Jina: Pendo Simon
Ulemavu: Kiziwi
Elimu: Shahada/Degree
Huyu hapa pichani ni dada mwenye fani mbalimbali
ambazo zinamtosha kujitegemea kwenye maisha yake. Pia anaweza akaisaidia jamii kwa namna ambayo wengi wasingeweza kuifikiria. Pendo Simon anaweza, ni mthubutu na mchapa kazi kwa kutumia fani alizonazo.
Fani zake
Ualimu
wa elimu maalum
Mchoraji
wa katuni
Designer
(kama vile T-shirt designs)
Pendo Simon amewahi kufanyia kazi kwenye
makampuni na asasi mbalimbali wakati akiwa bado ni mwanafunzi wa chuo kikuu. Kila
akipata likizo makampuni na taasisi mbalimbali zilimtafuta ili afanye kazi zao. Kwa sasa amemaliza elimu yake ya chuo kikuu na yuko kwenye kipindi cha kutafuta kazi ya kudumu kwa ajili ya maisha yake na familia yake.
Mtazamo Wangu
Kwa muda mrefu jamii zetu zimekuwa na
ubaguzi kwenye eneo la ajira kwa watu wenye ulemavu; mbaya zaidi ni pale mtu
mwenye ulemavu alipotazamwa kwa jicho lililokosa ujuzi wa kutathmini uwezo wa
mtu. Namkumbuka rafiki yangu mwalimu asiyeona (visually impaired)- ambaye kwa
sasa ni Lecturer, ana PhD. Siku aliyokwenda kuripoti kwenye kituo chake cha
kwanza cha kazi alikataliwa na wanafunzi pamoja na mwalimu wa taaluma wa shule
hiyo kukosa imani naye. Alijitambulisha kisha akawauliza mahali mwalimu wao
alipoishia kufundisha. Alitumia dakika 15 kuwaonyesha namna anavyoweza
kufundisha, kisha akaaga kuacha hilo darasa. Baada ya dakika 5 akiwa ofisini
alifuatwa na wanafunzi, wakamwomba msamaha, halafu wakamtaka aendelee
kufundisha.
Ukweli ni kwamba, watu wenye ulemavu
wanapopata ujuzi fulani wanautumia kikamilifu, wanakuwa waaminifu kwa taaluma
zao, wanakuwa na juhudi ambazo ni za juu sana. Jamii inatakiwa kufahamu kuwa
watu wenye ulemavu wanachangia maendeleo kwa familia zao, kwa jamii na kwa taifa kiujumla.
Pia tukumbuke kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza akafundishwa na kuumbiwa stadi anuai sambamba na watu wengine kwenye jamii zetu. Kwa mfano, tunao watu wenye ulemavu, mathalan wasioona, ni walimu kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo vikuu. Tena watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya kazi ambazo tunahisi hawaziwezi. Kitu cha msingi ni kutengeneza mazingira jumuishi na yenye kufikika na watu wote kwenye jamii. Tujumuike
kwa pamoja na kwa umoja ili kujenga nchi yetu bila kubaguana.
Tuwe ni watu wa kuona UWEZO wa mtu mwenye ulemavu mbali zaidi
ya ULEMAVU alionao, yaani “SEEING ABILITY BEYOND DISABILITY” na tuwe na uwezo na wepesi wa kutathmini stadi za mtu mwenye ulemavu kabla ya kuhoji anachoshindwa kwa kuwa ulemavu si kukosa
uwezo, yaani "DISABILITY IS NOT INABILITY".
"Think Inclusively ~~~ Act Inclusively
~~~ Create an Inclusive Nation".