Na Betty Kangonga
KUNA andiko katika Biblia Takatifu lisemalo kuwa; watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hivi ndivyo jamii yetu inavyoangamia.
Tunashindwa kufanyakazi na kujishughulisha ili kujikomboa kiuchumi lakini wapo baadhi ya wachache wetu katika jamii ambao wamebobea kuamini nguvu za giza zisizo na maana.
Hatua hiyo ndiyo inasababisha kundi hilo kuangaika usiku na mchana kuua ndugu zetu, wenzetu, jirani zetu watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino). Huko nyuma Serikali iliamua kuchukua hatua kuwasaidia ndugu zetu hawa ambao wamekuwa kama wakimbizi ndani ya taifa lao.
Wamekuwa wakiwindwa kama wanyama na kundi hilo ambalo limepofushwa macho na akili pia na kufikia kuua binadamu wenzao. Huko nyuma baada ya mauaji ya wenzetu hawa kushika kasi, serikali iliamua kusaidiana nao kwa kiasi na kujaribu kutoa ulinzi.
Nimeshindwa kuelewa ulinzi huo wa serikali uliishia wapi maana hadi sasa bado vilio, simanzi, huzuni zimetawala kwa ndugu zetu hawa. Hawana uhakika wa kuishi wamekuwa kama watu wasio na uhakika hasa inapofika usiku.
Maana wanajua watoa roho zao wanaweza kuwafikia wakati wowote. Hivi kundi la wauaji hawa wanashindwa kupembua akili zao na kupata utashi kuwa damu za ndugu zetu hao wanaowaua ni laana kwa taifa hili? Au wanafikiri kuwa watabaki wao salama?
Pamoja na kuwa tunaweza kujiondoa katika dhambi hiyo lakini bado kama taifa tutaadhibiwa tu, maana swali la kujiuliza tumefanya jambo gani kuhakikisha wenzetu hawa wanabaki salama? Je, tumeamua kuwa kimya ni kutokana na mauaji kupungua?
Mbona hadi sasa mauaji yanaendelea kila kukicha, huku serikali ikiwa kimya katika kupambana na tatizo hilo. Ni nani aliye nyuma na mauaji ya albino? Kama tutashindwa kutafuta njia ya kuwasaidia ndugu zetu hawa nina hakika taifa hili halitakuwa salama kamwe.
Tunahitajika kusimama kwa umoja wetu tunaouhubiri kila kukicha kudai haki za wenzetu hawa kuishi. Yupo wapi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi? Yupo wapi Waziri wa Sheria na Katiba? Mbona wapo kimya kama vile hawaoni mauaji hayo.
Katika kusoma kwangu nakumbuka, mwaka 1977, Waziri Ali Hassan Mwinyi alilazimika kujiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Mambo ya Ndani kutokana na kukiukwa kwa utawala wa sheria na haki za kibinadamu.
Matukio yaliyomlazimisha Mwinyi ajiuzulu yalitokea Kanda ya Ziwa na yalihusiana na imani za kishirikina pia. Baadaye Mwinyi akafanywa kuwa Balozi wetu Misri.
Mbona sasa Serikali ipo kimya au imeenda likizo? Mbona hawa mawaziri hawaoni uzito wa tatizo hilo? Au kwao sio tatizo, tatizo kwao ni vifo vya watu wengi zaidi kwa wakati mmoja ndiyo wainuke na kutoa matamko yasiyo na tija.
Kuna mkakati upi wa kufanya msako kuwabaini wauaji hao? Ama serikali inaona ni vigumu kuwabaini kama ilivyo katika masuala mengine? Mbona tumekuwa tukisikia kuna vitengo vya intelejensia kwani hivi vinaishia wapi?
Katika hili Serikali inapaswa kuja na maamuzi magumu na sio majibu mepesi kama yanayotolewa sasa, tena tunahitaji maamuzi mengine ya haraka yatakayoweza kuleta amani.
Kama itapuuzwa basi tukubali kuwa wapo wanaoweza kuchukua maamuzi magumu ambayo yanaweza kuleta kukiukwa kwa utawala wa sheria na haki za kibinadamu. Yatatuongezea machungu zaidi kuliko kuponyesha majeraha tuliyo nayo.
