Kwa asilimia kubwa, ulemavu wenyewe
sio tatizo, bali mtazamo wa jamii juu ya ulemavu huo ndio tatizo kubwa zaidi.
Ukiacha ulemavu unaohusisha ubongo, ulemavu mwingine wote una faida ya
kumwongezea akili nyingi mhusika mwenye ulemavu. Anakuwa na maisha ya utafiti
wa kila siku juu ya tabia za binadamu na utamaduni wao. Ulemavu unaleta hamasa
ya ugunduzi wa asili wa binadamu na tabia zake.
Hata hivyo, maisha ya ulemavu
yamejaa kuanguka na kusimama kwa nyakati tofauti kutokana na tamaduni kinzani
juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Nafsi rahisi (easy minds) za watu wenye
ulemavu na washirika wao huanguka kwa anguko kubwa kwenye maisha ya kila siku. Hii
inatokana na uzito na ugumu wa taratibu za mila na desturi kwenye jamii zetu. Pia
kumbuka kuwa ukiona mtu shujaa mwenye ulemavu kwenye kila jambo ujue kapigana
kwa nguvu zana ili kushinda mapito hayo. Mtu mwenye ulemavu hukutana na maneno
makali yenye kukatisha tama, vitendo vya ukinzani, mitazamo kinzani kama tufani
ya bahari, kila hatua ya makuzi na maisha yake ni ukinzani tupu. Ndio maana
kuna makabila fulani ya kitanzania wakiona dalili ya ulemavu kwa mtoto mchanga
wanamuua siku ile ile ya kwanza kwa kisingizio kuwa si “riziki”.
1. Athari ya kiuchumi
Familia nyingi zenye watoto wenye
ulemavu, hasa wa akili zinakumbwa na ugumu kiuchumi kwa kuwa muda mwingi
wanatakiwa wawe na watoto wao wenye ulemavu. Hali hii inapelekea wazazi hao
kuacha kazi zao za kiuchumi. Zipo shuhuda nyingi kwa watu ambao nimepata
kuongea nao wenye watoto wenye ulemavu.
2. Athari za kijamii
Jamii zetu zina mtazamo hasi juu ya
ulemavu. Mtu mwenye ulemavu amekosa sifa kwenye jamii, anaonekana ni mtu
tegemezi, hana haki, mnyonge, amelaaniwa na matokeo yake ni kutengwa na jamii
yake. Nimeona watu wengi ambao kabla ya kuwa na ulemavu walikuwa maarufu
kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini mara walipopata ulemavu “status” zao
zilibadilika.
3. Athari za kimazingira
Watu wenye ulemavu wa aina
mbalimbali wanatakiwa watengenezewe njia wezeshi kwa maisha yao, yaani “deviated
programs and means for people with disabilities”. Tumepungukiwa vifaa jumuishi.
Mazingira mengi ya watu wenye ulemavu ni changamoto.
4. Sera za nchi
Zipo sera za watu wenye ulemavu na
zingine kama miongozo kwa maisha ya wananchi kwa ujumla. Sera za watu wenye
ulemavu ni ngumu kutekelezeka, na zile jumla hazina dalili ya ukaribu na mtu
mwenye ulemavu.
Ushuhuda: Kuna rafiki mmoja ambaye
ni mwalimu kipofu. Aliomba kazi ya kufundisha kwenye shule ya binafsi, kwa vile
ufaulu wake ulikuwa mzuri walimwita kwenye usaili. Alipofika wakamwona kipofu,
wakamwambia kwa kimombo”we need a teacher but not you, sorry for that.”
Wakaongeza kusema: “Hatukujua kama wewe ni kipofu”.
Kiukweli ipo mifano mingi ya aina
hiyo!
5. Utu wa mtu mwenye ulemavu
Fanya jaribio la uchunguzi: Fuatilia
mahali ambapo ghafla ametokea mtu mwenye ulemavu usikie maneno ya watu juu
yake. Hata kama hawasemi chochote utaona “facial expressions” zao tu. Kiukweli utagundua
ya kuwa kwa mitazamo ya jamii zetu mtu mwenye ulemavu anawekwa kwenye jamii ya
upili. Kila mtu hufikiri ana mamlaka juu ya mtu mwenye ulemavu, mtu mwenye
ulemavu hakui kwenye jamii, siku zote hufikiriwa ni tegemezi, ana akili za
kitoto, na kila afanyacho huonekana si sahihi.
Ugumu kwa wapatao ulemavu ukubwani
ni ile hali ya kuzoea aina mpya ya maisha. Marafiki hupungua, imani ya watu
kwake hupungua. Hii hali huwafanya watu hawa wenye ulemavu kuishi maisha ya
simanzi siku zote.
Ushuhuda
Mwanafunzi wangu mmoja wa zamani
alipata ajali na kukatwa mguu (unyayo wote), amekuwa na mazingira magumu sana. Amekuwa
ni mtu wa kutoa machozi tu akifikiria ugumu anaoupata.
Usione shida kwa msisitizo ambao
huwa nautoa kila siku juu ya mambo ya watu wenye ulemavu. Ukichunguza kwa
makini haya madhara ya mtu kuwa na ulemavu unakuta mtu asiye na ulemavu
anaogopa neno “ulemavu” kuliko ulemavu wenyewe. Akisikia habari za ulemavu na
watu wenye ulemavu anahisi masikio yanapata kuumia. Kwa hakika, ulemavu
unamgusa kila mtu kwa namna yake.
Je, ulishawahi kujiuliza mapito ya
watu albino nchini? Mapito ya watu albino na watu wenye ulemavu mbalimbali ndiyo
sababu kubwa inayonifanya niendelee kuzungumzia masuala ya ulemavu kwa kadri
Mungu anavyoniwezesha kuwa na uhai kwa manufaa yetu sote. Tujifunze juu ya
ulemavu, tujifunze tunavyoweza kuishi na ulemavu na/au watu wenye ulemavu.
Tufikiri Kijumuishi…..Tutende
Kijumuishi……Tujenge Taifa Jumuishi…