Naikumbuka siku ile! Nikiwa stationery moja hapa mkoani Morogoro, kwa nje kidogo kuna sofa ya kukaa wateja. Mara akaja kijana mmoja aliyekuwa na mtindio, akakaa kwenye sofa hilo. Katika hilo sofa alikuwa amekaa mama mtu mzima, tena ni mfanyakazi, zaidi ya yote ni mwalimu. Ghafla nikaona yule mama amesimama pembeni mwa sofa huku anajisemea polepole huku akisonya. Nikamwangalia kwa dakika kama tano hivi, nikaona amekosa amani kwa vile lile sofa amekalia kijana mwenye ulemavu.
Nilichogundua ni kwamba kuna baadhi ya watu hudhani ulemavu wameandikiwa jamii fulani tu ya watu. Pia kwa kukosa uzoefu wa kuchangamana na jamii ya watu wenye ulemavu kunawapelekea wao kuwa na mitazamo ya kibaguzi. Siku inapotokea wamepata watoto wenye ulemavu hawa watu ndio huwaficha ndani watoto wao, au wanawaua mapema kabla hawajawa wakubwa.
Hata kama hawataki kuwaona watu wenye ulemavu, lakini wajue ubinadamu wa binadamu wote unafanana, na kuwa na haki sawa za kimaisha. Pia, binadamu ni mtu yeyote aliyezaliwa na binadamu, na anayo haki ya asili kwa kuwa amezaliwa binadamu bila kujali umbile lake.
Fikiri kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi!
No comments:
Post a Comment