Saturday, October 12, 2013

JE, NI NANI AJUAYE KUWA KESHO NI ZAMU YAKE YA KUWA MLEMAVU?

Miongoni mwa vitu vinavyomwogopesha binadamu kwenye maisha yake ni ulemavu. Ulemavu hauzoeleki kwa watu ambao si walemavu isipokuwa kwa wenye ulemavu tu. Mtu akiambiwa kuwa anaweza kuwa mlemavu kama asipotimiza jukumu fulani basi atafanya kila aina ya juhudi kutimiza hilo jukumu ili mradi tu aepuke ulemavu. Yupo rafiki yangu mmoja ambaye ni mwalimu wa watoto wenye mahitaji maalum, siku aliyoenda kuonana na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya yake akiomba ruzuku kwa ajili ya watoto wa shule aliambiwa hakuna hela. Mwalimu huyo alipomtolea mfano wa wazi na kumwuliza, “Je, wewe au watoto wako wangekuwa wenye ulemavu ungekuwa unajibu kama unavyonijibu leo hii?” Jibu la haraka kutoka kwa mkurugenzi huyo lilikuwa ni kutoa maagizo kwa wasaidizi wake ili wampe huyo mwalimu fedha alizohitaji ili kuepuka laana inayoweza kumpata, yaani ulemavu.

Mfano mwingine wa dhahiri
Rafiki zangu wawili ambao ni vipofu walisafiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam hadi mitaa ya Kigogo hapohapo Dar es Salaam, na mwenyeji wao aliwauliza hivi; “kutoka huko mlimani hadi hapa kigogo nani amewaleta?” Rafiki zangu vipofu wakajibu; “tumekuja peke yetu”. Majibu ya mwenyeji wao kwa hisia kali alijibu; “jamani, Mungu wa ajabu sana, utadhani nao ni watu vile!”.

Vilevile yupo mwalimu mmoja ambaye naye ni kipofu, wakati anakwenda kuanza kazi alikataliwa na walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo- wakidhani hawezi kufundisha kwa sababu ya upofu wake. Yule mwalimu kipofu baada ya kujitambulisha aliwauliza swali dogo tu kwa kusema “mara ya mwisho mlisoma mada gani na mliishia wapi?” Wanafunzi wakamwelekeza mada waliyosoma na mahali walipoishia. Yule mwalimu akafundisha kwa muda wa dakika 10 tu na akawaambia “kwaherini, nadhani sitaingia hili darasa kwa kuwa hamko tayari niwafundishe tangu mlipojua niko hapa shuleni kwenu”, kisha akaenda kukaa ofisini. Cha ajabu baada ya dakika 5 kupita, wanafunzi walituma wajumbe watano kwenda kumwomba mwalimu aendelee kufundisha hilo darasa kwani hapo awali hawakujua kuwa anaweza kufundisha.

Nitoe mfano mwingine wa mkuu wa wilaya moja hapa nchini. Mtawala huyu alitembelea shule fulani na kukuta walimu kadhaa wasio vipofu, na lengo la kiongozi huyo lilikuwa ni kuwapata wanafunzi wa kusimama barabarani kwa ajili ya kuupokea mwenge wa uhuru. Mkuu huyo wa wilaya aliuliza, “mkuu wa shule yuko wapi?”, akaelekezwa kuwa mkuu wa shule pamoja na uongozi wake wa juu hawapo, bali majukumu yote ameachiwa mwalimu wa zamu. Mkuu huyo wa wilaya akataka kuonana na huyo mwalimu wa zamu ili awapeleke wanafunzi kuupokea mwenge, ndipo walimu wale wakamjibu mkuu huyo wa wilaya kuwa mwalimu wa zamu ni mtu asiyeona (kipofu). Hoja iliyotoka kwa mkuu huyo wa wilaya ilikuwa, “Je, huyo mwalimu anawafundisha vizuri watoto wetu? Asije akatuharibia watoto wetu kitaaluma” (mwalimu kipofu aliyasikia mazungumzo hayo akiwa chumba cha ofisi mojawapo kwa kuwa mkuu huyo wa wilaya hakuingia ofisini).

