Kwanza kabla ya yote niseme tu kuwa ukiona mtu anaelewa haraka juu ya mambo ya watu wenye ulemavu ujue kuwa kwa namna moja au nyingine aliwahi kupata aidha kwa ndugu wa karibu mwenye ulemavu na/au ana rafiki mwenye ulemavu.
Watu wengi ambao nimeongea nao inonyesha kuwa walishaguswa na huu ulemavu, iwe kwa watoto wake, wazazi wake, wenzi wao, na watu wao wengine ambao ni wa karibu sana.
Nimegundua kuwa masuala ya ulemavu hayazungumzwi sana kwenye jamii kutokana na tamaduni zetu.
Watu wamefanya ulemavu kuwa ni siri kubwa. Watu wengi wenye ndugu zao wenye ulemavu wanawafungia ndani ndugu hao wenye ulemavu, wamewakosesha fursa ya elimu na haki ya kuchangamana na jamii. Hii ni kwa sababu elimu juu ya watu wenye ulemavu na ulemavu wenyewe haitiliwi mkazo.
Watu wengi wakishindwa kutafsiri masuala ya ulemavu kitaalam hujikita katika imani za dini, na kishirikina. Wengi kwa imani huamini kuwa mtu kupata ulemavu ni laana ya ukoo. Wababa wengi wamewakimbia familia zao (wake wao wazaao watoto wenye ulemavu) zenye watoto wenye ulemavu.
Kwa hakika ulemavu umetafsiriwa na binadamu kwa ajili ya binadamu. Kila binadamu ni mhanga wa ulemavu. Tuvumiliane, tuheshimiane, tusaidiane inapobidi, tuuangalie uthamani wa binadamu na ubinadamu wake. Ulemavu ni sehemu tu ya haiba ya mwanadamu.
Je, una mtoto mlemavu?, rafiki mlemavu?, mzazi mlemavu?, mwenzi mlemavu? au wewe mwenyewe una ulemavu?
Usijali maneno na mitazamo ya watu wengine juu ya ulemavu huo. Ishi kwa kadri ulivyojizoeza!
Fikiri Kijumuishi...Tenda Kijumuishi....Jenga Taifa jumuishi!
No comments:
Post a Comment