"Leo nimekuja hapa kuweka
jiwe la msingi, siyo kutoa hotuba. Kwa hiyo kuna mambo mawili tu ninayotaka kuyasema tena kwa
kifupi sana.
Kwanza, Azimio la Arusha
linatamka wazi wazi kwamba Taifa letu limekubali wajibu wa kuwaangalia wananchi
wenzetu wasiojiweza: vipofu, viziwi, viwete, na wagonjwa wa akili. Lakini kwa
kweli tunazo shughuli nyingi mno hata hatuna nafasi ya kuwashughulikia wale
wenzetu wachache ambao kwa bahati mbaya viungo vyao vina vilema. Serikali, na
hata TANU, hushindwa kupata muda wa kutosha kuanzisha shughuli za kuwasaidia
wasiojiweza ili kuwawezesha kushirikiana na wenzao katika hali ya usawa. Kama
uwezo wenyewe mtu ulio nao ni wa kuwasomesha nusu tu ya watoto wote wa
Tanzania, basi huna budi kutumia nguvu zako zote za Kiserikali kuwafunza
walimu, kutafuta vifaa, na kujenga shule zitakazowatosha hao nusu
watakaofaidika kutokana na huduma hizo za kawaida. Huna uwezo wa kufanya zaidi.
Lakini kufanya hivyo maana
yake siyo kwamba watoto wengine sasa hawastahili huduma; kwa kweli udhaifu wao
unawapa haki zaidi ya msaada wetu. Kwa sababu hiyo sisi viongozi wa TANU na wa
Serikali tunafurahi sana tunapoona watanzania, na marafiki wa Tanzania,
wanaanzisha mipango ya kuwahudumia watu wa aina hiyo, hasa watoto wadogo.
Tunashukuru kupata watu wanaojitolea kuanzisha na kuendesha shule za kuwasaidia
vipofu, viwete, na viziwi, nasi tutakuwa tayari kuwaunga mkono kwa furaha na
kwa uwezo wote tulio nao.
Chama cha Tanzania cha
Kuwasaidia Viziwi ni chama kipya, kimeanzishwa miezi michache tu iliyopita; na
sherehe ya leo ni ushahidi wa kwanza wa juhudi zake. Napenda kuwapongeza
wanachama wa chama hicho kwa kazi yao waliyokwisha kuifanya, na kuwashukuru
wale waliowasaida. Natumaini kwamba wananchi kwa ujumla, na vyama vyao,
watafanya kila linalowezekana kuharakisha kazi yao na kuifanya iwe na manufaa
zaidi.
Jambo langu la pili
linafanana na hilo la kwanza. Wasiojiweza wa nchi hii wanachohitaji sana ni
nafasi ya kushiriki kwa ukamilifu na kwa usawa katika mambo ya nchi yao.
Kulemaa miguu au mikono maana yake siyo kwamba mtu yule sasa ni mtu nusu. Maana
yake tu ni kwamba yako mambo fulani kilema huyu hawezi kuyafanya; na kwa hiyo
ziko kazi fulani hawezi kuzifanya, na matumaini fulani, ambayo hawezi kuwa
nayo. Lakini yako mambo mengi mengine ambayo angeweza kufanya kama sisi tulio
na viungo vyetu kamili tungemsaidia ayafanye. Vivyo hivyo kwa mtu aliye kipofu,
au aliye kiziwi.
Watu hao si wapumbavu, wala
si magogo, eti kwa sababu tu ya vilema vyao. Wanahitaji msaada wetu kuwawezesha
kuvishinda vipingamizi walivyo navyo, na kuwawezesha kuyafanya kwa ukamilifu
yale mengine wanayoweza kuyafanya.
Katika shule ya watoto
vilema ya Mgulani; katika shule za vipofu za Lushoto, Tabora, na kwingineko;
katika shule ya viziwi ya Tabora pamoja na hii (itakapokuwa inafanya kazi)
watoto wetu wanafunzwa kuyafanya yale ambayo wanayaweza kuyafanya. Wanafunzwa jinsi
ya kujisaidia, wanafunzwa kujitegemea; na wanapata ufundi utakaowawezesha
kujitegemea. Jambo hilo linalingana na haki za binadamu; na liko katika mstari
wa siasa ya nchi yetu.
