Friday, October 11, 2013

NYAKATI ZITATUAMBIA KUWA UKWELI WA LEO SI LAZIMA UWE UKWELI WA KESHO

Jamii Zetu na Mitazamo Juu ya Watu Wenye Ulemavu:

Ni muda muafaka kabisa kwa kila binadamu kujua kuwa binadamu ni binadamu tu. Amezaliwa na binadamu mwenzake na wanaendelea kuzaliwa binadamu kutoka kwa binadamu mwingine. Katika historia ya maisha ya binadamu, hakuna binadamu aliyewahi zaa kiumbe kingine zaidi ya binadamu mwenzake. Utofauti huja wakati binadamu anapozaliwa akiwa na maumbile tofautitofauti.

Binadamu huyu huwa mrefu na mwingine kinyume chake, yaani mfupi; Yule ana rangi nyeusi na mwenzake ni nyeupe; huyu amezaliwa na viungo vyote na mwingine amezaliwa kapungukiwa viungo vya mwili. Pia binadamu wote wana mwanzo na mwisho unaofanana; wote huzaliwa na mwisho wao ni mauti. Bado tena hawa binadamu wana mahitaji ya msingi yanayofanana, yaani chakula-malazi-mavazi. Utofauti huu haumpi mtu mmoja kuwa na sifa ya binadamu na mwingine kuikosa hiyo sifa. Naendelea kusema kama kibwagizo kwa msisitizo kuwa “binadamu aliyezaliwa na binadamu ni binadamu, na ana haki ya asili kwa kuwa amebahatika kuzaliwa binadamu na kwamba binadamu wote wana haki sawa mbele ya sheria ya mwanadamu na ile ya ki-Mungu.

Muasisi wa taifa la Tanzania (zamani ikiitwa Tanganyika), Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tarehe 18/02/1974, aliwahi sema maneno mazito juu ya kutetea ubinadamu wa watu wenye ulemavu ambao kwa karne nyingi umegubikwa na dhana potofu. Hii ni kwa sababu mtu anaweza akaigiza anazungumza ukweli kwenye jukwaa na baadae akiwa chini ya jukwaa akatekeleza kinyume na kauli yake ya jukwaani. Alisema hivi:

“Wasiojiweza wa nchi hii wanachohitaji sana ni nafasi ya kushiriki kwa ukamilifu na kwa usawa katika mambo ya nchi yao. Kulemaa miguu au mikono maana yake siyo kwamba mtu yule sasa ni mtu nusu. Maana yake tu ni kwamba yako mambo fulani kilema huyu hawezi kuyafanya; na kwa hiyo ziko kazi fulani hawezi kuzifanya, na matumaini fulani, ambayo hawezi kuwa nayo. Lakini yako mambo mengi mengine ambayo angeweza kufanya kama sisi tulio na viungo vyetu kamili tungemsaidia ayafanye. Vivyo hivyo kwa mtu aliye kipofu, au aliye kiziwi.
Watu hao si wapumbavu, wala si magogo, eti kwa sababu tu ya vilema vyao. Wanahitaji msaada wetu kuwawezesha kuvishinda vipingamizi walivyo navyo, na kuwawezesha kuyafanya kwa ukamilifu yale mengine wanayoweza kuyafanya”.

Pia rais mstaafu wa Jamhuri ya watu wa Afrika ya kusini, Nelson Mandela, 4 Disemba 1995, Johannesburg wakati akifungua michezo kwa watu wenye ulemavu wa viungo vya miguu alisema hivi juu ya ulemavu:

“…to recognise the presence of disability in our human midst as an enrichment of our diversity”.

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi:

“…kuutambua uwepo wa ulemavu katikati ya binadamu kama utajirisho wa utofauti wetu”.

Biblia, kitabu ambacho binadamu anaamini ni matokeo ya maagizo ya Mungu kwa mwanadamu kimezungumza mengi juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Angalia mafungu machache kutoka kwenye hiki kitabu kitakatifu.
Mambo ya Walawi 19:14, Biblia imeandikwa hivi:

“Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; mimi ndimi
Bwana”.

  Pia katika kitabu cha Kutoka 4:10-17, Biblia imenena wazi kuwa ni kusudi la Mungu kuweka huo utofauti:

 “Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kipofu? Si mimi Bwana?”

