Sunday, April 10, 2016

JE, WAJUA ATHARI ZA ULEMAVU KWA MAISHA YA MTU?




Kwa asilimia kubwa, ulemavu wenyewe sio tatizo, bali mtazamo wa jamii juu ya ulemavu huo ndio tatizo kubwa zaidi. Ukiacha ulemavu unaohusisha ubongo, ulemavu mwingine wote una faida ya kumwongezea akili nyingi mhusika mwenye ulemavu. Anakuwa na maisha ya utafiti wa kila siku juu ya tabia za binadamu na utamaduni wao. Ulemavu unaleta hamasa ya ugunduzi wa asili wa binadamu na tabia zake.
Hata hivyo, maisha ya ulemavu yamejaa kuanguka na kusimama kwa nyakati tofauti kutokana na tamaduni kinzani juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu. Nafsi rahisi (easy minds) za watu wenye ulemavu na washirika wao huanguka kwa anguko kubwa kwenye maisha ya kila siku. Hii inatokana na uzito na ugumu wa taratibu za mila na desturi kwenye jamii zetu. Pia kumbuka kuwa ukiona mtu shujaa mwenye ulemavu kwenye kila jambo ujue kapigana kwa nguvu zana ili kushinda mapito hayo. Mtu mwenye ulemavu hukutana na maneno makali yenye kukatisha tama, vitendo vya ukinzani, mitazamo kinzani kama tufani ya bahari, kila hatua ya makuzi na maisha yake ni ukinzani tupu. Ndio maana kuna makabila fulani ya kitanzania wakiona dalili ya ulemavu kwa mtoto mchanga wanamuua siku ile ile ya kwanza kwa kisingizio kuwa si “riziki”.
1. Athari ya kiuchumi
Familia nyingi zenye watoto wenye ulemavu, hasa wa akili zinakumbwa na ugumu kiuchumi kwa kuwa muda mwingi wanatakiwa wawe na watoto wao wenye ulemavu. Hali hii inapelekea wazazi hao kuacha kazi zao za kiuchumi. Zipo shuhuda nyingi kwa watu ambao nimepata kuongea nao wenye watoto wenye ulemavu.
2. Athari za kijamii
Jamii zetu zina mtazamo hasi juu ya ulemavu. Mtu mwenye ulemavu amekosa sifa kwenye jamii, anaonekana ni mtu tegemezi, hana haki, mnyonge, amelaaniwa na matokeo yake ni kutengwa na jamii yake. Nimeona watu wengi ambao kabla ya kuwa na ulemavu walikuwa maarufu kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini mara walipopata ulemavu “status” zao zilibadilika.
3. Athari za kimazingira
Watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali wanatakiwa watengenezewe njia wezeshi kwa maisha yao, yaani “deviated programs and means for people with disabilities”. Tumepungukiwa vifaa jumuishi. Mazingira mengi ya watu wenye ulemavu ni changamoto.
4. Sera za nchi
Zipo sera za watu wenye ulemavu na zingine kama miongozo kwa maisha ya wananchi kwa ujumla. Sera za watu wenye ulemavu ni ngumu kutekelezeka, na zile jumla hazina dalili ya ukaribu na mtu mwenye ulemavu.
Ushuhuda: Kuna rafiki mmoja ambaye ni mwalimu kipofu. Aliomba kazi ya kufundisha kwenye shule ya binafsi, kwa vile ufaulu wake ulikuwa mzuri walimwita kwenye usaili. Alipofika wakamwona kipofu, wakamwambia kwa kimombo”we need a teacher but not you, sorry for that.” Wakaongeza kusema: “Hatukujua kama wewe ni kipofu”.
Kiukweli ipo mifano mingi ya aina hiyo!
5. Utu wa mtu mwenye ulemavu
Fanya jaribio la uchunguzi: Fuatilia mahali ambapo ghafla ametokea mtu mwenye ulemavu usikie maneno ya watu juu yake. Hata kama hawasemi chochote utaona “facial expressions” zao tu. Kiukweli utagundua ya kuwa kwa mitazamo ya jamii zetu mtu mwenye ulemavu anawekwa kwenye jamii ya upili. Kila mtu hufikiri ana mamlaka juu ya mtu mwenye ulemavu, mtu mwenye ulemavu hakui kwenye jamii, siku zote hufikiriwa ni tegemezi, ana akili za kitoto, na kila afanyacho huonekana si sahihi.
Ugumu kwa wapatao ulemavu ukubwani ni ile hali ya kuzoea aina mpya ya maisha. Marafiki hupungua, imani ya watu kwake hupungua. Hii hali huwafanya watu hawa wenye ulemavu kuishi maisha ya simanzi siku zote.
Ushuhuda
Mwanafunzi wangu mmoja wa zamani alipata ajali na kukatwa mguu (unyayo wote), amekuwa na mazingira magumu sana. Amekuwa ni mtu wa kutoa machozi tu akifikiria ugumu anaoupata.


Usione shida kwa msisitizo ambao huwa nautoa kila siku juu ya mambo ya watu wenye ulemavu. Ukichunguza kwa makini haya madhara ya mtu kuwa na ulemavu unakuta mtu asiye na ulemavu anaogopa neno “ulemavu” kuliko ulemavu wenyewe. Akisikia habari za ulemavu na watu wenye ulemavu anahisi masikio yanapata kuumia. Kwa hakika, ulemavu unamgusa kila mtu kwa namna yake.
Je, ulishawahi kujiuliza mapito ya watu albino nchini? Mapito ya watu albino na watu wenye ulemavu mbalimbali ndiyo sababu kubwa inayonifanya niendelee kuzungumzia masuala ya ulemavu kwa kadri Mungu anavyoniwezesha kuwa na uhai kwa manufaa yetu sote. Tujifunze juu ya ulemavu, tujifunze tunavyoweza kuishi na ulemavu na/au watu wenye ulemavu.

Tufikiri Kijumuishi…..Tutende Kijumuishi……Tujenge Taifa Jumuishi…

No comments: