Thursday, September 18, 2014

Wanafunzi walemavu waomba kuboreshewa miundombinu

Kutoka mkoani Tanga

WANAFUNZI walemavu wa shule ya Msingi Kisosora mkoani hapa, wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya mazingira ya shule hiyo iwe rafiki kulingana na uhitaji wao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.
Wanafunzi wenye ulemavu, Lucy Apolinali na Nyamkala Egness, waliiambia Tanzania Daima kuwa, kilio chao kikubwa ni ukosefu wa vitabu vya maandishi makubwa, miwani ya kusomea na usafiri.
"Tunakabiliwa na changamoto kubwa ya vitu hivi ambayo inatupelekea kushindwa kufanya vizuri katika masomo yetu, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea," alisema Nyamkala.
Awali, mwalimu wa walemavu shule ya Kisosora ambaye naye ni mlemavu, Selina Mremba, alisema shule yake inakabiliwa na upungufu wa walimu wenye taaluma ya kufundisha makundi maalumu, hali ambayo huathiri kiwango cha ufaulu wa wanafunzi walemavu.
Naye Ofisa Utetezi wa Haki za Walemavu Kituo cha Kutolea Mazoezi ya Viungo kwa Walemavu (YDCP), Prisca Mwakasindile, aliwataka wanafunzi wasiwabague walemavu, badala yake washirikiane nao katika masomo, stadi za kazi na michezo kwa lengo la kuwajengea elimu shirikishi ili wanapomaliza shule wawe na cha kujivunia.


Shule ya Msingi Kisosora, ina wanafunzi walemavu 25 katika madarasa tofauti, licha ya kukabiliwa na tatizo la upungufu wa vifaa, miundombinu ya vyoo  na majengo si rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: