Simulizi ya Mheshimiwa January Makamba
Kazi
yangu kumhudumia Mark miaka 17 iliyopita na ninayojifunza katika maisha ya kila
siku.
Niliandika
kumbukumbu hii mwaka jana mwezi Novemba nikiwa safarini kwenda Magu.
Nilimkumbuka rafiki yangu wa zamani aliyekuwa na matatizo ya akili, rafiki
ambaye sitamsahau. Mwaka 1998, mwaka mmoja baada ya kufika nchini Marekani kwa
masomo yangu ya Chuo Kikuu, nilitafuta na kupata kazi ya muda katika majira ya
joto katika jiji la Boston kuhudumia wagonjwa wa akili katika nyumba ambazo wagonjwa
hao huwekwa kwa uangalizi maalumu. Kazi ya namna hii ilikuwa kazi ya kawaida
kwa wanafunzi na wahamiaji kama mimi katika kujikimu kwa kipato - ilikuwa
rahisi kupata, masaa ya kufanya kazi uliweza kuyapanga kwa namna nyingi, malipo
yalikuwa ya kuridhisha, na uliweza kuendelea na masomo chuoni huku ukifanya
kazi.
Boss
wangu alikuwa mtu mwenye kuelewa wafanyakazi wake na hali zao kwa ukaribu,
Mmarekani mwenye asili ya Ugiriki kwa jina la Nick. Alianza kunipanga kazi kwa
wagonjwa ambao hawakuwa katika hali mbaya, ambao wakati mwingi walikuwa sawa na
ambao walikuwa katika mwelekeo wa kurudi katika maisha ya kawaida bila
kusimamiwa na watu wengine. Kazi yangu ikawa kuwapeleka kwa madaktari miadi yao
ya kupelekwa inavyofika kuendana na ratiba, kuhakikisha wanameza dawa kwa
wakati, kuwapeleka katika mafunzo ya kazi ili kujiandaa kurudi katika maisha ya
kawaida na wakati mwingine kuwapeleka kwenye kazi zao halisi - baadhi walikuwa
waosha vyombo katika migahawa maarufu ya MacDonald's, walinzi kwenye maduka
makubwa ya bidhaa, n.k; ikimaanisha kwamba kazi yangu wakati mwingine ilikuwa
kuwatazama wao wakifanya kazi zao. Mara nyingi hakukuwa na tukio la ajabu
isipokuwa mara chache ambapo unakuta mmoja wao anakasirika ghafla na kufanya
fujo kiasi ambapo ilinibidi kuingilia kati na labda kutatua au kumrudisha
katika nyumba ambapo tulikuwa tukiwahudumia.
Kazi
hii ilihitaji kupewa mafunzo ya namna ya kuhudumia watu na uelewa wa hali ya
juu wa historia ya mgonjwa ikiwa ni pamoja na kujua maneno gani ukitumia kwa
mgonjwa fulani yangeweza kumtuliza kama hali yake kiakili ingebadilika ghafla.
Kazi pia ilihitaji uwe na leseni ya udereva, na mimi nilikuwa ndio nimepata
leseni lakini nilikuwa sijawahi kuendesha gari mjini mbali na wakati niko
mafunzoni, kwa hiyo sikujua njia kwenda huku na kule. Siku moja boss wangu Nick
akaacha ujumbe wa maandishi kwamba niwapeleke wagonjwa kwa daktari sehemu moja
inayoitwa Lynn, hapo Boston. Kwenye karatasi aliandika pia anuani ya sehemu
anakopatikana daktari, akaniachia na funguo za gari. Mmoja ya wagonjwa ambaye
alikuwa katika kundi la ninaopaswa kuwapeleka kwa daktari akasema anapajua
Lynn, alipo daktari ni wapi na angenielekeza njiani hadi tufike. Baada ya
dakika kama kumi za kuendesha gari tukielekea Lynn, akawa amesahau! Tukapotea
na kuzunguka mjini, hatukula siku nzima, tukakosa kumuona daktari, wakakosa
kumeza dawa kwa wakati. Wakapoteza subira na walikuwa karibu kuanza kugombana
na mimi.
Nick
alipigiwa simu na daktari masaa mawili baada ya muda wa miadi kupita kwamba
mimi na kundi la wagonjwa tulikuwa hatujafika kwake. Akapata mshangao, asijue
la kufanya. Sikuwa na simu, gari lilikuwa na simu (outbound-only) lakini sikuwa
nafahamu namna ya kuitumia. Nilichofanya ikabidi niendeshe hadi kwa Polisi
wanaosimamia Barabara Kuu (Highway Police) ambao walituongoza hadi nyumbani.
Nilijua siku ile ningefukuzwa kazi bali Nick alinielewa, hakunifukuza lakini
ikabidi kulipia kosa lile kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Baada
ya hapo Nick akanihamishia kwenye nyumba nyingine ambayo ilikuwa na mgonjwa
mmoja tu - Mark. Mark alikuwa na umri wa miaka 37 lakini alikuwa na mwili kama
wa mtoto wa miaka 10. Mark alikuwa na akili nyingi (super-genius) mwenye uwezo
mkubwa wa kuweka kumbukumbu, uwezo katika hisabati na utaalamu wa kompyuta.
Sijawahi kukutana na mtu aliyejaliwa vipaji katika hayo kama Mark. Lakini Mark
alikuwa na magonjwa mengi ya mishipa ya fahamu, magonjwa ya kupenda jambo
kupita kiasi (Obsessive Compulsive Disorder), ulevi wa madawa ya kulevya, pombe
na mengine mengi. Alikuwa ametumia madawa mengi, mengi sana katika kutibiwa
ambayo yalikuwa na athari hasi pia katika mwili wake. Mark alikuwa na ratiba ya
kipekee kabisa - na kabla ya kupangiwa kazi ya kumhudumia ulipatiwa mafunzo kwa
wiki mbili. Mark alikuwa mpole lakini angeweza kudhuru pia. Alikuwa pia mwongo
mwerevu na angeweza kupima kiwango cha uvumilivu cha mtu yeyote hadi uvumilivu
wa mtu huyo ufikie kikomo kwa kukuchezea akili.
Hakuna
aliyetaka kupangwa amhudumie Mark, angekuchosha kimwili na kiakili - macho yako
yalitakiwa yawe naye wakati wote hata akiwa chooni kwa sababu kuna nyakati
alikuwa akijiumiza mwenyewe makusudi. Akipangiwa mfanyakazi mpya, Mark alikuwa
anazunguka nyumba nzima kwa haraka haraka na kukuagiza hiki na kile kwa masaa
matatu bila kupumzika ili tu akuchoshe halafu anakuuliza, "Hujioni mjinga
kunifuata muda wote?" Tabia yake mbaya zaidi ilikuwa kukimbia toka
nyumbani na kwenda kwenye duka lolote karibu la vinywaji kisha anachukua chupa
ya bia au wiski (bila kulipa) na kuinywa yote kwa mkupuo kisha anazimia. Kwa hiyo
kumhudumia Mark ilibidi milango yote ufunge na funguo uzitunze, lakini Mark
alikuwa na tabia ya kuwachomolea funguo wale waliokuwa wanamhudumia.
Mark
alifanya kitendo hiki cha kukimbia, kuchukua pombe madukani na kunywa mara tatu
wakati mimi nikiwa namhudumia. Wakati mmoja kwa sababu alikuwa na umbo dogo
sana alijificha kwenye mashine ya kufulia nguo. Nilimtafuta nyumba nzima lakini
sikufanikiwa kumpata, nilipofungua mlango kuangalia nje akapata upenyo akatoka
nje na kujificha nyuma ya nyumba kwenye maua marefu, sikumuona na niliporudi
ndani akaondoka. Baadaye nilimkuta katika duka la jirani na alikuwa
ameshakunywa nusu lita ya dawa ya kuosha mdomo - Listerine. Kumbe Listerine ina
kilevi ndani yake.
Mark
alikuwa na haki zake ambazo tulipaswa kuziheshimu. Alikuwa na haki ya kwenda
nje ya nyumba lakini chini ya uangalizi wangu, kununua vitu lakini sana sana
kuvua samaki. Alikuwa ana mapenzi ya kupitiliza na uvuvi wa samaki. Alikuwa na
haki ya kutumia kompyuta kwa lisaa limoja kwa siku - na mimi nikiwa nyuma yake
nilipaswa kutazama kila anachofanya. Ikiwa ni moja ya matatizo yake kiakili
Mark alitaka kuwa mbele ya kompyuta yake saa kumi na mbili kamili jioni, sio
kasoro, wala na dakika 5, 6, hapana. Kumi na mbili juu ya alama. Kikubwa
alichokipenda katika kompyuta ni kupiga soga - chatting, wakati huo AOL chat
ilikuwa maarufu. Nilipaswa kutazama hizi chats zake na kujua anafanya nini,
ilikuwa ni sehemu ya kazi yangu, lakini kiukweli sikuweza kwa sababu Mark
angeweza kuwa na chats katika kurasa mbalimbali kama 12, zote kazifungua na
anapitia moja baada ya nyingine kwa kasi kama ya upepo, zote 12 kwa wakati
mmoja.
Siku
moja, Mark, kirafiki akaniambia anajua siri yangu: kwamba natumia leseni feki
ya udereva. Haikuwa kweli. Akasema anataka kunionyesha tofauti kati leseni feki
na leseni orijino. Kwa hiyo nikatoa pochi yangu mfukoni pamoja na leseni na
kadi zangu za benki. Haikupita dakika moja baada ya kuziangalia kadi zangu
akawa ameshakariri taarifa zangu za kadi ya benki - tarakimu zote 16, tarehe ya
mwisho kutumika, n.k.
Siku
iliyofuata saa tatu asubuhi kengele ya mlango ikagongwa, haikuwa kawaida.
Nikaenda mlangoni na kukutana na kina dada wawili ambao walionekana wanafanya
biashara ya kujiuza wakiwa mlangoni na kuniuliza kama pale ni anuani sahihi ya
Mr. Makamba. Mark alikuwa ametumia kadi yangu ya benki kuagiza kina dada
wanaojiuza kupitia mtandao wa intaneti. Nilipowaonyesha mshangao na kuwaambia
kwamba sijui lolote, Mark akaniomba tuongee pembeni kidogo. Alikubali kwamba
alifanya kitendo kile na kuniambia, "Usiwe na wasiwasi, wewe ni mwanaume,
chukua mmoja ambaye unamtaka nami nitachukua mwingine". Sikujua nicheke au
nimchape kibao. Nikawaambia wale kina dada waondoke, nao wakaondoka. Baadaye
Nick alinirudishia fedha ambazo Mark alitumia kuagiza huduma hiyo toka katika
akaunti yangu.
Mark
hakuwahi kukaa na mfanyakazi mmoja zaidi ya wiki tatu, kwa sababu aliwachosha
na watu kuamua kuacha kazi na pia kwa sababu kila wakati alitaka mfanyakazi
mpya. Alikuwa anakusoma haraka na kama ulikuwa mpenzi wa mpira kwenye TV, yeye
angeomba umpeleke kuvua samaki wakati mpira unaanza. Kwa kuwa ingekukera
angesema kitu gani umpe ili akuache utazame mpira. Wakati wa baridi japo bwawa
liikuwa limeganda barafu bado alitaka umpeleke kuvua samaki, niliambiwa kwamba
kama angeona hupendi kabisa baridi angeomba umpeleke kuvua hadi mara tatu kwa
siku - na ili akuache labda umkubalie kufanya kitu ambacho hatakiwi kufanya.
Nilikaa
naye miezi miwili, Mark sasa hakuwa tena "mgonjwa" tu ninayemhudumia
bali rafiki. Tulielewana vizuri. Wakati nahamishwa kutoka kuwa mhudumu wake,
ilikuwa majonzi kiasi fulani, niliona upande wa pili wa Mark, Mark aliye na
hisia na nafsi ya kuumia kwa hisia kama binadamu wengine, kwa mara ya kwanza.
Alinikumbatia akaniambia: "Nitakukumbuka siku zote kwa kitu kimoja, hukuwahi
kunipiga wala kuniumiza". Mpaka wakati ananiambia maneno haya sikuwa najua
kama alitarajia katika muda niliomhudumia siku moja ningempiga.
Nimeandika
jina lake katika mtando wa Google leo kuangalia taarifa zake (Kwa sababu za
faragha sitataja jina lake la pili) lakini sikupata taarifa yoyote kumhusu.
Nimekutana na watu wengi maishani lakini Mark alikuwa mtu wa kipekee.
Lengo
la kuandika hili ni kwamba maisha yana mafunzo mengi - baadhi ya mafunzo haya
huja kutoka sehemu au watu tusiowatarajia. Nimejifunza uvumilivu katika
kumhudumia Mark. Nimejifunza pia kushukuru Mungu kwa kuwa na afya njema jambo
ambalo mara nyingi tunasahau. Nimejifunza kutohukumu na kuwa na chuki dhidi ya
wengine. Lakini pia nimefunza magonjwa ya akili yapo na wagonjwa wa akili nao
wana hisia na ubinadamu kama sote tulivyo licha ya magonjwa yao. Nimejifunza
pia jamii isiyo na mfumo na utamaduni kuhudumia watu wake wenye mapungufu bado
haijastaarabika. Hatuongelei sana kuhusu magonjwa ya akili Tanzania.
Tunawatelekeza haraka wagonjwa wetu wa akili na kusema ni kwa sababu tu ya:
uchawi, dawa za kulevya au laana. Ni muda wa kubadilika.
Tufikiri Kijumuishi ~~ Tutende Kijumuishi ~~ Tujenge Taifa Jumuishi