Sunday, March 9, 2014

Sista Theopista- Muuguzi kipofu kwa miaka 28!

Ni harufu ya dawa, damu,  mandhari iliyotawaliwa na bomba za sindano, dripu na mavazi meupe.
Wagonjwa wenye vidonda vya kutisha, wenye nyuso zilizojaa simanzi, wengine wanaonekana katika bonde la uvuli wa mauti na baadhi... Pengine wameshakata roho.
Hii ndiyo picha halisi ya nini maana ya uuguzi na utaipata pale tu utakapofika hospitali. Ni picha isiyopendeza machoni mwa wengi, wengi huishuhudia kwa lazima tu kwa sababu ama wanaugua au wanauguliwa. Hivyo basi Theopista Kamugisha, haya  ni mazingira yanayompendeza, kumfariji na amekuwa katika mazingira haya kwa zaidi ya miaka 38 sasa, kumi akiwa mzima, 28 akiwa kipofu.
Sista Theo, kama wafanyakazi wenzake wanavyopenda kumuita, ni muuguzi  katika Hospitali ya Amana. Amekuwa hapa kwa kipindi kirefu sasa licha ya kuwa na ulemavu wa macho, lakini bado anaendelea kuifanya kazi hiyo kwa mapenzi mazito au tuseme ya kina hasa.
Namkuta akiwa anampa ushauri mwanamke mmoja, ambaye anauguza mtoto wake.
Anamuhoji uzito wa mtoto, chakula anachompa, umri na kipi kinachomsumbua mtoto huyo. Anampima joto kwa kiganja cha mkono kabla ya kuanza kumpa ushauri.
“Unampa chakula gani kwa sasa, pengine unatakiwa umbadilishie aina ya lishe kwa sababu uzito wake bado ni mdogo’ anatoa ushauri sista Theo kwa mmoja wa wagonjwa katika wodi ya watoto Amana.
Sista Theo alizaliwa miaka 60 iliyopita mkoani Kagera. Alizaliwa akiwa mzima wa afya, bila kasoro yoyote ile ya kimaumbile. Wazazi wake walimpeleka shule kama ada na alifanikiwa kufaulu vyema masomo yake.
Ufaulu huo, ulimuwezesha kuingia Shule ya Uuguzi, Ndolage (Ndolage Nursing School) huko Muleba na baadaye aliongeza ujuzi zaidi, Katika Shule ya Uuguzi  ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisomea Ukunga na Uuguzi.
Alianza kufanya kazi, mkoani Kagera na baada ya kipindi kifupi tu, miaka ya 80  alianza kuugua maradhi ya macho, kitaalamu yanafahamika kama ‘Uveitis’. Ni maradhi ya mzio ambao husababisha kuvimba na kuharibiwa kwa tishu za macho. Maradhi haya huweza kusababisha mtu kuona kwa mbali au kushindwa kuona kabisa.
“Maradhi yangu hayakuwa ya ghafla, nilianza kuumwa taratibu kwa maana ya kwamba, sikuwa kipofu moja kwa moja bali, niliumwa macho na kutibiwa, napata nafuu na baadaye nikawa kipofu moja kwa kwa moja,” anasema Sista Theo.
Ingawa alikuwa  akiumwa macho kwa kiasi kikubwa, Sista Theo, bado aliendelea kufanya kazi yake kwa kipindi kirefu lakini ilipofika mwaka 1986, alikuwa kipofu kabisa.

“Ulikuwa ni wakati mgumu kwangu, niliumia roho nikijua kuwa sasa ndiyo mwisho wa taaluma yangu ya uuguzi niliyoipenda. Ukweli ni kwamba, nilipungua uzito kilo 12 baada ya kugundua kuwa siwezi kuona tena,” anasema.
Kilichomuumiza Sista Theo, siyo kushindwa kuona tu, bali kitendo cha kushindwa kufanya kazi yake, ambayo aliamini kabisa ni kipaji alichozaliwa nacho na kukipenda.
Hata hivyo, madaktari walimpa moyo na kumfariji kwa kiasi kikubwa wakimwambia kuwa, huo siyo mwisho wa maisha kwani cha muhimu ana taaluma yake kichwani.
“Waliniambia nishirikiane na ofisi ya Ustawi wa Jamii ili wanisaidia katika michakato ya maisha yangu na kitaaluma na nikafanya hivyo,” anasema.
Baada ya kufarijiwa kiasi hicho, kufundishwa baadhi ya hatua za kufanya unapokuwa mlemavu wa macho, aliamua kuanza maisha mapya.
“Sikutaka kuacha taaluma yangu hata kidogo kwa sababu niliipenda hata kabla sijawa kipofu. Namshukuru Mungu kuwa nina viungo vyangu vyote, nimesoma lakini sina macho, kwa hiyo niliamini bado nina uwezo wa kufanya kazi yangu,” anasema.
 Anasema, kwa kuwa aliipata hali ya upofu akiwa tayari amesoma na ameshafanya kazi kwa muda kwa hilo, aliweza kusonga mbele kwa kishindo.
 Sista Theo, aliendelea na kazi  katika hospitali mbalimbali ikiwemo Ndolage, Sinza, Mwananyamala na baadaye alihamia katika Hospitali ya Amana ambako yupo kwa miaka zaidi ya kumi sasa.
 Familia
Hata hivyo Sista Theo anapohojiwa kuhusu watoto au familia yake, anasema hataki kuzungumzia hilo kwani ni mambo yanayomrudishia kumbukumbu mbaya asizopenda kuzungumzia.
 “Nina ndugu, jamaa na marafiki, wengine ninaishi nao nyumbani kwangu, wananisaidia,” anasema.
 Anafanyaje kazi?

Hapa Amana, Sista Theo ana kazi kubwa ya kutoa ushauri kwa wagonjwa hasa wanawake na watoto, katika wodi ya watoto.
“Nikifika hapa hospitali asubuhi, kazi yangu kubwa ni kusikiliza ripoti za wodini, baada ya kuzisikiliza, naanza kazi yangu ambayo ni kupita kitanda baada ya kitanda kuwapa ushauri wanawake wajawazito na wale wenye watoto wagonjwa,” anasema.
Anasema anaweza kutoa ushauri wa jumla kutokana ujuzi wake wa uuguzi na ukunga kwa miaka mingi, lakini pia anapita kila kitanda na kuwahoji wazazi wanaouguza watoto ili kuwapa ushauri wa lishe na afya.
Sista Theo anasema, watu humuuliza maswali mengi kuwa anafanyaje kazi ya uuguzi akiwa kipofu na yeye huwajibu hivi:
“Uuguzi ni mambo mengi si kuchoma sindano au kufunga vidonda pekee. Jambo kubwa ni kumfariji mgonjwa na kumpa ushauri. Watu wananishangaza wanapouliza mlemavu wa macho anafanyaje kazi kama hii?” anasema.
Mkunga huyu mkongwe anasema kuwa, hata kama angekuwa anaona bado angeendelea kutoa ushauri kwa wanawake na watoto kwa sababu hilo ni jambo kubwa katika fani ya uuguzi.
Changamoto
Katika nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo walemavu bado hawapewi kipaumbele cha kutosha, Sista Theo naye hakosi kukumbana na changamoto.
 Anasema changamoto kubwa anazokumbana nazo ni usafiri wa kutoka nyumbani kwenda kazini kwake Amana, kila siku.
“Kuvuka barabara ni kazi kubwa, kupanda basi ni kazi zaidi. Mvua zikinyesha ni tabu zaidi. Hata hivyo bado nafurahia kwenda kazini kila siku,” anasema.
Anataja changamoto nyingine na kusema:“ Kuna maneno wakati mwingine ya kuudhi kama vile mtu anakuambia, kama huoni si ukae nyumbani tu,” anasema Sista Theo.
Hata hivyo, Sista Theo licha ya kukutana na changamoto hizi njiani, akifika hospitali hufarijika kwani wodini ni eneo linalomfariji na hasa anapopata ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyakazi wenzake.
Ujumbe wake Siku ya Wanawake Duniani
Sista Theo anasema, licha ya kuwa mlemavu, bado yeye ni binadamu kama binadamu wengine na anafanya shughuli zake zote.
“Wanawake walemavu wasijidharau. Wanawake wana karama kubwa ya kujenga jamii, kuwa mlemavu isiwe sababu ya kufanya uketi chini, wanawake ni mama wa taifa,” anasema.
 Anasema wanawake wanatakiwa wawe viongozi katika ngazi ya familia, wakipata watoto walemavu wasiwaache wakae nyumbani bila kupata elimu na wasiwafiche nyumbani.

 Sista Theo anasisitiza kuwa: “Naipenda kazi yangu, na ninapenda kwenda kanisani kwani huko ndiko ninakopata faraja ya maisha yangu, hasa ninaposikia neno la Mungu.”

Disability Is Not Inability ~~~ Ulemavu Si Kukosa Uwezo!

Chanzo cha habari hii: Gazeti la Mwananchi (LTD).

No comments: