Tuesday, September 16, 2014

Haki za watu wenye ulemavu zitambuliwe kikatiba


WAKATI mchakato wa katiba ukisuasua bado watu wenye ulemavu wamekuwa wakitaka marekesho ya katiba itayopatikana lazima haki za msingi zinazowahusu zingizwe kwenye katiba hiyo.
 Wanadai kuna haki ambazo wamezikosa kwa miaka mingi, wakidhani hali hiyo ilitokana na kutokuwemo katika katiba ya nchi.
 Hivyo, wanaamini kwa kuwa nchi imo katika fukuto la kuandika katiba mpya, ni vema mchakato huo ukazingatia haki za makundi yote ambayo yalisahauliwa katika katiba iliyopita.
 Ikumbukwe jamii ya watu wenye ulemavu imekuwa ikilalamikia ubaguzi katika kupata haki zao huku wakiamini kuwa hayo yametokana na udhaifu wa katiba iliyopo.
 Haki ambazo wanazikosa ni kama elimu bora, mpango mzima wa ujenzi wa miundombinu, masuala ya ajira, ugatuaji wa madaraka pia uwakilishi katika nafasi za kisiasa kwa mfano kupata ubunge na usalama wao kutozingatiwa.
 Umefika wakati kwa katiba ya mpya itakayoandikwa ikazingatia na kuijali  jamii hiyo, kutokana na takwimu za watu hao kuongezeka kila kukicha hadi kufikia watu milioni 5.
 Licha ya kuwa wako wale wanaozaliwa wakiwa na hali hiyo, lakini hivi sasa kuna ongezeko la kubwa la watu hao ambalo limekuwa likisababishwa na majanga mbalimbali ikiwemo ajali zinazotokana na uzembe kwa mfano  wa madereva.
 Hivyo, kutokana na ongezeko hilo ni vema kila penye huduma za kijamii za watu hao, sheria zikatungwa kwa kuongeza watendaji wanaotokana na jamii yao.
Hayo yatawezekana baada ya katiba mpya kupanua wigo wa kutoa nafasi mbalimbali ikiwemo nafafasi ya uwakilishi bungeni kwa asilimia tano ya bungeni wote.
Katiba itakapotoa nafasi hiyo, itasaidia kuwa uwakilishi mpana wa watu hao, wa kuwasemea wenzao masuala yanayowahusu.
 Ukiangalia yote hayo, wanayodai watu hao wenye ulemavu ni mambo ya msingi hivyo, ni suala la  jamii kwa ujumla kuwaunga mkono hususan kupitia wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
 Kama Wajumbe wa bunge hilo wataweka maslahi na itikadi zao za kisiasa pembeni na kusimamia haki za makundi yote basi hayo yote yatawezekana.
 Naamini kuwa hivi sasa umefika wakati wa watu hao kutungiwa sheria mbalimbali ndani ya katiba zitakazolinda maslahi yao badala ya kutungiwa maazimio kila mwaka huku watunga sera wakishindwa kuyatekeleza.
Iwapo haki zao zitatambulika kikatiba, naamini hakutakuwa na ujanja ujanja wa uvunjaji wa haki zao, na kwamba watu hao wana mchango mkubwa katika taifa hili.
Chanzo: Tanzania Daima