Jamii Zetu na Mitazamo Juu ya Watu Wenye
Ulemavu:
Ni muda
muafaka kabisa kwa kila binadamu kujua kuwa binadamu ni binadamu tu. Amezaliwa na
binadamu mwenzake na wanaendelea kuzaliwa binadamu kutoka kwa binadamu
mwingine. Katika historia ya maisha ya binadamu, hakuna binadamu aliyewahi zaa
kiumbe kingine zaidi ya binadamu mwenzake. Utofauti huja wakati binadamu
anapozaliwa akiwa na maumbile tofautitofauti.
Binadamu
huyu huwa mrefu na mwingine kinyume chake, yaani mfupi; Yule ana rangi nyeusi
na mwenzake ni nyeupe; huyu amezaliwa na viungo vyote na mwingine amezaliwa
kapungukiwa viungo vya mwili. Pia binadamu wote wana mwanzo na mwisho
unaofanana; wote huzaliwa na mwisho wao ni mauti. Bado tena hawa binadamu wana
mahitaji ya msingi yanayofanana, yaani chakula-malazi-mavazi. Utofauti huu
haumpi mtu mmoja kuwa na sifa ya binadamu na mwingine kuikosa hiyo sifa. Naendelea
kusema kama kibwagizo kwa msisitizo kuwa “binadamu aliyezaliwa na binadamu ni
binadamu, na ana haki ya asili kwa kuwa amebahatika kuzaliwa binadamu na kwamba
binadamu wote wana haki sawa mbele ya sheria ya mwanadamu na ile ya ki-Mungu.
Muasisi
wa taifa la Tanzania (zamani ikiitwa Tanganyika), Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, tarehe 18/02/1974, aliwahi sema maneno mazito juu ya kutetea ubinadamu
wa watu wenye ulemavu ambao kwa karne nyingi umegubikwa na dhana potofu. Hii ni
kwa sababu mtu anaweza akaigiza anazungumza ukweli kwenye jukwaa na baadae
akiwa chini ya jukwaa akatekeleza kinyume na kauli yake ya jukwaani. Alisema hivi:
“Wasiojiweza wa nchi hii
wanachohitaji sana ni nafasi ya kushiriki kwa ukamilifu na kwa usawa katika
mambo ya nchi yao. Kulemaa miguu au mikono maana yake siyo kwamba mtu yule sasa
ni mtu nusu. Maana yake tu ni kwamba yako mambo fulani kilema huyu hawezi
kuyafanya; na kwa hiyo ziko kazi fulani hawezi kuzifanya, na matumaini fulani,
ambayo hawezi kuwa nayo. Lakini yako mambo mengi mengine ambayo angeweza
kufanya kama sisi tulio na viungo vyetu kamili tungemsaidia ayafanye. Vivyo
hivyo kwa mtu aliye kipofu, au aliye kiziwi.
Watu hao si wapumbavu,
wala si magogo, eti kwa sababu tu ya vilema vyao. Wanahitaji msaada wetu
kuwawezesha kuvishinda vipingamizi walivyo navyo, na kuwawezesha kuyafanya kwa
ukamilifu yale mengine wanayoweza kuyafanya”.
Pia rais
mstaafu wa Jamhuri ya watu wa Afrika ya kusini, Nelson Mandela, 4 Disemba 1995, Johannesburg wakati akifungua michezo kwa watu
wenye ulemavu wa viungo vya miguu alisema
hivi juu ya ulemavu:
“…to recognise the presence of disability in our
human midst as an enrichment of our diversity”.
Kwa tafsiri
yangu isiyo rasmi:
“…kuutambua uwepo wa ulemavu katikati ya binadamu
kama utajirisho wa utofauti wetu”.
Biblia,
kitabu ambacho binadamu anaamini ni matokeo ya maagizo ya Mungu kwa mwanadamu
kimezungumza mengi juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Angalia mafungu
machache kutoka kwenye hiki kitabu kitakatifu.
Mambo
ya Walawi 19:14, Biblia imeandikwa hivi:
“Usimlaani
kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; mimi ndimi
Bwana”.
Pia katika kitabu cha Kutoka
4:10-17, Biblia imenena wazi kuwa ni kusudi la Mungu kuweka huo utofauti:
“Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa
cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au
kipofu? Si mimi Bwana?”
Katika
kitabu cha Injili ya Yohana 9: 2 & 3 (Yohana 9: 2, 3) tunasoma maneno haya:
“Wanafunzi
wake wakamwuliza, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, hata mtu huyu azaliwe
kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za
Mungu zidhihirishwe ndani yake”.
