Saturday, October 5, 2013

Je, ulemavu ni laana? Ni mikosi? Au ni dhambi?

Tufundishe nafsi, roho na akili zetu

Awali ya yote, napenda kukushukuru wewe msomaji wa makala hizi, na pia ninapenda na kufurahi sana ninapoona mrejesho wenu wa maoni. Inaonyesha kuwa mnayaona haya kwenye jamii zetu halisi yakitukia.
Sasa hebu tujikite kwenye mada yetu hii “Je, ulemavu ni laana? Au ni mikosi? Au  ni dhambi?

Maana ya ulemavu
Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (2004) inafafanua kuwa ulemavu ni hali inayotokana na dosari mwilini au/na akilini ambayo inasababisha mtu kushindwa kutenda mambo ambayo kwa kawaida angetegemewa kuyaweza na hivyo kumletea mtu huyo kizuizi katika utekelezaji wa majukumu yake katika jamii. Kizuizi katika utendaji kinatokana pia na mfumo wa mtizamo wa jamii dhidi ya mtu huyo.

Ulemavu ni neno linalotumika kwa mapana kuainisha maeneo matatu muhimu yafuatayo:
• Hali ya tatizo kadri linavyoonekana (impairment)
• Upungufu wa uwezo wa kutenda/kufanya jambo kwa njia ya kawaida kulingana na hali yake (Disability).
• Kizuizi katika kutenda jambo (handicap) kutokana na hali ya ulemavu  (Disability).

Maana ya mikosi (misfortune)
Ni hali ya kukosa bahati, kukosa kupata mema kwa njia ya imani aliyonayo mtu. Kushindwa kufanikiwa na/au kuandamwa na matukiomabaya ambayo chanzo chake ni laana.
Katika kitabu cha 1Samweli 28: 6; tunaona mfalme Sauli akipatwa na majanga makubwa ya kupigwa na Wafilisti, mkosi ambao ulitokana na dhambi yake ya kiburi mbele za Mungu wake. Imeandikwa hivi katika mstari wa 6:
“Lakini Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii”.

Maana ya Laana na Dhambi
Laana ni kukataliwa na wanadamu au Mungu kutokana na kosa lisiloweza kusameheka. Neno Dhambi (mistarget) inamaanisha ni UASI, kukosea lengo au shabaha ya kile ulichotegemea kukitimiza. Umeamriwa kufanya hiki wewe ukafanya kile-hiyo ni dhambi.

Je, ulemavu ni laana? Je, ni mikosi? Ni dhambi?
Mambo ya Walawi 19:14, Biblia imeandikwa hivi:
“Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; mimi ndimi Bwana”.

Maneno ya msingi katika mstari huu:
          Usimlaani, lina maana usimkatae au usimtenge (mtu mwenye ulemavu).
  …wala usitie kikwazo (stumblingblock), maana yake ni kwamba binadamu yeyote asimjengee mazingira magumu ya kuishi binadamu mwenzake mwenye ulemavu.
        …bali umche Mungu wako;
Umche Mungu wako kwa lipi?
Umche Mungu wako kwa uumbaji wa aina yake,na wala usimkosoe wala kumpinga Mungu kwa uumbaji huo.
…mimi ndimi Bwana.
Inamaanisha yeye Mungu ndivyo alivyoamua na wala mtu mwingine asihoji hilo.

Pia katika kitabu cha Kutoka 4:10-17, tunasoma maneno haya:
“Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kipofu? Si mimi Bwana?”
Haya maelezo yalitolewa na Mungu wakati nabii Musa alipokuwa akikataa kwenda kuwakomboa wana wa Israel katika nchi ya Misri. Musa alihofia kuwa angeshindwa kuongea mbele za Farao na kwamba huenda na wana wa Israel wasingemsikiliza kwa sababu ya ulemavu wake wa ugumu wa kuongea (speech impairment). Hii ilitokana na uzoefu wake kwenye jamii yake. Yawezekana yalikuwa yanamkuta hayo aliyokuwa akijitetea kwa Mungu.

Katika kitabu cha Injili ya Yohana 9: 2 & 3 (Yohana 9: 2, 3) tunasoma maneno haya:
“Wanafunzi wake wakamwuliza, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, hata mtu huyu azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.

Ni swali zuri sana na liko wazi likidokeza mtazamo wa jamii walimoishi kipindi hicho. Wanafunzi wa Yesu hawakuwa na shida ya kujua ULEMAVU ni matokeo ya dhambi au la, kwani tayari walikuwa wanafahamu hivyo kuwa mtu kupata ulemavu ni matokeo ya dhambi. Shida yao kubwa ilikuwa kujua ni nani hasa aliyetenda dhabi kati ya aliyezaliwa kipofu au wazazi waliomzaa huyo kipofu.
Yesu alikuja na majibu yaliyowashangaza, pia  majibu haya yalibadilisha mtazamo wa wanafunzi wake. Majibu ya YESU yalikuwa hivi:
 “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.

Kwa tafsiri nyingine ya maneno ya Yesu ni kwamba si wazazi au mtoto aliyezaliwa akiwa na ulemavu ni wenye dhambi, bali hayo ni matokeo na makusudi ya uumbaji wa Mungu. “…baki kazi za Mungu zidhihirike (zionekane wazi, zitofautiane na kazi zingine zisizo za ki-Mungu) ndani yake (ndani ya huo uumbaji)”.

Hitimisho
Ulemavu kwa ukweli wake ni kwamba unaleta madhara katika utendaji kazi kwa maisha ya kila siku ya mhusika mwenye ulemavu pamoja na kuleta ugumu wa mitazamo kwa familia yenye mtu mwenye ulemavu. Pia tuweke kwenye fahamu zetu kuwa ulemavu, kwa elimu ya kisayansi husababishwa na vigezo viwili tu ambavyo ni “mazingira na urithi”. Na kwa upande wa imani itokanayo na kitabu kitakatifu kiitwacho “Biblia”, ulemavu umeelezwa kuwa ni sababu za kiuumbaji, na pia tunaambiwa katika uumbaji huo kuna kusudio halisi. Si bahati mbaya wala mikosi, si laana wala dhambi pia.
Watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu, wote kwa pamoja tujitambue, tujue kuwa na ulemavu au la ni sehemu ya vionjo vya maisha ya binadamu. Wengine wamepata mafanikio kutokana na misukumo ya ulemavu, na vilevile wapo watu ambao ulemavu ndio umewafanya washindwe kufikia malengo yao katika maisha. Tena tusisahau kuwa wapo watu ambao kutokuwa na ulemavu kumewafanya wakaona mazingira ni rafiki, wakasahau kupambana na mazingira, na hatimaye wakashindwa kufikia malengo yao kimaisha pia.

Hivyo, nionavyo mimi, ulemavu unamfanya mtu kuwa makini na mazingira, humwezesha kuwafahamu marafiki na maadui wa kweli katika maisha. Huweza kumwezesha mhusika kujua asili ya binadamu na utofauti wa binadamu mmoja na mwingine. Hubainisha watu wenye haiba dhaifu dhidi yao walio imaira, hututenganishia kati ya wenye fikra potofu dhidi ya wale wabebao na kutemelea ukweli kwenye katika maisha yao.


 "FIKIRI KIJUMUISHI ~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI"

REJEA
BIBLIA TAKATIFU (1952)
Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (2004)

No comments: