Mwanafunzi mwenye mahitaji maalum anamhitaji mwalimu mwenye taaluma ya elimu maalum; pia mwalimu wa elimu maalum anamhitaji mwanafunzi mwenye mahitaji maalum. Ni mtegemeano wa aina yake.
Tanzania, kama nchi zingine duniani, ina wanafunzi wenye mahitaji maalum. Pia ni bahati iliyoje kuwa na vyuo vyenye kutoa elimu maalum kwa walimu ili kukidhi mahitaji maalum ya wanafunzi hao wenye mahitaji maalum.
Hata hivyo kuna kila dalili ya kushuka kwa huduma za elimu maalum nchini Tanzania. Walimu wengi wanaomaliza kozi za vyuo vya elimu maalum wamekuwa wakipangiwa shule za kawaida (normal schools) zenye watoto wasio na mahitaji maalum.
Kwa upande mwingine wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini wameendelea kuwepo mitaani bila kwenda shule kwa kigezo kuwa hakuna walimu wa kuwafundisha hawa watoto.
Elimu jumuishi bila mipango inaumiza wachache.
HOJA
Walimu wenye fani ya elimu maalum wapelekwe kwenye shule maalum za watoto wenye mahitaji maalum; sambamba ni hilo, pia kuanzishwe shule maalum kwa watoto hao kwenye maeneo yasiyo na shule hizo. Zipo wilaya nyingi zisizo na shule maalum, mfano halisi ni wilaya ya Mvomero, haina shule za viziwi na wasioona.