Tuesday, January 6, 2015

Jifunze chanzo cha ualbino


By Neristera Kihoza

Albino ni watu wenye ulemavu wa ngozi unaosababishwa na ukosefu wa madini aina ya melanin mwilini ambapo madini haya husababisha kutokuwepo kwa rangi nyeusi kwenye ngozi na nywele pia, hivo basi wanandoa wanapokutana kimwili kwa lengo la kutafuta mtoto, kama mmoja wao ana madini haya, haijalishi ni albino au sio, kuna uwezekano mkubwa wa kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino).

Kwa hiyo mtu yeyote akijifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi sio laana, mikosi, wala balaa n.k kwa mtu huyo kama jamii kubwa ya kitanzania inavyoamini. Naomba tufunguke sasa ili tuwaone kuwa nao ni watu wa kawaida kama wewe na mimi, tofauti tu ni ngozi ila shughuli zote anaweza kuzifanya.

Nanyi washirikina mnaotaka utajiri wa haraka haraka kwa kutumia viungo vya binadamu wenzenu hivi hiyo dhambi mtaitubu wapi? Mmewafanya wenzetu kuwa wakimbizi kwenye nchi yao wenyewe kweli! na hata kutengana na familia zao! Naomba tutoke mapangoni jamani! Kwanini wenzetu wa nchi za nje hawana haya mauzauza?

Leo hii nimepata taarifa kuwa kuna mtoto mwenye ulemavu wa ngozi aitwaye Upendo Emanuel wa Mkoa wa Mwanza wilaya ya Kwimba ametoroshwa na wajinga wachache wasiowatakia heri wenzetu, cha ajabu sasa eti hata watu wanaojiita eti ni wasomi bado wana dhana potofu dhidi ya albino.

Naomba wewe mwenye upendo na hawa wenzetu tuungane pamoja ili tuwaelimishe watu waweze kuondokana na ubaya huu pengine shetani amewakamata pasipo kujitambua. Mwisho nawaomba watanzania wote tujenge hali ya upendo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi tule nao, tucheze nao na hata kushirikiana kwa mambo yote, kwani wengine huogopa hata kuwagusa jamani! Tusiwatenge kwa sababu we are under the same sun, mimi nawapenda sana hawa ndugu zangu.


Ubarikiwe sana kwa ushirikiano wako!

No comments: