Hali ya elimu Tanzania inaendelea
kukaa vibaya na itazidi kuwa mbaya hadi hapo wavamizi wa elimu watakapoiacha
huru tena ikiwa kwenye mikono salama ya wanaelimu.
Tatizo kubwa hapa Tanzania
ni kwamba kila mtu anadhani anaifahamu vizuri elimu. Wanasiasa wasio na utaalam
wa elimu wanafanya maamuzi ya kitaalam kuhusu elimu bila kuwashirikisha wataalam wa elimu. Walimu
wamepuuzwa, wamebezwa, wameonekana hawafai. Inafika mahali watu wenye madaraka katika nchi hii wanasema kama walimu wameona ualimu haulipi waende wakatafute kazi nyingine. Kauli
hizi ni za watu wasioitakia mema nchi yetu.
“Big Result Now” nasema
haiwezekani mpaka walimu waheshimiwe, warudishiwe utu wao, waachiwe wafanye
mambo ya kitaalam kuhusu elimu. Kila mwanasiasa anaongea anachoweza kuhusu
elimu, waende wakafundishe tuone kama wanaweza. Majina mazuri, slogan nzuri na
misemo mizuri si utendaji.
Division Five nayo iko
mbioni na ni lazima ilete majanga. Naionea huruma sana sekta ya elimu, itakaa
utumwani kwa miaka mingi kama wana wa Israel hadi hapo mkombozi wake
atakapokuja. Huyu mkombozi bado hata hajatabiriwa, na haijulikani atatokea kona
ipi.
Nasisitiza, mambo ya
elimu waachiwe wanaelimu, maslahi ya walimu ni haki yao, waachiwe kilicho chao.
Siasa itatuliwe na wanasiasa na mambo ya elimu yatatuliwe na wanaelimu. Nchi bila
elimu iko gizani kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Pole Elimu, Poleni
wanaelimu, Poleni wanafunzi, Pole nchi yangu. Japo nchi yangu iko ICU kielimu
lakini hakuna juhudi yoyote kuinusuru na kifo kilichoikaribia. Elimu inaendelea
kupambwa majina mazuri sana japo uhai wake umefikia mwisho. Salaam Big Result
Now, Karibu Division Five. Na walimu wengi sasa watatoka hapa Division Five.
Siko Tayari Kushuhudia Umauti wako Elimu, Nitafumba Macho yangu nisione ukitoa pumzi yako ya mwisho. Sitahudhuria mazishi yako wala kuja kuanua matanga. Ni msiba ambao haujawahi tokea kwa nchi hii tangu hayati baba wa taifa aanze kuiongoza Tanganyika hadi kufikia Tanzania. Si kwamba sikupendi elimu, bali waliokuteka ni hatari hata kwa maisha yangu pia.
Kwaheri Elimu, Kwaheri ya kuonana!
No comments:
Post a Comment