Katika kitabu cha Injili ya Yohana 9: 2 & 3 (Yohana 9: 2, 3) tunasoma maneno haya:

“Wanafunzi wake wakamwuliza, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, hata mtu huyu azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.

Ni swali zuri sana na liko wazi likidokeza mtazamo wa jamii walimoishi kipindi hicho. Wanafunzi wa Yesu hawakuwa na shida ya kujua ULEMAVU ni matokeo ya dhambi au la, kwani tayari walikuwa wanafahamu hivyo kuwa mtu kupata ulemavu ni matokeo ya dhambi. Shida yao kubwa ilikuwa kujua ni nani hasa aliyetenda dhambi kati ya aliyezaliwa kipofu au wazazi waliomzaa huyo kipofu.
Yesu alikuja na majibu yaliyowashangaza, pia  majibu haya yalibadilisha mtazamo wa wanafunzi wake. Majibu ya YESU yalikuwa hivi:

 “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.

Kwa tafsiri nyingine ya maneno ya Yesu ni kwamba si wazazi au mtoto aliyezaliwa akiwa na ulemavu ni wenye dhambi, bali hayo ni matokeo na makusudi ya uumbaji wa Mungu. “…bali kazi za Mungu zidhihirike (zionekane wazi, zitofautiane na kazi zingine zisizo za ki-Mungu) ndani yake (ndani ya huo uumbaji)”.

MAPITO MBALIMBALI AMBAYO BINADAMU WENGINE WALIYAPITIA KAMA HAYA YA WATU WENYE ULEMAVU

Wanawake na mfumo dume
Hili ni kundi la binadamu ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likidharauliwa, kubezwa, kuonekana hawawezi, si binadamu kamili na hata kufikia hatua ya wazi ya kumtawala na kumnyanyasa kama siyo binadamu mwenzake. Kundi hili liliwezeshwa na limeweza na tumeweza kushuhudia wanawake wakifanya mambo makubwa kwenye jamii, wameaminiwa uongozi kwenye jamii, wamesoma na wanaheshimika kwa ubinadamu na uwezo wao. Hebu tuwataje wanawake wachache maarufu; Angel Merkel (chancellor wa Ujerumani), Ellen Johnson Sirleaf (rais wa Liberia), Joyce Banda (rais wa Malawi), Asha Rose Migiro (naibu katibu mkuu mstaafu wa umoja wa mataifa), (Anne Makinda (spika wa bunge la Tanzania) nk.

Ubaguzi wa rangi
Kwa miaka mingi ubaguzi wa rangi ulikuwa umetanda juu ya dunia nzima. Mfano mzuri ni watu wa Jamhuri ya Afrika ya kusini ambako makaburu waliweka sera za kibaguzi hadi hapo mnamo mwaka 1994 walipopata kiongozi mzalendo Nelson Mandela. Tumeshuhudia pia nchini marekani watu weusi walivyobaguliwa, na jinsi Martin Luther King alivyopambana hadi kuuawa kwa harakati zake. Lakini sasa yupo rais mwenye rangi nyeusi nchini humo aitwaye Barrack Obama.

Ukoloni
Nchi nyingi za Afrika, Latin America na Asia zimetawaliwa na wazungu kwa muda mrefu sana. Mfano mmoja mzuri sana kwa bara la Afrika ni nchi ya Msumbiji ambayo ilitawaliwa na taifa la Ureno kwa muda takriban miaka 500. Ni mateso mengi waliyapata waliotawaliwa. Lakini mwisho wa siku tumeshuhudia nchi hizi ziko huru japo matokeo ya ukoloni huo bado yanaonekana kwa mbali. Kinachozingatiwa hasa ni kujitawala wenyewe wenye nchi.

Uundaji wa Kizazi Shupavu na Vita dhidi ya Wanyonge (Creation of the World Master Race & the War Against the Weak)
Hili ni tukio lililoanzia ulaya na kisha kusambaa nchi za Amerika na Asia. Mchakato huu ulianzishwa na mwanasayansi wa uingereza Sir Francis Galton (1822–1911), akiamini kuwa upo uwezekano wa kutengeneza kizazi imara duniani. Walitenga jamii kwenye makundi mawili makuu, yaani wasiofaa (unfit) na wanaofaa (fit). Upande wa wanaofaa kwenye jamii walikuwa ni wasomi na matajiri wasio na hitilafu za kimaumbile. Kundi la pili la wasiofaa kwenye jamii lilijumuisha watu wote wasio matajiri, na watu wote waliokuwa na ulemavu wa aina yoyote ile. Ili kuonesha kuwa ni kweli walidhamiria na mpango huo Adolf Hitler wa Ujerumani aliwatumbukiza watu wenye ulemavu kwenye chemba ya gesi na wakafa wote waliowekwa humo akiwatuhumu kuwa ni walaji wasio na matumizi (useless eaters).