Ni lazima tufikiri kwa bidii. Tujiulize, ni nini kitatokea baada ya wimbi la mauaji ya albino? Kuangamia kwetu kwa kukosa maarifa ndiyo kulichangia kwa kundi lingine huko nyuma wakaibuka na kuwasaka kisha kuua watu wenye vipara.
Wakatokea wachuna ngozi pia. Naam. Tulifatute shina la tatizo, tushughulike nalo. Tukipuuzia hili la kufikiri kwa bidii kuna hatari ya kuiingiza nchi kwenye matatizo makubwa.
Wapo wasomaji watakaoona kuwa nalalamika lakini ni muhimu kulalamika sasa wakati kuna uwezekano wa kukabiliana na hilo, lakini tukisubiri tuje kulalamika wakati mambo yameharibika hakuna anayeweza kubaki salama.
Hivyo ni wakati muafaka kwa viongozi wa dini pia kutumia karama zao walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwafungua watu akili na mawazo yao, ili waelewe kuwa utajiri na heshima vinatoka kwa Mungu.
Hakuna aliyewahi kuua sio albino tu hata binadamu aliyekamilika akabaki salama, ni lazima tuondoke huko tulipo, sio busara hata kidogo waganga wa kienyeji kutudanganya na kutusababisha tuumizane na kuwindana kama wanyama.
Lakini, kwa sasa, iwapo wimbi hili la kuua albino litaendelea, na hao wauaji ninaowaita majuha wakabaini kuwa dawa ya albino inafaa kwa siasa pia, albino wetu watakwisha, na watakaowamaliza ni wanasiasa.
Ni wazi kuwa mauaji ya albino yanatia woga, ghadhabu, fedheha na kinyaa kwa taifa. Hawa ni binadamu ambao maisha yao yanakatishwa kwa vitendo vya kinyama vinavyotokana na imani zisizokuwa na msingi na ambazo hazitarajiwi kujitokeza katika jamii yenye watu wa kutosha wenye akili timamu.
Hakuna shaka kwamba, kutokana na vyanzo mbali mbali zimekuwa zikieleza kuwa, albino wanauawa kwa sababu wapo watu wanaoamini kwamba vipande vya viungo vyao vinaweza kufanyiwa mazingaombwe na vikawatajirisha wale wanaofanyiwa uganga huo, ni ujuha na uhayawani kuamini hayo.
Ndiyo maana nasema hivi tunaangamia kwa kukosa maarifa, kuna ujinga unatokana na ukosefu wa elimu, na nchi yetu imekuwa ikiwekeza katika ujinga kwa muda mrefu, kiasi kwamba, kama kungekuwa na kufuzu katika fani hii, si ajabu tungekuwa tumesha shiriki katika mahafali ya kuhitimu.
Maana haiwezekani kundi hili la wajinga wachache wakaendelea kushika hatamu ya kuua wenzetu hawa na kama taifa linaendelea kufumbia macho na kunyamaza kimya.
Pia uroho wa madaraka na kupata fedha za haraka nalo ni tatizo lingine linalofanya mauaji hayo kuzidi kushamiri. Si tunashuhudia watawala wetu wanavyotafuna uchumi wa nchi hii bila huruma.
Uroho umekuwa ni sehemu muhimu ya jinsi tunavyoendesha mambo yetu kiasi kwamba inakuwa vigumu kumtambua yeyote ndani ya siasa na utawala ambaye hajihusishi na uroho wa aina moja au nyingine.
Uroho na tamaa ya kutajirika haraka haraka.Huu ndiyo ninaouona unazidi kuchipuka kwa kuwa wanaamini kuwa kuua albino ndiyo mwanzo wa ujinga wa kushindwa kupambanua mambo.
Kuna haja ya vyombo vya usalama kuchukua hatua kali dhidi ya majuha hawa hatari. Lakini haitasaidia sana iwapo mbegu za ujinga tulizozipanda miongoni mwa watu wetu zimezaa matunda kama tunavyoona.
Njia ya kumaliza tatizo hili ni kung’oa magugu haya na kuyachoma, na kupanda mbegu mpya za elimu ambayo ni elimu, sio ujinga unaoendelea kupandikizwa na waganga waongo ambao ni wachumia tumbo.
La sivyo mauaji hayo yataendelea kutufanya na kutudhalilisha kuwa taifa la wajinga mbele ya mataifa mengine. Tunapaswa kuondoa ujinga huo haraka kabla haujaenea kwa kizazi kingine.
Chanzo: Tanzania Daima