Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad amesema chama chake cha CUF hakiko tayari kujadili mfumo wa
Muungano wa serikali mbili kama inavyotetewa na wabunge wa CCM na Rais Jakaya
Kikwete.
Amesema tayari amewaandikia barua Rais Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo huo.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Isitoshe, alisema CUF imebaini kuwa kuna njama za kufuta
kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; “Zanzibar ni nchi” na kwamba
hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa Wazanzibari kamwe
hawatakubali kufanya hivyo.
Maalim Seif alisema haikuwa mwafaka kwa Rais Kikwete kukosoa
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa Muungano kuwa wa serikali
tatu.
Alisema Jaji Warioba aliweka kando itikadi yake ya CCM katika
utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuja na uamuzi huo kwa
vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba hayakuwa maoni
yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti la Muungano, ametoa
ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza Muungano wenye mfumo wa
serikali tatu,” alisema Maalim Seif.
Alisema Muungano wa serikali mbili hauvumiliki na kama kuna watu
wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza kutumia sheria yake ya kura ya
maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka jambo hilo.
“Nimemwandikia barua Rais Kikwete, nakala nimempelekea Rais wa
Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara wanataka Zanzibar iondoe kifungu
cha Katiba kinachosema Zanzibar ni nchi, jambo hilo halitapita...tutafanya
kampeni wananchi walikatae,” alieleza Katibu Mkuu huyo wa CUF.
Alisema ni jambo la kusikitisha katika hotuba yake alijisahau
kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge Maalumu badala yake akaegemea kuwa
mwenyekiti wa CCM.
Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho na kutaja ikiwa Serikali ya
Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi litachukua madaraka ya nchi.
“Rafiki na ndugu yangu Kikwete, usifikiri huu ni wakati ule wa
Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga. Mambo yamebadilika, usijifanye
ni Nyerere mpya, hakuna atakayekusikiliza na kubabaika,” alisisitiza Maalim
Seif.
Alisema ikiwa viongozi wa Muungano wanajiandaa kutisha
watu na kusababisha ghasia katika nchi, mahakama ya kimataifa ya makosa ya
jinai ipo na watakaosababisha fujo na umwagaji wa damu watafikishwa mbele ya
mikono ya sheria bila ya kujali nyadhifa na madaraka yao.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Seif--Hatuko-tayari-kujadili-serikali-mbili/-/1597296/2259296/-/item/1/-/x85oso/-/index.html
No comments:
Post a Comment