Hitimisho
Matukio haya yote yaliyofanywa na binadamu waliojiona kuwa wao ni bora kuliko wengine yalifika kwenye wakati ulioonyesha ukweli kuwa watu wanawake ni binadamu halali kama wengine, watu weusi ni jamii ya binadamu ambayo nayo yastahili kupewa heshima yake ya kiutu. Pia kwenye mchakato wa ukoloni binadamu wa Afrika, Latin Amerika na Asia nao walipewa hadhi ya kujitawala, na hata kwenye mchakato wa kutengeneza kizazi bora ulioanzishwa na Francis Galton bado napo binadamu aliyeonekana kuwa “unfit” alipewa hadhi ya kuwa “fit”, japo bado kundi la watu wenye ulemavu  liko nyuma kuachiwa huru. Jamii zetu nyingi zinawaona watu wenye ulemavu kuwa hawafai, ni mzigo kwa familia na taifa kwa ujumla.

Kwa kuonyesha kuwa tatizo kwa watu wenye ulemavu bado ni kubwa ni pale matukio mbalimbali yanapotokea kwa watu wenye ulemavu na familia zenye watu wenye ulemavu. Tumeshuhudia albino wakiuawa kinyama kuashiria kuwa bado hawatambuliwi kuwa ni binadamu kwenye jamii wanamoishi. Pia tumekuwa mashaihidi juu ya mahusiano mabaya ya wanandoa mara azaliwapo mtoto mwenye ulemavu. Wazazi wa kiume wamekuwa ni wepesi wa kuwakataa watoto wenye ulemavu wakidhani ni laana imeingia kwenye nyumba. Vilevile tumeshuhudia watu maarufu wapatapo ulemavu hupotea kabisa kwenye ramani walizokuwemo, mfano kwenye siasa. Tumekuwa mashahidi jinsi jamii zenye watoto wenye ulemavu zinavyotupiwa kila aina ya lawama kwa kuzaa watoto wenye ulemavu, familia hizo zinakosa raha, zinafadhaika na hata wakati mwingine kuamua kujidhuru kama vile kunywa sumu, kujinyonga nk.

Ninaamini kuwa wakati na ukweli kwa pamoja vitasema dhahiri juu ya watu wenye ulemavu. Itafika wakati ambapo watu wenye ulemavu watakomboka kama walivyofanikiwa binadamu wengine. Wakati upo binadamu wawalaanio watu wenye ulemavu watatia neno la Baraka juu ya hao watu wenye ulemavu. Wakati upo tutakapoongea lugha moja katika maeneo yote yamfaayo binadamu kama vile mahakamani, hospitalini, kwenye uwaziri na hata ikulu. Maana wakati huo binadamu watatambuliwa kwa ubinadamu wao na si kwa maumbile. Ndipo tutakaponyamaza kusema na kuacha kuandika mambo ya kufikiri kijumuishi, kutenda kijumuishi, na kuhimizana kujenga taifa jumuishi. Wakati huo binadamu wote watakuwa wamejawa na fikira na matendo jumuishi na hakutakuwa na binadamu atakayemhimiza mwenzake juu ya hilo kwani nyakati za uhalisia zitakuwa zimetimia kwa binadamu wote.

Tumalizie kwa kufahamu ya kuwa; Mungu amemuumba mtu kwa namna ambayo maisha yake yapitie majira na nyakati. Hii ni kwa sababu ulimwengu huu umeumbwa ili ufanye kazi kwa kufuata majira na nyakati. Kwa kuwa imeandikwa:

“Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma ”(Mwanzo 8:22).

“BINADAMU ATABAKIA KUWA BINADAMU MILELE YOTE KAMA ASILI YAKE ILIVYO SASA”

Kwa maoni nitafute kupitia hapa kwa mawasiliano haya:
sokime2012@gmail.com
+255655410031
+255766750941