Lakini kipofu aliyefunzwa
kuendesha mitambo ya simu ofisini anaweza tu kujipatia riziki yake kwa kazi
hiyo kama akiajiriwa kuifanya kazi hiyo. Kijana aliye kiwete anaweza tu kuwa
karani, au mwendesha-mitambo wa kiwandani, kama atapatiwa nafasi ya kazi huko
ofisini au kiwandani wakati atakapoomba. Mtoto anayefunzwa katika shule hii
jinsi ya kuzungumza na wenziwe ataweza tu kutumia ujuzi wake kujipatia riziki
kama sisi wengine tutajitahidi kufikiria kitu anachoweza kufanya, na kama
tutachukua hatua za kutekeleza mawazo hayo. Haifai kuhesabu tu yale mambo
ambayo hawezi kuyafanya.
Baadhi ya watoto
watakaoingia katika shule hii watapata elimu yao yote katika shule hii, au
shule nyingine ya mafunzo maalum. Wengine wataweza, baada ya hapa, kuingia
katika shule za kawaida baada ya kujaribiwa na kupewa vifaa vya kuwasaidia
kusikia, au baada ya kufunzwa kuelewa neno kwa kutazama midomo. Ni wajibu wetu
kuhakikisha kwamba wanapata nafasi ya kuingia katika hizo shule za kawaida, na
kuhakikisha kwamba sisi wenyewe na watoto wetu tunawasaidia katika kupambana na
matatizo yao ya shida ya kusikia. Huo ndio wajibu wetu kama Watanzania, na kama
wajamaa. Vile vile ni wajibu wetu, kama Watanzania na kama wajamaa, kuweka
mipango katika nchi yetu itakayowasaidia hawa na vilema wengine wote waweze kushiriki
kwa ukamilifu katika maendeleo ya taifa letu. Na yako mambo mengi tunayoweza
kuyafanya, bila kutumia fedha au wataalamu ambao hatuna wengi, lakini ambayo
hatuyafanyi hivi sasa. Kwa mfano. Sasa hivi tunajenga maofisi ya serikali
ambayo huwezi kuingia bila ya kupanda ngazi. Lakini huwezi kupanda ngazi ukiwa
unajikokota kwa kigari, na ni vigumu sana kupanda ngazi kwa magongo. Matokeo
yake ni kwamba viwete hawawezi kuingia katika benki, au katika ofisi ya bima, au
wakati mwingine hata katika ofisi ya TANU au ya Serikali kupeleka shida zao,
achilia mbali kufanya kazi katika ofisi hizo. Na hata kama kwa bahati, nafasi
ya kuingilia, si ngazi bali ni mteremko mdogo, utaona mlango wenyewe ni
mwembamba mno hata kigari cha kiwete hakiwezi kupenya.
Natumaini kwamba wachoraji
picha wa majumba wote, na hasa wale wanaotayarisha makao makuu mapya huko
Dodoma watakumbuka sana mambo haya. Na endapo watasahau, itafaa sisi wengine
tuwakumbushe.
Vitendo vingine vidogo–vidogo
vinavyofanana na hivyo vinaweza kufanywa na wananchi kuwasaidia vipofu na
viziwi kushiriki katika kujenga Tanzania ya Kijamaa. Maana wanayo haki kutudai
nafasi zitakazowawezesha kujitegemea, siyo huruma inayompa sadaka “Yala
Maskini.”
Wale wote wanaotoa ama nguvu
zao ama fedha kujenga shule hii, na shule nyingine za aina hii za kuwasaidia
vilema, wanaweka msingi utakaowafanya watoto wasiojiweza wajitegemee katika
siku za mbele. Wao, pamoja na sisi wengine wote, tunapaswa kuindeleza kazi hiyo
katika maisha yetu ya kila siku na katika uhusiano wetu na viziwi, vipofu na
vilema.
Kwa moyo huo na kwa
matumaini hayo nina furaha kuliweka jiwe la msingi la shule hii. Huu ni mwanzo
mdogo sana wa kuwasaidia viziwi. Basi na tudhamirie kuikuza kazi hiyo.
Asanteni sana".
"FIKIRI KIJUMUISHI ~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA SHIRIKISHI"
No comments:
Post a Comment