Maamuzi unayofanya leo juu ya mwanao ndiyo hatima ya maisha yake ya baadae. Maisha yake ya baadae yatakuwa ni matokeo ya maamuzi utakayomfanyia leo juu ya maisha yake. Maisha yetu ni matokeo ya maamuzi yaliyofanywa juu yetu na watu wengine.
Kabla ya kuzaliwa
Mama mjamzito afuate na kuzingatia maelekezo yote ya kitabibu juu ya ujauzito wake. Kula vyakula stahiki na fanya mazoezi sahihi kwa makuzi bora ya mtoto tumboni. Upo uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na ubovu wa mifupa, kuharibika akili, kulemaa viungo nk.
Club foot (Kifundo mguu) |
Wakati wa kuzaliwa
Fuata maelekezo ya madaktari ili mtoto wako azaliwe kwa wakati husika. Usisahau kumwomba Mungu ili awe nawe wakati huu. Mtoto akichelewa kuzaliwa kwa wakati na kwa kutumia vifaa saidizi kuna madhara ya kuharibiwa ubongo wake.
Wakati amezaliwa
Hakikisha unamlinda mwanao na vihatarishi vyote juu ya ulemavu unaoweza kumpata mwanao. Mfano: Epuka kumpa mwanao vifaa vyenye ncha kali kama sindano ambavyo vinaweza kutoboa macho na masikio, Epuka uwezekano wa kumwangusha mwanao (anaweza kulemaa akili na viungo), epuka kukaa na mwanao maeneo yenye kelele (ili kuepusha ukiziwi na kukosa utulivu-Hyperactivity). Epuka kumweka mtoto kwenye mchanga kama ule wa kupigia sakafu za nyumba. Ni hatari kwa macho ya mtoto. Upo ushuhuda mwingi juu ya watu waliopata upofu kupitia mchanga.
Pia mchunguze mwanao viungo vyake baada ya kuzaliwa. Kuna ulemavu uitwao "Club foot" au "Kifundo mguu" ambapo mtoto anakuwa na unyayo uliojikunja, matege yasiyo kawaida. Ukigundua mapema mpeleke mwanao hospitali kwa tiba zaidi.
Haya niliyoyataja na yale ambayo sikuyataja na mengine mengi unayoyafahamu yazingatie sana kwa ustawi wa maisha ya mwanao.
Msisitizo: Ulemavu una athari kubwa kwa mtu mwenyewe mwenye ulemavu, familia yake na hata ukoo wake. Athari hizi zinahusisha nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni kwa ujumla wake.
Najiandaa kukuletea mada ya athari za ulemavu kwenye maisha!
Fikiri Kijumuishi.....Tenda Kijumuishi..... Jenga Taifa Jumuishi......
No comments:
Post a Comment