Kwanza kabisa, niwatake radhi wasomaji wangu kwa kutokutaja majina halisi ya watu hawa na mahali walikokuwa. Kusudi si kuumbuana, kuchongeana wala kusemana vibaya. Lengo kuu hapa ni kujua kwa hakika kuwa haya matukio kwa watu wenye ulemavu yanatokea pande za watu wa kawaida, wasomi na viongozi wa nchi hii na kwingineko duniani kunakofanana  na utamaduni wetu huu.

Lakini hoja yangu ya msingi si kuwalaumu ni kwanini hawa wananchi, watawala na wasomi walitenda haya, bali ni kubainisha sababu zipi na vigezo vipi viliwasukuma kusema na kutenda hayo tuliyoyaainisha. Hebu sasa tuchunguze sababu zinazopelekea watu hawa kusema maneno na kufanya vitendo vinavyotafsiriwa kuwa havifai miongoni mwa binadamu.

Utamaduni
Kimaana, utamaduni ni mambo yote yanayojenga maisha ya mwanadamu. Ndiyo jumla ya njia na mbinu zote azitumiazo mwandamu ili aweze kuishi na kupambana na mazingira yake. Utamaduni ndio humuumbia mwanadamu uwezo wa kufikiri, ndio kipimo cha ufahamu wake. Mojawapo ya vipengele muhimu kwenye utamaduni wa jamii yoyote ile ni lugha.

Matumizi ya Lugha na Watu Wenye Ulemavu
Haya ni matumizi ya lugha kwenye jamii zetu ambayo yanaashiria dhahiri kuwa kwenye jamii zetu watu wenye ulemavu wamekuwa wakifikiriwa vibaya kunakopelekea vitendo viovu dhidi yao. Hapa chini ni baadhi ya methali kongwe kwenye jamii zetu ambazo zimehusika kwa namna moja ama nyingine kuchangia vitendo viovu juu ya watu wenye mahitaji maalum, hususan, watu wenye ulemavu.

1.    Kipofu hamwelekezi kipofu mwingine kwa mwenge
Hii ina maana kwamba watu vipofu hawawezi kaa pamoja na kupangilia mambo yahusuyo maisha. Hawawezi elekezana njia za mafanikio katika maisha.

2.    Kummulikia kipofu ni kumaliza mzigo wa nyasi na wala awezi kuona
Hapa tunapata maana ya moja kwa moja kuwa jamii zisipoteze muda na raslimali kuwekeza kwa mtu aliye kipofu (au mtu yeyote mwenye ulemavu). Mfano mmojawapo wa uwekezaji kwa watu wenye ulemavu ni pamoja na kutowasomesha shule.

3.    Nduguyo akifa sikio utapata shida kuita
Katika methali hii tunaona jinsi jamii inavyoogopa ulemavu na kubainisha jinsi mtu mwenye ulemavu anavyohesabika kuwa ni mzigo kwenye jamii zao.

4.    Kumwimbia kiziwi ni kumaliza nyimbo bure
Kuimba, kwa maana ya kisanaa ni kuleta burudani, kupendezesha mtu, kumfanya mtu awe na furaha katika maisha yake. Katika methali hii wanajamii wanaonyana kuwa wasifanye lolote kwa kuwapendezesha watu wenye ulemavu.

5.    Agana na nyonga kabla ya kuruka
Hii ni methali inayoonyesha ubaguzi kwa watu wenye ulemavu wa viungo. Mtu aliyelemaa kiuno hawezi agana na nyonga yake. Maana halisi ya kuagana na nyonga ni kufanya maandalizi kabla kuanza kufanya jambo lolote kwa vitendo. Je, watu wenye ulemavu hawawezi kufanya mambo yao kimaisha kwa kupangilia?

6.    Mzee (mgonjwa au mlemavu) anajifahamu mwenyewe au Aliye dhaifu yapasa ajifahamu mwenyewe.
Hii methali inatufundisha tabia mbaya ya kuwatenga watu wenye ulemavu.

7.    Asiyesikia la mkuu huvunjika guu
Kuvunjika guu ni laana kwa mujibu wa methali hii. Hivyo inaonyesha kuwa watu wote waliopata matatizo yaliyopelekea ulemavu wao ni matokeo ya laana ya kutokuwa wasikivu.

8.    Ukila na kipofu, usimshike mkono
Hii methali inahimiza wanajamii kutengana, kutokuwa karibu na watu wenye mahitaji maalum. Tufanye mambo kimyakimya ili watu wenye ulemavu wasijeiga na kufanikiwa kama watu wengine wasio na ulemavu.

9.    Ni bora uwe nacho cha thamani ndogo kuliko kukosa kabisa
Ni methali ambayo ilitumika kuwafariji watu/familia ambazo zilizaa watoto wenye ulemavu. Waliambiwa kuwa japo mtoto mwenye ulemavu si bora kama watoto wengine lakini ni bora kuliko wangekosa kabisa huyo mtoto.

10. Hata kama ni jinga litengenezee upinde
Methali hii ilitumika kuwafariji watu waliokuwa  na watoto waliokuwa na ulemavu ya kuwa motto ni mtoto hata kama ana ulemavu anastahili sehemu yake ya urithi toka kwa baba na mama.

Methali zingine kuhusu watu wenye ulemavu na dhana ya ulemavu

11. Usimwonyeshe kipofu njia
12. Katika nchi ya vipofu, chongo ni mfalme
13. Sikio la kufa halisikii dawa
14. Kichaa huponywa, ujinga hauponywi
15. Asiyesikia husafiri mbali sana, maana hata akiambiwa anakokwenda hatasikia
16. Kula na kipofu ni sawa na kula peke yako
17. Apendaye, chongo huita kengeza
18. Kipofu hadanganywi jicho
19. Mbona wanidanganya kana kwamba nina chongo?
20. Sijali hata akiwa na usaha masikioni, si mwanangu
21. Ukioga pamoja na mjinga hutakati
22. Hata kama ni mjinga ni wako
23. Kwa matendo haya uliyonitendea, kama hukufa utalemaa
24. Ngongo ni zuzu na Ngomisho ni zuzu
25. Kichaa huponywa, ujinga hauponywi
26. Heri kufa macho kuliko kufa moyo
27. Jicho ni moja, nalo laingia mchanga
28. Nduguyo akifa sikio utapata shida kuita
29. Afadhali kuchakaa nguo kuliko kuchakaa akili
30. Asiyekiuno naye huvua
31. Ukienda na mwenye chongo nawe jidai chongo
32. Mtu asiyekamilika viungo au akili, ukimtania hudhani unamtukana

Hitimisho
Ni nani ajuaye kuwa kesho atapoteza macho, masikio na viungo vingine? Nani ameandikiwa kuwa mlemavu?
Hii misemo imegharimu na kupelekea ugumu wa maisha pale inapotokea vinara wa matumizi ya kukejeli watu wenye ulemavu nao wapatapo ulemavu. Wanaumia viungo na saikolojia yao. Wengi wao hupata magonjwa mengine kama msongo wa mawazo na hata kufa, si kwa sababu ya ulemavu, bali ni mwangwi wa matumizi mabaya ya lugha kwenye jamii.


Hitaji pekee la kizazi cha sasa ni kupata shule thabiti za mawazo (school of thoughts) zitakazoweza kubainisha ukweli na uhalisia wa utamaduni wetu. Si shule hizi za mawazo zinazosisitiza kuenzi kazi za mababu zetu bila kuona athari katika ulimwengu wa sasa (contemporary world). Utamaduni ndio umekuwa adui mkubwa kwa maisha ya watu wenye ulemavu. Japo utamaduni unapofika kilele chake cha makuzi huwa ni mgumu kama chuma cha pua, lakini juhudi za dhati zikifika tutaweza kuubomoa na kuupandikiza utamaduni wetu pendwa. Penye nia pana njia na kila lenye mwanzo halikosi mwisho.

"Tufikiri Kijumuishi ~~~ Tutende Kijumuishi ~~~ Tujenge Taifa Jumuishi"

No comments: