Sunday, October 6, 2013

Ndoa ya aina yake: Mume kipofu-kiziwi, mwanamke kiziwi


Ni mara chache sana kuona ndoa za aina hii, mume na mke wote kuwa ni watu wenye ulemavu. Imezoeleka kuona ndoa ambazo mmoja wa wanandoa ni mwenye ulemavu. Tumezoea pia kushuhudia mtu mwenye ulemavu akitaka kuolewa ama kuoa anapitia kwenye magumu kwanza ya kupata mchumba na pili upinzani kutoka kwa wazazi na ndugu wa mmojawapo wa wachumba hao.


Hivi majuzi jijini Dar Es Salaam manispaa ya kinondoni tarehe 14/09/2013, saa 10:00 jioni katika ukumbi wa brajec palifungwa ndoa ya kiserikali na mkuu wa wilaya ya kinondoni. Wanandoa hao, raia wa Finland, ambao wote ni walemavu, walifungua ukurasa mpya wa ufahamu wa binadamu kwa maamuzi yao. Mwanaume anaitwa Laura, ambaye pia ni kipofu-kiziwi (deaf-blind); na mwanamke anaitwa Flora ambaye nae pia ni kiziwi.

Bi. Flora akiwa na matron wake, ni mtafsiri wa lugha ya alama

Bw. Laura akihojiana na mtafsiri wake, pia yupo mpambe wake

Wanandoa Bw. Laura na Bi. Flora

Bi. Flora akimvalisha pete ya ndoa bw. Laura

Tunajifunza nini kutokana na ndoa hii?

Kwanza, kama taifa la Tanzania, tunahitaji kufahamu kuwa watu wenye ulemavu wa aina ya Laura na Flora ni wengi sana hapa nchini, tena wengi wao wanatoka familia masikini na za vijijini. Wamefichwa huko hata kupata elimu kwao ni vigumu. Pia taifa la Tanzania tunahitaji kuweka mipango thabiti ya kuongeza idadi ya wataalam wa mambo ya mahitaji maalum kama walimu, madaktari na watu wengine kwenye jamii kupitia kwenye mitaala iliyoboreshwa. Niliwahi pendekeza kuongezwa kwenye mtaala wa elimu Tanzania somo liitwalo "HUMAN DIVERSITIES". Hili ndilo somo ambalo lingeweza kutusaidia mawasiliano kwa watu wote kwenye jamii yetu ya Kitanzania.

Pili, kila binadamu ana uhuru wa kupenda na kupendwa, kuoa au kuolewa kama sheria, mila na desturi za nchi zinavyodai. Tendo la maamuzi kuhusu mwenzi wa maisha ni la watu wawili tu, na hao ndio watakaoishi pamoja. Si wazazi, ndugu wala wapambe wanaweza wakaingilia mahusiano ya watu wenye ulemavu. Ni maamuzi ya hao wawili tu.

Watu wenye ulemavu wanatakiwa kujiamini, kuthubutu, kufanya maamuzi magumu inapobidi kufanya hivyo, na jamii kwa ujumla nayo inatakiwa kubadili mitazamo juu ya ubinadamu, binadamu na jinsi binadamu anavyotofautiana na viumbe wengine. Binadamu huzaliwa na binadamu mwenzake, na ana haki ya asili kwa kuwa amezaliwa binadamu.

Mwisho, sote tujifunze kufikiri kijumuishi, kutenda kijumuishi kutakakopelekea kujengeka taifa jumuishi. Ujumuishi huu unakuja kwa sababu hakuna binadamu ambaye hupenda kutengwa na binadamu mwenzake kwa namna yoyote ile.

Mungu Bariki ndoa ya hawa wanandoa!

FIKIRI KIJUMUISHI ~~~ TENDA KIJUMUISHI ~~~ JENGA TAIFA JUMUISHI

No comments: