa na sumu ya kuharibu seli za binadamu? Ni watoto wangapi waanaharibiwa ubongo na madaktari wakati wa kuzaliwa? Ni watu wangapi wanaugua malaria sugu na kuharibu ufahamu wao ambao tumezoea kuwaita vichaa? Ni mara ngapi umeona mtu ana msongo wa mawazo ambao unampelekea kuharibu mfumo wa ubongo wake? Ni kesi ngapi unasikia eti mzazi amempiga mwanae kwenye masikio na kumsababishia ukiziwi?

Tuungane kujifunza mambo yote yanayohitajika kumsaidia mtu mwenye ulemavu, tupate ufahamu juu ya hatari zinazoweza pelekea mtu kupata ulemavu, tujifunze kuwashirikisha watu wenye ulemavu ili nasi ikitokea bahati nzuri tukapata ulemavu nasi tusaidiwe na kushirikishwa kama binadamu wengine. Mbali na haya, tujifunze mapito ya milima na mabonde ambayo watu wenye ulemavu hupitia ambayo asilimia kubwa husababishwa na sisi tunaojiita hatuna ulemavu.




              Fikiri Kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi