Thursday, August 22, 2013

Under the Same Sun wataka Katiba iwafanyie haya watu wenye ulemavu

MCHAKATO wa kuunda Katiba Mpya bado unaendelea na sasa upo katika hatua ya uundwaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yatakayokuwa na jukumu la kuipitia Rasimu ya Katiba. Kazi hiyo inatarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
Pamoja na kuanza kwa mchakato huo wa uundwaji wa mabaraza ya katiba, wananchi wanaendelea kutoa mapendekezo yao yenye lengo la kuboresha mchakato huo wa upatikanaji katiba mpya.
Shirika linalojishughulisha na utetezi wa watu wenye ulemavu la Under The Same Sun ni miongoni mwa wadau wa katiba waliotoa maoni kuhusu mchakato huo ambapo kwa upande wake linasema “lingependa kuona Katiba Mpya inaheshimu, kuzitambua na kulinda haki za Walemavu”.
Meneja Uendeshaji wa Shirika hilo Gamariel Mboya na Mkurugenzi Mtendaji wake Vicky Ntetema wanasema kwa nyakati tofauti kuwa Shirika hilo limejikita katika kutetea watu wenye ulemavu wa ngozi nchini kwa kupitia programu kuu mbili ambazo ni elimu na uhamasishaji.
Kwa kuzingatia majukumu na malengo ya Shirika lao, wanaona vyema Katiba Mpya ikaboresha haki za kibinadamu za watu wenye ulemavu wa ngozi na hali za watu wenye ulemavu mbalimbali nchini.
Usawa na haki za Walemavu
Under The Same Sun inataka Katiba Mpya kutambua na kuweka mkazo juu ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu kwa kutambua mahitaji yao maalumu.
“Watu wenye ulemavu wa ngozi wanahitaji visaidizi katika elimu, visaidizi hivyo ni vikuza maandishi, vitabu vyenye maandishi makubwa (siyo chini ya font 14), nyongeza ya muda katika mitihani iliyochapwa kwa mujibu wa mahitaji yao, kutambuliwa kwa changamoto zao za uoni hafifu pamoja na matatizo ya ngozi,” anafafanua Gamariel Mboya.
Mboya anapendekeza Katiba ijayo ihakikishe kuwa Walemavu wa ngozi wanapatiwa tiba sahihi na huduma ya utambuzi wa viashiria vya saratani ya ngozi na kutibiwa katika hatua za awali.
“Pia ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ni suala linalochafua sura ya taifa kila uchao. Ili kuliondolea taifa sura hii na kuwafanya watu walemavu wa ngozi waishi kwa amani na utulivu, tunapendekeza mfumo wa nyumba kumi uwe wa kiserikali,” anasema na kuendelea;
“Shughuli za upigaji ramli, kuagua, kutambua wachawi, kuroga wengine, kupandisha cheo, kutajirisha watu, mafanikio katika biashara, kushinda uchaguzi, mitihani na kutumia viungo vya binadamu vipigwe marufuku kikatiba,”anasisitiza Mboya.
Wasiyoona na walemavu wa viungo
Watu wenye ulemavu wa kutoona na wale wenye ulemavu wa viungo, wanapaswa kutambuliwa kikatiba kwa kupatiwa mahitaji yao muhimu.
Mahitaji ya wasiyoona yameelezwa kuwa ni urasimishwaji wa maandishi ya nukta nundu (brail) kwenye vitabu, magazeti, mitihani na maeneo mengine ya kitaaluma na masuala ya habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Under The Same Sun Vicky Ntetema anasema Katiba inapaswa kuwajali walemavu wa viungo kwa kuhakikisha kuwa majengo katika sekta zote yanakuwa na miundombinu ambayo itawasaidia walemavu hao kufika kwa urahisi.
“Katiba Mpya inatakiwa kutambua mahitaji yote maalumu katika elimu kwa watu wenye ulemavu katika makundi yao mahususi; Wizara ya Elimu iandae mitaala ya elimu itakayotoa uelewa juu masuala ya ulemavu katika ngazi zote za elimu; ulemavu liwe somo la kujumuishwa kwenye mtaala wa kitaifa na lifundishwe kuanzia elimu ya msingi,” anaeleza Ntetema.
                Mtoto mlemavu wa viungo

Uwakilishi katika maamuzi
Ntetema anazungumzia pia uwakilishi wa Watu wenye ulemavu katika ngazi mbali mbali za kimaamuzi, akisema hawana uwakilishi kisheria katika ngazi ya kijiji hadi Bungeni.
Kutokana na hali hiyo, Shirika la Under The Same Sun wanapendekeza Katiba ijayo itoe fursa maalumu ya kuwapatia uwakilishi Watu wenye ulemavu kufuatana na makundi yao.
Wanasema siyo rahisi kwa mtu asiyeoona kueleza mahitaji ya kiziwi au kiziwi kutambua mahitaji ya walemavu wa ngozi, hivyo wanataka Tume ya Uchaguzi ya Taifa iangalie namna bora ya upatikanaji wa wawakilishi wao bila kupitia Vyama vya Siasa.
Kauli ya Chavita


Mawasiliano na kiziwi-kipofu


Wakati Under the Same Sun ikitoa kauli hiyo, Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Wilaya ya Ilala kimetaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili waweze kumweleza matatizo yao ambayo kwa muda mrefu yameshindwa kupatiwa ufumbuzi katika Katiba iliyopo.
Viongozi wa chama hicho walieleza nia yao hiyo walipofika ofisi za gazeti hili, ambako pamoja na mambo mengine, walifafanua namna katiba isivyowajali.
“Tumekuja na haya mabango moja likiwa na Picha ya Rais Kikwete na jingine lenye rangi na nembo ya Chama  Cha Mapinduzi (CCM) lakini pia yana lugha ya alama ili yawekwe kwenye Ofisi ya Rais na Ofisi za CCM kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao kwetu sisi watu wenye ulemavu wa kusikia na watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali,” Katibu wa chama hicho Gervas Komba.
Chavita pamoja na mambo mengine, wanataka Watu wenye ulemavu kuhamishwa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kuwa chini ya Ofisi ya Rais.
Wanasema kwa muda mrefu Wizara hiyo imeshindwa kukidhi mahitaji yao hivyo wanataka wawe karibu na Rais ili wamfikishie matatizo yao moja kwa moja.
Kuhusu matumizi ya lugha ya alama, Komba anasema Serikali ihakikishe kuwa lugha ya alama inajulikana na wananchi wote ili kurahisisha mawasiliano kati yao na watu wasio na ulemavu.
Kwa mujibu wa Komba, watu wenye ulemavu wa kusikia wamekuwa wakitengwa na jamii ikiwa ni pamoja na kukosa ajira  na huduma zingine kutokana na ugumu wa mawasiliano kati yao na jamii.
“Serikali ihakikishe kuwa lugha ya alama inatumiwa na jamii nzima kama ilivyo kwa lugha nyingine. Waajiri wengi wanakataa kutuajiri kutokana na ugumu wa mawasiliano kati yao na sisi, lakini pia tunashida ya kupata huduma za jamii kwa urahisi kwa sababu hiyo hiyo,”anasema Komba.
Anaeleza kuwa kufuatana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) wa mwaka 2010 unaozitaka nchi wanachama kuuridhia katika kutoa ajira kwa walemavu, Bunge la Tanzania bado halijafanya vya kutosha katika kuhakikisha sheria hiyo ya Kimataifa inatumika ipasavyo hapa nchini ili kutoa fursa sawa ya ajira kati ya walemavu na watu wasio na ulemavu.


Source: 
http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/-/1625946/1747930/-/item/2/-/145gel1/-/index.html

No comments: