Tuesday, November 11, 2014

Hatari kwa watu wapatao ulemavu ukubwani


Watu wengi hudhani kuwa ulemavu ni laana, mikosi au balaa. Watu wengine huenda mbali zaidi kwa kuwabagua watu wenye ulemavu kwa ulemavu wao. Hebu tuweke bayana madhara wayapatao watu wenye dhana hizi potofu mara wao wenyewe wakutwapo na ulemavu.

Moja, watu hawa maisha yao huwa ni mafupi sana kwa kuwa huwa na msongo wa mawazo wakijiona kuwa wamebeba uzito wa dunia. Huishia kuwa na msongo wa mawazo.

Pili, watu hawa hushuka sana umaarufu wao.  Watu hawa huanza kujitenga na wenzao kwa kujinyanyapaa wao wenyewe.

Tatu, ni watu wa lawama sana. Hupenda kulalamika na kunung'unika mno baada ya kukosa uwezo wa kufanya vitendo fulanifulani ambavyo awali alipendelea kuvifanya.

Nne, watu hawa hujishusha thamani, hawaoni umuhimu tena wa kuishi.

Ushauri!

Ni vema tukawa na msimamo chanya juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Hii itatusaidia kipindi ambacho tunakutwa na ulemavu; kwa kuwa ulemavu si wa mtu mmoja; ulemavu unaweza kumpata mtu yeyote, wakati wote na mahali popote. Hata hivyo ulemavu hauepukiki kwa namna yoyote kwenye jamii zetu. Ukimwona mtu mzee lazima atalalamika kuhusu macho kutokuona vema, masikio kukosa ufanisi wake, kumbukumbu kupungua, nk.

Cha zaidi sana, ni kwamba, ulemavu ni fikira za mtu binafsi. Tumeshuhudia watu wengi tunaowaita wanaulemavu wakiwa wasomi wa juu, wenye uchumi mzuri, wana familia za kutamaniwa na wengi, nk.