Ni
swali zuri sana na liko wazi likidokeza mtazamo wa jamii walimoishi kipindi
hicho. Wanafunzi wa Yesu hawakuwa na shida ya kujua ULEMAVU ni matokeo ya
dhambi au la, kwani tayari walikuwa wanafahamu hivyo kuwa mtu kupata ulemavu ni
matokeo ya dhambi. Shida yao kubwa ilikuwa kujua ni nani hasa aliyetenda dhambi
kati ya aliyezaliwa kipofu au wazazi waliomzaa huyo kipofu.
Yesu
alikuja na majibu yaliyowashangaza, pia
majibu haya yalibadilisha mtazamo wa wanafunzi wake. Majibu ya YESU
yalikuwa hivi:
“Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake;
bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.
Kwa
tafsiri nyingine ya maneno ya Yesu ni kwamba si wazazi au mtoto aliyezaliwa
akiwa na ulemavu ni wenye dhambi, bali hayo ni matokeo na makusudi ya uumbaji
wa Mungu. “…bali kazi za Mungu zidhihirike (zionekane wazi, zitofautiane na kazi
zingine zisizo za ki-Mungu) ndani yake (ndani ya huo uumbaji)”.
MAPITO MBALIMBALI AMBAYO BINADAMU
WENGINE WALIYAPITIA KAMA HAYA YA WATU WENYE ULEMAVU
Wanawake na mfumo dume
Hili
ni kundi la binadamu ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likidharauliwa, kubezwa,
kuonekana hawawezi, si binadamu kamili na hata kufikia hatua ya wazi ya
kumtawala na kumnyanyasa kama siyo binadamu mwenzake. Kundi hili liliwezeshwa
na limeweza na tumeweza kushuhudia wanawake wakifanya mambo makubwa kwenye jamii,
wameaminiwa uongozi kwenye jamii, wamesoma na wanaheshimika kwa ubinadamu na
uwezo wao. Hebu tuwataje wanawake wachache maarufu; Angel Merkel (chancellor wa
Ujerumani), Ellen Johnson Sirleaf (rais wa Liberia), Joyce Banda (rais wa
Malawi), Asha Rose Migiro (naibu katibu mkuu mstaafu wa umoja wa mataifa), (Anne Makinda (spika wa bunge la Tanzania) nk.
Ubaguzi wa rangi
Kwa miaka
mingi ubaguzi wa rangi ulikuwa umetanda juu ya dunia nzima. Mfano mzuri ni watu
wa Jamhuri ya Afrika ya kusini ambako makaburu waliweka sera za kibaguzi hadi
hapo mnamo mwaka 1994 walipopata kiongozi mzalendo Nelson Mandela. Tumeshuhudia
pia nchini marekani watu weusi walivyobaguliwa, na jinsi Martin Luther King
alivyopambana hadi kuuawa kwa harakati zake. Lakini sasa yupo rais mwenye rangi
nyeusi nchini humo aitwaye Barrack Obama.
Ukoloni
Nchi
nyingi za Afrika, Latin America na Asia zimetawaliwa na wazungu kwa muda mrefu
sana. Mfano mmoja mzuri sana kwa bara la Afrika ni nchi ya Msumbiji ambayo
ilitawaliwa na taifa la Ureno kwa muda takriban miaka 500. Ni mateso mengi
waliyapata waliotawaliwa. Lakini mwisho wa siku tumeshuhudia nchi hizi ziko
huru japo matokeo ya ukoloni huo bado yanaonekana kwa mbali. Kinachozingatiwa hasa
ni kujitawala wenyewe wenye nchi.
Uundaji wa Kizazi Shupavu na Vita dhidi
ya Wanyonge (Creation of the World Master Race & the War Against the Weak)
Hili
ni tukio lililoanzia ulaya na kisha kusambaa nchi za Amerika na Asia. Mchakato huu
ulianzishwa na mwanasayansi wa uingereza Sir Francis Galton (1822–1911), akiamini
kuwa upo uwezekano wa kutengeneza kizazi imara duniani. Walitenga jamii kwenye
makundi mawili makuu, yaani wasiofaa (unfit) na wanaofaa (fit). Upande wa
wanaofaa kwenye jamii walikuwa ni wasomi na matajiri wasio na hitilafu za
kimaumbile. Kundi la pili la wasiofaa kwenye jamii lilijumuisha watu wote wasio
matajiri, na watu wote waliokuwa na ulemavu wa aina yoyote ile. Ili kuonesha
kuwa ni kweli walidhamiria na mpango huo Adolf Hitler wa Ujerumani
aliwatumbukiza watu wenye ulemavu kwenye chemba ya gesi na wakafa wote waliowekwa
humo akiwatuhumu kuwa ni walaji wasio na matumizi (useless eaters).
Hitimisho
Matukio
haya yote yaliyofanywa na binadamu waliojiona kuwa wao ni bora kuliko wengine
yalifika kwenye wakati ulioonyesha ukweli kuwa watu wanawake ni binadamu halali
kama wengine, watu weusi ni jamii ya binadamu ambayo nayo yastahili kupewa
heshima yake ya kiutu. Pia kwenye mchakato wa ukoloni binadamu wa Afrika, Latin
Amerika na Asia nao walipewa hadhi ya kujitawala, na hata kwenye mchakato wa
kutengeneza kizazi bora ulioanzishwa na Francis Galton bado napo binadamu
aliyeonekana kuwa “unfit” alipewa hadhi ya kuwa “fit”, japo bado kundi la watu
wenye ulemavu liko nyuma kuachiwa huru. Jamii
zetu nyingi zinawaona watu wenye ulemavu kuwa hawafai, ni mzigo kwa familia na taifa
kwa ujumla.
Kwa kuonyesha
kuwa tatizo kwa watu wenye ulemavu bado ni kubwa ni pale matukio mbalimbali yanapotokea
kwa watu wenye ulemavu na familia zenye watu wenye ulemavu. Tumeshuhudia albino
wakiuawa kinyama kuashiria kuwa bado hawatambuliwi kuwa ni binadamu kwenye
jamii wanamoishi. Pia tumekuwa mashaihidi juu ya mahusiano mabaya ya wanandoa
mara azaliwapo mtoto mwenye ulemavu. Wazazi wa kiume wamekuwa ni wepesi wa
kuwakataa watoto wenye ulemavu wakidhani ni laana imeingia kwenye nyumba. Vilevile
tumeshuhudia watu maarufu wapatapo ulemavu hupotea kabisa kwenye ramani
walizokuwemo, mfano kwenye siasa. Tumekuwa mashahidi jinsi jamii zenye watoto
wenye ulemavu zinavyotupiwa kila aina ya lawama kwa kuzaa watoto wenye ulemavu,
familia hizo zinakosa raha, zinafadhaika na hata wakati mwingine kuamua
kujidhuru kama vile kunywa sumu, kujinyonga nk.
Ninaamini
kuwa wakati na ukweli kwa pamoja vitasema dhahiri juu ya watu wenye ulemavu. Itafika
wakati ambapo watu wenye ulemavu watakomboka kama walivyofanikiwa binadamu wengine.
Wakati upo binadamu wawalaanio watu wenye ulemavu watatia neno la Baraka juu ya
hao watu wenye ulemavu. Wakati upo tutakapoongea lugha moja katika maeneo yote
yamfaayo binadamu kama vile mahakamani, hospitalini, kwenye uwaziri na hata
ikulu. Maana wakati huo binadamu watatambuliwa kwa ubinadamu wao na si kwa maumbile.
Ndipo tutakaponyamaza kusema na kuacha kuandika mambo ya kufikiri kijumuishi,
kutenda kijumuishi, na kuhimizana kujenga taifa jumuishi. Wakati huo binadamu
wote watakuwa wamejawa na fikira na matendo jumuishi na hakutakuwa na binadamu
atakayemhimiza mwenzake juu ya hilo kwani nyakati za uhalisia zitakuwa
zimetimia kwa binadamu wote.
Tumalizie
kwa kufahamu ya kuwa; Mungu
amemuumba mtu kwa namna ambayo maisha yake yapitie majira na nyakati. Hii ni
kwa sababu ulimwengu huu umeumbwa ili ufanye kazi kwa kufuata majira na
nyakati. Kwa
kuwa imeandikwa:
“Muda
nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari,
wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma ”(Mwanzo
8:22).
“BINADAMU
ATABAKIA KUWA BINADAMU MILELE YOTE KAMA ASILI YAKE ILIVYO SASA”
Kwa maoni nitafute kupitia hapa kwa mawasiliano haya:
sokime2012@gmail.com
+255655410031
+255766750941
Kwa maoni nitafute kupitia hapa kwa mawasiliano haya:
sokime2012@gmail.com
+255655410031
+255766750941
4 comments:
Binadamu wote ni sawa. Pendo
Hakika Pendo umenena vema
disability is not inability.by Ben
That's true Benezeth
Post a Comment