Friday, August 16, 2013

Utamaduni unapogeuka kuwa Simba mla watu




Maana ya utamaduni
Utamaduni ni jumla ya mambo yote yanayotengeneza na/au yanayounda maisha ya binadam. Utamaduni ndio huwa kipimo cha kufikiri na kutenda. Utamaduni ndio hutufanya tutafsiriwe jinsi tulivyo.
Utamaduni wetu huhusika na maisha ya binadamu kiuchumi, kisiasa na kijamii. Chochote afanyacho binadamu huongozwa na utamaduni, na hapa ndipo tunaweza kujipima kama utamaduni wetu unatufaa au la.

Leo nazungumzia utamaduni katika Nyanja ya uchumi. Kama nilivyotangulia kusema kuwa kufikiri kwetu hutawaliwa na utamaduni tulionao. Vilevile mambo ya kiuchumi hutegemea fikira za binadamu zilizotawaliwa na utamaduni.

Uchumi wetu na watu wenye ulemavu (albino)
Miaka ya hivi karibuni kumetokea kuwa na kundi dogo la binadamu ambao utamaduni wao kiuchumi lazima wapate viungo vya albino. Kwa mtindo huu si rahisi sana kumbadilisha mtu atafute utamaduni mwingine ambao hajauzoea. Maisha yao yote wanaamini mafanikio na maisha mazuri kwao kiuchumi ni lazima wapate viungo vya wenzetu albino.

Ukiangalia kwa makini utaona kuwa adui mkubwa wa ndugu zetu albino ni utamaduni wa jamii zetu. Imefika mahali sasa tunapotambua kuwa utamaduni wetu tunaweza kuufananisha na mtu aliyefuga mnyama akidhani ni mbwa kumbe ni simba, na huyu mnyama alivyoendelea kuwa mkubwa ndipo alipojidhihirisha kuwa ni simba mla watu, na anajua mbinu zote za kumkamata binadamu.

Ushauri wangu kwa wanajamii wenzangu ni kwamba, tunatakiwa tubadili namna ya kufikiri, tubadilike kimtazamo, tufahamu ubaya na uzuri wa tamaduni zetu. Tuwe wepesi wa kung’amua mahali panapohitaji marekebisho kiutamaduni.
      Watoto albino wakionyesha kufurahia mazingira yao.



Mama mzazi akiwa na wanae wawili ambao ni albino. Mwanamke yeyote anaweza akazaa watoto wakiwa albino.



Chanzo cha picha:     http://24.media.tumblr.com/ccb063953efcb5113c5430005d53b5fe/tumblr_mjkddmFIQ31qhookmo1_500.jpg

http://www.scientificamerican.com/media/inline/killing-albinos-tanzania-albinism_1.jpg


1 comment:

Anonymous said...

Kwa Tanzania bado tuna safari ndefu sana, tunahitaji uvumilivu na juhudi katika kuondoa utamaduni huu wa mateso kwa binadamu wenzetu.