Wagonjwa
wenye vidonda vya kutisha, wenye nyuso zilizojaa simanzi, wengine wanaonekana
katika bonde la uvuli wa mauti na baadhi... Pengine wameshakata roho.
Hii ndiyo
picha halisi ya nini maana ya uuguzi na utaipata pale tu utakapofika hospitali.
Ni picha isiyopendeza machoni mwa wengi, wengi huishuhudia kwa lazima tu kwa
sababu ama wanaugua au wanauguliwa. Hivyo basi Theopista Kamugisha, haya
ni mazingira yanayompendeza, kumfariji na amekuwa katika mazingira haya kwa
zaidi ya miaka 38 sasa, kumi akiwa mzima, 28 akiwa kipofu.
Sista
Theo, kama wafanyakazi wenzake wanavyopenda kumuita, ni muuguzi katika
Hospitali ya Amana. Amekuwa hapa kwa kipindi kirefu sasa licha ya kuwa na
ulemavu wa macho, lakini bado anaendelea kuifanya kazi hiyo kwa mapenzi mazito
au tuseme ya kina hasa.
Namkuta
akiwa anampa ushauri mwanamke mmoja, ambaye anauguza mtoto wake.
Anamuhoji
uzito wa mtoto, chakula anachompa, umri na kipi kinachomsumbua mtoto huyo.
Anampima joto kwa kiganja cha mkono kabla ya kuanza kumpa ushauri.
“Unampa
chakula gani kwa sasa, pengine unatakiwa umbadilishie aina ya lishe kwa sababu
uzito wake bado ni mdogo’ anatoa ushauri sista Theo kwa mmoja wa wagonjwa
katika wodi ya watoto Amana.
Sista Theo
alizaliwa miaka 60 iliyopita mkoani Kagera. Alizaliwa akiwa mzima wa afya, bila
kasoro yoyote ile ya kimaumbile. Wazazi wake walimpeleka shule kama ada na
alifanikiwa kufaulu vyema masomo yake.
Ufaulu
huo, ulimuwezesha kuingia Shule ya Uuguzi, Ndolage (Ndolage Nursing School)
huko Muleba na baadaye aliongeza ujuzi zaidi, Katika Shule ya Uuguzi ya
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisomea Ukunga na Uuguzi.
Alianza
kufanya kazi, mkoani Kagera na baada ya kipindi kifupi tu, miaka ya 80
alianza kuugua maradhi ya macho, kitaalamu yanafahamika kama ‘Uveitis’. Ni
maradhi ya mzio ambao husababisha kuvimba na kuharibiwa kwa tishu za macho.
Maradhi haya huweza kusababisha mtu kuona kwa mbali au kushindwa kuona kabisa.
“Maradhi
yangu hayakuwa ya ghafla, nilianza kuumwa taratibu kwa maana ya kwamba, sikuwa
kipofu moja kwa moja bali, niliumwa macho na kutibiwa, napata nafuu na baadaye
nikawa kipofu moja kwa kwa moja,” anasema Sista Theo.
Ingawa
alikuwa akiumwa macho kwa kiasi kikubwa, Sista Theo, bado aliendelea
kufanya kazi yake kwa kipindi kirefu lakini ilipofika mwaka 1986, alikuwa
kipofu kabisa.
“Ulikuwa
ni wakati mgumu kwangu, niliumia roho nikijua kuwa sasa ndiyo mwisho wa taaluma
yangu ya uuguzi niliyoipenda. Ukweli ni kwamba, nilipungua uzito kilo 12 baada
ya kugundua kuwa siwezi kuona tena,” anasema.
Kilichomuumiza
Sista Theo, siyo kushindwa kuona tu, bali kitendo cha kushindwa kufanya kazi
yake, ambayo aliamini kabisa ni kipaji alichozaliwa nacho na kukipenda.
Hata
hivyo, madaktari walimpa moyo na kumfariji kwa kiasi kikubwa wakimwambia kuwa,
huo siyo mwisho wa maisha kwani cha muhimu ana taaluma yake kichwani.
“Waliniambia
nishirikiane na ofisi ya Ustawi wa Jamii ili wanisaidia katika michakato ya
maisha yangu na kitaaluma na nikafanya hivyo,” anasema.
Baada ya
kufarijiwa kiasi hicho, kufundishwa baadhi ya hatua za kufanya unapokuwa
mlemavu wa macho, aliamua kuanza maisha mapya.
“Sikutaka
kuacha taaluma yangu hata kidogo kwa sababu niliipenda hata kabla sijawa
kipofu. Namshukuru Mungu kuwa nina viungo vyangu vyote, nimesoma lakini sina
macho, kwa hiyo niliamini bado nina uwezo wa kufanya kazi yangu,” anasema.
Anasema,
kwa kuwa aliipata hali ya upofu akiwa tayari amesoma na ameshafanya kazi kwa
muda kwa hilo, aliweza kusonga mbele kwa kishindo.
Sista
Theo, aliendelea na kazi katika hospitali mbalimbali ikiwemo Ndolage,
Sinza, Mwananyamala na baadaye alihamia katika Hospitali ya Amana ambako yupo
kwa miaka zaidi ya kumi sasa.
Familia
Hata hivyo
Sista Theo anapohojiwa kuhusu watoto au familia yake, anasema hataki
kuzungumzia hilo kwani ni mambo yanayomrudishia kumbukumbu mbaya asizopenda
kuzungumzia.
“Nina
ndugu, jamaa na marafiki, wengine ninaishi nao nyumbani kwangu, wananisaidia,”
anasema.
Anafanyaje kazi?
Hapa
Amana, Sista Theo ana kazi kubwa ya kutoa ushauri kwa wagonjwa hasa wanawake na
watoto, katika wodi ya watoto.
“Nikifika
hapa hospitali asubuhi, kazi yangu kubwa ni kusikiliza ripoti za wodini, baada
ya kuzisikiliza, naanza kazi yangu ambayo ni kupita kitanda baada ya kitanda
kuwapa ushauri wanawake wajawazito na wale wenye watoto wagonjwa,” anasema.
Anasema
anaweza kutoa ushauri wa jumla kutokana ujuzi wake wa uuguzi na ukunga kwa
miaka mingi, lakini pia anapita kila kitanda na kuwahoji wazazi wanaouguza
watoto ili kuwapa ushauri wa lishe na afya.
Sista Theo
anasema, watu humuuliza maswali mengi kuwa anafanyaje kazi ya uuguzi akiwa
kipofu na yeye huwajibu hivi:
“Uuguzi ni
mambo mengi si kuchoma sindano au kufunga vidonda pekee. Jambo kubwa ni
kumfariji mgonjwa na kumpa ushauri. Watu wananishangaza wanapouliza mlemavu wa
macho anafanyaje kazi kama hii?” anasema.
Mkunga
huyu mkongwe anasema kuwa, hata kama angekuwa anaona bado angeendelea kutoa
ushauri kwa wanawake na watoto kwa sababu hilo ni jambo kubwa katika fani ya
uuguzi.
Changamoto
Katika
nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo walemavu bado hawapewi kipaumbele cha
kutosha, Sista Theo naye hakosi kukumbana na changamoto.
Anasema
changamoto kubwa anazokumbana nazo ni usafiri wa kutoka nyumbani kwenda kazini
kwake Amana, kila siku.
“Kuvuka
barabara ni kazi kubwa, kupanda basi ni kazi zaidi. Mvua zikinyesha ni tabu
zaidi. Hata hivyo bado nafurahia kwenda kazini kila siku,” anasema.
Anataja
changamoto nyingine na kusema:“ Kuna maneno wakati mwingine ya kuudhi kama vile
mtu anakuambia, kama huoni si ukae nyumbani tu,” anasema Sista Theo.
Hata
hivyo, Sista Theo licha ya kukutana na changamoto hizi njiani, akifika
hospitali hufarijika kwani wodini ni eneo linalomfariji na hasa anapopata
ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyakazi wenzake.
Ujumbe wake Siku ya Wanawake Duniani
Sista Theo
anasema, licha ya kuwa mlemavu, bado yeye ni binadamu kama binadamu wengine na
anafanya shughuli zake zote.
“Wanawake
walemavu wasijidharau. Wanawake wana karama kubwa ya kujenga jamii, kuwa
mlemavu isiwe sababu ya kufanya uketi chini, wanawake ni mama wa taifa,”
anasema.
Anasema
wanawake wanatakiwa wawe viongozi katika ngazi ya familia, wakipata watoto
walemavu wasiwaache wakae nyumbani bila kupata elimu na wasiwafiche nyumbani.
Sista
Theo anasisitiza kuwa: “Naipenda kazi yangu, na ninapenda kwenda kanisani kwani
huko ndiko ninakopata faraja ya maisha yangu, hasa ninaposikia neno la Mungu.”
Disability Is Not Inability ~~~ Ulemavu Si Kukosa Uwezo!
Chanzo cha habari hii: Gazeti la Mwananchi (LTD).
Chanzo cha habari hii: Gazeti la Mwananchi (LTD).